Tuesday, April 2, 2013

RIWAYA: WASALIMIE KUZIMU---2

 

MTUNZI: Hussein Wamaywa

SIMU: 0755 697335


... Ni ile mikono yenye nguvu iliyokuwa imembana kiunoni kwa nguvu ndiyo iliyomshitua na kumuondoa toka katika njozi hiyo tamu aliyokuwa akiiota, alipogeuka nyuma akakuta jamaa linataka kumbaka.
Halfan akakurupuka baada ya kuhisi nini kinataka kuendelea hata hivyo juhudi zake za kutaka kujinasua zilikwama baada ya kujikuta amedhibitiwa vizuri na jamaa yule.Hakutaka kukubali kirahisi akakunja mkono upesi na kuachia kipepsi kilichotua sawia shingoni mwa jamaa. Akainuka na kuliacha likigugumia kwa maumivu.
Akashukuru Mungu na kuona kwamba njemba lile lilikuwa halijafanikiwa kutimiza lengo lake. Macho yake yalipozoea giza ndipo alipotambua kwamba aliyetaka kumbaka hakuwa mwingine zaidi ya Jofu Gideon.
Mbele yake aliwashuhudia wababe wengine watatu wakiwanajisi vijana wengine wawili ambao hawakuwa na muda mrefu toka walipoongezwa katika chumba hicho. Ilikuwa picha isiyopendeza ambayo alilazimishwa kuitazama.
Hakulala tena! Badala yake akakaa pembeni na kuitafakari ndoto aliyokuwa akiiota ambayo tayari ishamfanya aichafue Kaptura yake.
Jina Shania halikuwa kabisa katika kumbukumbu zake. Alijitahidi kumkumbuka na kumtafuta tena na tena kati ya wanawake wengi aliokwisha rusha nao roho, wasichana wa shule, mabaamedi, wanamitindo, makarani, warembo na hata mabosi!
Bado jina Shania halikuingia katika reli zake.
Aliposhindwa kabisa akaachana nae na kuyafiria maneno ya Shania, kiasi yalikuwa na ukweli ndani yake. Ni kweli Nasra hajawahi kuja walau kumpa hata pole, wachilia mbali kumjulia hali.
Hakuwa Nasra pekee tu bali hata marafiki zake wengine waliokuwa nae sambamba wakati akiwa uraiani. Sasa ndio akagundua ni kwa nini marafiki wanaitwa wanafiki, aliamini yeye sio mtu wa kupata dhiki ya vitu vidogo vidogo kama maji, sabuni nyembe, mafuta na hata sigara.
Hivi vilikuwa vitu vidogo sana ambavyo marafiki zake wengeweza kumsaidia pasipo kupata hasara yeyote. Lakini wachilia mbali kumpelekea vitu hivyo wameshindwa kwenda hata kumuona.
Ni wakati huo alipopambazukiwa na ukweli kwamba ni kwa nini wahenga walisema rafiki wa kweli hupatikana wakati wa shida. Aliendelea kuwaza hili na lie na kumlaumu huyu na yule mpaka kulipokucha.
Naam! Alikuwa ameingia katika mkondo wa maisha mapya kwa kosa la kipumbavu kabisa na ndio maana wafungwa na gereza walimdharau yeye na kosa lake…!


