Sunday, December 9, 2012

CHOMBEZO: GUBERI LA KIMANYEMA


MTUNZI: INNOCENT A. NDAYANSE (ZAGALLO)

SIMU: 0713 59 35 46/0755 04 05 20


SEHEMU YA TATU



“Hidaya, tafadhali unielewe. Tuko peke yetu muda huu, na tuko ndani ya gari. Hakuna anayetuona. Tafadhali Hidaya, niruhusu nikubusu japo kidogo…”
“Hilo tu?” Hidaya alimuuliza kwa sauti ya chini.
“Ni hilo tu, Hidaya, mpenzi.”
Ukimya mfupi ukatawala. Hidaya akashusha pumzi ndefu. Kiwembe akahisi kuwa tayari kibali kimetolewa. Akautupa mkono juu ya paja la Hidaya, paja lililonona. Mkono huo ukateleza taratibu juu ya paja hilo. Hidaya akabadilika, hema yake ikawa ya taabu. Kiwembe hakuishia hapo, mara akaupeleka mkono kwenye titi moja la Hidaya na kuanza kulitomasatomasa huku akiuwinda ulimi wa Hidaya.
Muda mfupi baadaye wakawa katika hatua ambayo walishindwa kustahimili, nguo zikachojolewa. Gari la kifahari, Mercedes Benz 320 SE likageuzwa kuwa gesti. Hidaya na Kiwembe wakaifurahia dunia mpya. Huo ukawa ni mwanzo wa uhusiano wa penzi la wizi.
Penzi kati yao likakua na kumea. Wiki tatu baadaye walikuwa wameshaingia gesti bubu kadhaa katika maeneo ya Buzebazeba, Mwanga-Majengo na Gungu, wakizifurahisha nafsi zao kwa namna waliyotaka.
Hata hivyo pamoja na kuwa walijitahidi sana kuufanya siri uhusiano wao wa kiroho na kimwili, wakijinafasi katika gesti za mafichoni, bado hiyo haikuwa ‘dawa’ ya kuwatia upofu watu wachache wanaowafahamu. Umaarufu wa Khalifa Mwinyimkuu na mkewe ulizagaa takriban Manispaa nzima ya Kigoma/Ujiji. Watu wengi waliwafahamu, hivyo kati ya hao, mmoja wao alimwona Hidaya akiingia katika gesti moja eneo la Mwanga- Majengo saa 2 usiku huku akionyesha wazi kuwa hakutaka kutambulika.
Mwingine walipishana kwenye korido ya gesti fulani katika kitongoji cha Buzebazeba, Ujiji, Hidaya akiingia akiwa amekumbatiana na Kiwembe huku jamaa huyo akitoka.
Minong’ono ya wambea ikazagaa kwa kila aliyemfahamu Khalifa Mwinyimkuu na Hidaya Sufiani. Minong’ono hiyo iliendelea kuzagaa hata ikayafikia masikio ya Khalifa Mwinyimkuu mara tu alipotoka katika moja ya safari zake za kibiashara. Na kama hakuna siri duniani, ni kipi kingemfanya bwana huyo asipate habari?
