Monday, April 8, 2013

RIWAYA: WASALIMIE KUZIMU---------------- 5


MTUNZI: Hussein Wamaywa

SIMU: 0755 697335


SEHEMU YA TANO

Kwa yakini hakuna, hakuna kwa maana ya watu wanaojua kupenda, natumai ushujua naongelea nini!” Akahitimisha. Nasra akatikisa kichwa kukubaliana nae. Akasema.
“Ni kweli uyasemayo baba. Saadan ana moyo wa peke yake! Lakini mimi…..” Akasita na kumtupia jicho baba yake. Alitaka kusema ‘simpendi kabisa!’ macho ya Alwatan Dafu ndiyo yaliyombadilihia uelekeo wa maongezi.
“Lakini mimi simjui fika! Nahitaji kumjua kwanza baba pengine inawezekana yeye akawa mbaya zaidi kuliko wote uliowataja. Inawezekana anajifanya Simba mwenda pole ili ale nyama! Huwezi kujua baba!”
“Inawezekana wala sio uongo, wala sikatai utabiri wako. Lakini pamoja na yote bado sijaelewa unataka kuniambia nini? Ujue sitaki kabisa kuusikia upuuzi wa Halfan!”
“Swali zuri Daddy! Nataka kwenda Oman kwa Saadan. Nikakae walau mwezi mmoja, miwili au miattu! Nione hali halisi ya maisha ya kule, nimjue vilivyo, naamini nikirudi hapa nitakuwa nimerejea na tarehe ya harusi!”
“Good Nasra. Ndio sababu nakupenda Nasra. Wewe ni msichana wa ajabu. Ninajivunia hilo, I love you Nasra!” Baba Nasra akishangilia kwa vigelegele “Sasa umeamua jambo la busara kuliko yote uliyowahi kuamua katika maisha yako!” Akainuka na kuingia ndani, akarudi na vitabu vitatu vyenye majalada ya plastiki.
“Hizi ni Passport zenu aliniachia Saadan siku chache kabla ya kuondoka. Ni wewe tu kuamua uondoke lini! Sawa mwanangu? Juu ya nauli usiofu aliacha fedha za kutosha tu.
“Sawa baba, lakini naomba kitu kimoja tu ukifanya hicho utanihakikishia ni kiasi gani unanipenda na kunithamini.
“Kuwa huru na usema unachotaka.”
“Ni juu ya Halfan!” Alwatan akakunja uso.
“Najua ni kiasi gani ninakukera na kukuudhi kila ninapotaja jina hili. Lakini baba wewe ni mtu mzima sasa. Na ugomvi wako na yeye ulishamiri wakati ule nilipomkataa Saadan, lakini sasa nimeshamkubali! Sioni kama kuna haja ya ugomvi tena. Halafu ujue hata kama mimba ile iliingia kwa bahati mbaya, lakini ndo tayari watoto wameshazaliwa na hatuwezi kuwaangamiza au kumsusIa!
Hivyo tutake tusitake tumeshaunga undugu na Halfan, ingawa ninaolewa kwingine! Ingawa nitakuwa nimeolewa tayari; Halfan kama Halfan ataendelea kuwa mzazi mwenzangu forever! Na wewe lazima umuheshimu kama mkweo! Kama Saadan.
Naomba upunguze chuki dhidi yake na ikiwezekana muondoleane uhasama baina yenu. Please baba, temeni mate chini Shetani apite!