NASRA ALWATAN DAFU

Siku ilikuwa inachangamka kwa maana ya kupata nuru angavu toka angani na hivyo kuifanya nchi ianze kuyaonja makali ya jua. Promota, mtoto wa kwanza wa Nasra ndio kwanza alikuwa amerejea toka shuleni alikoanza hivi karibuni katika shule ya Awali ya Kumekucha Nursery School!
Mtoto wa pili aliyezaliwa siku moja na Promota, Romota alikuwa amefariki siku nyingi nyuma na ilikuwa imefanyika kazi ya ziada kuyaokoa maisha ya Promota.
Kwa nini Nasra aliamua kuwaita ‘Promota’ na Romota watoto wake mapacha waliozaliwa njiti siku ya fainali za mashinano ya kumtafuta Miss Temeke Academia pale Diamond Jubilee?
Mwenyewe anasema Romota ni jina la mama yake mdogo anayeishi Jeddah Saudi Arabia na kwa maelezo yake anasema mtoto huyo mdogo wa kike alikuwa amefanana sana na huyo mama yake mdogo ambaye yeye alimpenda sana. Ingawa wengi walidai kuwa Romota alifanana na Nasra zaidi kuliko mtu mwingine yeyote.
Jina la Promota hakuna aliyejua hasa limetokea wapi na hata walipombana zaidi aeleze Nasra alidai Promota ni jina kama linavyoweza kuwa Dickson, Masimango, Hussein, Gideon na kadhalika. Waliposhindwa kumshawishi walimuacha alivyo.
Nasra akamkimbilia mwanae aliyekuwa mikononi mwa mtumishi wao wa ndani, akamnyanyua na kumkumbatia, akambusu na kumnyang’anya mkoba aliokuwa nao mkononi.
“Baba yangu huyooh! Umesoma nini leo?” Akamuuliza kwa upendo.
“Tumethoma… tumethoma hethabu dha kikwetu!” Promota akajibu kwa kithembe.
“Woooh! Umezielewa lakini?”
“Kidogo mama akini ngumu hicho!”
“Usijali baba, kidogo kidogo utazielewa!”
Wakaingia ndani akamtenga katika makochi na kwenda kumletea uji, aliporudi hakumkuta “We Promota!” Akaanza kuita akamtafutia huku na huko.
“Iko uku mama!” Sauti ilitoka chumbani kwa babu yake mzee Alwatan Dafu. Promota alikuwa mtundu hujaona, Nasra akamtazama na kuachia tabasamu kwa chati akimfurahia mwanae aliyekuwa mcheshi kuliko.
Promota nae akatabasamu akimfuata mama yake mbio akamfikia na kumrukia. Nasra akamdaka akimkaripia kwa utani, wakageuza na kurudi sebuleni ambako shughuli ya kumpa chakula ilianza.
Shughuli iliyomalizika muda mfupi baadae, akamvua nguo za shule halafu akamtumbukiza katika sinki la maji na kumuogesha. Muda mfupi baadae walikuwa kitandani ‘akimpetipeti’ mwanae tayari kwa kumvutia usingizi.
Naam! Haikuchukua muda Promota alilala. Nasra akamuacha taratibu na kuondoka kitandani katika mtindo ule ule wa kunyata akihofu kumuacha mwanae. Wakati ananyoka kitasa cha mlango, Promota akakohoa.
Nasra akageuka na kumtazama alimkuta akimalizia kikohozi chake na papo hapo akaachia tabasamu dogo la kiutoto utoto. Mungu wangu, tabasamu hilo la Promota likaamsha mambo.
Wakati anaendelea kulitazama tabasamu la mwane. Nasra akajihisi kama anayemuona Halfan vile! Hisia za ajabu zikauvaa moyo wake, akaacha kuufunga mlango alikokuwa ameushika akarudi taratibu na kuketi kitandani ubavuni mwa mwanae ambaye bado tabsamu laini lilikuwa limeupamba uso wake.
Sasa ndio akagundua mwanae zaidi ya marehemu Romota alikuwa Halfan mtupu. Toka sura, umbo, tabsamu, miondoko na hata ucheshi uliozidi mipaka.
Alipomkumbuka pacha wa Promota, Romota ambaye watu walidai amefanana nae sana machozi ya uchungu yakateleza mashavuni mwake. Akajitahidi kumsahahu na mawazo juu ya Halfan yakakamata hatamu.
Mawazo hayo hayakudumu sana pale kumbukumbu ya yaliyojiri siku ya fainali za kumtafuta Miss Temeke Academia katika ukumbi wa Diamond Jubilee kutawala kichwani mwake.
