Wednesday, April 3, 2013

RIWAYA: MREMBO ALIYEPOTEA---------- 3

 

MTUNZI: Andrew Carlos

MAWASILIANO: 0713133633

SEHEMU YA TATU

...
Alice aliita kwa sauti ya uoga uoga huku akijiumauma kwa kutokujiamini bila majibu yeyote kwani ndio kwanza Angel alijigeuza na kuendelea kuuchapa usingizi. Uzalendo ukamshinda baada ya kuona Angel hashtuki wala kuamka. Alichokifanya akaufungua mlango taratibu huku akinyata nakutoka nje.
“Samahani, eti uani wapi?”
Sasa Alice akawa amekutana uso kwa uso na jirani mmojawapo. Yule jirani akamsikiliza na kumwangalia Alice kwa jicho la dharau kisha akamfyoza na kuendelea na shughuli zake bila kumjibu chochote. Alice akajiskia mwenye bahati mbaya na watu lakini akajikaza moyo na kuendelea kuangaza kila pande hadi alipofanikiwa kuuona mlango wa choo. Kitendo cha yeye kuongoza mpaka chooni na kisha kuvua nguo haraka haraka. Ule mkojo uliokuwa unamsumbua sasa ukawa haupo tena kwake kwani ulishaijaza nguo yake ya ndani, ikawa imelowa tepetepe. Alice akaogopa sana kutoka chooni akiwa amelowa katika nguo yake ya ndani, woga ukazidi kutanda na hakuwa na jinsi zaidi ya kuendelea kukaa chooni huku akitafakari ni jinsi gani ataweza kurudi chumbani akiwa amelowa nguo yake ya ndani tepe tepe.
“Alice?, Alice mdogo wangu upo chooni?”
Sauti ya Angel tayari ilikuwa nje ya choo ikimtafuta Alice na sasa alikuwa nje ya kile choo akigonga ili Alice atoke.
Woga ukawa bado umemtanda Alice. Mwili wote ukawa ukiendelea kumtetemeka, mapigo yake ya moyo yakaanza safari ya kwenda kasi mithili ya gari liliopo katika mteremko mkali. Akaiangalia ile nguo yake ya ndani kwa hasira huku akijuta kitendo cha yeye kuchelewa kuwahi chooni.
“Abee dada!! , nipo huku chooni!”
“Aanhaa!!, nilishtuka mdogo wangu nilidhani umeondoka”
“Hapana dada!”
“Haya endelea tu, mimi nipo chumbani nakusubiri”
“Sawa dada”
Alice aliitika kwa sauti ya chini na ya kunyenyekea. Akaendelea kuishikilia ile nguo yake ya ndani vyema na kuikamua kisha akahakikisha kojo lote limekauka vilivyo. Dakika tano zikamtosha kabisa Alice kuikausha kwa kuikamua ile nguo yake ya ndani na kisha kuivaa. Akaivaa hivyo hivyo japokuwa ilikuwa bado ina unyevu nyevu na kisha kurudi chumbani alipomuacha Angel.
“Dada nimeshamaliza!”
