Sunday, April 7, 2013

RIWAYA: PAINFUL TRUTH (UKWELI WENYE KUUMA)============ 4

 

MTUNZI: Nyemo Chilongani

MAWASILIANO: 0718 06 92 69


SEHEMU YA NNE

Maisha ya Happy hayakuwa na furaha tena hali iliyompelekea kuondoka nyumbani kwa shangazi yake na kurudi nyumbani kwao Machame. Kichwa chake kilikuwa kikifikiria kuhusu mimba ambayo alikuwa nayo, hakujua ni kitu gani ambacho angekifanya mpaka kuanza kuwaeleza wazazi wake kuhusiana na mimba ile.
Moyo wake ulikuwa ukimuuma, akaanza kumchukia Wayne ambaye alikuwa amempa ujauzito ule na kisha kuondoka kurudi nchini Marekani. Alijiona kuwa mpweke, akakosa amani kabisa.
Mpaka katika kipindi ambacho alikuwa akiingia nyumbani kwao, Happy alikuwa akilia tu. Wazazi wake, Mzee Lyimo na Bi Vanessa wakabaki wakimshangaa Happy, hawakujua ni kitu gani ambacho kilikuwa kikimliza binti yao katika kipindi hicho.
Kila walipojaribu kumuuliza Happy kitu ambacho kilikuwa kimetokea, alikuwa kimya, hakutaka kuwaambia wazazi wake kitu ambacho kilikuwa kimetokea katika kipindi ambacho alikuwa jijini Arusha. Alibaki kimya, siri ya kwamba alikuwa mjauzito ikabakia moyoni mwake.
Siku zikakatika mpaka katika kipindi ambacho matokeo ya kidato cha nne yalipotangazwa. Happy alikuwa amefanya vizuri sana zaidi ya wanafunzi wote wa Machame Girls Secondary School. Matokeo hayo yaliinua furaha kwa wazazi wake,
Kitu kilichowashangaza ni pale walipompa Happy matokeo yale. Badala ya Happy kuwa na furaha hata zaidi ya wao waliyokuwa nayo, akaanza kulia kwa uchungu. Kitendo kile kikaonekana kuwashangaza wazazi wake jambo ambalo liliwapelekea kumuuliza sababu ilikuwa nini. Happy hakutaka kuongea kitu chochote kile, tayari wazzi wake wakajua kwamba kulikuwa na tatizo limetokea.
“Kaongee nae. Nadhani ana tatizo” Mzee Lyimo alimwabia mkewe.
Bi Vanessa hakuwa na jinsi, alichokifanya ni kuanza kuelekea chumbani kwa Happy na kuanza kuongea nae. Alichukua saa moja kuongea nae lakini Happy hakuwa tayari kuufungua mdomo kueleza ni kitu gani ambacho kilikuwa kimetokea.
Bi Vanessa alitumia ujuzi wake wote na hatimae Happy kumwambia ukweli. Bi Vanessa akaonekana kama mtu aliyechanganyikiwa, hakuonekana kuyaamini maneno yale, alimwangalia binti yake mara mbili mbili huku akionekana kutokuamini.
“Una mimba?” Bi Vanessa aliuliza huku akionekana kutokuamini.
“Ndio” Happy aijibu huku akiangalia chini.
“Ya nani?”
“Wayne”
“Ndiye nani?”
“Mvulana mmoja hivi”
“Anakaa wapi? Hapa hapa Machame au Arusha?” Bi Vanessa aliuliza.
“Anakaa Marekani”
“Marekani!”
“Ndio”
Bi Vanessa hakutaka kubaki ndani ya chumba hicho, alichokifanya ni kutoka na kisha kwenda kumwambia mumewe, mzee Lyimo.
Mzee Lyimo akaonekana kuchanganyikiwa, hasira zikaanza kumshika, akaanza kuondoka kumfuata Happy chumbani kwake. Alipoingia tu, akajikuta hasira zake zote zikipotea haa mara baada ya kuyaona machozi ya Happy ambayo yalikuwa yakimtoka mfululizo.
Mzee Lyimo akaanza kupiga hatua kumfuata Happy pale kitandani alipokuwa na kisha kukaa karibu nae. Moyo wake ukaonekana kuumia, alijua kwamba alitumia kiasi kikubwa sana cha fedha kumsomesha Happy mpaka kufikia hatua hiyo ambayo alikuwa mefikia, kupata ujauzito hata kabla hajaendelea na masomo kulionekana kumuumiza.
Alijua fika kwamba kumchapa Happy au kumfukuza nyumbani isingekuwa suluhisho la kile ambacho kilikuwa kimetokea, aliona kuwa na umuhimu wa kuwa pamoja na Happy na kumfariji katika hali ambayo alikuwa nayo katika kipindi hicho.
“Wayne ndiye nani?” Mzee Lyimo aliuliza japokuwa alikuwa ameambiwa kila kitu na mkewe.
“Mwanaume kutoka Marekani” Happy alijibu.
“Ni mzungu?”
“Ndio” Happy alijibu.
Mzee Lyimo akaonekana kukosa nguvu, alichokifanya ni kuinuka mahali hapo na kwenda nje. Hakujua ni kitu gani ambacho alitakiwa kukifanya, kupata ujauzito kwa Happy kulionekana kumnyima furaha kabisa.
Huo ndio ukawa mwisho wa Happy kusoma, hakuendelea tena na elimu, akawa msichana wa kukaa nyumbani na kuwasaidia wazazi wake kazi mbalimbali hasa shambani. Miezi ilikuwa ikiendelea kukatika, Happy alikuwa akiutunza ujauzito wake huku wazazi wake wakimpa kila msaada ambao alikuwa akiuhitaji.