Alikumbuka vizuri sana kuwa ni pale alipotangazwa kuwa mshindi wa Miss Temeke Academia ndipo kizaa zaa kama sio mshike mshike ulipoanza. Sauti ya MC Dickson iliyomtamka kuwa ameshinda ndiyo iliyomletea mshtuko wa hali ya juu. Mshtuko uliomfanya ajisikie vibaya, aliporudi jukwaani kwa mara ya pili kusalimia watu, hali ilizidi kuwa mbaya ingawa watu walizidi kumshangilia kwa nguvu.
Machozi yakamtoka.
Machozi ambayo machoni mwa waandishi wa habari, mashabiki wake na vyombo vya habari yalichukuliwa kama machozi ya furaha, furaha ya ushindi.Lakini ukweli haukuwa hivyo. Yalikuwa machozi ya uchungu, uchungu wa maumivu ya tumbo, nyonga na kiuno. Uchungu wa uzazi! Alitamani sana kupiga kelele na kuomba msaada, lakini alipotazama hali halisi akakata tamaa! Angeanzia wapi wakati alishatangazwa mshindi?
Machozi yakazidi kumtoka, watu wakazidi kumshangilia! Mpaka anavishwa taji hali ilikuwa bado haijawa sawa kwake. Na alipolikaribia gari baada ya kukabidhiwa funguo akahisi mambo yanaharibika na kweli yaliharibika.
Kwani alipoinuka mguu tu kuingia garini, ndipo alipojikuta akijikamua kwa nguvu bila kupenda na matokeo ya kujikamua huko ikawa ni kujifungua watoto mapacha njiti. Uchungu mkali ambao hakuwahi kuuhisi maishani ukampata, yowe kali lililoashiria maumivu aliyonayo likamtoka.
Nguvu zikamuishia taratibu, akahisi kizunguzungu kikali na wakati anakwenda chini akasikia mikono minene yenye vinyweleo laini ikimdaka, kageuka kwa taabu na kutazama, alikuwa Saadan! Akajitahidi kufyonya uso akiukunja.
Haikusaidia! Hakuwa na nguvu tena, nguvu za kujinasua toka mikononi mwa Saadan akaishia kufyonya fyonya!
Kelele zikazimika. Ukumbi ukawa kimya ghafla kama ungepata bahati ya kupita nje ya ukumbi huo siku ile usingeweza japo kuhisi kama ndani kulikuwa na shughuli pevu.
Nasra aliyekuwa hoi bin taaban aliweza kumuona kwa taabu mama yake akihangaika kuwahifadhi vizuri watoto waliozaliwa na yeye muda mfupi tu uliopita.
Aidha aliweza kumuona baba yake kwa taabu pia jinsi alivyofura kwa hasira akimfuata Halfan na kuanza kumpiga huku akumtuhumu kumpa mimba binti yake.
“Nooo! Baba usimpige, muache!” alijitahidi kumtetea lakini bahati haikuwa yake. Sauti iligoma kutoka.
Wakati huo huo watu ambao walizisikia shutuma za Alwatan Dafu dhidi ya Halfan walimvamia na kuanza kumtwanga mangumi. Warembo ambao walikosa nafasi ya kwanza na hivo kulikosa Caddilac walilokuwa wakilimezea mate, licha ya kuliwa uroda na Promota Halfan wakishangilia pasipo kwenda kumsaidia Halfan.
Hii likamuumiza sana Nasra na ingawa hakuwa na nguvu hata moja, akajikakamua na kukusanya nguvu zote zilizosalia na kupiga kelele kwa nguvu
“Nooo! Nooo! Msimpige Promota Halfan. Msimpige! Mnamuonea bure nimempenda mwenyewe!” Masikini Nasra, sauti iliyotoka ilikuwa ndogo sana ambapo haikuweza kumfikia hata Saadan aliyekuwa amepakata mikononi.
Lakini kwa vile alitumia nguvu nyingi kuitoa sauti hiyo, alijikuta akianza kuona giza kwa kasi kabla hajapoteza kabisa fahamu muda mfupi baadae.
Halfan nae alizidiwa na kipigo na kupoteza fahamu. Mpaka polisi walipoingilia kati kumnusuru, tayari alishakuwa na hali mbaya sana. Wakampeleka Polisi akapata PF3 kisha akapelekwa Temeke Hospital alikopata matibabu chini ya ulinzi mkali wa Polisi.
Nasra yeye alipelekwa katika hospital ya Aga Khan na kupatiwa tiba chini ya uangalizi wa madaktari bingwa. Madakatari waliobobea.
Alipozinduka siku chache baadae alijikuta hospital pembeni ya vitoto viwili vidogo vilivyofanana kama reale kwa ya pili, alikuwa amepoteza kumbukumbu hivyo hakuwa anajua chochote.
