Saturday, April 6, 2013

RIWAYA: WASALIMIE KUZIMU========4

 

 

MTUNZI: Hussein Wamaywa

SIMU: 0755 697335


SEHEMU YA NNE


Saadan akamtazama Nasra na kuyafikia majibu yake, zilikuwa hoja za uhakika ambazo zingemgharimu muda mwingi kuziweka sawa ili kuondoa mashaka kwa Nasra, akajikuta akishusha pumzi za kukata tamaa na kusema.
“Sasa unataka kuniambia nini? Kwamba hunipendi na hutaki kuolewa na mimi?”
Ikawa zamu ya Nasra kumtazama Saadan kwa muda kabla hajayarudisha macho chini, kwa ujumla Saadan alikuwa amekata tamaa. Akaachia tabasamu dogo na kumuonea huruma.
“Sikiliza Saadan! Nikikwambia nakupenda, upendo kama huo ulionao wewe kwangu ninakuongopea! Baba wa watoto hawa ndiye haswa aliyeushika moyo wangu. Hata hivyo juhudi zako zimenifanya nigundue ni namna gani unavyonipenda.
Na wanadiplomasia, wanasaikolojia na hata wanaaikolojia wote wanakubali kwamba ni vizuri zaidi ukaishi na mtu anayekupenda sana kuliko wewe unavyompenda!
Kwa kuzingatia usemi huu na sababu nilizokueleza hapo nyuma, sioni kwa nini nikukatishe tamaa huenda nikakubali unioe, lakini kwanza unifanyie yafuatayo:-
“Kwanza nataka kuja Oman kama mtalii ili wazazi na ndugu zako wanione na pia unitambulishe kwao nione watanipokea vipi. Na labda ikiwezekana niishi nao kwa muda fulani nione tabia zao, waone tabia zangu. Baadae nafikiri nitakuwa nimeshajua nifanye nini!”
“That is good. Very good Nasra!” Saadan akishangilia. Nasra akamuonea huruma moyoni na kuendelea “Kwa sasa ningekushauri urudi Oman ukaendelee na shughuli zako. Acha umenikatia Pasport yangu na za wanangu pamoja na nauli sawa Saadan?”
Furaha ya Saadan ikazimika. “kwa nini tusiondoke wote Nasra?”
“We nenda tu, watoto wangu bado wanahitaji matunzo na wangalizi wa karibu. Sio busara kuwaanzisha mikimiki ya safari kwa sasa!” Saadan akaelewa.
“Sasa utakuja lini?”
“Munkari wa nini? Mawasiliano yapo, hali itakapokuwa shwari nitakufahamisha tu. Muhimu shughulikia Passport kwanza!”
“Nitashughulikia!” Saadan akasema akiwa ameridhika na kuongeza “Naomba uniruhusu nikuage kwa kukumbatia na kukubusu?”
Nasra akatabasamu na kuinua uso.
“Tuliza boli Saadan! Mambo yakiwa sawa, tutakuwa na karibuni robo karne ya kuishi pamoja! Katika kipindi chote hicho utanikumbatia, kunibusu na kukuruka nami tani yako!! Kwa sasa nione huruma, kumbuka mimi ni mzazi.
“Usijali Nasra!” Saadan akainuka na kuaga kabla hajaondoka, moyo na mwili ukiwa na furaha ambayo hakuwahi kuwa nayo kabla. Akamuaga pia mama Nasra alieyekuwa akimalizia kufua na kuondoka.
Mama Nasra akarudi wodini hima akiwa na mshawasha wa kutaka kujua kilichoongelewa. Akamuuliza Nasra juu juu hata kabla hajakaa chini.
“Ah! Nimeamua kumtosa tu ili arudi kwao salama. Vinginevyo angerudi ndani ya sanduku!” Nasra akamwambia.
“Una maana gani?” akauliza. Nasra akamsimulia kila kitu.
“Lakini hukufanya vizuri mwanagu kwa nini usimkatalie moja kwa moja ili akatafute Mwarabu mwenzake huko kwao? Unajua kama ni dhambi kumpa mtu matumaini ambayo hayapo?
“Dhamira mama! Ilinisuta. Alitaka kulia, tayari alishalengwa na machozi. Halafu vile alivyonisaidia pale ukumbini na fedha anazolipa hapa hospitali vimenifanya nisifanye hivyo!”
“Vizuri nilidhani utakaosa utu na kusahau fadhila. Sasa vipi utakwenda Oman? Manake ni lazima tu ataleta Passport kwani mie tayari ameniuliza juu ya cheti chako cha kuzaliwa!”
“Nitakwenda mama! Hii itakuwa ni fursa nyingine nzuri ya kwenda kutalii. Sikuwahi kufikiria kama nitakuja kufika Sultanate! Imetokea wacha niende, nitakwenda!”
“Angalia isije ikawa ile hadithi ya mwonja aslali…” Akatania
“Never mama!” Nasra akakataa kwa dhati “Haiwezi kutokea kwangu!” wakacheka kwa bashasha na kufurahi pamoja!
Jioni ya siku hiyo mama Nasra alikwenda kwake alikokutana na Alwatan Dafu. Akajua akianzisha madahalo hapo hawataelewana akajiandaa kwa mechi na kumwita ndani.
Dafu alipofika ndani, akakuta hali imebadilika mazingira yakamlazimisha afike kifuani kwa mkewe chezo la nguvu lakini la taratibu likaanza kuchezwa. Lilikuwa chezo la kiutu uzima!
