Friday, April 5, 2013

RIWAYA: PAINFUL TRUTH (UKWELI WENYE KUUMA)------------------- 1


MTUNZI: Nyemo Chilongani

MAWASILIANO: 0718 06 92 69

SEHEMU YA KWANZA


Msichana Happy alikuwa akilalamikia uchungu ambao ulikuwa umemshika katika kipindi ambacho alikuwa shambani akilima. Damu zikaanza kumtoka katika sehemu zake za siri, akalitupa jembe lake pembeni na kuanza kulishika tumbo lake ambalo aliliona kuwa katika maumivu makali.
Mama yake ambaye alikuwa pembeni pamoja na wakulima wengine wakaanza kumsogelea, Happy alionekana kuhitaji msaada kwa wakati huo. Wakatandika kanga zao chini na kisha kuanza kumzalisha pale pale shambani. Mpaka wanafanikiwa kumtoa mtoto, Happy alikuwa amepoteza damu nyingi sana mwilini mwake.
Mtoto mchanga alikuwa akilia, walipomwangalia vizuri, waligundua kwamba alikuwa mtoto wa kiume. Walichokifanya ni kumuinua Happy na kisha kumpeleka katika kivuli cha mti wa mwembe ambao ulikuwa pembeni kidogo ya shamba hilo.
Happy bado alikuwa akiendelea kulia, maumivu makali bado yalikuwa yamelikamata tumbo lake. Kwa haraka haraka mzee Lyimo akachukua baiskeli yake aliyokuwa ameiegesha pembeni na kisha kumpakiza Happy na safari ya kuelekea katika zahanati ya Machame kuanza.
Njia nzima Happy alikuwa akilia, maumivu yalikuwa yakiongezeka kadri muda ulivyozidi kwenda mbele. Mpaka wanafika Zahanati, Happy alikuwa hoi, hakuwa akiweza hata kusogeza kiungo chake chochote cha mwili wake.
Manesi ambao walikuwa nje wakipiga stori, wakaanza kuwasogelea, wakamteremsha Happy kutoka katika baiskeli ile na kisha kuelekea ndani ya Zahanati hiyo. Mama yake Happy, Vanessa alikuwa amembeba mjukuu wake huku akijitahidi kumbembeleza aache kulia.
Happy akaingizwa ndani ya moja ya chumba cha zahanati ile na kisha kulazwa kitandani. Bado alikuwa akiendelea kulia kutokana na maumivu makali ambayo alikuwa akiyasikia yakizidi kadri muda ulivyozidi kwenda mbele. Manesi wakaanza kumhudumia Happy mpaka pale ambapo dokta wa zahanati ile alipofika.
Mzee Lyimo na mkewe, Bi Vanessa walikuwa nje wakisubiri kusikilizia ni kitu gani ambacho kilikuwa kimeendelea ndani ya chumba kile. Wala hazikupita dakika nyingi, dokta akatokea mahali pale. Akaanza kuwaangalia huku macho yake yakionyesha wasiwasi fulani, aliporidhika, akaiweka vizuri miwani yake.
“Mtoto wake yupo wapi?” Dokta aliuliza.
“Huyu hapa” Bi Vanessa alimwambia huku akimkabidhi dokta mtoto yule.
Dokta alibaki akishangaa, mtoto yule alikuwa mweupe kupita kawaida, kichwani hakuwa na nywele nyingi kama ambavyo watoto wengi wa kiafrika wanavyozaliwa. Dokta hakuonyesha mshangao wake waziwazi, alichokifanya ni kumchukua mtoto yule na kuingia nae ndani ya chumba kile.
Mzee Lyimo na Bi Vanessa waliendelea kukaa nje ya chumba kile kwa takribani dakika kumi, mlango ukafunguliwa na dokta kutoka. Wote wakajikuta wakisimama kutoka katika viti vyao, dokta akawaomba wamfuate. Safari iliiishia ndani ya ofisi ya dokta yule.
“Kama msingemuwaisha binti yenu, hakika hali ingekuwa mbaya sana” Dokta aliwaambia.
“Kivipi?” Mzee Lyimo aliuliza.
“Amepoteza damu nyingi sana mwilini katika kipindi cha kujifungua, mbaya zaidi njia yake haikuwa kubwa kabisa jambo ambalo lilikuwa linamletea matatizo sana” Dokta aliwaambia.
