Monday, April 8, 2013

RIWAYA: PAINFUL TRUTH (UKWELI WENYE KUUMA)

 MTUNZI: Nyemo Chilongani

MAWASILIANO: 0718 06 92 69


SEHEMU YA TANO

Happy alionekana kuchanganyikiwa, hakuamini kama kweli Wayne alikuwa akitoka chumbani kwake huku akionekana kuwa na hasira mara tu alipothubutu kumwambia kuhusiana na ule ujauzito ambao alikuwa nao. Mshtuko mkubwa ukampata moyoni mwake hali iliyompelekea kuinuka pale kitandani na kuanza kumfuata Wayne.
Wayne alikuwa akitembea kwa mwendo wa haraka haraka, Happy akajitahidi kukimbia kumfuata huku akiita lakini Wayne hakugeuka nyuma. Happy hakutaka kuendelea kumfuata Wayne, akasimama na kisha kuanza kulia.
Tukio lile ambalo lilikuwa limetokea lilikuwa limemuumiza moyoni mwake zaidi ya tukio lolote ambalo liliwahi kutokea maishani mwake. Akaanza kupiga hatua kurudi nyumbani kwao, macho yake yalikuwa yakitoa machozi mfululizo.
Mama yake na shangazi yake wakaonekana kushangaa, hawakujua ni kitu gani ambacho kilikuwa kimetokea mpaka Wayne kutoka chumbani mule na kuondoka huku akionekana kubadilika. Hapo ndipo Happy alipoamua kuwaambia kile ambacho kilikuwa kimetokea.
“Yaani amekataa mimba yake?” Bi Vanessa aliuliza huku akionekana kushtuka.
Happy hakujibu kitu, bado alikuwa akiendelea kulia mfululizo. Alihisi kwamba kulikuwa na kitu kilichokuwa na ncha kali ambacho kilikuwa kimeuchoma moyo wake. Hakujua ni kitu gani ambacho alitakiwa kukifanya ili siku moja Wayne aamini kwamba mtoto yule alikuwa wake.
Happy akarudi chumbani na kujifungia, siku hiyo wala hakutaka kuongea na mtu yeyote yule, alikuwa akilia kwa uchungu. Kuna wakati alikuwa akinyamaza, ila kila alipokuwa akiliangalia tumbo lake, akaanza kulia zaidi na zaidi.
Mpaka katika kipindi ambacho mzee Lyimo alikuwa akitoka shambani na kuingia hapo nyumbani, bado Happy alikuwa amejifungia chumbani kwake. Alipopewa taarifa juu ya kilichoendelea, mzee Lyimo akaanza kupiga hatua kuufuata mlango wa kuingia chumbani kwa Happy.
Mlango ulikuwa umefungwa kwa ndani, akaanza kugonga lakini wala haukufunguliwa kitu ambacho kilimfanya kuanza kuliita jina la Happy huku akiendelea kugonga. Hazikupita hata dakika nyingi, Happy akafungua mlango na mzee Lyimo kuingia.
Macho ya Happy yalikuwa mekundu huku yakiwa yamevimba hali iliyoonyesha kwamba alikuwa amelia kwa muda mrefu sana. Mzee Lyimo akakaa kitandani na kuanza kuongea nae. Moyo wa mzee Lyimo ulimuuma zaidi, kamwe hakutarajia kama mzungu Wayne angeweza kuikataa mimba ile.
“Haiwezekani. Ameikataa?” Mzee Lyimo aliuliza huku akionekana kutokuamini.
“Ndio. Ameikataa” Happy alijibu.
Mzee Lyimo akasimama na kutoka nje ya chumba kile. Akauona mwili wake ukiwa umekufa ganzi kabisa. Hakuaamini kile ambacho alikuwa amekisikia kutoka kwa Happy, alitamani akutane na Wayne na kuongea nae ili aone kama alikuwa na ujasiri wa kuukataa ule ujauzito mbele ya macho yake.
Baada ya hapo, maisha ya Happy yakaendelea kama kawaida ingawa muda mwingi alikuwa akitawaliwa na huzuni. Alikuwa akijitahidi kula vyakula vizuri ambavyo vilikuwa vikimpa afya bora yeye pamoja na mtoto.
Mara kwa mara alikuwa akihudhuria kliniki kama ambavyo madaktari walivyotaka afanye. Kamwe hakulala katika kitanda kisichokuwa na neti, alikuwa akiyalinda maisha yake na ya mtoto wake ambaye alikuwa tumboni.
Ingawa ilikuwa ni vigumu sana lakini akaamua kujisahaulisha kuhusu Wayne, akaamua kuishi maisha yake peke yake, hakutamani kabisa kumuona Wayne mbele ya macho yake, alionekana kumchukia kuliko kiumbe chochote duniani.
