Thursday, November 22, 2012

HATIA--- 14

MTUNZI: George Iron.

CONT: 0655 727325


SEHEMU YA KUMI NA NNE

"Hapana sivyo!!! ila huyo John huyo John Mapulu namfahamu hana uwezo wa kuzaa iweje useme mkewe ana ujauzito?" aliuliza kwa sauti ya chini Rashid, macho yakamtoka Minja akabakia na pande la nyama mdomoni bila kutafuna, kauli ile ilikuwa imefungua akili yake kwa kiasi kikubwa.

Akatulia hivyo kwa sekunde kadhaa bila kusema lolote. Kisha akatikisa kichwa kumaanisha kuwa ametambua jambo. Akili yake ilifanya kazi harakaharaka tamaa ya pesa ya kichaga ikamwingia, ikamtuma kumchenga Rashid ili aweze kula peke yake.

"Ah!! wanawake wa mjini hao, hebu achana naye" alisema Minja. Rashid akaafiki, baada ya nusu saa wakaagana. Safari hii kila mmoja aliondoka kivyake.

ENDELEA>>>>>>



****

Matha baada ya kumhadaa Minja na kumsimamisha kazi aliamua kutokuwa mbinafsi na kumshirikisha suala hilo Michael ambaye mara nyingi alikuwa msikilizaji. Lakini katika maongezi ya siku hiyo hakuwa ameridhia maamuzi hayo yaliyotaka kufanywa na Matha, yaani kumtafutia kazi nyingine Minja ili kumuweka mbali na John.
"Na vipi siku akikutana na John, au akimpigia simu???" aliuliza Michael, Matha akakiri kuwa hali bado ni tete.
"Minja sio mropokaji ni muelewa sana" alijaribu kutetea Matha, Michael akakubali kwa shingo upande.
"Akithubutu kunichezea nitamuua!!!" alijisemea kwa sauti ya chini lakini Michael aliweza kumsikia.
"Kuliko kuua ni heri tutoroke Matha!!" alishauri Michael, Matha akamkazia macho, Michael akawahi kukwepesha macho yake. Matha akaaga na kuondoka, John na Bruno hawakuwa nyumbani.
Huo ni uoga wa kunguru!!! Akawaza Matha juu ya kauli ya Michael kuhusu kutoroka.

****

Ukaidi wa Minja mbele ya John ilikuwa dharau kubwa sana, John alijua lazima kuna kitu, hisia za kwamba Minja anaweza kuwa 'informer' na huenda ameishtukia dili yao ya kwenda kuiba Supermarket. John akawaeleza wasiwasi huo wenzake, hisia za John zikawashtua wenzake, mara moja msako Minja ukaanza. Sehemu ya kwanza kabisa ilikuwa kazini kwa Minja yaani sheli ambapo hakuwepo. Msako haukuishia hapo lilikuwa jeshi la watu wanne wenye mioyo ya kuua.
Minja alikuwa katika hatia asiyoitambua.
John alikuwa amekerwa sana na dharau aliyofanyiwa. Msako huu kwa upande wa John ulikuwa kwa faida ya Matha, alitaka kujua kuwa ni kwa jinsi gani Minja amemfahamu Matha tena kwa majina yote mawili kiufasaha.
"Au Matha ana uhusiano naye jamaa ananifanyia jeuri!!!" alihisi John, wivu ukachukua nafasi yake ukaanza kuikwaruza nafsi ya John, hasira ikajikaribisha katika kiti kilichokuwa wazi katika moyo wake.
"Nitamuua kwa mkono wangu!!!" aliapiza baada ya kumkosa pale sheli kwa mara ya tatu.
Wenzake na John walichukulia kuwa hizo ni hasira za kawaida ambazo John alikuwanazo lakini haikuwa hivyo ni wivu wa mapenzi ulikuwa unamshambulia tena shambulio la nguvu na la ghafla.
Msako ukatoka pale sheli na kuhamia nyumbani kwake, ramani ilikuwa tayari mkononi mwa kundi hili.
Wakashauriana waende usiku!!!!