“Lakini anaendelea vipi?” Bi Vanessa aliuliza huku akionekana kuwa na wasiwasi.
“Anaendelea vizuri. Ila inabidi tumpeleke KCMC kwa matibabu zaidi kwa sababu kuna baadhi ya dawa hapa ambazo hatuna” Dokta aliwaambia.
“Sawa”
Kama ilivyoongelewa na ndivyo ilivyotokea, siku iliyofuata Happy akapelekwa katika hospitali ya mkoa ya KCMC mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kupata matibabu zaidi.
*****
Happy alikuwa mtoto wa tatu katika familia ya mzee Lyimo ambaye alikuwa mkulima mkubwa aliyekuwa akivuma kuliko mtu yeyote Machame. Mzee huyu alikuwa akimiliki mashamba makubwa ya Migomba pamoja na mpunga. Kwake, ukulima ndio ilikuwa kazi yake kubwa ambayo alikuwa akiifanya akisaidiana na mke wake, Bi Vanessa.
Waliwasomesha watoto wao katika shule za kawaida sana ila waliwapatia kila kitu ambacho kilikuwa kikihitajika shuleni huko. Walitaka watoto wao wasome kwa sababu katika vipindi vyote vya maisha yao walikuwa wakiamini sana katika elimu.
Miaka ikazidi kukatika. Happy akaanza kubadilika na kuanza kuonekana mzuri. Weupe ambao alikuwa nao ulikuwa ukimvutia kila mwanaume ambaye alikuwa akimwangalia. Happy alikuwa akizidi kunawiri kadri siku zilivyokuwa zikizidi kwenda mbele.
Kama kawaida yao, wanaume hawakuwa nyuma, kila siku walikuwa wakijaribu kumuita Happy ambaye wala hakuonekana kuukubali wito. Kila mvulana akamuona Happy kama miongozi mwa wasichana ambao walikuwa wakiringa sana katika sehemu yote ya Machame.
Happy akafanikiwa kumaliza kidato cha nne katika shule ya Machame Girls Sekondary School. Hiyo ilikuwa ni faraja kwa wazazi wake, kumaliza shule kwa binti yao huyo ambaye alikuwa mtoto wao wa mwisho kulionekana kuwafurahisha. Mapenzi yao yalikuwa makubwa sana kwa Happy kuliko kwa watoto wao waliotangulia, David na Steve.
Wakamwandalia binti sherehe kubwa kama ya kumpongeza kwa kile ambacho alikuwa amekifanya. Kwenye sherehe, watu walikula na kunywa vya kutosha, kwa wale ambao walikuwa walevi, pombe ya ndizi ilikuwa nyingi na ya kutosheleza.
Kila kijana ambaye alikuwa mahali hapo alikuwa akihitaji kupata nafasi ya kuongea na msichana Happy. Nafasi hiyo ilionekana kuwa ngumu kwani muda wote Happy alikuwa pembeni mwa mama yake ambaye alionekana kuwa kila kitu katika maisha yake.
Sherehe ikaisha na kila mtu kuelekea nyumbani kwake. Siku iliyofuata asubuhi na mapema Happy akatakiwa kuondoka mkoani Kilimanjaro na kuelekea Jijini Arusha. Bila ubishi, Happy akaelekea huko kuanza maisha mapya huku akisubiri majibu ya kidato cha nne.
“Do you speak English? (Unaongea Kingereza?)” Ilisikika sauti ya mvulana mmoja wa kizungu akiwauliza vijana ambao walikuwa wamekaa kwenye benchi wakicheza drafti.
Hakukuwa na mvulana yeyote ambaye alilijibu swali lile kutokana na kutokuielewa lugha ya Kingereza, walibaki wakiangaliana tu huku kila mmoja akitamani mzungu huyo aondoke mbele ya macho yao.
Mzungu yule akabaki akiangalia huku na kule huku begi kubwa likiwa mgongoni mwake, kwa muonekano ambao alikuwa nao, alionekana kuhitaji msaada wa kitu fulani. Wala hazikupita dakika nyingi, Happy akaanza kuonekana mahali hapo. Mzungu yule akaonekana kushtuka, hakuamini kama msichana aliyefanana na Happy angeweza kuwa katika nchi kama Tanzania.
