Friday, April 5, 2013

RIWAYA: MREMBO ALIYEPOTEA-----------------5

 

MTUNZI: Andrew Carlos

MAWASILIANO: 0713133633

SEHEMU YA TANO


Ule mkojo uliokuwa ukimchuruzika John kidogo kupitia suruali yake kwa uoga sasa ukawa umeongeza kasi nakuwa mwingi sana hali iliyofanya suruali yake yote kulowana na lile kojo. Alijikaza kiume na kisha akamnyanyua Angel kwa kumbeba mithili ya wacheza mieleka kisha akaongoza mpaka kwenye gari lake nje nakumuhifadhi halafu akarudi tena ndani kumchukuwa Alice naye akampakazia kwenye gari lake nakuelekea hospitali ya Amana.
“Mungu nisidie nifike salama, Eeeh Baba niongoze ningoze Baba” OOohhh!!”
Barabara haikuwa na foleni kabisa sababu ilikuwa ni usiku sana, gari zilikuwa chache sana alizokuwa akipishana nazo John, njia nzima alikuwa akimuomba Mungu afike salama. Japo mikono yake ilikuwa ikimtetemeka lakini alijitahidi kujikaza kiume mpaka akafanikiwa kuingia katika hospitali ya Amana kisha akaomba msaada pale mule ndani.
“Umesema umekuja na maiti au mgonjwa”
“Mimi nahisi watakuwa wote wagonjwa maana nahisi kama wamezi mia kwani huyu mmoja alizinduka baada ya kumpepea sana akazimia tena ila huyu mwingine sikumuona akizunduka”
John alikuwa akiongea na daktari wa zamu ambaye kwa muda huu alikuwa karibu na ile miili ya Alice na Angel kwenye wodi ya wagojwa mahututi akiikagua vizuri.
“Umesema walipatwa na nini?”
“Hapana Dokta wala sijui mie nilikuwa ofisini sasa nimerudi nakuta wote wamezimia..”
“Hawa ni kama nani kwako?”
“Huyu hapa mmoja ni mke wangu anaitwa Angel na huyu ni mdogo wake anaitwa Alice wote wanaishi pamoja”
Dakatri alichukuwa vipimo vyake kwa kuwapima mapigo ya moyo kisha akaingiza mkono wake mifukoni na kutoa tochi za kupimia wagonjwa waliokufa halafu akafungua macho ya Alice na kummulika.
“Huyu hapa mzima hana tatizo.., itakuwa kaishiwa na pumzi tu hivyo atapelekwa mule wodini akawekwe oksijeni?”
“Na huyu mke wangu dokta..”
John alikuwa na haraka zaidi ya kujua jibu gani atapewa na yule daktari kuhusiana na Angel. Yule dokta aliendelea na zoezi lake la kuchukuwa ile tochi kisha akamfungua Angel macho yake na kummulika huku akiandika kwenye karatasi yake. Muda wote John alibaki akiyatolea macho yale maandishi aliokuwa akiyaandika yule daktari bila kuelewa yana maana gani..
“Alikuwa ni mjamzito?”
“Ndio Dokta.., alikuwa mjamzito tena mimba ni changa sana ndio kwanza ilikuwa ikikua”
Yule daktari sasa akaichukuwa ile tochi yake nakuingiza mpaka sehemu za siri za Angel huku akichungulia kwa kutumia ile tochi yake akainuka huku akiwa na ile damu katika glovu zake nakuendelea kuandika maelezo katika ile karatasi yake ya mwanzoni.
“Bwana mkubwa?, embu njoo kwa hapa pembeni mara moja”
Yule daktari alimvuta John kwa pembeni huku akionesha kuwa anajambo anataka kunena.
“Samahani lakini ndio ukubwa pia, na pia uvumilivu wako kama mwanaume. Kujikaza ni jambo la busara katika maisha haya haswa kwa sisi wanaume tunapopatwa na matatizo”