Hapo ndipo mama Nasra alipopata nafasi ya kumlaumu mumewe kwa kitendo kilichotokea mchana kule hospitalini, Dafu akakiri kosa na kuahidi kutorudia. Lakini alipoelezwa azma ya Nasra ya kutaka kumuwekea wakili Promota Halfan, hamu ya uroda ikamtoweka ghafla akawa mbogo mfano hakuna.
Ilimlazimu mama Nasra kufanya kazi ya ziada kumrudisha tena kitandani, hali iliyopelekea mjadala wa Nasra kufungwa mara moja.
Hata hivyo tayari Alwatan Dafu alirudi akiwa na wazo moja na msimamo mmoja kwamba atadhibiti gari na akaunti ya Nasra isitolewe hata senti moja mbovu! Alipomueleza haya mkewe aliishia kutazamwa kwa mshangao kama anayemuhurumia.
Ni kweli mama Nasra alimuonea huruma mumewe ambaye hasira zake zilikuwa sawa na zile za mbogo aliyejeruhiwa ambaye hupambana hata na mti!. Mama Nasra hakutia neno tena, alizidi kunyonga nyonga kwa hasira! Huku mawazo yakiwa mengi kichwani. Alimsapoti sana mwanae Nasra, lakini pia alikuwa akimuheshimu na kumuogopa sana mumwewe Alwatan D!
Vitu hivi viwili vilimfanya ausubirie msuguano mwingine wa Nasra na baba yake kwa mshaka makubwa!
Ndivyo ilivyokuwa. Miezi mitatu baadae, watoto wa Nasra walikuwa na hali nzuri kiafya isipokuwa yule mdogo aliyeitwa Romota hali ya huyu haikuwa inaridhisha sana.
Miezi miwili baadae aliruhusiwa na kurudi kwao. Ulinzi wake uliongezeka mara dufu, sasa aliajiriwa mtu mwingine kwa ajili ya kumlinda Nasra tu! Hili halikuwa geti kali tena. Bali geti chungu hasa.
Bahati mbaya hali hii ambayo haikumfurahisha mama Nasra wala Nasra iliondoa amani iliyokuwa imetawala katika nyuma hiyo na kukaribisha machafuko. Nasra akazidisha kiburi na lugha mbaya.
Mara kwa mara Alwatan Dafu alikuwa akimpiga mwanae hasa pale Nasra alipomtamkia maneneo yasiyofaa.
Wakati huo Promota Halfan alishahukumiwa kifungo chake katika siku zote za kesi, Nasra hakuwa amepata nafasi ya walu hata ya kutoka nje ya nyumba yao wachilia mbali kuhudhuria kesi ya Halfan kule Mahakamani.
Gari lake la ushindi ‘Caddilac’ lilidhibitiwa vilivyo na hata siku moja hakuwahi kuiona funguo wala kadi yake. Mambo yote haya yalimuinamia Nasra na kumfanya aishi katika msongo mkuu wa mawazo pamoja na unyonge uliokithiri.
Mama yake alimuonea huruma sana na pengine ili kumpumzisha na madhila haya, akamshawishi aende Oman kwa Sadaam akabadilishe walau hali ya hewa. Wazo ambalo Nasra aliliafiki.
Lakini kabla wazo hilo halijafikishwa kwa Alwatan Dafu, Alwatan akaja na wazo jingine la kumpeleka Tanga kwa mdogo wake Dafu. Wazo ambalo pamoja na Nasra na mama yake kulipinga, bado Nasra alipelekwa Tanga kwa nguvu!
Mungu bariki mke na watoto wa baba yake mdogo walikuwa wakarimu hujaona, taabu ilikuja kwa huyo baba yake mdogo Mansoor! Alikuwa mkali na mkatili mara mbili ya Alwatan Dafu.
Ulinzi aliopata Tanga ulichusha na kuudhi na vile Alwatan Dafu alikuwa amemueleza kila kitu, hali ikawa mbaya zaidi. Nasra alivumilia kwa muda lakini aliposhindwa kabisa akamtolea uvivu na kuanza kumfanyia kama vile anavyomfanyia Alwatan Dafu, kipigo kikachukua nafasi.
Ni pale Nasra alipotishia kuingamiza familia nzima ya baba yake mdogo kwa sumu, ndipo Mansoor aliposalenda. Akainua mikono na kumrudisha Nasra Dar es Salaam.
Nasra akafurahia kwani alijua endapo atakuwa anaongea na mama yake, basi atapata mawazo na ushauri mzuri na hivyo kujipatia faraja ya pekee!
Jioni Alwatan Dafu alirudi akiwa mbogo vibaya akitataka kujua ni kwa nini Nasra ametishia kuangamiza familia ya mdogo wake kwa sumu.
“Ilinichosha baba. Na hata hapa naweza kufanya hivyo mkizidi kunifuatafuata!” Akajibu kijeuri.
“Eti?” Jibu la Nasra likaibua hasira kali iliyoamsha mvua ya kipigo kilichokuja kuamuliwa na mama Nasra. Usiku huo mama Nasra aliutumia muda wake mwingi akimfariji Nasra pamwe na kumkumbusha ‘wazo la Oman’ kabla hajamshauri la kufanya.
Nasra akapokea ushauri huo. Mpaka mama Nasra anaondoka kwenda kulala kwa Alwatan Dafu; Nasra alikuwa bado anatabasamu kwa furaha ya ushauri wa mama yake.
Unadhani walikosea walikosea walionena mtoto wa kike kwa mama yake? Hata kidogo!