Alizipata! Ndiyo, alizipata, lakini kwa kuwa hakuwa mshiriki sana wa maneno ya hisiahisia, yasiyokuwa na uthibitisho wowote, wala hakupenda kushiriki kwenye vibaraza vya kahawa ambako huenda angezisikia tetesi, alizipuuza habari hizo.
Siku zikaja, siku zikapita akiendelea kuzipuuza habari hizo. Lakini jambo la kusikia lina maudhi na maumivu yake. Linauma ingawa halitoi damu. Chukulia kuwa siku moja uko na rafiki yako wa karibu, rafiki mliyeshibana, halafu anapita mwanamume mmoja mbele yenu. Baada ya mtu huyo kupita, rafiki yako anakunong’oneza, “Unamwona huyo mshikaji?”
Labda na wewe unaitika, “Ndio, nimemwona. Vipi?”
Rafiki yako anakukazia macho na kutamka kwa msisitizo, “Ukae ukijua kuwa huyo nd’o mume mwenzio.”
Utajisikiaje baada ya kusikia hivyo?
Japo Khalifa Mwinyimkuu hakuwa mtu wa kupokea habari ambazo hakuzithibitisha mwenyewe lakini taarifa ya rafiki yake mmoja wa siku nyingi kuhusu nyendo za mkewe, hakuichukulia kama aina nyingine ya habari za uzushi na umbea. Hapana, taarifa hiyo aliipa uzito wa juu, akaamua kuifanyia kazi.
Kila kikeracho moyo kina mwisho wake wa uvumilivu. Khalifa Mwinyimkuu alishindwa kuvumilia zaidi. Akaamua kufanya uchunguzi huo baada ya kuona mabadiliko fulani katika mienendo ya mkewe, Hidaya. Tangu alipotoka safari Hidaya hakuonesha kuwa na furaha wanapokuwa pamoja. Na isitoshe, katika wiki nzima ambayo alikuwa amerudi, Hidaya hakuwa amempa unyumba kwa kutoa visingizio hivi na vile.
Hidaya alikuwa amebadilika. Hakuwa akimliwaza kama ilivyokuwa kawaida yake. Hawakuwa wakicheka pamoja, wakichekea penzi lao.
Je, kwa tabia hiyo kwa nini Khalifa Mwinyimkuu asiamini kuwa mkewe ana mwanamume wa nje aliyemmalizia hamu yake ya mapenzi? Ndipo alipoamua kufanya uchunguzi wa kumjua huyo aliyemzuzua mkewe, Hidaya.
Khalifa Mwinyimkuu alishangaa, akasononeka. Akawaza, iweje Hidaya afanye uhuni kiasi hicho? Ni shida ipi inayomsumbua? Hakuwa na familia ya kuitunza. Familia ya ndugu wa mume ilikuwa ikijitunza yenyewe. Kipi sasa kimfanye awe malaya?
Aliishi katika nyumba kubwa, nzuri iliyoenea kila kitu ndani. Alipewa gari zuri la kutembelea. Ni kipi kingine alichohitaji? Roho ya mtu?
Hakupata jibu.