*****

Kitanda kilikuwa hakilaliki, si kwa sababu ya godoro lililokuwa limechakaa sana bali kutokana na mgogoro wa nafsi, mke wa Rashid aliigundua hali hiyo kwa mumewe ambaye siku hiyo alipendezesha chumba kwa harufu ya bia tofauti na siku nyingine ambazo hunuka pombe za kienyeji.
"Baba Karim!!!....vipi mbona hulali"
"Sina tu usingizi mke wangu" alijibu kwa sauti ya kukwaruza.
Rashid alikuwa katika dimbwi kubwa la mawazo baada ya kupata taarifa kutoka kwa Minja. Umasikini ulikuwa unamtia katika fedheha kubwa, alidharauliwa na wala hakupendwa na mtu yeyote maana hakuwa na msaada wowote kwao. Wazo la utajiri kupitia kuusema ukweli unaomuhusu mke wa John lilimwingia lakini kisu kilikuwa kimeshikiliwa na Minja. Tamaa ikamwingia Rashid akatamani akishike yeye kisu hicho.
"Nitamweleza Minja na kama akikataa je?" alijiuliza.
"Akikataa nitaenda mwenyewe kwa John Mapulu" alijipatia jibu.
Mgogoro mkubwa wa nafsi ukautwaa usingizi wake, maumivu ya kichwa yakayeyusha usingizi wake. Rashid akaamua kuamka na kukaa kitandani, wakati huo mke wake alikuwa amelala tayari.
Nimeuchoka umasikini!!! alisema kwa nguvu kisha akajaribu tena kuutafuta usingizi.
Safari hii usingizi ulimchukua.
Siku iliyofuata akaamua iwe siku ya vitendo hakutaka kuchelewa zaidi. Kwa kuwa alipajua nyumbani kwa Minja aliamua kwenda usiku baada ya kuwa ametoka lindoni majira ya saa kumi na mbili jioni.
Siku nzima lindoni Rashid alikuwa anatazama vitu vya thamani huku akiamini kuwa iwapo Minja atakubaliana naye basi baada ya muda mfupi atakuwa na uwezo wa kuvinunua.
Ujio wa Minja nyumbani kwake siku moja iliyopita ulimzidishia tamaa zaidi ya kuipata pesa, miaka yake 40 aliyokuwanayo bado ilimruhusu kuwa na tamaa za kimwili, Rashid aliwatamani wanawake waliokuwa wakipishana katika maduka mbalimbali kununua vitu vya gharama.
"Nikizipata hawa watakuwa wananiheshimu na pia watakuwa wakinisalimia, hebu tazama wanavyonipita kama hawanioni vile!!!" Aliwaza Rashid, donge la hasira likamkaa kooni akajilazimisha kumeza mate lakini hayakupita. Akasonya!!
Alitamani jioni iweze kufika aijaribu bahati yake ya kupata pesa.
Jioni ilifika akaaga na kurejea nyumbani, hapo pia hakukaa sana alimuaga mkewe kuwa anatoka kisha akatoweka!! Hakusema anakwenda wapi.



*****


Chumba cha Minja kilikuwa kimya sana wakati anaingia, alijaribu kuita lakini hakupewa jibu lolote, lile giza lilimlazimu kutumia simu yake ya tochi kuweza kuona vyema ndani.
Chumba kilikuwa na harufu nzuri za manukato jambo ambalo halikuwa kawaida hata kidogo.
Jeuri ya pesa!!! aliwaza Rashid huku akichukua nafasi na kukaa.
Baada ya dakika kadhaa pakiwa na giza hivyo hivyo alisikia vishindo vya watu vikiingia ndani. Miale mikali ya tochi ilitua katika macho yake, alitumia viganja vyake kujikinga.
Maumivu makali katika paji la uso wake aliyasikilizia huku mwili wake ukiwa ardhini.
"Kwa nini leo hujaingia kazini??, kwa nini umeacha kazi tangu tufike siku zile??" Alisikia maswali yakimuelekea.
"Ni juzi tu ndio sijaenda jamani!!! sijaacha kazi, hata leo mchana nilikuwepo" alijitetea.
John alipatwa na ghadhabu akiwa nje ya chumba kile akiangalia hali ya usalama.huku akipuliza sigara yake.
"Fala huyo anawadanganya!!!" alikoroma kwa sauti ya hasira tena yenye kisilani, wivu juu ya mpenzi wake ulimtwaa kwa kiasi kikubwa. Aliamini kuwa yule ndani ya chumba kile alikuwa ni Minja.
Waliokuwa wameingia ndani waliposikia kauli inayoitwa kudanganywa moja kwa moja wakajua kuwa aliyekuwa mbele yao ni adui.
Dakika tano pekee zilitosha kumbadilisha Rashid na kuwa tayari kwa kuhamia kaburini. Ilikuwa ni kabali baabkubwa iliyomzidi nguvu mlinzi huyu ambaye hata chakula cha usiku alikuwa hajapata.
Timu nzima ya John ikajua kuwa imemuangamiza Minja.
Tamaa zikawa zimemponza Rashid, utajiri alioutaka ukawa umeingia shubiri. Mchezo asioujua mwanzo wake ukawa umetwaa uhai wake.
Rashid akatokomea na tamaa yake!!

