Tuesday, April 2, 2013

RIWAYA: MREMBO ALIYEPOTEA-------------------------2


MTUNZI: Andrew Carlos

MAWASILIANO: 0713133633

SEHEMU YA PILI

...
Ndani ya mwezi Maisha ya Alice yalikuwa yameanza kubadilika kwa kiasi kikubwa ikiwa ni pamoja nakupungua mwili. Kutokumuona mama yake takribani miezi tangu baba yake ampige na kuni na kisha kutoroka mara ya mwisho ni kati ya mawazo yaliokuwa yakimtawala sana Alice. Tayari ilikuwa kama tabia kwa baba Alice kufanya mapenzi na Alice. Baba alice akamchukulia Alice kama mke wake badala ya mtoto. Japokuwa wakati mwingine alikuwa akitumia nguvu mpaka kufanya mapenzi na Alice. Kadri siku zilivyokuwa zikienda na hali ya Alice ikaanza kubadilika na kudhohofika. Ule mtaji aliokuwa nao wa samaki ukapukutika wote kutokana na baba yake kuchukuwa zile pesa kinguvu. Kila baba Alice akiondoka asubuhi kurudi kwake ni usiku na lazima ahakikishe ametukana nyumba yote ndipo aingie ndani na hata akifika ndani asipokutana na chakula basi Alice atapigwa na vile vile kufanya naye mapenzi kinguvu. Akili ya Alice ikawa ni kutafuta ni jinsi gani ataweza kujinasua katika tatizo la njaa yeye na baba yake.
Kuna kipindi Alice alikuwa akikata tamaa kabisa kimaisha kwanza kutokana na elimu yake ndogo aliyoishia ya darasa la saba, ambayo aliona ni vigumu kwa yeye kupata kazi. Kuvaa kwake ilikuwa ni mabaki ya kanga ambayo mama yake alikuwa akiyatumia pindi alipokuwa akipika samaki. Moyo wa Alice ulikuwa tayari ni mkakamavu kwa mateso na manyanyaso ambayo alikuwa akikutana nayo kila kukicha kutoka kwa baba yake.
Maisha ya kiukatili yaliokuwa tayari yameukomaza ubongo wa Alice yalimuamuru moja kwa moja kuwa mtoto wa mtaani. Alice akawa ni mtu aliyedhamiria kuondoka pale tena kutoroka bila ya baba yake kujua wala majirani. Usiku ndio ulikuwa muda muafaka wa yeye kuondoka. Siku nzima Alice akaivumilia kushinda na njaa huku akitamani sana usiku ufike aweze kuondoka pale kwao nakutokomea kusikojulikana. Ndani ya saa mbili za usiku Alice akawa tayari kishaiacha nyumba yao aliokuwa akiishi yeye na baba yake na wapangaji. Hasira kali zilizochanganyika na mateso aliyokuwa akiyapata kutoka kwa baba yake yalimfanya hata kutokuandika ujumbe wowote juu ya kumjulisha baba yake kama ameondoka au la! Alice akaumia sana moyo kitendo cha kumuacha baba yake peke yake kwani alijua kuwa baba yake kamwe hawezi kuishi peke yake bila msaada wowote.
“Nani sasa atampikia?, nani atamfulia?”
Ni kati ya vitu alivyokuwa akijiuliza Alice mara mbilimbili kichwani mwake bila ya jibu lolote.