Miezi tisa ikatimia na ndipo Happy akajifungulia shambani katika kipindi ambacho alikuwa akilima pamoja na wazazi wake hatua iliyowapelekea kumpeleka hospitalini.
Happy alikuwa amelala juu ya kitanda ndani ya chumba kimoja katika hospitali ya KCMC iliyokuwa Moshi mjini. Bado hakuwa ameongea kitu chochote kile. Dripu moja baada ya nyingine zilikuwa zikiingiza maji katika mishipa yake.
Happy alikuja kufumbua macho yake baada ya masaa nane kupita. Akayapeleka macho yake huku na kule, yakatua katika nyuso za wazazi wake. Tabasamu likaanza kuonekana usoni mwake. Mzee Lyimo na Bi Vanessa wakaanza kupiga hata kumfuata.
“Mtoto wangu yuko wapi?” Happy aliuliza kwa sauti ya chini.
“Kimaro. Tulikuja nae hapa. Amewekwa katika chumba maalumu” Mzee Lyimo alijibu.
“Silitaki jina hilo baba. Sitaki mtoto wangu aitwe Kimaro” Happy alisema kwa sauti ya chini.
“Sawa binti yangu. Unataka aitwe nani?”
“Aitwe Andy” Happy alijibu.
“Kwa hiyo aitwe Andy Wayne?”
“Hapana. Aitwe Andy Ryn. Hili ni jina la babu yake. Sitaki achukue jina la baba yake” Happy alisema.
Hicho ndicho kilichoamuliwa. Jina likawa limekwishapatikana. Baada ya siku mbili, Happy akaruhusiwa kurudi nyumbani. Kila wakati alikuwa pembeni ya mtoto wake, watu mitaani walikuwa wakishangaa namna mtoto yule alivyokuwa mweupe.
Afya yake ilikuwa bora hata zaidi ya watoto wengine ambao walikuwa wamezaliwa mitaani hapo. Happy alimthamini sana mtoto wake hata zaidi ya alivyojithamini yeye mwenye. Miezi ikakatika, Andy Ryn akaanza kujifunza kutembea.
Katika kila hatua ambayo alikuwa akiifikia, Happy alionekana kuwa na furaha. Ila kamwe hakuweza kumsahau Wayne kwani kadri alivyokuwa akimwangalia Andy, alifanana sana na baba yake. Mpaka katika kipindi hicho hakujua ni kitu gani kilikuwa kimetokea katika maisha ya Wayne katika kipindi ambacho alikuwa ameondoka na kuelekea nchini Marekani.
Mwaka wa kwanza ukapita, wa pili ukaingia na kupita, Wayne hakuwa ameonekana kabisa mbele ya macho yake. Mwaka wa tatu ukaingia na kupita na mwaka wa nne kuingia. Hapo ndipo Happy akaamua kumuanzisha Andy katika shule ya chekechea iliyokuwa hapo Machame.
“Atakuwa na akili kama za mama yake” Happy alijisemea huku akimvarisha Andy nguo tayari kwa kumuanzisha shule.
Katika kipindi ambacho Happy alikuwa akiingia shuleni hapo pamoja na mtoto wake, walimu wote wakaonekana kushangaa, mtoto wa Happy alionekana kuwa tofauti kabisa. Alikuwa ni mzungu kwa asilimia themanini huku ishirini zilizobaki akiwa amechukua asili ya mama yake.
Andy akaanza kusoma katika shule hiyo. Kwa siku ya kwanza tu aliyofika shuleni hapo, uwezo wake ulijionyesha wazi. Ingawa alikuwa na umri mdogo lakini alikuwa na uwezo mkubwa sana kiasi ambacho kila mwalimu alikuwa akishangaa.
“Mmmh! Huyu mtoto ni wa maajabu nini?” Mwalimu Nuru alimuuliza mwalimu Leonila ambaye nae alikuwa akishangaa tu.
“Wala sijui. Ila uwezo wake unanishangaza sana. Nimewahi kufundisha watoto zaidi ya elfu tano katika shule hii, lakini mtoto huyu ameonekana kuwa wa kipekee sana” Mwalimu Leonila alimjibu mwalimu Nuru.
Mwaka wa tano na wa sita ukaingia. Andy akaanzishwa darasa la kwanza katika shule ya Machame Primary School. Kila mwanafunzi alikuwa akimshangaa, hawakuwahi kumuona mtoto wa kizungu akiwa anasoma katika shule kama ile.