******


Minja akiwa na jeuri ya pesa ambayo sasa ilikuwa imebaki kama shilingi elfu sitini. Aliichukia sana hali ya chumba chake kutokuwa na umeme, siku hiyo hakutaka kuuvuta moshi mkali wa kibatari, giza lilivyoanza kuwa totoro akaamua kutoka, kwa kuwa hakuwa na chochote cha thamani kinachoweza kuwavutia wezi aliurudishia mlango wa chumba chake na kutoweka, alikuwa amevalia nguo mpya alizokuwa amenunua siku hiyo, aliamini kuwa alikuwa amependeza sana. Pesa zile kidogo zilikuwa zinamuwasha, taratibu huku akiepuka kuchafua kiatu chake kilichokuwa kimeng'arishwa haswa alizipiga hatua hadi akafika katika 'bar' maarufu pande za Mabatini iliyokwenda kwa jina la 'Corner bar', akachagua meza ambayo ilikuwa tupu ikiwa imepambwa na viti vinne visivyokuwa na watu.
"We mwanamke!!!" alikoroma Minja, muhudumu akajikimbiza mara moja akasimama mbele ya Minja.
"Kasto laga (Castle lagger)" alibwatuka.
Muhudumu akachukua pesa na kuondoka kisha akarejea na kinywaji, Minja alianza kunywa taratibu kama mwanaume asiyekuwa na hofu ya pesa kumuishia. Baada ya pombe kumkaa sawa kichwani alipata ujasiri wa kwenda kumhadaa muhudumu ambaye alikuwa anashangaa shangaa huku na kule kutazama kama kuna mteja atamuita kwa ajili ya kutoa huduma.
"Njoo saa nne!!" yule muhudumu alimpa ahadi hiyo Minja. Minja hakutaka kurejea katika kijumba chake alichokuwa anakichukia kwa siku hiyo kutokana na giza lililokuwepo. Alichofanya ni kuhamia 'bar' nyingine huku akienda sawa na muda.
Saa nne kamili alikuwa amerejea 'Corner bar', muhudumu alikuwa tayari amevua sare zake. Akatokomea na Minja kama mpenzi wake wa siku nyingi sana.
Safari yao ikaishia nyumba ya kulala wageni.
"Mi silali lakini mwisho saa saba"
"Usijali" alijibu Minja huku akizivua nguo zake haraka haraka.
"Kwanza nipe pesa yangu kabisa!!"
"Shilingi ngapi??"
"Elfu tano"
Minja akatoa elfu kumi akampatia.
"Sihitaji chenji baki nayo" alisema kwa ujivuni Minja baada ya yule binti kuulizia kama Minja anayo 5000 iliyoshikana.
Binti akatabasamu na yeye akaanza kuzipunguza nguo zake mwilini. Tayari kwa kutoa huduma.
Hakuna aliyekumbuka suala la kutumia kinga, na hakuna aliyejutia baada ya tendo.
Saa sita usiku Minja alikuwa anarejea nyumbani kwake, alijihisi mwepesi na aliyechangamka sana baada ya tendo hilo alilokuwa amelikosa kwa siku nyingi sana.