Alwatan Dafu akafikiria kwa muda na kushusha pumzi. “Nitafikiria ‘I mean’ nitajitahidi kufanya uliyoinambia. Hakuna haja ya uhasama, aghalabu maelewano huwa ni bora zaidi kuliko mifarakano. Nitajitahidi mwanangu!”
“Good baba! Very Good!” Ikawa zamu ya Nasra kufurahi.
“Sasa unaweza kwenda kazini baba, nakutakia kazi njema yenye afya, furaha na bashasha!” Nasra akahitimisha kwa kumkumbatia na kumbusu baba yake.
“Na wewe pia, nakutakia mapumziko mema hapa nyumabni unatarajia kuondoka lini?”
“Nafikiri wiki ijayo, lakini natarajia kushauriana na mama juu ya siku nzuri ya kuondoka!” Akajibu wakiachiana. Alwatan Dafu akienda kazini. Nasra akirudi chumbani kwake!”
Kwisha kazi yake! Kila mmoja kwa upande wake aliwaza hivyo. Walikuwa wamewezana! Hawakurofautiana sana na ile hadithi ya mjanja mjanjuzi.
Chumbani hakukukalika. Nasra akatoka mbio mpaka kwa mama yake, akafika anamkumbatia kwa nguvu huku machozi ya furaha yakimtoka “Thank you mama, Thank you. Nashukuru sana kwa ushauri wako mzuri”
“Enhe nipe habari mwanangu, mambo yamekwendaje?”
“Imekuwa rahisi nisivyotegemea, yaani kama kumsukuma Mlevi vile!” akamueleza mama yake kila kitu. Mama mtu akabaki mdomo wazi kwa ujasiri wa mwanae.
“Sasa …?” Alikuwa mama Nasra “Sasa unaweza kufanya mambo yako taratibu kabisa bila usumbufu wowote ule!” Baadae walipanga tarehe ya safari kuwa ingekuwa wiki mbili zijazo.
Jioni Dafu aliporudi akapewa habari hizo na kuzidi kufurahia. Siku zikasogea. Na kadiri muda ulivyozidi ndivyo hali ya Romota, mtoto mdogo wa Nasra ; pacha wa Promota ilivyozidi kuwa mbaya kiafya.
Walimpeleka hospitali hii na ile bila mafanikio. Siku ya safari ilipowadia bado hali ya Romota ilikuwa haijakaa sawa. Wakaiahirisha na kumpigia simu Saadan na kumueleza sababu za kuiahirisha safari ya Nasra.
Miezi michache baadae hali ya Romota ilizorota zaidi, ikawa mbaya kupindukia, hatimaye akafariki dunia. Nasra alilia mno kumlilia mwanae kiasi cha kupoteza fahamu mara kadhaa.
Habari za msiba wa mototo wa Nasra zilitambaa na kufika mbali zaidi. Siku mbili baadae watu walikuwa wamefurika nyumbani kwao. Saadan nae alikuwepo.
Wakazika na kumaliza matanga. Siku chache za kumfariji mfiwa zikakatika. Hatimaye Nasra akakubali kuwa kazi ya mungu haina makosa. Miezi michache baadae waliondoka na Saadan pamoja na Promota na kuelekea Omani!
Ilikuwa safari ndefu na ya ajabu kwa Nasra ambaye hakuwahi kupanda ndege kabla. Alijifunza mengi na vingi njiani. Mpaka wanafika Oman, tayari alishaelimika vya kutosha!