John tayari akili yake ikawa imeshagundua ni kitu gani anachotaka kuambiwa, bahari ya machozi ikawa imeanza kujikusanya tena katika uso wake huku kamasi likianza kuteleza kupitia mdomo wake. Mishipa ya hasira pembezoni mwa uso wake ikawa imechukuwa nafasi na kuamsha kwikwi huku akijilaziimisha kuvuta pumzi kwa haraka na kuchochea mapigo yake ya moyo ambapo sasa yalikuwa kama yamechochewa na kuni. Alijihisi mwili wote upo katika karai lililojaa mafuta ambapo chini yake kuna mafiga matatu yaliozungukwa na kuni zenye kuwaka ule moto mkali.
“Dokta niambie tu mke wangu kafa, Angel kafaaa?”
“Ndio maana nikakwambia jikaze wewe mwanaume mwenzangu, hali kama hii lazima itamtokea kila mmoja aliye ndani ya ndoa, na haya yote ni matakwa ya mwenyezi Mungu.. Mungu kampenda zaidi”
“Hapana dokta na kiumbe changu”
“Ni kwamba mimba inaonesha ilikuwa ndogo sana hivyo imesharibika na hii harufu kali unayoendelea kuisikia ambayo hii damu iliobadilika rangi na kuwa ya kijani na manjano imetokana na hii mimba iliyoharibika, Na huenda mimba ikawa imechangia kifo cha huyu japo sijapima vipimo vingine vilivyompelekea kifo chake. Cha muhimu ni kumshukuru Mungu kwa kazi yake aliyoitenda”
“Noo, Noo, Nooo dokta siwezi kuvumilia!!, dokta nashindwa kujizuiani nani ataliziba pengo hili, nani atanizalia doktaaaa”
Daktari akabaki na mshangao, Mshango wa kile anachoendelea kukishuhudia kwa John, Alijitahidi sana kumbembeleza lakini ndio kwanza alikuwa akizizidisha hasira za John ambazo sasa zilikuwa zinamshinda nguvu na kusababisha mdomo wake kuanza kuropoka ovyo na kwa sauti ya ukali. John na yule daktari Wakiwa bado wodi ya wagonjwa mahututi mara Nesi akatokea huku akionesha anahema sana na amekuja kwa taarifa.
“Dokta..??, dokta?, dokta? Yyyuuu uule mgonjwa uliyetuambiaa tu.. tu.. tuumpeleke kule wooddini.., tumemuwekea ile oksijeni ili apate hewa lakini oksijeni yote imejaa damu na sasa yupo anafurukuta kama anataka ku..”
“Unasemaje?, Alice anakufaa?”
John alishikwa na butwaa nakuropoka.., hakuamini maneno ya yule nesi, wakaondoka wote na yule dokta mpaka kwenye wodi alipokuwa amelazwa Alice napo walipofika walishuhudia kitanda chote kikifurika bahari ya damu huku Alice akijikunja kunja mithili ya mtu anayetaka kukata roho..
“Lete mashuka mengine??, Na muondoe mashuka haya hapa?”
“Sawa dokta tumekuelewa!!”
Haraka haraka kukafanyika kwanza kitendo cha kubadilisha mashuka ambayo yalikuwa yametapakaa damu na kuweka mashuka mengine.
“Haya nawaombeni wote mtoke nje mniache kama baada ya nusu saa niweze kumtibu huyu mgonjwa..”
Dokta aliamrisha kisha baadhi ya manesi wa zamu wakiongozwa na John wakatoka nje na kumuacha dokta akiendelea na zoezi la kumtibia Alice. Akili ya John muda wote bado ilikuwa imeganda kwa marehemu mpenzi wake Angel na haswa alikuwa akifikiria kiumbe kilichopotea tumboni mwa Angel. Alijitahidi kuvuta kumbukumbu vizuri kuanzia kipindi kile ambacho alimkuta Angel akijiuza posta usiku wa manane na kisha akamshawishi kumuomba amzalie na wakakubaliana hadi Angel mwenyewe ndio aliotoa taarifa kwa John kuwa ameshika ujauzito. Ile furaha na ahadi ambazo John alikuwa amemuhaidi Angel sasa akawa anaona kama ni ndoto ambayo amelala usiku nakuamka asubuhi hamna kitu. Alitamani sana tukio lote aliloshuhudia usiku ule ligeuke nakuwa ndoto.