Alipokikaribia kibanda chake furaha yake ilianza kupungua kwa kasi, alilitambua joto lililokuwa linamnyanyasa katika kijumba chake ambacho hakikuwa na 'sealingboard'. Alitamani kurejea katika nyumba ya kulala wageni ila akakumbuka kuwa alilipia kwa masaa kadhaa tu na wala si kulala hadi asubuhi.
Akapiga kite cha hasira kisha akaingia katika kijumba chake cha kupanga kama amelazimishwa hivi. Giza lilimpokea, lakini kwa kutumia uzoefu wa eneo hilo alipapasa hadi akakifikia kitanda chake akajibwaga bila kushusha neti. Usingizi haukumpitia kwa wepesi alipanga mipango kabambe ya siku inayofuata.
"Hivi nianzie na John ama nile pesa za Matha!!!" Alijiuliza huku akijipiga bega lake kupambana na mbu waliokuwa wanamzengea. Minja alikuwa katika wakati mgumu wa kufanya maamuzi, kauli aliyokuwa amepewa na rafiki yake Rashid juu ya tatizo la John la kutozaa na kijitambulisho cha ujauzito wa Matha vitu hivi vilimtia kizunguzungu, akajiuliza ni nini cha kufanya. Hakika alikuwa masikini na hii kwake aliiona kama bahati ya walau kuukwaa huu ugonjwa unaotawala Tanzania, ugonjwa wa umasikini, ugonjwa uliokosa tiba ya kudumu.

Tamaa za kuwa na mahusiano na Matha zilimtawala, roho mpenda sifa alimkaa mwilini akashindwa kubanduka.
"Matha atake asitake atakuwa mpenzi wangu wa siri....na kama akikataa namueleza John ukweli" Alijisemea Minja huku akizikumbuka raha alizozipata na yule muhudumu wa 'bar' katika nyumba ya kulala wageni. Aliamini kuwa sasa atakuwa akizipata raha hizo bila kulipia bali kulipwa.
Hali ya hewa ilibadilika taratibu, ulianza kuvuma upepo ambao ulipunguza joto kidogo pale ndani, kisha ikafuata miungurumo. Bila shaka ilikuwa dalili ya mvua.
Minja alikereka kutokana na hali hiyo kwani dari la chumba chake lilikuwa linavuja. Kwa mara nyingine alipiga tena kite cha hasira.
Miale ya radi za hapa na pale ilileta mwanga pale ndani, Minja akaona kitu ambacho hakukitilia maanani sana kwani aliamini yalikuwa mawazo tu.
Alikuwa ameiona sura ya Rashid mbele yake.
Rashi cha ulevi!! Huyu jamaa anakunywa pombe huyu!! Alisema kwa sauti ya juu kidogo kisha akacheka.
Akapuuzia akiamini ni mawazo tu, akaendelea kuwaza na kuwazua, mwanga wa radi ulipopiga tena, Minja akaamini hapakuwa na mawazo ya namna hiyo, kulikuwa na kitu chini ya kimeza chake.
Mara moja akaiwasha simu yake akapapasa kidogo akapata kiberiti akakiwasha kimshumaa kilichokuwa kinakaribia kuisha. Kama vile amesukumwa kwa mitambo maalum alijikuta anajibamiza kitandani akasimama tuli akiwa ameyakodoa macho yake.
Alikuwa ni Rashid akiwa amekodoa macho na kutoa ulimi nje!!! Hakuwa Rashid tena alikuwa hayati Rashid.
Minja alitamani kumeza mate kulainisha koo ili aweze kupiga kelele lakini kinywa kilikuwa kimekauka sana ikashindikana. Upepo ukavuma tena. Mshumaa ukazimika!!! Hofu ikaongezeka, haikuwa ndoto tena Minja alikuwa chumba kimoja na maiti. Alitamani kukimbia lakini akajivika ujasiri alikuwa anatetemeka akapapasa tena akakipata kiberiti akawasha tena mshumaa, ukawaka. Akapiga hatua, akafika mahali ulipokuwa mwili wa Rashid.
"Minja! Minja! usimguse!!! utaacha ushahidi" Sauti ya ndani (Conciousness) ikamwambia Minja, akashtuka akasimama wima akaanza kurudi nyuma, joto katika suruali yake mpya lilitoa jawabu la mkojo uliopita bila idhini maalumu kutoka kwa muhusika.
Upepo ulivuma tena, mshumaa ukazima Minja hakuuwasha tena.
Wazo la kukimbia likavamia ubongo wake, wazo hilo likaambatana na milango ya jela. Minja akatetereka kidogo aanguke akahimili kuendelea kusimama. Harufu ya kwenda jela ikamtuma kukimbia, hakuna kitu alichokiogopa kama polisi bila kuchukua chochote zaidi ya pesa alizokuwa amezihifadhi chini ya godoro lake Minja alitoka usiku uleule bila kumwambia yeyote.

