Thursday, November 22, 2012

SITAISAHAU facebook------- 8

MTUNZI: Emmy John P.

CONTACTS: 0654 960040


SEHEMU YA NANE


ILIPOISHIA


Akapoteza uelekeo kuniona naruka vile nikataka kukimbia nje.

Akanidaka kanga yangu. Kanga ikateleza ikauacha mwili.

Shanga nane za rangi tofauti zilizokishika vyema kiuno changu ndio pekee zilizosalia katika mwili wangu. Sasa John alikuwa amebaki na kanga mkononi mimi nikiwa nina shanga kiunoni. Nusu nilikuwa nje na nusu nilikuwa ndani.

Swali likavamia kichwa changu.

Nikimbie na shanga kiunoni kwenda nje ama nirudi chumbani kwa John huyu wa maajabu!!! John niliyemuhisi kuwa sasa ni ………….

Nikabaki katika kizungumkuti.


JE ISABELA ATAKIMBIA NA SHANGA KWENDA NJE AMA ATARUDI KWA JOHN???

NINI KINATOKEA HAPA!!!!!!!


ENDELEA

Nikiwa katika kujiuliza iwapo nirejee ndani ama nikimbie hivyo hivyo uchi na shanga kiunoni, mara John akaanza kunisogelea huku akiniomba mkono wangu.
Anauita akuue!!! Sauti iliniambia.
Hapohapo nikaamua kutimua mbio uchi. Ilikuwa ni kama bahati kwenye kamba ya kuanikia nguo nikakutana na kanga nikaikwapua nikawa nakimbia huku naifunga.
Ikawa kama ni muendelezo wa igizo. Wakati nadhani nipo peke yangu katika kukimbia mara nikashangaa tukiwa watatu. Wote wasichana. Mimi nilikuwa kimya. Wenzangu walikuwa wakipiga kelele za kuomba msaada. Msaada wa nini? Nilijiuliza.
John anatafuna watu!! Niliwaza. Nikaongeza mwendo zaidi. Sikuwa tayari kutafunwa. Mawazo yangu yote yalikuwa kwa mwalimu Nchimbi. Anavyonitegemea!!! Atabaki na nani? Nikazidi kukaza mwendo. Kanga ikiwa imenikaa vizuri katika staili ya kupitia shingoni.
Mara mmoja akaanguka huku akipiga kelele. Ni hapo ndipo niligeuka, kutazama kulikoni. Niliamini kabisa kuwa ni John anatafuna mtu pale lakini ghafla nikashuhudia mbwa mkubwa akimgalagaza msichana mwingine. Nikatoa ukelele wa hofu kuu.
He!! John kageuka mbwa!!! Nimekwisha mimi. Ewe mwenyezi Mungu nisaidie. Sasa nilikumbuka kusali. Dalili za kupoteza matumaini.
Msikimbie nyie!!! Sauti kutoka nyuma ilitukanya. Haikuwa sauti ya John lakini ilikuwa sauti ya kiume.
“Spider acha!! Spider shenzi acha!!! Acha!!!.” Sauti ile ilikuwa inakanya kwa ghadhabu. Waliposimama na mimi nikasimama. Lakini nikiwa nimejiweka tayari tayari kukimbia iwapo itabidi.
Yule mbwa aliheshimu amri ile akaacha kumshambulia yule binti pale chini. Akaondoka kuifuata sauti ilipotokea. Baada ya yule mbwa kuondoka alitokeza yule kijana aliyekuwa anaamrisha. Alitutaka radhi wote kwa pamoja.
Mh!! Mimi sihusiki na hili lakini!! Nilijikanya.
Kumbe huyu mbwa sio John!!!
Au au au!! Ile ndoto imeniathiri akili!!!
Nilitaka kurudi chumbani ili niweze kuzungumza na John lakini wasiwasi ukanitawala zaidi.
Sikurudi, siku hiyo nililala kwa rafiki yangu.
Mbwa!! Hiyo ndio ikawa pointi ya kujitetea, hakuna aliyejua ni kipi kimenikimbiza kiasi kile.
Nikaoga, kisha nikalala na kuamka salama.

“HOFU YATAWALA CHUONI SAUT” Alizungumza kwa sauti kuu mtangazaji. Akaanza kuielezea habari hiyo. Mimi nilikuwa nimelala bado. Lakini sikio lilikuwa wazi.
“Kijana mwingine amekutwa amekufa kwa kugeuzwa shingo yake, amekutwa na kisu kikiwa na damu lakini hakuwa na kovu lolote mwilini mwake. Huenda alikuwa katika kupambana na muuaji kabla ya mauti kumkuta.”
Sijui hata ni muda gani niligeuka, na kukaa kitako. Habari ilikuwa imenishtua. Nilidhani kuwa ni ndoto tena imejirudia lakini haikuwa ndoto hii ilikuwa ni habari inaendelea.
Salma alikuwa ameshika tama akisikitika, hakupata nafasi ya kuniona jinsi nilivyokuwa katika mshtuko mkuu. Nilijilazimisha kulala tena lakini haikusaidia, taarifa hiyo ikanirudisha katika kumfikiria John.
Hapana John hawezi kuwa muuaji!!! Nilipingana na maono yangu ya usiku. Nikapuuzia.