Alice hakupajua vizuri mjini zaidi ya kuishia feri tena alikuwa akija kununua samaki na dagaa kwa ajili ya kukaanga na kuuza. Alizurura mjini usiku kutwa huku akipishana na magari yaliokuwa yakimuwashia taa kali. Njaa kali ikawa imeanza kumzidia Alice. Hakujua ni wapi atapata chakula, mfukoni hakuwa na hata senti ya kununua chochote na hata kama angekuwa na hela kwa maeneo ya katikati ya mji aliokuwepo hakukuwa na duka hata moja lililokuwa wazi kwa muda ule. Tumbo lake likawa likikoroma na kumkumbusha kuwa toka asubuhi hajaingiza chochote. Alice akabaki kutoa machozi huku akiliangalia lile furushi la nguo alizobeba nakuona kama linazidi kumlete uzito hivyo kuamua kulitupa na kuendelea na safari yake kwa masikitiko makubwa. Akiwa njiani huku katika dimbwi la mawazo Alice akajikuta akipuliziwa moshi mzito wa sigara. Akahema juu juu kisha akatoa macho kuangaza huku na kule lakini bado hakuambulia kujua moshi huo unatokea upande gani. Ile hali ya usingizi na njaa ambayo tayari ilikuwa ikimnyemelewa ikaanza kuisha taratibu kutokana na woga ambayo tayari ulishatawala katika halmashauri ya kichwa chake. Akanyanyua mguu na kuanza kuondoka katika lile eneo.
“Unafanya nini hapo wewe?”
Kinadada takribani watatu waliovalia vinguo vifupi huku eneo lote la juu wakiachia nusu ya matiti yao wazi wakawa tayari wameshamzunguka Alice. Mapigo ya moyo ya Alice yakawa yamebadilisha uelekeo na kuanza kwenda kwa kasi huku akijihisi kuishiwa nguvu katika viungo vyake vya mwili. Mdomo wake ukabaki kumtetemeka huku akijihisi jasho kumtoka katika kila pembe za mwili wake.
“Nipo na.. na.. naa..”
Akiwa katika hali ya kujing’atang’ata ghafla akashangaa vicheko vikirindima kumzunguka kutoka katika lile eneo.
“Bwana tuondokeni katatupotezea muda hapa, embu tukachangamkie pesa sisi?”
Aliropoka mmoja wa wale madada hali iliyomfanya Alice asielewe wana maana gani waliposema wakatafute pesa.
“Inamaana pesa kumbe inatafutwa hadi usiku?”
Alice alijiuliza kimoyo moyo huku akitamani kuwauliza wale wadada lakini hali ya uwoga aliokuwa nao ikamfanya kukaa kimya huku akiendelea kuwatolea macho. Katika maisha yake yote Alice hakuwa anajua kuwa pesa inatafutwa hadi usiku tena na kina dada zaidi ya kuamini wanaotafuta pesa usiku ni walinzi peke yao. Mmoja kati ya wale wadada alionesha kumuonea sana huruma Alice. Kila wenzake wakitaka kuondoka yeye alionesha kuweka mgomo na kubaki na Alice katika lile eneo.
“Nyie nendeni nitawakuta, si mtakuwepo hapo mtaa wa ohio? tangulieni nakuja”
Alice alishangaa yule dada kuwaambia wenzake vile kisha wakaondoka na kuwaacha wawili tu usiku ule.
“Embu niambie binti unaitwa nani?”
“Mimi?”
Alice bado alikuwa muoga na mtu wa kutokujiamini. Woga uliokuwa umeendelea kumwandama ukamsababisha hata kupoteza ujasiri japokuwa walikuwa wamebaki wawili tu.
“Ndio naongea na wewe binti, kwani si tupo wawili tu jamani?”
“Anhaa, mimi naitwa Alice”
“Alice mbona usiku wote upo peke yako?, na kwa jinsi ulivyovaa unaonesha una matatizo kwani nyumbani wapi jamani?”
“Hapana dada wala sina hata tatizo”
Alice alimjibu yule dada huku akijiuma uma kwa kushika vidole vyake huku akivikunja kunja.