Hatia ya mauaji ikatembea naye kila hatua aliyokuwa akinyanyua. Ladha tamu ya pesa yake ikapotea, mawazo ya utajiri yakayeyuka.
Minja akawa mfuasi wa Hatia, kila mara Hatia ilivyochachamaa ndivyo ndugu yake aitwae hofu alikurupuka na kumtetemesha Minja. Jasho likawa linamvuja 'Singlend' yake ikazidiwa ikaruhusu na shati lake kuubeba mzigo wa jasho. Minja hakujua ni wapi anaelekea. Alichowaza wakati huo ni kutoroka!!! Hatia ikawa inampa suluba takatifu!!

*****

John Mapulu baada ya tukio hilo la mauaji alitaka kurejea nyumbani kwake lakini akakumbuka kuwa zilikuwa zimepita siku mbili hajaenda kumjulia hali Joyce Keto katika kasri lao jingine walilolipata kwa shughuli za kijambazi. Aliagana na wenzake akaelekea Nyasaka, jirani na shule ya mwanzo na upili ya Jerry's.
Ulikuwa ni usiku sana lakini John aliamua kuwa kwa usiku huo azungumze na Joyce kuhusu Michael Msombe. Hatia iliyokuwa inamkabili kuhusu ujauzito wa Joyce ilikuwa imemzidi uzito akaamua kuigawa kwa Joyce ili aone kama nafsi yake itakuwa huru, kwa kiasi kikubwa kifo cha Minja kilikuwa kimempa ahueni, aliamini kuwa mwanaume huyo kuna jambo la siri alikuwa anafanya na Matha, hivyo hata kabla hajalifahamu ni vyema alikuwa amemwondoa duniani.
John hakuwa tayari kumshuhudia Matha na mwanaume mwingine. Alikuwa anampenda sana, japo hakuwa na uwezo wa kumzalisha. Hiyo pia ilimsumbua kichwa kwani Matha hakuwa akijua lolote juu ya tatizo hilo..
Bahati nzuri Joyce alikuwa hajalala hadi muda huo kuna mfululizo wa sinema ya 'Nikita' alikuwa anaitazama. Ni yeye aliyekwenda kumfungulia John mlango.
Sura ya Joyce Keto ilimsababisha John kukosa ujasiri wa kuzungumza naye juu ya suala la Michael, ujasiri wote ukawa umeyeyuka!!!
"Mambo bro!!"
"Poa Joy, hulali wewe"
"Nimelala sana mchana, hata sina usingizi kwa sasa"
"Aaah!! ok!!" alijibu John huku akichukua nafasi katika moja ya sofa pale sebuleni.
John alikaa bila kusema lolote kwa dakika mbili, Joyce alikuwa bize anatazama mtiririko ule wa 'Nikita'.
"Rajab yupo!!" aliuliza.
"Yeah!! watakuwepo lakini walilala mapema"
"Basi utamwambia nilikuja" alisema John kisha akasimama na kuaga.
Ujasiri wa John ulikuwa umeyeyuka, alikuwa amepata wazo la kwenda kwa Matha aliamini huenda ndiye mtu sahihi wa kugawana naye ile hatia, japo Matha alikuwa hajui kama Michael alikuwa na uhusiano na Joyce ama la. John alikanyaga mafuta ya gari kwa kujitawala hadi akafika Buzuluga. Akazima injini ya gari yake katika moja ya sehemu za kuhifadhi magari akatembea kwa mwendo wa miguu kuanza kuzipanda ngazi ambazo zingemfikisha katika chumba cha Matha ghorofani.
"Kesho saa kumi jioni nitakutafuta"
"Uwe na namba hiyo hiyo usiweke ile ya zamani"
"Usijali usijali"
"Hakitaharibika kitu!!"
Ilisikika sauti ya Matha ikijibishana katika simu na mtu ambaye sauti yake haikusikika bali ilikoroma kumaanisha kwamba alikuwa ni mwanaume, John alisikia kila neno alilosema Matha kwa sababu ilikuwa ni usiku sana na kila mtu alikuwa amelala.
Wivu ukamvamia!! ukampiga mtama akaanguka, akajikongoja akainuka. Wivu aliodhani ameuzika kwa kumuua Minja ulikuwa umefufuka tena. Hasira zilipanda zikapita kipimo, John akauma meno kupambana na ghadhabu yake. Kinyumenyume akarejea hatua kadhaa, akataka kuondoka mara anataka kuendelea agonge hodi akawa anaenda mbele na kurudi nyuma.
Akawa kama kichaa hivi!! hatimaye akaamua kuondoka. Alikuwa amechukia sana japo hakuwa na uhakika huyo mwanaume ni nani kwa Matha.
"Matha kwanini ananifanyia hivi??" alijiuliza John wakati anaitoa gari sehemu alipokuwa ameihifadhi.
"Unasemaje bosi!!" aliulizwa na aliyehusika na kuingia na kutoka kwa magari. Kumbe alivyoongea alisikika. John hakujibu kitu akaondoka zake. Akaamua kuelekea nyumbani, mawazo tele yakamtawala, alimfikiria mwanaume aliyetaka kuingia katika anga zake kwa kumchukua Matha wake.
Kesho nitamjua lazima, saa kumi jioni!!!! alifikiria John huku akizidi kuiendesha gari yake kwa umakini.