*****

Jina langu lilikuwa limeanza kukua pale chuoni kutokana na elimu ya mahusiano niliyokuwa naitoa. Mwanzoni watu hawakujua ninamaanisha nini lakini mwishowe wakaanza kunielewa. Wasichana waliotendwa katika mapenzi walikuwa wanakuja kupata ushauri kwangu. Waliokuwa wakigombana na wapenzi wao nilihusika katika kusuluhisha. Isabela nikawa Isabela kweli.
Nilianzisha vikundi kadhaa vya kupinga unyanyasaji wa wanawake hasahasa katika suala la mapenzi. Kwa kuwa mapenzi yalikuwa yameteka asilimia kubwa ya mawazo ya watu basi nilieleweka kirahisi. Nikawapata wafuasi wa kutosha. Nikaipenda kazi yangu!!
Kwa kutumia pesa alizokuwa akituma Davis na kampuni yake niliweza kuandaa semina kadhaa huku nikialika wataalamu wa saikolojia. Masomo waliyotoa yaliwagusa wengi.
Sasa kila mtu aliweza kunifahamu walau kwa jina kama hajapata nafasi ya kujua sura yangu.
Kampuni iliyoniajiri ya SAVE THEM ilipotuma wajumbe wake kutoka marekani kufika chuoni kwetu kwa ajili ya tamasha kubwa kabisa lililohusisha mambo kadha wa kadha huku nikipandishwa cheo na kuwa muwakilishi wao katika vyuo vikuu vyote nchini ni hapo ndipo jina langu lilikuwa zaidi.
Vile vifo vya wanafunzi sita katika siku sita mfululizo vilikumbukwa kwa kusimama kimya dakika moja kabla ya ufunguzi wa tamasha lile.
Vifo vikasahaulika na mambo mengine yakaendelea.
Ile ndoto niliyoota kisha nikamfuma John na damu mgongoni niliamini kuwa yalikuwa ni mauzauza tu haukuwepo ukweli wowote.
John alikuwa amerejea kuwa mpenzi wangu rasmi na penzi lilikuwa moto sana. Jesca akasahaulika!!!
Isabella mimi sikushangaa sana sasa nilipoteuliwa katika baraza la mawaziri wa serikali ya wanafunzi. Nilikuwa naheshimika.
Malipo makubwa niliyokuwa napata yalibadilisha maisha ya nyumbani. Yote haya yalikuwa ndani ya miezi miwili.
Kila mara nilikuwa nikifikiria kuhusu hapa nilipo naishukuru facebook, kwani ni hii ilinikutanisha na dokta Davis na sasa nilikuwa mtu kati ya watu.