*****

Angel Mahipsi kama jina lilivyozoeleka kwa baadhi ya marafiki zake haswa anaofanya nao kazi. Weupe aliokuwanao na hata maumbile mazuri ya mwili wake ni kati ya vitu ambavyo vilikuwa kivutio kikubwa sana kwa wanaume haswa wale wenye tamaa za kimapenzi. Angel alijipenda sana na mara nyingi alipenda vitu vizuri, kuvaa vizuri, kula vizuri na hata kuishi maisha mazuri japokuwa alitoka kwao Kigoma na kuja Dar kutafuta maisha nakuwaacha wazazi wake huko Kigoma wakiwa katika hali mbaya ya kimaisha ya kutegemea milo miwili kwa siku. Tangu alipoingia Jiji la Dar akitokea kwao Kigoma Angel hakuwa na ndugu wakuweza kusaidiana naye katika maisha. Alipitia maisha ya mtaani mpaka alipokuja kufanikiwa kufanya kazi za ndani kwa mzee wa kitajiri Mzee Khalfani. Hata hivyo Angel hakudumu sana kufanya kazi kwa mzee Khalfani kutokana na kudharaulika na kufanyishwa kazi nyingi na familia ya Mzee Khalfani hivyo miezi mitatu ilimtosha kabisa kuingiza kipato alichokihitaji nakuamua kuachana na kazi za kufanya kazi za ndani kwa mzee Khalfani nakujitafutia maisha yake binafsi. Kwa mara ya kwanza Angel alifanikiwa kujinunulia godoro, kitanda na vyombo vya ndani viwili vitatu. Chumba alichokipata hakikuwa hata na umeme kutokana na hela aliyolipa haikukidhi kupatiwa chumba chenye umeme. Maisha yalikuwa yakibadilika kadri siku zilivyokuwa zinaenda. Kile kiasi cha hela ambacho alikivuna kwa mzee Khalfani alipokuwa akifanya kazi za ndani kilizidi kupungua mpaka nakubakiwa kiasi cha shilingi elfu thelathini tu. Wazo la kuanza kuuza matunda kwa kuweka kwenye beseni na kutembeza mtaani lilikuwa sahihi sana kwa Angel. Alihangaika kila kukicha kutanga na jua huku akitembeza matunda mbalimbali zikiwemo ndizi, machungwa, maembe, matango na mananasi maeneo ya katikati ya mjini. Kuna waliokuwa wakiidharau biashara yake kutokana na uzuri aliokuwa nao na biashara aliokuwa akiifanya. Wengi wa wateja wake walikuwa wakimshauri aachane nayo lakini ilikuwa ni kama kumtukana Angel tena matusi ya nguoni kwa kuwa siri kubwa aliijua moyoni mwake juu ya biashara hiyo iliokuwa ikimuingizia kipato kiduchu kwa siku. Kutoka kwake asubuhi na kurudi jioni huku akiwa amechoka kulimfanya ajikaze na kuamini ipo siku matatizo yake yataisha. Ndoto yake kubwa ilikuwa ni kuja kuwa Mwanamke mashuhuri Tanzania na Duniani kwa ujumla na mwenye kuwakomboa kina Mama wenye matatizo mbali mbali kwa kuwashauri na hata kuwawezesha kwa vipato. Lakini sasa ndoto hiyo ilikuwa nzito kwa angel kufikia malengo yake, iliyeyuka mithili ya barafu linapokutana na maji ya moto. Kadri siku zilivyokuwa zinakwenda ndipo na Angel alikuwa akikata tamaa kila kukicha nakuamua sasa kuachana rasmi na biashara ya kuuza matunda mtaani iliokuwa imeshamchosha haswa kwa kipato kidogo cha shilingi elfu tatu kwa siku alichokuwa akikiingiza na pia kusumbuana na mgambo kila kukicha na hata wakati mwingine kumwagia matunda yake chini.