Umbo na uzuri wa Happy ukaonekana kumvutia, akaanza kupiga hatua kumfuata. Happy alipoyapeleka macho yake usoni mwa mzungu yule ambaye alikuwa akimfuata, akabaki akitetemeka. Alitamani kukimbia, ndio, lugha ya Kingereza alikuwa akiifahamu vilivyo ila kamwe hakujiamini kuongea na mzungu.
Akaanza kuongeza mwendo wake, mzungu nae akazidi kuongeza mwendo zaidi na zaidi. Happy akaonekana kutokuwa na ujanja, akaupiga konde moyo wake na kusimama. Mzungu yule akaanza kumsogelea zaidi, alipomkaribia, tabasamu pana likaanza kuonekana usoni mwake.
“Do you speak English? (Unaongea Kingereza?)” Mzungu yule aliuliza.
“I do (Naongea)” Happy alijibu. Mzungu akaonekana kufurahi zaidi.
“I need your help, can you just help me (Ninahitaji msaada wako, unaweza kunisaidia?)” Mzungu yule aliuliza.
“Yeah! I can help you (Yeah! Ninaweza kukusaidia)” Happy alijibu.
“Okey! Am a tourist from U.S.A. I come here in Tanzania for two main reasons, fistly, I want to visit Ngorongoro National Parks and secondly I wanna see mount Kilimanjaro (Mimi ni mtalii kutoka nchini Marekani. Nimekuja nchini Tanzania kwa sababu kuu mbili, kwanza ningependa kutembelea mbuga ya wanyama ya Ngorongoro na pili ninataka kuuona mlima Kilimanjaro)” Mzungu yule alimwambia Happy.
“So, what can I help you? (Kwa hiyo nikusaidie nini?)” Happy aliuliza.
Mzungu yule alibaki kimya kwa muda, akayagandisha macho yake usoni mwa Happy, kadri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo uzuri wa Happy ulivyozidi kuonekana usoni mwake. Alijiona kuwa na kila sababu ya kumwambia Happy kile ambacho kilikuwa kimeanza kujengeka moyoni mwake.
“Helllow...” Happy aliita mara baada ya kumuona mzungu yule akiwa ameduwaa huku amemkodolea macho.
“Where were we? (Tulikuwa wapi?)” Mzungu yule aliuliza huku akionekana kutolewa katika lindi la mawazo.
Happy akaonekana kukasirika, alichokifanya ni kugeuka nyuma na kisha kuendelea na safari yake. Mzungu yule hakuweza kuvumilia hata kidogo, akaanza kupiga hatua kumfuata Happy ambaye alikuwa akitembea kwa mwendo wa haraka haraka kama mtu ambaye alikuwa akiwahi kitu fulani.
“Exccuse me (Samahani)” Mzungu yule alisema na Happy kusimama.
“Can you tell me your name? (Unaweza kuniambia jina lako?)” Mzungu alimuuliza.
“No. I can’t (Hapana. Siwezi)” Happy alisema na kisha kuendelea na safari yake.
Mzungu yule hakuonekana kushindwa, kumruhusu Happy aondoke katika mikono yake ingeonekana kuwa kosa kubwa ambalo angejutia katika kipindi chote cha maisha yake. Alijiona kuwa na sababu ya kufanya jambo lolote lile ili mladi tu amueleze Happy jinsi alivyojisikia moyoni.
“My name is Wayne Ryn. Am from U.S.A. What is your name? (Jina langu ni Wayne Ryn. Ninatokea nchini Marekani. Unaitwa nani?)” Wayne aliuliza.
Happy akasimama na kuanza kumwangalia Wayne usoni. Watu wote ambao walikuwa wakiendelea na shughuli zao wakazisimamisha na kuanza kuwaangalia. Uso wa Happy ukaonekana kukasirika lakini uso wa Wayne ukaonekana kutabasamu.
“Happy” Happy alijibu na kisha kuanza kupiga hatua tena kuondoka.