Maswali mengi yalikuwa yakimiminika vichwani mwa walimu wa shule hiyo asili halisi ya mtoto huyo. Kila mmoja alikuwa akiongea lake. Mpaka amefikisha miaka sita, hakukuwa na mtu ambaye alikuwa akifahamu kama Andy alikuwa mtoto wa Wayne ambaye alikuwa ameikataa mimba yake kipindi cha miaka sita iliyopita.
****
Ilikuwa ni taarifa mbaya ambayo ilikuwa imesikika masikioni mwa Bwana Brown na mkewe, Bi Lydia. Waliiangalia simu ile ya mezani ambayo ilikuwa imepigwa na kupewa taarifa ile ya ajali mbaya huku wakionekana kutokuyaamini masikio yao.
Wakaonekana kuchanganyikiwa, wote walijiona kuwa kwenye ndoto iliyojaa huzuni ambapo baada ya muda wangeshtuka kutoka usingizini na kumuona Wayne akiendelea kujiandaa na harusi pamoja na mchumba wake, Kristen.
Hiyo haikuwa ndoto, lilikuwa ni tukio halisi ambalo lilikuwa limetokea katika maisha yao. Walichokifanya ni kuondoka na kuelekea katika hospitali ya Jackson Heights ambayo walikuwa wameelekezwa iliyokuwa katika mji wa Albertson hapo hapo jijini New York.
Gari likafunga breki ndani ya eneo la hospitali ile, wote wakateremka na kuanza kuelekea ndani ya hospitali hiyo kubwa. Waandishi wengi wa habari walikuwa mahali hapo kwa ajili ya kupiga picha na kuandika kila kitu ambacho kilikuwa kinaendelea kwani tukio lile la ajaili lilikuwa limegusa hisia za watu wengi nchini Marekani.
Bwana Brown na mkewe wakaingia ndani ya jengo lile huku wakipigwa picha na waandishi wale waliokusanyika katika eneo la hospitali ile. Breki ya kwanza ilikuwa ni nje ya chumba cha wagonjwa mahututi ambacho alikuwa amelazwa Wayne.
Wote wawili wakajikuta wakitokwa na machozi hasa mara baada ya kuuangalia mlango wa chumba kile kilichoonekana kutisha. Wakakaa vitini huku bado machozi yakiendelea kuwatoka. Walitakiwa kusubiri mahali hapo mpaka pale ambapo wangeruhusiwa kuingia ndani ya chumba hicho kwa ajili ya kumuona mtoto wao.
Masaa yalikatika lakini hakukuwa na yeyote ambaye alikuwa ameruhusiwa kuingia, nao hawakutaka kuondoka mahali hapo, waliendelea kusubiri zaidi na zaidi. Usiku ukaingia na hata asubuhi kufika lakini bado hawakuruhusiwa zaidi ya madaktari kupishana mlangoni.
Hali ya Wayne ilionekana kuwa mbaya kiasi ambacho akatolewa chumbani akiwa juu ya machela na kisha kuanza kupelekwa katika hospitali ya St’ Albert ambayo ilikuwa kubwa sana nchini Marekani. Hawakutaka kubaki mahali hapo, walichokifanya ni kuanza kuifuatilia machela ile huku Bi Lydia akilia kama mtoto.
Katika maisha yao walikuwa wamepitia katika hali ngumu sana lakini kwa wakati huo, hali hiyo ndio ilikuwa ikionekana kuwa ngumu zaidi katika maisha yao. Wayne akapakizwa ndani ya helkopta ya hospitali ile na kisha kuanza kupelekwa katika hospitali ya St’ Albert huku dripu zikining’inia.
Bwana Brown na mkewe, Bi Lydia wakaingia katika gari lao na kisha kuanza kuelekea katika hospitali hiyo iliyokuwa katika mji wa RockVile uliokuwa karibu na uwanja wa ndege wa Kimataifa wa John F Kennedy.
Ni ndani ya dakika mia moja wakawa wamekwishafika katika eneo la hospitali hiyo. Wakateremka na kuanza kuingia ndani ya jengo la hospital hiyo. Kama kulia walikuwa wamelia sana na kama macho yao kuvimba yalikuwa yamevimba sana.
Miili yao ilikuwa ikitetemeka kupita kawaida, tayari hali ya wasiwasi ilikuwa imewashika, walikuwa wakiogopa kupita kawaida, waliona kwamba muda wowote ule wangeweza kumpoteza mtoto wao ambaye walikuwa wakimpenda sana hata zaidi ya walivyokuwa wakimpenda mtoto wao mwingine, Esther.