Biashara ya kuuza mwili ndio ilikuwa jibu sahihi kwa Angel kubadilisha kutoka kuuza matunda. Hakujua kunywa pombe wala kuvuta sigara lakini sasa Angel akawa ni msichana mmoja wapo anayejua kupuliza sigara na hata kunywa bia zaidi ya sita na wala asilewe. Kulala na wanaume zaidi ya watano kwa siku kwake ilikuwa ni jambo la kawaida na wala halikumuumiza kutokana na mazoea ambayo tayari yalikuwa yamejijenga katika halmashauri ya kichwa chake. Angel hakuwa na mahusiano mazuri na majirani wake alipopangisha kwani hakutaka urafiki kabisa na majirani anaoishi nao na pia alikuwa msiri sana katika mambo yake haswa katika biashara hii ya kujiuza mwili ambayo hakukuwa na jirani yeyote aliokuwa akijua zaidi ya kila mmoja kumuhisi kwa kitendo cha yeye kutoka usiku na kurejea alfajiri. Mawindo yake yalikuwa ni Ohio, Kinondoni na Magomeni kwa Macheni japo hakupendelea sana kwenda kwenye makasino kwa sababu aliamini kuwa katika makasino wazungu wako wengi nayeye elimu yake ya darasa la saba ilimfanya asijue kabisa lugha ya kiingeeza ambayo huzungumzwa na wazungu wengi wa kwenye makasino. Marafiki aliokuwa akipenda kuongozana nao katika Biashara hiyo ya kujiuza mwili walikuwa ni wawili tu, Miriam na Josephina na sasa walimuacha Angel akiwa na Alice pale barabarani huku wao wakienda kujitafutia wanaume kwa upande mwingine.
“Sasa unawaona marafiki zangu wameniacha?, ila nipo pamoja na wewe mdogo wangu Alice”
“Sawa dada”
Angel aliongea na Alice kwa sauti ya chini chini huku akionesha dhahiri kutaka kumsaidia Alice kwa kumchukuwa na kuishi naye. Ile dhahama anayokutana nayo kila kukicha akirudi nyumbani akiwa amechoka na hata ile hali ya kujipikia nyumbani na kufua nguo ilikuwa imemchosha sana Angel. Akaona amepata mfumbuzi baada ya kukutana na Alice mjini. Hakuwa akimjua vizuri lakini tayari Angel alijiwekea moyoni kwamba Angel atakuwa msaidizi katika kumsaidia kazi ndogondogo za nyumbani kwake.
“Alice?”
“Abee!!”
“Kwani nyumbani kwenu wapi? na baba yako na mama wako wapi?”
Alice aliposikia anaulizwa tu wazazi wake alishindwa kujizuia nakuachia mchozi huku makamasi yakiwa karibu katika pua zake. Akakohoa. Mishipa ya pembeni taratibu ikaanza kujikusanya na kumvimba kwa haisra kali. Siri kubwa ikawa bado imebaki moyoni kwa Alice na alihaidi kutokumwambia mtu yeyote juu ya wazazi wake.
“Mhh!!, mama na baba wanaishi Bukoba”
“Kwani wewe ni Muhaya?”
“Ndio Dada!”
Alice alijitahidi kudangaya tena kwa kujiuma uma huku mkono wake mmoja akiutumia kufuta machozi ambayo tayari yalikuwa yameuzunguka uso wake na mengine yakilowesha kifua chake. Angel akaamua kughairi kufanya kazi yake ya kujiuza mwili kwa siku hiyo. Wateja watatu aliokuwa amewapata walimtosha kujipatia kiasi kidogo cha pesa kwa siku hiyo.