Alice alimwambia Angel kwa kuogopa ogopa kutokana na yeye kutokumfahamu vizuri. Akajitahidi kukaa katika kochi japokuwa bado alikuwa hajakakuka vizuri katika nguo yake ya ndani. Baada ya muda Alice akaelekea na Angel sokoni ambapo walinunua vitu vidogodogo vya kupika na vingine wakavihifadhi kama akiba ya baadaye. Alice akayafurahia maisha yale, ushamba bado ulikuwa umemtawala. Japokuwa alipewa nguo mbili tatu na Angel lakini yeye bado aling’ang’ana kuvaa kanga zake alizokuja nazo. Hali ya kutokwa damu ya hedhi hakuwa anajua zaidi ya kutetemeka nakuhofia huenda anafanyiwa vitendo vibaya usiku anapokuwa amelala. Akawa ananyemelea muda ambao Angel anaenda kwenye mawindo yake basi yeye akatumia muda huo huo kuvikata vipande vidogo vidogo vya kanga yake ili viwe vinamsaidia kukinga damu iliyokuwa ikimtoka kila kipindi cha hedhi kinapomfika. Takribani miezi miwili Alice hakuwa akijua kama kuna kitu kinaitwa pedi. Kutokana na biashara ya Angel ya kujiuza mwili kila siku hivyo Angel alikuwa akitumia vidonge vya uzazi na hata wakati mwingine alikuwa akichomwa sindano za kuzuia bleed. Maisha ya Angel na Alice yakawa ni mazuri sana na yakuvutia. Alice akahakikisha anafanya kazi vizuri ili kumfurahisha Angel. Kwa upande wa Angel Akajitahidi kumchukulia kama ndugu yake wa damu. Akamfanya Alice apendeze na akahakikisha anampa mahitaji karibu yote aliyokuwa akiyataka.
Weupe kidogo aliokuwa nao Alice akiongozana na Angel lazima utasema mdogo wake wa damu. Kama kawaida ya Angel kutokuwa karibu na majirani zake ndio tabia ikajijenga mpaka kwa alice. Alice alijifunza mengi kutoka kwa Angel. Hakutaka hata kuwa karibu na majirani zaidi ya kuwaangalia tu na kuwapita tena bila hata salamu. Biashara ya kujiuza mwili aliokuwa akiendelea nayo Angel sasa ikazidi kumtajirisha. Alipata pesa nyingi zaidi kupitia biashara hiyo. Kamwe aliapa kutokubali Alice ajihusishe na biashara hiyo hivyo alikuwa mkali sana na kumuonya mara kwa mara ajitahidi kuepukana na vijana walaghai pindi yeye anapotoka usiku na kwenda mawindoni.
Karibu kila mwisho wa wiki Angel alikuwa akiupumzisha mwili wake kuufanya kazi na wanaume hivyo alijijengea mazingira ya kutoka na Alice sehemu mbali mbali kama vile kwenye kumbi za starehe na hata maonesho makubwa makubwa ili mradi Alice ajisikie vizuri na ajione mtu tofauti kidogo. Lile eneo alikokuwa akiishi Angel na Alice ambalo hata halikuwa na umeme wakaamua kulihama na kutafuta nyumba kubwa yenye vyumba viwili na sebule. Alice akajitahidi sana kusahau maisha ya nyuma japokuwa picha ya mama yake lilikuwa ikimjia sana ndotoni na akiamka huwa anatoa sana machozi. Hasira iliyoambatana na dukuduku kubwa aliyokuwa ameiweka rohoni kwa muda mrefu juu ya baba yake bado ikawa ikimsumbua mara kwa mara pindi anapofikiria kitendo cha yeye kubakwa na baba yake mzazi. Bado ikawa ni siri kubwa moyoni mwake na hata Angel hakuwa akijua chochote zaidi ya kuamini kuwa baba na mama Alice wako hai na wanaishi Bukoba.