“Happy...Ok! Let me call you Happiness. You are a beautiful girl that I’ve never seen (Happy...Sawa! Acha nikuite Happiness. Wewe ni msichana mzuri ambaye sijawahi kumuona)” Wayne alimwambia Happy ambaye alikuwa akipiga hatua kuelekea nyumbani kwa shangazi yake alipokuwa akiishi hapo Arusha.
Wayne hakutaka kunyamaza wala kusimama, bado alikuwa akionekana kuwa king’ang’anizi kupita kawaida. Aliendelea kumfuatilia Happy mpaka katika kipindi ambacho aliingia ndani ya geti. Bila hiyana wala aibu, nae akaingia ndani huku begi likiwa mgongoni mwake.
“Naona umekuja na mgeni” Shangazi yake, Bi Selina alimwambia mara alipomuona Happy akiingia huku Wayne akiwa nyuma.
“Yaanii nashangaa kwa nini ananifuata fuata. Nimechoka. Yaani anakera sana” Hapy alisema huku akiingia ndani.
Wayne akaanza kuongea na Bi Celina huku akijaribu kumwambia kuhusu msaada ambao alikuwa akiuhitaji kutoka kwa Happy. Hapo hapo Bi Selina akamuita Happy na kuanza kuongea nae pembeni. Mara ya kwanza Happy alionekana kukataa lakini baadae akakubali.
“Sawa nimekubali” Happy alimwambia shangazi yake.
“Usiogope. Anachokitaka kutoka kwako ni msaada tu wa kumtembeza hapa na pale. Atatoa kiasi cha dola kumi kila siku. Hauoni kama hizo ni fedha nyingi kwako?” Shangazi yake alimwambia.
Wayne hakutaka kuingia moja kwa moja na kulielezea lengo lake, alichokitaka ni kuingia kwa lengo jingine kabisa la kuhitaji msaada wa Happy na kuwa kama mwenyeji wake. Malipo ya dola kumi kwa siku zilikuwa fedha nyingi sana hasa katika mwaka huo wa 1990.
Siku iliyofuata, Wayne akafika nyumbani hapo na kuondoka na Happy. Njia nzima Happy alikuwa na jukumu la kumuelekeza Wayne kila kitu alichokuwa akikiona. Mawazo ya Wayne yalikuwa pengine kabisa, kichwa chake kiliwaza mapenzi tu.
Walitembelea sehemu nyingi tu hapo Arusha, mwisho wa safari yao, wakaamua kwenda hotelini. Mara ya kwanza Happy alionekana kuogopa lakini kutokana na maneno mengi ya Wayne, akajikuta akikubali na kwenda nae hotelini.
Ndani tena chumbani, Wayne akaonekana kubadilika. Akaanza kuongea mambo mengi ya mapenzi huku akijaribu kumbembeleza Happy. Muda wote huo, Happy alikuwa akiumauma vidole vyake tu. Happy hakuwa na nguvu za kumwangalia Wayne usoni, muda wote alikuwa akiangalia chini.
Hata alipoanza kushikwa bega alitulia tu, nguo yake ya juu ilipotolewa wala hakuleta ubishi wowote ule. Alikuja kushtuka mara alipojitazama na kujikuta akiwa mtupu. Akajaribu kuleta purukushani lakini akaonekana kushindwa.
Wayne akalala kifuani kwake, Happy akabaki akilia tu kwa maumivu makali. Bikira ambayo alikuwa nayo ndio ilikuwa siku ya mwisho kukaa mwilini mwake. Shuka likatapakaa damu. Happy akabaki akilia, hakuamini kama kweli kwa siku ile alikuwa amefanya mapenzi kwa mara ya kwanza.
“Mungu wangu! Kumbe niko kwenye tarehe zangu za kupata mimba” Happy alijisemea huku akionekana kushtuka katika kipindi ambacho Wayne akiwa pembeni akichukua taulo na kuelekea bafuni kuoga.

Je ni nini kitaendelea katika maisha ya Happy na Wayne?
Huu ni mwanzo wa hadithi hii ndefu ambayo kila siku haitoweza kukuchosha kuifuatlia.
Kwa hadithi zangu zaidi ungana nami kwenye PAGE yangu iitwayo NYEMO THE PRINCE.

ITAENDELEA.....

No comments:

Post a Comment

Recent Posts