Akamchukuwa Alice kisha wakakodi bajaji iliowasaidia kuwapelekea mpaka nyumbani alipokuwa akiishi Angel. Ukarimu aliounesha Angel kwa Alice ilikuwa ni faraja kubwa nakuona sasa amepata mkombozi. Alice akajitahidi kulificha tabasamu lake ambalo lilizungukwa kwa machozi karibu uso mzima. Safari ya kutokea Ohio alipokuwa akijiuza Angel ikaanza na sasa alikuwa na Alice ambaye alidhamiria kumchukuwa kwa lengo la kumpekela mpaka kwake kisha kumsaidia kazi ndogo ndogo zinazokuwa zikimkabili. Ikawachukuwa mwendo wa nusu saa kwa kutumia bajaji mpaka kulifikia eneo la Tabata bima ambapo Angel alikuwa amepanga. Angel akamlipa dereva bajaji hela yake kisha akamshika mkono Alice nakuongozana naye mpaka ndani. Akaufungua mlango na kutafuta kiberiti ambapo aliwasha mshumaa na kuingia mpaka ndani.
“Jisikie uko nyumbani mdogo wangu Alice”
“Asante sana Dada”
“Hapa ndipo ninapoishi na tena naishi peke yangu mdogo wangu”
Alice alitoa macho karibu kila pande ya chumba. Mwanga wa mshumaa haukutosha kujua ukubwa wa chumba kile zaidi ya kushuhudia kitanda kikubwa cha tano kwa sita na kochi mbili za kawaida na beseni lililojaa vyombo vya kupikia.
“Kwakuwa ni usiku sana sasa hivi nakuomba asubuhi ikifika ndio ukaoge mdogo wangu ila tulale tu kwa sasa hivi”
“Sawa Dada nimekuelewa”
Kwa mara ya kwanza Alice akajihisi mtu tofauti kwa kulala katika makazi mengine. Pia ile hali ya kupigiwa makelele na baba yake na kisha kupigwa na hata kubakwa sasa ikawa ndio kikomo kwake. Akajihisi kama barafu ya baridi inapenya ndani ya kifua chake. Akaona ni kama bahati imetoka mbinguni ya yeye kukutanishwa na Angel. Akapeana ahadi na moyo wake kumthamini sana Angel na kufanya kazi kwa bidii kila atakavyohitaji. Akaingia hivyo hivyo na kanga zake kitandani zilizokuwa zinanuka moshi wa harufu ya samaki aliokuwa akiwakaanga kipindi cha nyuma. Mawazo mengi yakazunguka kichwani mwake na kumkosesha usingizi usiku kutwa, mipangilio ya maisha mapya ikamzidia kichwani mwake.
“Alice mdogo wangu?”
“Abee Dada?”
“Yaani bado huko macho mpaka sasa?, embu tulale nini unafikiria hivyo?”
Angel alimuuliza Alice kwa sauti ya chini chini na ya kumbembeleza baada ya kwenda kuuzima ule mshumaaa na kumshuhudia Alice akiwa katika hali ya mawazo.
“Nitalala tu dada wala usihofu!”
Alice alimjibu Angel na kisha akajigeuza upande wa pili na kufumba macho tayari kwa kulala.
Asubuhi na mapema Alice akawa mtu wa kwanza kuamka. Akabaki kitandani akimtolea macho Angel ambaye bado alikuwa katika usingizi mkali. Mkojo ulimbana sana Alice lakini alijikaza na kuubana huku akishindwa jinsi ya kumuamsha Angel amuelekeze uani japokuwa kulikuwa kumeshakucha. Muda wa dakika arobaini ukawa kama masaa matatu kwa Alice ambaye sasa mkojo alihisi unamvuja kupitia nguo yake ya ndani. Kule kujibana sasa kukawa kumemshinda. Akajikaza nakusogea mpaka kwenye kochi pembeni yake, akaketi.
“Dada? dada?”
Alice aliita kwa sauti ya uoga uoga huku akijuma uma kwa kutokujiamini bila majibu yeyote kwani ndio kwanza Angel alijigeuza na kuendelea kuuchapa usingizi. Uzalendo ukamshinda baada ya kuona Angel hashtuki wala kuamka. Alichokifanya akaufungua mlango taratibu huku akinyata nakutoka nje.
“Samahani, eti uani wapi?”

ITAENDELEA




No comments:

Post a Comment

Recent Posts