****

Mabadiliko yakaanza taratibu kwa Angel. Uchovu wa mara kwa mara ukawa umeanza kupenya katika mwili wake hali iliyomsababishia homa za hapa na pale. Alice ndiye alikuwa mtu wa karibu kwa Angel. Akahakikisha anamjali kwa kumhudumia kwa hali na mali. Kadri siku zilivyokuwa zikisonga na hali ya Angel nayo ikawa inabadilka kila kukicha na kuzorota. Mwili wake ukaanza kubabuka na vipele vyeusi vodogo vidogo vikaanza kuchukuwa nafasi yake. Wiki mbili zikampita hivi hivi Angel akiwa kitandani bila hata ya rafiki yake mmojawapo kati ya wanaofanya nao biashara ya kujiuza mwili kutokea.
Ni Alice peke yake aliokuwa akijua Angel anavyojisikia. Sasa ikafika kipindi Angel anachagua vyakula vya kula. Akipewa wali anatapika na kukohoa sana. Vyakula alivyohitaji ni wali ule wa kusaga kama uji uji na mtori.
“Dada Angel jitahidi basi hata umalizie hiki kijiko cha mwisho”
“Hapana mdogo wangu Alice inatosha.., peleka tu jikoni nitakula tena baadaye!!”
Alice alijitahidi sana kumbembeleaza Angel lakini haikuwezekana zaidi ya kutapikiwa kile chakula na hata kukimwaga. Mwezi mzima Angel alikuwa bado yupo hoi kitandani. Hakutaka kupelekwa hata hospitali japokuwa na miguu yake ilikuwa imemvimba sana na mwili kukosa nguvu. Ule weupe wake uliokuwa ukifananishwa na Alice pamoja na mahipsi ambayo yalikuwa yakigombaniwa sana na wanaume pindi anapokuwa mawindoni katika kujiuza mwili sasa ukawa umebadilika.
Hakuwa Angel mahipsi tena bali alikuwa ni Angel mchina kwa kuwa yale mahipsi aliokuwa nayo yote yalishuka mpaka magotini. Rangi ya ngozi ile nyeupe aliokuwa nayo sasa ikawa ni mchanganyiko wa nyeusi na kijani. Sura ya chanjo chanjo mithili ya wamakonde ndio ilikuwa imemvaa Angel. Mwili wote ukamwisha na ulikuwa huwezi kumwangalia mara mbili mbili kwa jisi mdomo ulivyokuwa ukimtoka maudenda tena yale mazito. Siri kubwa akawa nayo Angel juu ya ugonjwa aliokuwa nao na ndio maana hata hakutaka kupelekwa hospitali, sasa akawa ni mtu aliyekata tamaa ya kuishi. Siri kubwa aliyojijengea rohoni mpaka moyoni mwake sasa siri ikawa imedumu kwa wiki tatu tu baada ya kuona hali tete. Alice akawa ameshaambiwa kila kitu na kuujua ukweli.
“Kumbe ukimwi hatari hivi?”
Alice alijisemea kimoyo moyo huku akiendelea kumnywesha Angel uji. Alikuwa akishuhudia kwenye televisheni na magazeti juu ya waathirika wa ugonjwa wa ukimwi na sasa alishuhudia moja kwa moja. Mpaka miezi inafika mitatu bado Alice hakuweza kupata usingizi wenyewe zaidi ya kuwa karibu na Angel masaa yote na kama akipitiwa na usingizi basi ni nusu saa au lisaa tu anashtuka nakuendelea kumuuguza. Kuugua kwa Angel kwa muda mrefu kulichochea mawazo mengi sana kwa Alice nayeye kusababisha kupungua lakini kupungua huko kwa Alice kulitokana na kuwa na mawazo mengi sana juu ya Angel. Akaona sasa ndoto zake zinaenda kukatika kwa mara ya pili baada ya ile ya kwanza alipokuwa akiishi na baba yake na kisha akaambuliwa kubakwa. Dawa za miti shamba kutoka Kigoma alizokuwa akitumia Angel tangu alipotoka Kigoma ambazo zilikuwa zikimpa sana nguvu pindi anapoumwa sana haswa haswa viungo au anapokuwa hoi sasa hazikuweza kusaidia chochote zaidi ya kumfanya ajisaidie haja zote kitandani. Kazi kubwa ya Alice ikawa ni kuhakikisha dada yake Angel anakuwa msafi muda wote kwa kumfulia nguo zake pindi anapojisaidia na pia kumvalisha nguo nyingine. Mwili wake wote Angel ulipukutika na sasa akawa akingojea siku yake ifike.
Akiba ya pesa ambayo Angel alikuwa amejiwekea ndani sasa ikawa imeisha yote kutokana na kununua mahitaji madogo madogo. Matatizo yakahamia kwa Alice ni jinsi gani atatafuta pesa ya kuweza kumtibia Angel. Alice akajitahidi kukopa hapa na pale baadhi ya maduka ambayo Angel aliokuwa akipendelea kununua vitu. Madeni yakamzidi nakuamua kubadilisha hadi njia napo kila kona kukawa ni madeni tu. Kuna kipindi alidiriki kushinda na njaa mpaka kesho yake yeye na Angel. Hakukuwa na dalili yoyote kuashiria Angel atapona wala kupata unafuu zaidi ya kuendelea kuumwa na kukohoa sana tena kile kifua kikali na kikavu. Mwezi wa nne sasa ukawa ukielekea kukatika ambapo hali ya Angel ilionesha kufikia ukingoni kutokana na kubanwa sana na pumzi. Usiku huo Alice hakupata kabisa usingizi kutokana na Angel kushindwa kuongea kabisa. Kile kikohozi kikavu ambacho Alice alikuwa akikisikia kila inapofika alfajiri sasa kikawa kimekatika.
Mwanzoni Alice alijua ni usingizi utakuwa umempitia lakini jibu lilikuwa pale pale kwamba Angel alikuwa ameshatangulia mbele ya haki kifupi ameshafariki.
“Angel?, dada Ange?”
Alice aliita kwa sauti ya juu huku akimtingisha kwa kutumia nguvu kidogo, lakini Angel hakushtuka wala kutoa macho. Alice akakisogeza kichwa chake mpaka kifuani mwa Angel lakini bado hakuambulia chochote kusikia zaidi ya kuhisi masikio yake yamezibwa. Nguvu zikamelegea Alice akajikuta akidondoka na kupoteza fahamu papo hapo.

***ANGEL ameiaga dunia kwa gonjwa hatari la UKIMWI…Alice amebaki pekee….je? atahimili mikikimikiki??

ITAENDELEA


No comments:

Post a Comment

Recent Posts