“Shiiiiit!!!, Why me God!!, Kwanini mimi tu Mungu wangu, Nimekosa nini kwako? najua umenipatia Mwanamke nikamuoa hakuwa na uwezo wa kuzaa.., Nikatafuta njia nyingine nikafanikiwa kumpa Mwanamke mwingine ujauzito na sasa amefariki, umemchukuwa?, Why me?, kwanini Mungu? Aahhh!!!”
John alijikuta akipiga mateke fuko la uchafu ambalo lilikuwa pembeni yake huku akijishika shati lake kwa nguvu kama anataka kulichana. Sura yake sasa ikawa imezoea mateso kwa muda. Ule uso wa huzuni ukamzidia mara mbili kwani ulikuwa umetuna haswa huku macho yake yakionekana kuwa mekundu sana. Alikuwa kama nusu chizi nusu mzima kwani hata lile shati lake alilikunja mikononi nakuwa kama mtu anayetaka kuingilia ugomvi ama kutaka kupigana kabisa. Hatua za kuelekea kule wodini zikaanza.
“Hapana haiwezekani Angel wangu afe hivi hivi?, Nani atakuwa amemuua?, ni nani nasemaa?”
“Wewe Kaka vipi?, unaenda wapi huko si dokta kasema asiingie mtu?”
“Niacheni!!, nielekezeni mochwari mlipompeleka mchumba wangu Angel nikamuage?, Nipelekeni nimesema?, Nipelekeee?”
John alikuwa mkali kidogo kwa awale manesi wa zamu. Alihitaji kumuona tena Angel wake. Bado hakuamini kabisa kama Angel wake amepoteza uhai. Kwa woga waliokuwa nao wale manesi na walitaka kutii ile amri ya Daktari wao kuwa asiingie mtu mule wodini, walijikuta waakimuelekeza John mochwari ilipo napo John akaongoza mpaka mlangoni nakukutana na mlinzi wa zamu ambaye alikuwa ni Mzee wa makamo.
“Namtaka mke wangu aliyeletwa humu usiku huu?”
“Unasemaje kijana?”
“Kama ulivyosikia namtaka mke wangu?, Ameletwa huku!”
John alikuwa mbishi hakutaka kabisa kujibizana na yule mlinzi wa ile monchwari, kwa kuwa yule mlinzi alikuwa mzee japo si sana lakini John alifanikiwa kumsukuma nakuingia mpaka ndani ya monchwari. Alipofika ndani hakuweza kuutambua mara moja kutokana na yale mazingira aliokuwa ameyakuta. Kuna maiti ambazo zilikuwa zimelaliana huku zikionesha zimevimba sana. John alijitahidi kuangalia kama atamuona kwa wale waliolaliana lakini hakuambulia kitu. Sasa zoezi likawepo kwenye kufungua yale majokofu yaliokua nayo yamehifadhiwa miili ya watu waliokufa moja baada ya jingine. Ile hali ya ujasiri ikaanza kumpotea John akajikuta akilegea kila akifungua jokofu na kushuhudia maiti za watu wengine. Kuna waliokuwa wamepata ajali sura zao zikiwa hazitamaniki, Wengine wamepondeka sura. Hatimaye akafanikiwa kukutana na jokofu lililokuwa limehifadhiwa maiti ya Angel. John alitoa sana machozi, alitumia mikono yake kushika kichwa cha Angel huku akikilila.
“Angel?, Kwanini hukuniambia kama unakufa? nani sasa atanizalia Angel.. nasema nani..? mdogo wako umemuacha peke yake na sasa nayeye anataka kukufuata huko ulipo, Pliiz japo fungua macho Angel uniage nitaridhika, fungua Angel?, Angeeeel?”
Nguvu zikaanza kumlegea John nakujikuta taaratibu miguu ikikosa nguvu huku mikono ikimtetemeka zaidi mithili ya mtu aliyepigwa shoti ama aliyemwagiwa maji ya barafu, hivyo akadondoka peke yake mpaka chini nakupoteza fahamu.