*****


Kelele za simu yake alizifananisha na ule mlio wa 'alarm' akajiuliza aliitegesha kwa sababu zipi za maana. Akabonyeza kitufe bila kufumbua macho ikaacha kutoa mlio, baada ya dakika moja mlio ukaanza tena akaamka akiwa ametaharuki, aliamini simu ile haikuwa ikimtendea haki, macho makubwa yaliyokuwa yamekodoa yalitua katika simu yake.
Haikuwa alarm kama alivyodhani, ilikuwa namba mpya inampigia. Kidogo Matha aipuuzie lakini pia aliamua apokee ili ampe vidonge vyake mpigaji ambaye hajui kuwa ule ni usiku.
Matha alipopokea alikutana na sauti ya kiume iliyokuwa katika uoga.
"Mi Minja..nahitaji sana kuonana nawe" Sauti hiyo ikampasua donge la usingizi likayeyuka, akakaa kitako, na hakujua kama amekaa uchi. Minja hakuielezea shida yake katika simu alihitaji kumuona Matha, ndipo Matha akampa ahadi wakutane siku inayofuata majira ya saa kumi jioni. Kumbe wakati wote wa mazungumzo sikio la John lilikuwa makini kunasa kila kitu.
Hofu kuu ilimtanda Matha hakujua ni nini kimeharibika ghafla kiasi hicho, alitaka kumpigia Michael lakini akasita alihofia huenda angeweza kuwa karibu na John.
Hatia kuu ikamkaba kooni, akainuka akachukua maji yasiyochemshwa katika moja ya ndoo zilizokuwa ndani akajaribu kunywa, yalikuwa ya moto tena yenye chumvi akajilazimisha kumeza funda moja.
Hakuongeza tena!!! akakaa kitandani, kichwa kikaanza kumuuma. Alijutia mengi sana lakini, kubwa lililomnyanyasa ni mimba aliyokuwa nayo.
Matha akatanabai kwamba yupo katika vita kubwa sana, halafu yeye hana silaha wala hajaamua kujihami.
Akaisogelea kabati yake akatoa bunduki yake akaitazama kwa jicho la upendo kisha akaibusu. Akachukua na kisu chake akakibusu pia.
Nitamuua Minja nipunguze mateso haya!!!! alijiapiza Matha kisha akazirudisha silaha zake pahala pake.
Baada ya hapo alirejea kitandani akafanya sala fupi kumuomba Mungu amuepushe na balaa lililopo mbele yake, sala ilikuwa katika mtindo wa kubahatisha kwani alikuwa na siku nyingi sana hajaenda kanisani. Aliulazimisha usingizi kwa kujigeuza hapa na pale hatimaye kifo hicho cha muda kikampitia.
Asubuhi na mapema tayari Matha alikuwa amedamka, alifanya usafi wa hapa na pale kisha akajitosa bafuni akapambana na maji ya baridi, tayari ilikuwa saa mbili asubuhi akajipamba kidogo, akavaa suruali yake na blauzi chini akaweka viatu vya wazi akaufunga mlango akaondoka na kuingia katika mizunguko isiyokuwa rasmi ilimradi tu muda usogee na kuifikia saa kumi.
Hapa na pale hatimaye ilitimu saa nane na nusu, funguo zilikuwa zinatekenya kitasa cha mlango wake, mlango ukafunguka akaingia ndani.
“Upo wapi muda huu??” aliuliza kwenye simu.
“Nipo huku Makoroboi”
“Tukutane hapo kwenye maduka ya nguo karibu na geti la kuingia chuoni” alitoa maelekezo Matha, Minja upande wa pili akawa ameelewa tayari, simu ikakatwa.
Matha akaingia kuoga tena kwa mara ya pili, akajipamba tena akatia kisu pamoja na bastola yake katika mkoba wake, akauweka kwapani akajiangalia kwenye kioo kisha akatoka.