*****

JAPO Hidaya alimtaarifu Kiwembe bayana kuwa baba mwenye nyumba kishahisi jambo, na kumtaka wasitishe mawasiliano kwa muda, hata hivyo Kiwembe hakukubali. Alishanogewa. Ndiyo, alishanogewa na kwa ujumla wote walinogewa kiasi cha kufikia hatua ya siku nyingine Kiwembe kuja hapo nyumbani ambako alipata maakuli kabla ya kujichimbia chumbani na kufanya yale waliyopenda kuyafanya.
Hidaya alikuwa mjanja. Alibaini kuwa mumewe kishamhisi siku alipomuuliza maswali ya kimtegomtego kuhusu ratiba zake za kutoka nyumbani. Kwa hali hiyo, siku ya pili tu walipokuwa na Kiwembe katika gesti fulani kwenye kitongoji cha Buzebazeba, ndipo alipoamua kumtaarifu kuhusu hadhari wanayopaswa kuichukua.
Na ni hapo ndipo Hidaya alipogundua kuwa kwa Kiwembe kutokuwa na simu ni tatizo kubwa. “Ungekuwa na simu…” alimwambia na kuiacha sentensi hiyo ikielea.
“Ningekuwa na simu, lakini sina, na pesa za kuinunua hiyo simu sina,” Kiwembe alisema kwa unyonge.
Hidaya alifikiri kidogo kisha akasema, “Any way, nipe siku mbili, tatu hivi. Nitakununulia simu ya bei ya kawaida. Lakini kwa siku tatu tusionane. Usije nyumbani, umenielewa?”
“Poa,” Kiwembe alijibu kwa unyonge. Akilini mwake hakuwa tayari kumkosa Hidaya hata kwa siku mbili.
‘Haiwezekani,’ alijisemea kimoyomoyo. Akajigamba mwanasagamba, kwani sagamba haiogopi lami wala kokoto. Na wala kijiko cha jikoni hakiogopi moto. Kichaa hicho! Kiwembe akafikia hatua ya kuwa na wivu, akitaka penzi analopewa na Hidaya asipewe mtu mwingine! Hata mumewe!
Ndiyo, alitaka awe yeye tu!
Yeye peke yake!
Akawa na hamu ya kuwa naye kila wakati, akifaidi wepesi wake kitandani sanjari na manung’uniko yake ya faraja yaliyomtoka kwa sauti ya kipekee iwezayo kumsisimua rijali yeyote.
Ni jana tu walipokuwa pamoja, na wakakubaliana Kiwembe asidiriki kutia mguu tena nyumbani kwa Hidaya. Lakini Kiwembe kwa uchu wake na ukichaa wake hakuweza kutii makubaliano yao. Saa 9 alasiri akawa ameshakanyaga nje ya geti la nyumba ya kifahari ya mzee Khalifa Mwinyimkuu. Akabonyeza kengele ya wito.
Hidaya akiwa hategemei kuwa Kiwembe angethubutu kukiuka makubalianao yao, alikwenda kufungua geti. Mshtuko alioupata baada ya kufungua geti hilo ulikuwa nusura umtoe ruho. Japo wakati huo Khalifa Mwinyimkuu hakuwepo, hata hivyo Hidaya alighadhibika. Hasira zikampanda kwa kiwango cha juu.
“We vipi?” alibwata huku akimtazama kwa macho makali. “Kwani tumeongeaje jana?”
Kiwembe hakujibu.
“Nakwambia kwa mara ya mwisho, usije tena, ondoka! Mume wangu akija sasa hivi na kukukuta hapa utasema nini? Ama mimi nitajielezaje?”
Kufoka kote huko kwa Hidaya, machoni na masikioni mwa Kiwembe ilikuwa kama sinema ifurahishayo.
“Sikiliza mpenzi, Hidaya,” Kiwembe alisema huku akichekacheka. “Acha jazba. Piunguza ukali. Nakuomba uelewe tu kuwa nisipokuona japo kwa siku moja tu, basi jinamizi huja na kuniiinamia…”
“Koma!”
“Tafadhali Hida…”
“Toka!”
“Nisikilize taf…”
“Koma we! Nakwambia tena koma! Uniondolee upuuzi wako hapa!”
Pamoja na ukali wote huo wa Hidaya, hata hivyo Kiwembe aliondoka huku roho yake ikiwa imesuuzika. Kumwona Hidaya na kuisikia sauti yake ilikuwa ni hatua kubwa sana kwake.