********
Namba za simu, Pasipoti ya kusafiria ambazo ziikuwepo katika mifuko ya suruali ya John vikiambatana sambamba na funguao za gari lake ndizo zilikuwa zikimjulisha John Mapunda. Kazi yake ya kusimamia warembo wa miss Tanzania ndio ilimpa jina sana. Sura yake haikuwa ngeni kwa baadhi ya wafuatiliaji wa mashindano ya ulimbwende. Taarifa juu ya John kuwa hoi na kulazwa hospitali ya Amana usiku wa manane sasa ikawa imeshamfikia mkewe Janet. Janet alipokea simu kwa mtu asiyemfamhamu lakini alijitambulisha kwa jina moja tu kuwa ni Daktari katika hospitali ya Amana, ndipo na simu nyingine kutoka kwa baadhi ya marafiki zake na john zikaendelea kumiminika kumpa taarifa juu ya mumewe. Akili ya Janet moja kwa moja ilihamia kwenye ajali, Alijua ni wazi John atakuwa amepata ajali ya gari kwa sababu tabia ya mumewe kuendesha gari huku amelewa ni tabia yake ya kila siku. Haraka haraka Janet akaingia jikoni nakutengeneza uji wa ulezi aliokuwa akiupenda sana mumewe kisha akapika ndizi zikawa laini sana akavipaki, halafu akampitia rafiki yake wakaribu, Mary na safari ya kuelekea hospitali ya Amana kwa kutumia teksi iliyowatoa magomeni ikaanza.
“Kwani jana hakukupigia simu alipotoka kazini?”
“Hapana!!, yaani nashangaa tu leo kupigiwa simu, Namimi nilishamkataza haya mambo yake ya kuendesha gari huku amelewa ona sasa yaliomtokea!!”
“Janet usisimeme hivyo jamani!!, yaani badala umsikitikie na kwenda kumpa pole wewe kabla hatujafika umeanza kumsemea vibaya!, usifanye hivyo mpendwa!”
“Hapana Mary!, John amezidi!, kwanza kutwa ni wasichana utafikiri hana mke?, na hiyo mipombe yake ndio kabisaa!”
Janet alikuwa bado anahasira kali. Njia nzima kuanzia kwenye teksi waliokodi yeye na mwenzake Mary, alikuwa akimsemea vibaya John.
“Yaani Mary, mie nimechoka, nimechoka, ni bora angekufa tu nikajua sina mume kuliko anavyonifanyia. Wewe rafiki yangu na ni kama ndugu tena wa muda mrefu unajua sana matatizo ambayo ninayo ya kutokuzaa, sasa John ndio amechukulia ni jambo la kumkosesha raha ya maisha wakati watu wengine wanaishi vizuri kwenye ndoa zao.
“Ndio Janet!!, Lakini John?, MMmhh!!!”
“Na jana nilipewa ushaurii juu ya ya tatizo letu nikaambiwa kuwa inawezekana sana tukapata mtoto wa kupandikiza. Sasa ndio nilikuwa nataka nije tushauriane ona alichokifanya kapata ajali huko na Malaya zake”
Njia nzima ilikuwa ni ya Janet kuongea huku Mary akiwa kimya kwa kumuitikia. Haikuwachukua muda wakawa wamefika hospitali ya Amana, alimkabidhi yule dereva teksi pesa yake kisha akachukuwa simu nakuanza kupiga zile namba alizopigiwa na okta.
“Samahani dokta!!, Nimeshafika hapa Amana na nilikuwa namuulizia mume wangu ambaye umeniambia yupo hapa hospitali kalazwa”
“Anhaa, nyosha na njia ya kuingilia hapo getini moja kwa moja kama unaelekea mochwari angalia wodi ya pembeni yako unayotizamana na hiyo mochwari halafu ungie hapo, Ingia mpaka kwenye kitanda namba 26 ndio utamkuta hapo”