******

MAUZAUZA MENGINE UPYA

Ilikuwa siku ya sita ya juma yaani kuanzia jumatatu sasa ilikuwa jumamosi. Siku hii kimvua cha rasharash kilinikumbusha kulitafuta sweta langu ambalo lilikuwa chini kabisa ya kabati langu la nguo.
Licha ya kuwa na nguo nyingi nilikuwa na sweta moja. Mafua yalikuwa kidogo yananisumbua, uchovu wa siku iliyopita pia ulikuwa unanisumbua. Siku iliyopita ilikuwa siku ndefu sana, ilikuwa ijumaa ya kukumbukwa, kampuni ninayofanyia kazi ilikuwa imenihamishia katika nyumba kubwa kabisa ya vyumba vinne, sebule na mahala pa kulia chakula. Ilikuwa na geti na ua kubwa tu. Baada ya kujaza vitu ndani, nilialika watu kwa ajili ya uzinduzi rasmi. Nilialika marafiki wapatao sitini, akiwemo raisi wa chuo, watangazaji wa redio SAUT, marafiki wenye hadhi ya kuwa marafiki zangu, waalimu wenye heshima zao pale chuoni akiwemo ‘Dean of students’ aliyeitwa Mama Nasania, John naye alialika marafiki zake. Hapakuwa na michango wala kadi za michango. Na katika shrehe hiyo hapakuwa na kipengele cha kutoa zawadi.
Ndio hakikuwepo hicho kipengele. Sasa zawadi gani ya wewe kumpatia Isabella akaifurahia. Nilikuwa na kila kitu.
Kwa kuwa sikuwa na ratiba yoyote zaidi ya kupumzika niliamua kumeza dawa aina ya pilton. Ili mafua yaweze kupungua kiasi kabla sijaamua kwenda hospitali kumwona daktari.
Sijui nilikuwa nawaza nini hadi nikabwia tembe mbili za Pilton.
Leo nitasinzia aisee!! Nilijisemea, huku nikiendelea na shughuli za hapa na pale ndani kwangu. Nilikiweka chumba katika hali ya usafi sana kwani siku hiyo John alikuwa na ratiba ya kulala nyumbani kwangu. Kwa mara ya kwanza!!!
Nilikuwa katika hali ya ufahari sana. Wadogo zangu waliopoteza heshima kwangu sasa wakawa wananiita dada kwa herufi kubwa.
Hatimaye ule wakati ukafika. Madawa yakanitwaa nikaanza kurembua macho. Sikuwa na ujanja wowote nilikiendea kitanda nikakiangukia usingizi ukanitwaa.
Giza nene likatawala hadi pale ulipokuja mwanga tena nikiwa natazama filamu katika kioo kikubwa.
Filamu hii ya sasa ilikuwa inachekesha na ilinisahaulisha kabisa uchovu niliokuwanao. Vijana mchanganyiko wa kike na wa kiume walikuwa wapo katika fukwe ambazo sijawahi kuziona kabla, mara wakimbizane mara warushiane maji. Wengine waoga wa kuogelea kama mimi. Wengine wamevaa nguo za kuogelea huku wale walionichekesha wakiwa wamevaa suti ufukweni.
Sikuanza tu kucheka kwa sababu wamevaa suti. Ila nilikuwa nacheka zaidi maana hata John na yeye alikuwa amevaa suti. Tena kibaya zaidi alikuwa amevaa suti na moka. Kama anaenda kanisani jamani!!!!
John hakujali lolote. Aliendelea kupunga upepo.
Kipengele cha kuchekesha mara kikaisha ghafla likatokea giza, nikakereka, ile giza ni kama iligundua kuwa nimekereka. Ikatoweka, mwanga ukarejea tena.
John hakuonekana. Nilipoangaza kidogo nikamuona John akiwa anaogelea na suti yake.
Wenzake wakiwa wameacha vichwa juu, yeye alikuwa amezamisha mwili mzima baharini.
He!! Nikashtuka nikataka kufumbua macho ila macho yakawa mazito!!! John anaogelea na suti na moka?
John ana mkia!!!! Mkia wa samaki!!!
Nikatapatapa nipige kelele lakini bado sikuweza nilijihisi nimewekewa kitu kizito kifuani. Na mdomo ulikuwa kama umewekewa zipu ya kuuzuia usiamke.
Ule mkia wenye kiwiliwili cha John ukaanza kuyakata maji katika hali ya kushangaza.
Mara!!! Meno, meno ya John yalikuwa mengi, huenda ni zaidi ya thelathini na mbili. Halafu yalikuwa makali.
Au ni ya bandia? Nilijiuliza.
Meno yale hayakuwa ya urembo kama nilivyodhani. Jibu likaanzia pale yaliporarua mikono ya mwanadada mmoja, mikono ikatoweka, wa pili akajaribu kukurupuka mguu mmoja akauacha baharini, wa tatu akasalia bila kichwa, mvulana wa nne aliyeshuhudia bahari ikiwa na rangi nyekundu alikuwa mtaalamu wa kuogelea alikata maji, John aliye katika mfumo wa samaki naye akamfuata kwa kasi. Yule bwana akafika ufukweni, John alipofika huko akashindwa kupiga mbizi. Alikuwa na mkia hakuwa na miguu!! Akawa kama anatukana kwa lugha anazojua mwenyewe. Yule aliyeokoka akawa anataka kukimbia lakini akaghairi akafanya kitendo ambacho kiliniharibia kabisa filamu yangu.
Akaokota mawe na kuanza kumrushia yule samaki mtu.
Mawe yakawa yanampata barabara. John samaki akawa anajaribu kukwepa. Yule mtu akajua anaishinda vita ile na kweli John alionekana kuzidiwa. Lakini pasipo kutegemea na katika hali ya kushtua sana. Nyuma ya yule mtu akatokea tena mtu aliyenishtua sana. Huyu sasa alikuwa ni John wangu huyuhuyu. Huyu alikuwa John kamili na hakuwa na mkia. Yule aliyekuwa anaponda alipogeuka kutafuta mawe akakutana na sura ya John, alikuwa kifua wazi.
Pasipokutegemea John alisukumwa chini, akapinduka, lakini yule bwana alijaribu kukimbia tayari mguu wake ulikuwa umekamatwa.
John alipogeuka ile alama ya kuchanwa na kisu ikaonekana. Nikabaki kama zoba siwezi kupiga kelele wala kutoa msaada wowote.
Huyu naye akageuzwa shingo, kisha ghafla pakawa giza sikuweza kuona mbele. Lakini nilihisi kama napoteza fahamu hivi.
Macho yalipopatra ujasiri na kufunguka nilikuwa nimezungukwa na watu wenye nguo nyeupe.
Kila jicho likinitazama mimi.
Hofu mpya ikaanza. Nguo hizi zilinikumbusha mahali. Inamaana…nipo wapi!!nilijiuliza. wenye nguo nyeupe walikuwa wamenuna!!!

***ISABELA katika mtihani mwingine!!!! nini kinamtokea????
na nini HATMA YAKE

No comments:

Post a Comment

Recent Posts