*****

SIKU zilipita, wiki zikaenda hatimaye miezi miwili ikakatika. Sasa hali ya amani, furaha na upendo ikarejea ndani ya nyumba ya Khalifa Mwinyimkuu na mkewe, Hidaya. Ule wasiwasi wa kulindana ukatoweka. Kila mmoja akawa na furaha na mwenzake. Lakini Hidaya hakuwa na furaha iliyotimilika. Katika ndoa yao kulikuwa na dosari iliyopaswa kutafutiwa ufumbuzi.
Ile haki ambayo kila mmoja alistahili kuipata katika ndoa, Hidaya hakuipata. Na kulikuwa na sababu. Khalifa Mwinyimkuu alikuwa ni mwanamume, ndiyo. Lakini alikuwa na udhaifu uliosababisha Hidaya asiifurahie ndoa yake. Kila usiku ulipoingia, na wanandoa hao kulakiwa na kitanda, hakukuwa na chochote cha ziada kilichotokea ambacho kilimfanya Hidaya ajione kuwa yuko katika maisha ya ndoa.
Usiku ulipita kama ulivyo, mapambazuko yakawakuta kama walivyokuwa. Tatizo la Khalifa Mwinyimkuu kutomtimizia haja zake Hidaya, lilianza baada ya kupata ajali mbaya akiwa safarini Arusha. Miongoni mwa athari zilizomkuta baada ya ajali hiyo ni kupungukiwa na nguvu za kiume kwa kiwango cha juu hivyo kutokuwa na uwezo wa kufanya tendo la ndoa na mkewe kwa kiwango kinachoridhisha.
Pamoja na amani kurejea ndani ya nyumba yao, hata hivyo bado Hidaya alijisikia kuteseka kwa kukosa kile alichokihitaji. Hali hiyo ikamfanya awe na msukumo fulani uliomtia kishawishi.
Ndipo ikaja siku. Ilikuwa ni siku ya kawaida tu kwake, akiwa katika safari zake za kawaida za sokoni. Siku hiyo alikwenda katika soko kuu la Kigoma mjini. Wakati alipoegesha gari tu, akamwona Kiwembe hatua chache kando ya gari. Kiwembe alikuwa na safari zake za kawaida zisizokuwa na malengo maalumu. Lakini alipomwona Hidaya akiegesha gari kando ya soko hilo, naye akasitisha safari yake. Akamfuata na kumsalimia.
Hidaya naye akifurahia kukutana kwao, baada ya kusalimiana akasema, “Kiwembe nimekukumbuka. Lakini hapa wanga wengi. Tuonane wapi? Sema haraka.”
Kiwembe aliwaza harakaharaka na kukosa jibu sahihi. Angesema wakutane wapi ilhali yeye hana pesa za kukodi chumba gesti?
“Pesa, Hidaya. Sina kitu.”
“Usijali,” Hidaya alimdaka huku akiangaza huku na kule kwa kumhofia mumewe.
Wakakubaliana haraka kuwa siku isiyokuwa na jina wakutane kwenye hoteli fulani wakumbukie.

*****

KHALIFA Mwinyimkuu hakuwa mjinga. Pamoja na ukimya wake wote, pamoja na upendo aliouonyesha kwa mkewe kwa siku zote hizo, hata hivyo kwa siri aliendelea kuzifuatilia nyendo zake kwa makini sana. Hakufanya papara, kwa kuwa alihitaji kuthibitisha mwenyewe hicho anachokitilia mashaka.
Akawapa tenda vijana watatu wa ‘njaa-njaa,’ tenda ya kumfuatilia kwa siri Hidaya. Kila mmoja katika vijana hao akapewa 10,000/-. Naam, pesa ni sabuni ya roho.Vijana hao walipopewa tenda wakaingia kazini. Wakawa wakimfuatilia Hidaya kila alikokwenda, na asubuhi ile ambayo Hidaya alikutana na Kiwembe sokoni, vijana wale wakashangaa na kushtuka. Wakati walipopewa kazi hiyo na Khalifa Mwinyimkuu, aliwadokeza juu tetesi alizowahi kuambiwa kuhusu uhusiano wa Kiwembe na Hidaya.
Hivyo, kuwaona Hidaya na Kiwembe wakizungumza kuliwafanya wazidi kuwafuatilia, na zaidi wakiwa wanamfuatilia Hidaya. Na taarifa za mwisho zilipomfikia Khalifa Mwinyimkuu, papohapo akaisereresha Land Cruiser barabarani kwenda kushuhudia. Bado hakuwa na papara hata pale alipowaona Hidaya na Kiwembe wakiingia ndani ya hoteli ile nzuri. Alivumilia japo moyo ulimuuma.
Aliwaona, lakini akawapa muda, wastarehe wapendavyo.


***KHALIFA MWINYI MKUU ameushtukia mchezo lakini amewapa muda KIWEMBE na HIDAYA……..Mh pabaya hapa……..utajisikiaje ukipewa muda uendelee kula raha na mali ya mtu????

ITAENDELEAAA

No comments:

Post a Comment

Recent Posts