Ramani yote aliyopewa na daktari sasa ikawa imeshahamia ndani ya halmashauri ya kichwa cha Janet. Janet alikuwa rahisi sana kunasa kitu. Sasa akawa njia moja na rafiki yake Mary huku wanaangaza huku na kule wakisoma namba za pembeni mpaka wakafikia namba waliotajiwa yaani namba 26. Watu waliokuja kumtembelea walikuwa ni wengi japo si sana. Janet alimkuta mumewe katika hali ambayo haikuwa nzuri kwani mwili wake kuanzia sehemu za usoni ulikuwa umemvimba sana japokuwa hakuwa na majeraha yeyote. Alichokifanya Janet ni kushusha kapu ambalo alikuwa amebebea vyakula na kisha akachukuwa mkono wake wa kulia na kumshika John maeneo ya usoni kuanzia mashavuni mwake. Uzalendo ukaanza kumpotea kabisa Janet, Akasahau yale yote aliokuwa akimlaani mumewe njiani na sasa akawa kama kuna kitu kimepungua katika mwili wake. Janet alijihisi kuchanganyikiwa ghafla, machozi ya hasira sasa yakaanza kupenya ndani ya uso wake huku akijihisi kama amepigwa ganzi.
“Mume wangu nini kimekusibu?, kwanini lakini? na kwanini hukunipigia simu wewe wakati unatoka kazini? kwanini? ona sasa ulivyokuwa?”
Maneno ya taratibu naya majonzi yakaanza kumtoka Janet huku akimsema mumewe John aliyekuwa bado katika usingizi, alilalamika sana kiasi cha kila mmoja aliyekuja pale kumshangaa. Muda wote huo John alikuwa bado hajahamka.
“Amka basi mume wangu unijibu maswali yangu? amka John wangu?, nakupenda sana mume wangu!, amka japo ule, amka John, mimi ni wako milele kama tulivyoahidi kanisani wakati tunafunga ndoa, amka nikulishe mume wangu?”
Taratibu John akaanza kufungua jicho lake moja na baadaye likafuatia jngine na sasa akawa anaangaza huku na kule nakushangaa watu waliokuja kumuona.
“Mke wangu yuko wapi? Angel wangu yupo wapi nimesema?”
John alishtuka nakuanza kumtaja Angel hali iliowafanya kila mmoja wa marafiki zake kumshangaa hadi mkewe wakajua atakuwa amechanganyikiwa na kukosea kwa kumtaja Angel badala ya mkewe Janet. Akili ya Janet sasa ikawa ni kuhakikisha mumewe anajua kuwa yupo pale nakuwa amrekebishe mumewe asimtaje Angel amtaje Janet.
“Mume wangu?, nimekuja ni mimi Mkeo Janet, amka ule?”
“Hapana najua wewe ni Janet lakini namtaka Angel wangu sasa hivi”
“Angel ndio nani?, kwanza Angel hayupo hapa yupo kwao hukoo!”
Janet alijikaza bila ya kujua angel anayezungumziwa na John hivyo akaona kama amemdanganya atatulia tu.
“Jamani sitaki mivyakula yenu namtaka Angel nimesema?, Kwanza Alice nayeye amepona? yupo wapi?”
Hasira kali zilizoambatana na wivu ndani yake zikaanza kujijenga kichwani mwa Janet, Ule uvumilivu aliokuwa ameuonesha toka mwanzo ukawa sasa umeisha. Akaona dunia chungu kwa muda, Hakuamini kama mumewe John yupo siriazi kwa kutaja hao wanawake asiyewajua hata kwa sura. Akafikiria mengi sana mpaka akajiona hana thamani hata kwa mwanaume yeyote, aliamini kila rafiki yake aliyekuja kumtembelea atakuwa anajua matatizo yake ya kutokuzaa hivyo hata hao anaowataja John watakuwa wanamjua ila wanamficha tu. Akaamua kujishusha kama mwanamke aliyefundishwa na wazazi nakuanza kumbembeleza John ale kwa mara nyingine.


ITAENDELEA

No comments:

Post a Comment

Recent Posts