* * *
Husemwa na kuimbwa kwamba mtaka cha uvunguni sharti ainame, mwombaji sharti mikono iwe nyuma na pengine haraka haraka haina baraka.
Misemo nahau na methali zinazokwenda sambamba na ile ya subra yavuta kheri huleta kilicho mbali, ilitumika haswa kutekeleza matakwa ya Nasra Alwatan Dafu.
Badala ya mwezi mmoja au miwili aliyokuwa ameipangilia, aliishi miezi mingi zaidi. Na ili kuweka mazingira mazuri ya kuondoa mizengwe, kauzibe na ukuta katika mioyo ya ndugu wa Saadan, Nasra na Saadan walikubaliana kumfanya Promota kuwa mtoto wa Saadan.
Ingawa rangi na matendo ya Promota vilikuwa beni beni na hali ya Saadan, Nasra na Saadan walijitia hawalioni hilo. Ndugu nao hali kadhalika, wengine wakadai kitanda hakizai haramu!
Saadan aliyekuwa mcha-Mungu kupindukia, aliwasha ngaza daadhi ya ndugu zake pale alipokubali kuwa ‘alimuingilia’ Nasra bila kufunga ndoa. Na mara zote alipoulizwa ni kwa nini alifanya hivyo, jibu lake lilikuwa moja tu, “Ibilisi jamani!”
Wengi kama siyo wote walimpokea Nasra vizuri. Na baadhi walikuwa wacheshi kama yeye mwenyewe. Na vile lugha ya kiarabu Nasra aliifahamu vizuri, hakuwa na shida katika mawasiliano.
Ajabu ni kwamba kwa kipindi chote alichokuwa Oman, Nasra hakumruhusu Saadan kuukurubia katika mwili wake.
Lakini vitendo vidogo vidogo kama kuiruhusu miili yao ikaribiane, kukumbatiana na pia kubusiana; Nasra alishindwa kuvizuia na kumruhusu Saadan afanye hivyo mara nyingi tu katika mwili wake.
Noor, mtoto wa kiume anayemfuata Saadan ndiye kidogo aliyeonekana kutokubaliana na ulaghai kwamba Promota alikuwa mtoto wa kaka yake. Yeye alitamka wazi kuwa Saadan amepigwa bao la kisigino na wabongo!
Huyu alikuwa kero kwao lakini kwa kuwa familia nzima ilimuona kama ambaye hajatulia, hakuna aliyezitilia maanani kauli zake ambazo zilikuwa kama msumari wa moto katika donda bichi la moyo wa Saadan.
Hali hii na lile la kupigwa marufuku asiusogelee mkate wa siagi wa Nasra, vilimuathiri sana. Lakini kwa vile moyo wake ulishatua kwa Nasra, na wenyewe wanasema ‘muhitaji ni khanithi;’ Saadan aliyameza haya kwa machungu makali na maumivu yasiyo na mfano.
Hatimaye siku ilifika, siku ya kuondoka kwa Nasra. Ilikuwa siku ngumu kwa Saadan ambaye moyo wake ulikuwa ukipata faraja kumuona Nasra pembeni yake kila wakati.
Wakiwa Air port pamwe na ndugu zao, Saadan alishindwa kabisa kuyazuia machozi yaliyotiririka mashavuni baada ya kufanya vurugu za mwaka katika macho yake. Hili likamgusa Nasra.
Akamchukua Saadan na kusogea nae pembeni. Huku naye machozi ambayo nilishindwa kung’amua mara moja kuwa ni ya furaha au uchungu yakimtoka;
Akamkumbatia kwa nguvu na kwa mara ya kwanza akampiga busu la kinywa. “Saadan! Naamini unanipenda mimi kuliko kitu kingine chochote. Na ninataka kukuahidi kitu kimoja. Kwamba amini sasa Nasra bint Dafu ataolewa na Saadan peke yake!
Kujizuia na kuzizuia tamaa za mwili wako kwangu ingawa mara nyingi tumeondakea kupewa ‘one room’, juu ya kitanda kimoja tukiwa kama bibi na bwana harusi mtarajiwa, kumenifanya niamini kwamba upendo wako kwangu haumaananishi tamaa za kimwili tu;
Bali umekwenda mbali zaidi. Ndivyo mapenzi ya kweli yanavyotakiwa kuwa! Umenionyesha kwamba unanipenda kwa dhati. Sioni kwa nini nisikupe tumaini. Nakupenda Saadan!” Nasra alinong’ona taratibu akiwa juu ya kifua cha Saadan. Saadan akafarijika. Kwa kila hali ilikuwa habari njema kwake.
Akafaulu kufuta machozi na kubaki akimtazama Nasra kwa matamanio. “Sasa kama unalitambua hilo ni kwa nini basi unasita nisilete washenga kwenu waje kuulipa mahari uwe wangu wa milele, tutenganishwe na kifo?”
“Sisiti kwa nia mbaya dia, mambo mazuri hayataki haraka. Fanya taratibu, pole pole. Utaona matokeo yake na unaweza kuona mambo yanakuwa vipi!
Mara ya kwanza nilikwambia nitakuja Oman. Na tayari nimetiza ahadi! Hiyo pekee inatosha kukuonyesha kwamba Nasra sio mtu wa kupoteza miadi! Ni mtu ambaye akiahidi anatimiza.
Naelewa kwamba ahadi ni deni na shuruti uitimize. Amini ahadi niliyotoa kwako itatimia. Jambo la muhimu ni subira tu hata hivyo nataka unihakikishie kwamba mdogo wako Noor hatambughudhi mwanangu endapo tutafunga ndoa!”
“Nakuahidi hatombughuddhi! Tone moja la damu kamwe haliwezi kuchafua maji ya mto au bahari. Nitamdhibiti istoshe ndugu wote wanamjua kuwa hajatulia.”
“No! tena hao wasiotulia ndio wabaya kwa kuumbuana. Maana akishtukia ishu tu, hakai kimya. Bahati nzuri au mbaya watu hawa wasiotulia hufikia wakati wakatoa mawazo ambayo waliotulia hushindwa hata kuyafikilia wachilia mbali kuyatoa. Mfano kama hili sio siri kanifanya nionekane Malaya na tapeli!”
“Usifadhaike mpenzi! Nakuahidi tutaishi raha mustarehe!”
Wakaachana pale wasafiri waliposikia tangazo lililowahitaji kuingia ndani ya ndege upesi Nasra akawaaga ‘wifi’ zake, ‘shemeji zake’ ‘wakwe zake’ na hata marafiki zake.
Akawaacha na nyuso zilizojaa simanzi na huzuri, akavuta hatua kuijongelea ndege mwanae Promota akiwa kifuani mwake Naam! Dakika kumi baadae alikuwa hewani.