Mara baada ya oparesheni ya kuwekewa ngozi nyingine kufanyika ndani ya chumba maalumu na ndipo wakaruhusiwa kuingia ndani ya chumba kile. Hawakutakiwa kupiga kelele zozote zile kwa kuhofia kuleta matatizo mengine zaidi.
Wayne alikuwa kitandani kimya, dripu zilikuwa zikiendelea kuingiza maji mwilini mwake huku mashine ya hewa ya Oksijeni ikiwa imeziba mdomo na pua yake. Wote wakashindwa kuvumilia, hali ambayo ilionekana kwa mtoto wao ikaonekana kuwatisha, wakaanza kulia.
Hayo ndio yalikuwa maisha ya Wayne. Ajali ilionekana kubadili maisha yake kabisa. Ila kila siku wazazi wake walikuwa wakimshukuru Mungu kwa kumnusuru mtoto wao kutokana na Kristen kufariki pale pale. Wayne akaonekana kuwa na bahati katika maisha yake.
Miezi ilikatika lakini Wayne hakufumbua macho yake. Mwaka wa kwanza ukakatika, wa pili ukafuata. Mwaka wa tatu ukaingia, wa nne na hata wa tano ukaingia, bado alikuwa amefumba macho yake vile vile.
Mishipa yake ya fahamu ilikuwa imelegea sana kutokana na ajali ile kumletea matatizo na ilikuwa imechukua muda mrefu sana mpaka kukaa sawa. Waliamini kwamba ni lazima kuna siku Wayne angekuja kufumbua macho iwapo tu kama mishipa ile ya fahamu ingekaa sawa.
Kama kulia, wazazi wake walilia sana. Katika kipindi cha miaka mitano, kila siku walikuwa wakifika hospitali hapo huku wakiwa na mtoto wao, Esther ambaye alikuwa na majonzi zaidi ya wote. Maisha ya kitandani bado yalikuwa yakiendelea kwa Wayne.
Mwaka wa sita ukaingia na siku kumi na mbili, Wayne akayafumbua macho yake. Manesi hawakuamini kile ambacho walikuwa wamekiona, walichokifanya ni kwenda kumuita daktari ambaye alifika mahali hapo na kumwangalia Wayne.
“Glory to Almight God (Utukufu kwa Mungu Mkuu)” Dokta Carthebert alisema huku akiinyoosha mikono yake juu.
Walichokifanya ni kuwapigia simu wazazi wake ambao walifika mahali hapo huku wakiwa na furaha kupita kawaida. Kitendo cha mtoto wao kufumbua macho kilionekana kuwafurahisha kupita kawaida. Wakaanza kumshukuru Mungu kwa jambo kuu ambalo alikuwa amelifanya katika maisha ya mtoto wao, Wayne.
Japokuwa Wayne alikuwa amefumbua macho lakini hakuweza kuongea kitu chochote kile kitandani pale. Kumbukumbu zake zikaanza kurudi upya, akaanza kukumbuka kila kitu ambacho kilikuwa kimetokea siku ile alipopata ajali.
Alitamani kuongea kitu lakini hakuweza kuufumbua mdomo wake kabisa. Miezi sita ikakatika na ndipo Wayne alipoanza kufumbua mdomo wake na kuanza kuongea. Madaktari wakaonekana kuwa na furaha, walichokifanya ni kuwapigia simu wazazi wake na kuwapa taarifa.
Bwana Brown na Bi Lydia wakafika hospitalini hapo huku wakionekana kuwa na furaha kupita kawaida. Taarifa walizoambiwa kwamba Wayne alikuwa amefumbua mdomo wake na kuongea zilikuwa zimewapa faraja.
Wakaingia ndani ya chumba kile na macho yao kutua kwa mtoto wao, Wayne. Wote wakajikuta wakitoa tabasamu pana. Wayne alikuwa akiongea vitu fulani kwa sauti ya chini kabisa hali iliyomfanya Bwana Brown kumsogelea na kulipeleka sikio lake karibu na mdomo wa Wayne.
“Say something my son (Ongea kitu chochote kijana wangu)” Bwana Brown alisema huku akitabasamu.
“I want my kid....I want to see my kid (Ninamtaka mtoto wangu.... Ninataka kumuona mtoto wangu)” Wayne alisema maneno yaliyomfanya Bwana Brown kushangaa.


Je ni nini kitaendelea?
Je Wayne ataweza kumuona mtoto wake?
Je wazazi wataweza kufahamu Andy anamzungumzia mtoto yupi?
Itaendelea

No comments:

Post a Comment

Recent Posts