Mama yake, muuguzi wake, walimueleza kila kitu na kumfariji. Nasra alilia sana alipogundua kwamba Promota Halfan alipigwa sana na Wananchi wenye hasira kama kibaka mzoefu na msumbufu kabla hajapoteza fahamu.
“Masikini Promota wangu! Amekufa?” akauliza kwa kihoro
“Hajafa bado? Lakini tayari amefunguliwa mashitaka akipona atapelekwa mahakamani, tena nasikia baadhi ya warembo wameamua kuwa mashahidi upande wa mshtakiwa katika kesi hiyo, wengi amefanya nao mapenzi akiwaahidi kuwapa ushindi bila kuwapa!
“Haiwezekani mama! Hao warembo waongo, tena waongo wakubwa! Wanamuonea bure tu Promota Halfan, wananionea gere kwa vile nimeshinda gari na taji ambavyo wao walivisumbukia kwa muda mrefu.
Na kwa hili, hapana sitakubali! Lazima nimuokoe Halfan wangu, lazima nimuwekee wakili atakayehakikisha anashinda kesi hii! Nasra akaendelea kulia.
“Fedha za kumuwekea wakili utazipata wapi mwanangu?” mama yake alimuuliza kwa upendo”
“Hilo siyo swali la kuuliza mama. Baba ana fedha za kutosha mimi nina akaunti yenye fedha za kutosha pia! Halafu lile Caddilac langu liko wapi?”
“Liko nyumbani limetunzwa vizuri katika sehemu ambayo italifanya lionekane jipya milele!”
“Ikishindikana nitaliuza nimlipe wakili siwezi kuwa na amani kwa kutembelea gari ya bei mbaya wakati mpenzi wangu anasota jela! Nitaliuliza tu”.
“Unasemaje? Halfan ni mpenzi wako? Mama Nasra akashindwa kuyaamini masikio yake.
“Sio mpenzi wangu tu mama, bali pia baba wa watoto wangu! Jibu hili likamfanya shushe pumzi ndefu.
“Ilikuwaje kuwaje hata ukaweza kurubuniwa na yeye, ukaweza kumpa usiachana wako, ukaweza kujishusha thamani kwa kuzaa nje ya ndoa? Niambie Nasra mwanangu!”
“Maswali hayo muulize mumeo Alwatan Dafu, tena wala hakunirubuni nilijirahisi mwenyewe kwa nini mnifuge kama kuku wa kisasa? Kosa langu nini kuwa mtoto wenu au kwa kuwa mimi ni mwanamke?” Nasra akalia zaidi.
“Basi mwanangu unajua fika kuwa wewe ni mtoto wetu wa pekee. Pengine ni hilo lililomfanya Alwatan Dafu afanye alivyofanya akiwa na lengo la kukuandalia future nzuri.
Kosa alilofanya ni kukunyima uhuru na kukugeuza mfungwa tena akasahahu kwamba ni rahisi kuchunga ng’ombe elfu tano kuliko binadamu mmoja! Msamehe Nasra, msamehe zaidi. Yule ni baba yako”.
Nasra hakujibu aliendelea kulia kimya kimya.
Kikapita chembe cha nukta kadhaa Nasra akilia taratibu kwa kwikwi
“Vipi,” Mama Nasra akasaili baadae. “Ungali unampenda Halfan?”
“Ndiyo mama, ningali nampenda, nampenda kuliko mnavyoweza kufikiria!”
“Lakini baba yako ndio hataki hata kumsikia kabisa!”
“Sikiliza mama! Kwa sasa lazima atanisikiliza tu, apende asipende! Nimechoka kuwa mtumwa katika nchi iliyo huru. Vile vile mjue anayeongea sasa ni Nasra mwingine aliyepevuka kiakili baada ya kuzaa!”
“Vipi kuhusu Saadan? Humtaki tena?”
“Kwani mwanzo nilikuwa namtaka? Si huyo baba mwenyewe! Sijui alimtafutaje wanaume wote waliopo Tanzania kaona hawatoshi mpaka aende kuniibulia mwanaume toka Oman. Lakini naamini kama Saadan ni mwenye akili hatoweza kunioa tena! Picha iliyokwishajionyesha imeunguza kila kitu ni waume wenye mioyo ya chuma pekee. Kama Dick Mau Mponda ndio wanoweza kukazania ndoa na mimi!”
“Unajidanganya Nasra Saadan ana zaidi ya moyo wa chuma. Anakupenda kuliko unavyoweza kufikiria ni yeye aliyekudaka pale jukwaani baada ya wewe kujifungua.
Kama ungelianguka sio kwamba ungeumia peke yake lakini pia ulikuwepo uwezekano mkubwa wa kupoteza maisha ya wanao kwa kuwaangukia. Na kana kwamba hilo halitoshi amekuwa anakuja hapa kila siku kukujulia hali mwenyewe anasema hiyo ni bahati mbaya na yuko tayari kuwalea watoto wako kama wanae wa kuzaa.