*****

John alifika na kujitupia katika kitanda chake bila kuvua viatu, alikuwa anashambuliwa na wivu mkali, alikuwa na hasira kali juu ya mwizi wa mpenzi wake. John Mapulu alikuwa anajiuliza ni nani huyo alikuwa na ujasiri wa kumgusa sharubu, midomo ikawa inatetemeka usingizi ukakataa kukaribia pale alipokuwa. Akasimama akajongea hadi sebuleni akaliendea jokofu akafungua akakutana na chupa ya kilevi, akaitwaa akaimimina katika glasi akainywa kwa vurugu, akawasha luninga akakutana na mechi ya mpira wa miguu akazimisha. Akaendelea kuubugia kwa fujo. Katika mawazo ya hapa na pale akapitiwa na usingizi hadi saa moja asubuhi aliposhtuka.
Alikodoa macho hapa na pale hakuna aliyekuwa ameamka hapo ndani, akaitwaa ile chupa ya mvinyo akaiweka juu ya jokofu akarejea chumbani kwake.
Akili yake ilikuwa katika mvutano mkubwa sana, siku hiyo ilikuwa ndio siku ya tukio la kwenda kuiba Supermarket kwa kutumia silaha lakini siku hiyo pia lilikuwepo tukio kubwa sana la kwenda kumfumania Matha. John akachekecha mawazo hapa na pale akaamua kuchagua moja. Kwenda kufumania!!!
Akanyanyua simu yake akabonyeza namba za mkuu wa kitengo cha maandalizi ya tukio la wizi.
“Mambo vipi kaka” alisalimia John kwa unyonge.
“Shwari kaka, vipi kwema”
“Ebwana si shwari sana, nitachelewa kuja huko, kichwa kinanisumbua sana” alidanganya John. Upande wa pili haukupinga akakubaliwa. Akakata simu.
Usingizi ulimchukua tena hadi saa nane mchana alivyoamka, akafanya maandalizi yake bila kumshirikisha mtu yeyote.
Saa tisa kasorobo tayari alikuwa maeneo yaliyomruhusu kuitazama vyema nyumba aliyokuwa akiishi Matha, ilimchukua dakika arobaini kumshuhudia Matha akitoka katika chumba chake. Laiti kama asingekuwa amelikariri umbo la Matha asingeweza kumtambua na angesubiri kwa muda mrefu bila kumuona. Matha alikuwa amevalia baibui la staili ya kininja alikuwa anaonekana macho peke yake. Hali hiyo ilimtikisa John, akazidi kuamini kuwa Matha alikuwa anaenda kufanya jambo baya.
Matha bila kujua kuwa anafatiliwa alielekea barabarani akaangaza hapa na pale akanyanyua mkono wake wa kuume akaita taksi, haraka haraka dereva aliyekuwa amemuona Matha aliifikisha gari yake Matha akaingia ndani.
John akasubiri ile teksi ilivyoanza kuondoka naye akaingia katika teksi aliyokuwa amekodi.
“Fuata gari hiyo!!” alitoa maelekezo hayo John, dereva akafuata maelekezo. Gari mbili zikawa zinafuatana bila gari ya mbele kuwa na habari juu ya hilo, John alikuwa amevaa miwani nyekundu kuziba macho yake yaliyokuwa mekundu sana, hakutaka kumtisha dereva.

*****


***WIVU umempelekea JOHN kuamua kumuua MINJA lakini bahati mbaya inamuangukia RASHID nakufa na umasikini wake.
***MINJA anajikuta katika HATIA ya mauaji...harufu ya jela inampa wazo kuu la kukimbia.......
***MATHA anapigiwa simu na mwanaume usiku...JOHN anasikia mazungumzo haya...WIVU unamkumba tena anaamua kufuatilia ni nani mwizi wake.
***MATHA ametembea na kisu na bastola...je? anaenda kuua ama???

HATIA INASUMBUA WAHUSIKA WOTE WA RIWAYA HII.

NAWE MSOMAJI UNA HATIA YAKO.

No comments:

Post a Comment

Recent Posts