* * *

“Baba naomba kuongea na wewe kabla hujaondoka!” Nasra alimfuata baba yake na kumueleza hayo muda mfupi kabla Alwatan Dafu hajaondoka kueleka katika shughuli zake.
Dafu akamtazama bintiye ambaye sasa amekuwa sugu na mwenye tabia za ajabu ajabu toka alipozaa mapacha, akatikisa kwa masikitiko.
Hapo kabla, Nasra hakuwahi kutaka kuongea na mzazi wake, tena kwa upole na heshima kama alivyofanya leo. Ushauri wa mama yake aliyeamini dawa ya moto ni maji ndio ulimfanya Nasra awe hivi.
“Hiyo ndiyo salaam Nasra?” Hasira zilificha nyuma ya swali hili.
“I am so sorry father!” Nasra akatahayari “Shikamoo!”
“Marhabaa! Enhe ulikuwa unataka kuongea na mimi kuhusu nini!”
“Mengi tu baba, mengi sana! Sidhani kama unaifurahia hii staili mpya ya maisha yetu ya paka na panya. Kumbuka wewe ndio baba yangu, nisipoongea na wewe juu ya shida zangu nani atafanya hivyo? Tafadhali nisikilize walau kwa dakika chache tu!”
“Wakati mwingine unakuwa binti mwenye busara Nasra. Nipo kwa ajili yako Mama, ninakusikiliza mwanangu!” Nasra akatabasamu, tayari alishamtoa mzee wake kunako uadui na kumfanya rafiki kitu ambacho kilikuwa kimeanza kuondoka katika kamusi za vichwa vyao.
“Ni kuhusu hili swala langu la kuolewa na Saadan!”
“Enhe, nakusikiliza endelea!”
“Samahani baba kama nitakuudhi kwa swali hili. Hivi baba ni kweli mimi ni mwanao kabisa kabisa?”
“Kwa nini unauliza hivyo mwanangu?!” Alwatan Dafu akamtazama vizuri.
“Nijibu kwanza baba, nijibu tafadhali”
“Of course! Wewe ni mwanangu wa kuzaa kabisa tena mtoto wangu wa pekee kwa nini unauliza swali kama hili Nasra?”
“Nina sababu baba! Nina sababu za kutosha. Kwanza mfumo wa maisha tunayokwenda nayo baada ya mimi kuzaa, ndio uliopelekea niulize swali hili. Kama mimi ni mwanao inaelekea hunipendi kabisa baba na uko tayari kunipoteza kama sitafanya kile ambacho unakitaka wewe.
Kitu ambacho wazazi wenye upendo wa dhati kwa watoto wao huwa hawathubutu. I think now you know kwa nini nimeuliza swali la aina hiyo”
“Sikiliza Nasra mwanangu, sio kwamba sikupendi la hasha! Nakupenda sana mwanangu tena nakupenda kuliko unavyoweza kufikiria! Unachojaribu kufanya wewe ni kupiga ngumi ukutani, kuuzia mkondo wa maji na wakati mwingine kujaribu kuyapandisha mlima! Kwa hili,huwezi kufanikiwa mwanangu!”
“Una maanisha nini baba?”
“Kwamba mimi ni baba yako mzazi niliyekuzaa, kukulea na kukusomesha. Mpaka sasa uko chini ya himaya yangu! Nimejaribu kukulea katika maadili mema kwa kadiri nilivyoweza, ili uje kuwa mke na mama mwema. Lakini yule khabith Halfan amenizidi ujanja na kuharibu kila kitu! Mungu amlaani atumikie kifungo kwa mateso makuu.
Tena inaonyesha amekujaza maneneo ya ajabu ajabu kiasi kwamba umeshindwa kupokea hata shauri wangu, umenidharau, kunidhalilisha na kuniona sifai! Umediriki hata…..!”
“Usiende mbali baba! Where are you going now?” Nasra akamuwahi alipoona ameanza kupandisha hasira ”Kwa hiyo endapo nitakubali kuolewa na Saadan amani itarejea baina yetu?”
“Bila shaka. Huo ndio ugonvi wetu mkubwa, Halfan sio mtu ni mnyama.”