* * *
Watu waliojitokeza kumpokea nyumbani Tanzania walikuwa wachache sana. Baba yake, mama yake na wafanyakazi wao kadhaa wa ndani. Pengine waliokuwa wageni ni washiriki wenzake wa Miss Temeke Academia ambao walishika nafasi ya pili na ya tatu.
Labda kilichomfurahisha ni kile kitendo cha wazazi wake kuja kumpokea na gari yake ya ushindi Caddilac. Wakajipakia garini na msafara wa kuelekea nyumbani kwa Alwatan Dafu ikaanza.
Nyumbani kwao kulikuwa na sherehe kubwa ikimsubiri. Nusura Nasra aanguke kwa Mshutuko alioupata. Akajumuika na wenzake wakasherehekea kurudi kwake. Wakala kunywa na kucheza muziki.
Sherehe ilipokwisha washiriki wenzake wa urembo waliondoka na kumuacha jioni akiteta na wazazi wake, ambao walikuwa wanahitaji kusikia mengi kutoka kwake.
Kwanza aliwaoongopea mengi kuhusu Saadan na Oman na mipango yao ya ndoa ambayo ilipangwa kufanyika mwaka mmoja baadae. Halafu akahitimisha kwa kuwapa zawadi zao alizotoka nazo ukweni.
Alwatan Dafu alikaribia kupasua kwa furaha. “Kwa nini mipango yenu ya ndoa mmeiweka mbali hivyo?” Alwatan akashindwa kujizuia.
“Kusomana baba, unajua Kusomana tabia sio kazi ndogo. Ni kazi isiyohitaji papara ili maamuzi yatakayofikiwa yasijekuwa na majuto baadae. Ni vizuri kufikiri kabla ya kutenda.”
“Sasa mnasomanaje na hali mko beni beni kama mbingu na ardhi? Mmoja Afrika, mwingine Asia! Inawezekana kweli?!”
Kwa nini isiwezekane baba? Huu ni mwanzo tu kuna wakati yeye atakuja huku na tutaishi kwa kipindi furani. Na kuna wakati tunaweza kusafiri na kwenda kuishi nje. Tutafanya mambo kadiri tutavyoona. Subira tu ndiyo inayohitajika.
“Oke! Whatever you like, I’m ready to listen you! (vyovyote mpendavyo ninawasikiliza nyie!)
“Good Baba! Ninajivunia kuwa wewe ni baba yangu!” kauli hii ilimuacha Alwatan Dafu akitabasamu, kabla hajambusu mwanae na kumtakia usiku mwema. Kisha akaingia ndani kulala.
Akawaacha mtu na mama yake wakiteta kwa nafasi. Hapo ndipo Nasra alipomueleza mama yake ukweli halisi ulivyo, vile alivyohisi na mipango yake ya baadae ambayo ilikuwa tofauti na mbali kabisa na Saadan.
“Mh! Mtoto una hatari wewe! Haki ya Mungu sijaona!” Mama yake akasema kwa kicheko mwisho wa maelezo ya Nasra. “Nataka kumuonyesha baba kuwa yeye akiujua huu, wenzie tunaujua ule.
Naomba nikushukuru tu kwa vile wazo lako la kwenda Oman limeniweka huru. Na tena ninaamini kuwa sasa nitaweza kuitumia Caddilac yangu. Naomba unifanye mpango wa kuipata kadi yake! Akaomba.
“Nitakufanyia mwanangu! Iko katika droo ya baba yako. Kumbuka furaha yangu inakuja pale unapokuwa na furaha nitakupatia!“ Na kweli alimpatia siku mbili zilizofuata.
“Thanks mama! I won’t stop loving you!” Nasra akashukuru wakati akiipokea kadi hiyo. Akiwa na funguo na kadi ile tena sasa akiwa na uhuru wa kufanya atakalo na kwenda atakako tena katika wakati atakao (isipokuwa usiku) Nasra alijihisi kama aliyetua mzigo mzito baada ya kazi ngumu! Alifurahia kuona akimiliki gari yake mwenyewe.
Ni hapo alipoamua kumpeleka mwanae katika shule za awali. Na taratibu ubongo wa Promota, mwanae pekee aliyesalia, ukaanza kunolewa…


***NASRA anaendelea na mkakati wake babkubwa....kimya kimya bila mzee wake kujua...SAADAN amedanganyika anahisi anapendwa kweli....
nini kitafuata???

ITAENDELEA KESHO

No comments:

Post a Comment

Recent Posts