Aidha amelipa kiasi kikubwa cha pesa za matunzo ya kitaalamu katika hospitali hii ili kuwanusuru watoto wako toka katika hatari ya kupoteza maisha! Si unakumbuka kama wanao wamezaliwa kabla ya siku yao?” Mama Nasra akaitimisha kwa swali.
Likawa swali lilikosa jibu. Nasra akashusha pumzi ndefu, akapenga kamzi na kufuta machozi kabla hajageuka na kumuangalia mama yake akaachia tabasamu jepesi na kusema.
“Inawezekana Saadan akawa anipenda kwa dhati mama, lakini pendo langu la kweli liko kwa Halfan!”
“Poa mwangu! Hiyo ni choice yako sikulaumu kwa hilo lakini…..”
Kabla hajamalizia kusema alichokuwa amekianza, Alwatani Dafu na kijana mwingine wa kiarabu waliingia wakiwa na makapu ya vyakula. Nasra akakunja uso na kugeukia pembeni baada ya kumuona baba yake.
Furaha iliyokuwa ameanza kuipata baada mzazi wake wa kike kuja na maelezo yanayotia moyo; sasa ilipotea na machozi yaanza kutafuta njia katika mboni za macho yake.
Alwatan Dafu na Saadan wakaketi pembeni ya Nasra na kumsalimia mama Nasra kabla kuulizia hali ya mgonjwa wakajibiwa kuwa ni njema sana.
Mama Nasra alipoondoka kwenda kuosha vyombo, ndipo Nasra alipogeuka na kumtazama mzee wake kwa chuki. Dafu akishangazwa na hali hiyo na kuuliza kulikoni.
“Kwa nini baba, kwa nini ukafanya vile?” Nasra akajibu kwa swali, tena kwa sauti kavu.
“Kwa nini nini Nasra? Nikafanya vile vipi?”
“Hujui siyo? Kwa nini ukampiga Halfan na kumfungulia kesi mbaya ambayo imeweza kumgharimu miaka mingi jela?”
“Mungu wangu! Kumpiga mtu aliyekutia mimba bila ridhaa yangu, bila harusi ni kosa?”
“Ni kosa ndiyo. Kama wewe ndiye mwenye idhini ya kuruhusu mimba iingie katika mwili wangu mbona umeshindwa kuzuia isiingie?”
Alwatan akashindwa kuyaamini haya ayasikiayo.
Nasra…! Nasra…! Aliwaza kwa hasira Alwatan Dafu na kuendelea Nasra yule yule aliyekuwa akinipenda, kuniheshimu na kunisikiliza leo anatema maneno makali yenye ncha kali kama mkuki! Haiwezekani!! Iko namna! akaitimisha kwa hasira zaidi.
“Lakini Nasra, si nilikwambia kwamba mchumba wako ni Saadan?” akajitia kupoa
“Uliniambia lini?”
“Wiki moja kabla ya shindano!”
“Wakati huo mimba ilikuwa imeshaingia au bado?”
Mzee Alwatan Dafu akatahayari “…Lakini ulipaswa kujilinda na kujitunza Nasra” Akakwepa kujibu swali.
“Na sio kulindwa na kutunzwa?” Nasra akaendelea kumshikia bango.
Alwatan Dafu alipochelewa kujibu hili, Nasra akaendelea “Hivi baba ulipokuwa ukinifuga na kuninyima uhuru, ulitegemea mimi nifanye nini? Baada ya kumpata mwanaume?” Majibu ya Nasra yalikuwa makavu kama mtumba wa Manzese.
Isingekuwia rahisi kuamini kwamba yaliyotoka kinywani mwake kwa minajili ya kuingia katika masikio ya baba yake mzazi! Kiasi Alwatan Dafu aliona aibu akatahayari na kutazama pembeni.
Alivunga kwa hili na lile kabla hayajashusha pumzi ndefu na kusema “Oke, hayo tuyaache yashamwagika hayazoleki tena. Vipi kuhusu Saadan, anasema bado anakupenda licha ya yote yaliyotokea yuko tayari pia kukuoa na kuwalea watoto wako iwapo utakubali kwenda kuishi nae Oman. Unasemaje Nasra mwanangu?”
Nasra akaachia tabasamu dogo, akageuka na kumtazama Saadan, alikuwa kijana mzuri sana ingawa kwake hakuwa na mvuto kama ule aliokuwa nao Promota Halfan.

***NASRA amekolea na anamtetea promota…hataki kusikia juu ya Saadan…..
****Nini kitaendelea???
****Shania ni nani????

No comments:

Post a Comment

Recent Posts