“Oke, kukuonyesha ni kiasi gani ninakupenda baba yangu mimi nimekubali kuolewa na Saadan….”
Nasra akatua kwa muda kuangalia Alwatan Dafu anaipokeaje kauli hiyo. Dafu aliruka na kupiga ngumi hewani, akarukaruka na furahi mno. Akamkumbatia na kumbusu mwanae kwa fujo mpaka alipotosheka, akamuachia.
Nasra akaendelea “Lakini naomba uniambie kitu kimoja Daddy! Hivi ni kwa nini ukaamua kunitafutia mchumba toka mbali mbali hivi? Unataka kuniambia kuwa Tanzania nzima na nchi dada za Afrika mashariki amekosekana mtu wa kunioa hata uniletee Saadan toka Oman?”
“Inawezekana wapo! Lakini kwa jinsi nilivyokulea, nilitarajia upate mume mstaarabu kwa maana halisi ya neno hilo tena atakayekupenda kwa dhati. Oman ni nchi ya kiislam, nasi ni waislaam nilikuwa na yakini kabisa kule atapatikana kijana mstaarabu kama ninavyotaka. Na kweli, kama hutakuwa mnafiki utakubaliana na mimi kwamba Saadan ni mstaarabu!
Wangelikuwa wachumba wa kibongo na pengine wa kiafrika, hadithi ingekuwa nyingine pengine ningepigwa, ningetukanwa, ningedhalilishwa na kuwekwa katika daraja ambalo hata Matonya yule bingwa wa kuomba hastahili kwalo kuwako huko.
Lakini ilikuwa tofauti.
Ni Saadan aliyehisi tofauti toka mwanzo, akakukimbilia na kukudaka toka ulipojifungua, akawa bega kwa bega na sisi pamoja na mama yako kukupeleka hospitali ili kuokoa maisha yako na ya wanao. Kumbuka anafanya hivi akiwa hahusiki kabisa na mimba yako.
Hiyo tisa kumi ni pale alipokubali kukuoa hivyo hivyo ulivyo na watoto wako na kuahidi kuwalea na kuwatunza. Wachilia mbali kuwalipa gharama za matibabu na matunzo pale Agha Khan hospital! Tanzania ya leo nani anaweza kufanya kama yeye? Nani?!! Na ajitokeze tumuone.
Kwa yakini hakuna, hakuna kwa maana ya watu wanaojua kupenda, natumai ushujua naongelea nini!” Akahitimisha. Nasra akatikisa kichwa kukubaliana nae. Akasema.
“Ni kweli uyasemayo baba. Saadan ana moyo wa peke yake! Lakini mimi…..” Akasita na kumtupia jicho baba yake. Alitaka kusema ‘simpendi kabisa!’ macho ya Alwatan Dafu ndiyo yaliyombadilihia uelekeo wa maongezi.
“Lakini mimi simjui fika! Nahitaji kumjua kwanza baba pengine inawezekana yeye akawa mbaya zaidi kuliko wote uliowataja. Inawezekana anajifanya Simba mwenda pole ili ale nyama! Huwezi kujua baba!”
“Inawezekana wala sio uongo, wala sikatai utabiri wako. Lakini pamoja na yote bado sijaelewa unataka kuniambia nini? Ujue sitaki kabisa kuusikia upuuzi wa Halfan!”
“Swali zuri Daddy! Nataka kwenda Oman kwa Saadan. Nikakae walau mwezi mmoja, miwili au miattu! Nione hali halisi ya maisha ya kule, nimjue vilivyo, naamini nikirudi hapa nitakuwa nimerejea na tarehe ya harusi!”
“Good Nasra. Ndio sababu nakupenda Nasra. Wewe ni msichana wa ajabu. Ninajivunia hilo, I love you Nasra!” Baba Nasra akishangilia kwa vigelegele “Sasa umeamua jambo la busara kuliko yote


***NASRA anamuhadaa babake, naye ameingia mkenge.....
Je akienda OMAN atatoka hivi hivi ama ndo penzi litachipukia huko??

ITAENDELEA KESHO


No comments:

Post a Comment

Recent Posts