Dalili zote za kuwa mjamzito zikaanza kuonekana, akaanza kutapika mfululizo huku akipoteza hamu ya kula. Muda mwingi alikuwa akijisikia uchovu hali iliyompelekea kulala. Mpaka miezi mitano inatimia, hali ya ujauzito ikaanza kuonekana waziwazi.
Happy alikuwa amelala chumbani kwake huku pembeni yake kukiwa na maembe mabichi pamoja na udongo. Hivyo ndivyo vilikuwa vitu ambavyo alikuwa akipenda sana kuvitumia kila siku. Mara mama yake akaingia chumbani humo, uso wake ulikuwa umejaa tabaamu pana.
Maswali mfululizo yakaanza kujikusanya kichwani mwa Happy, hakujua sababu iliympelekea mama yake kuwa na tabasamu namna ile. Akainuka kitandani na kukaa. Mama yake akaja na kukaa pembeni yake huku tabasamu likiendelea kuonekana usoni mwake.
“Kuna nini?” Happy aliuliza.
“Amekuja” Bi Vanessa alijibu.
“Nani?”
“Wayne. Yupo nje anakusubiri” Bi Vanessa alimwambia Happy.
Badala ya kuonyesha furaha, Happy akaanza kutokwa na machozi. Hali ile ilionekana kumshangaza mama yake ambaye akaamua kuanza kumbembeleza. Alipoona Happy amenyamaza, akatoka chumbani mule na moja kwa moja kwenda kumuita Wayne ambaye alikuwa nje ya nyumba lle.
Ni ndani ya sekunde kumi tu, mlang wa chubani ukafunguliwa na Wayne kuingia ndani. Usowa Wayne ukaonekana kuwa na furaha mara baada ya kumuona Happy kwa mara nyingine tena. Huku akionekana kuwa na tabaamu pana, akakaa kitandani pale.
Happy akashindwa kuvumilia, akajikuta akimsogelea Wayne na kumkumbatia kwa furaha huku machozi yakiendelea kumtoka. Wayne akaipitisha mikono yake na kumkumbatia. Walikaa katika hali hiyo kwa dakika mbili, Wayne akayapeleka macho yake usoni mwa Happy, akaonekana kufarijika.
“Nimekukumbuka mpenzi” Wayne alimwambia Happy.
“Nimekukumbuka pia” Happy alijibu.
Furaha ya Wayne ikaonekana kurudi moyoni mwake, tayari alikuwa amekwishasahau kama alikuwa amemuacha Kristen hotelini. Alikaa pamoja na Happy kwa muda wa masaa mawili na ndipo walipoanza kupiga stori.
“Mbona ulikimbia chumbani siku ile?” Wayne alimuuliza Happy.
“Nilikuwa nikiogopa, kuna kitu nilikuwa nimekikumbuka” Happy alijibu.
“Kitu gani?”
“Kwamba nilikuwa katika siku zangu za kupata mimba” Happy alitoa jibu ambalo likaonekana kumshtua Wayne.
“Unasemaje?”
“Nilikuwa katika siku zangu za kupata mimba. Hapa unaponiona, nina ujauzito wako” Happy alimwambia Wayne.
Wayne akaonekana kushtuka, akamwangalia vizuri Happy, akaipandisha blauzi ambayo alikuwa ameivaa na kisha kuliangalia tumbolake, aliona mabadiliko makubwa lakini cha ajabu katika kipindi ambacho alikuwa akifanya nae mapenzi hakuyaona mabadilko hayo.
Wayne akaonekana kubadilika, wasiwasi ukaanza kuonekana machoni mwake, hakuamini kama alikuwa amempa ujauzito msichana wa kiafrika, akamwangalia Happy huku dhahiri uso wake ukionekana kuukataa ujauzito ule.
Wayne akainuka, akaanza kuvaa nguo zake na kuufungua mlango, kilichoendelea mahali hapo ni kuondoka huku akiwa kama mtu aliyechanganyikiwa. Hakujua ni kitu gani alitakiwa kukifanya, moyo wake haukuwa tayari kukubali kama alikuwa amempa mimba msichana wa Kiafrika.
“Haiwezekani. Ile sio mimba yangu. Siwezi kumpa mimba msichana wa Kiafrika” Wayne alisema katika kipindi ambacho alikuwa akielekea kituoni huku akiwaacha watu nyumbani pale wakiwa hawaelewi ni kitu gani ambacho kilikuwa kimetokea ndani ya chumba kile.
Wayne alifika hotelini baada ya saa moja. Kristen alikuwa na wasiwasi akimsubiri. Japokuwa Kristen alionekana kuwa na wasiwasi lakini hakuuliza kitu chochote kile. Tayari Wayne alikuwa amebadilika, uso wake ukaonekana kuwa na hasira kupita kawaida, kitendo cha kumpa mimba msichana wa Kiafrika kilionekana kumuumiza.
“Kuna nini?” Kristen alijikuta akiuliza.
“Tuondoke. Inatupasa turudi nyumbani haraka iwezekanavyo” Wayne alimwambia Kristen.
“Unasemaje? Mbona ni maamuzi ya haraka namna hiyo?”
“Ndio hivyo. Nakuomba usiulize kitu Kristen. Nimechanganyikiwa baada ya kusikia kwamba marafiki zangu kutoka Uingereza wameelekea Marekani tayari kwa kuhudhuria harusi yetu” Wayne alidanganya.
“Harusi gani? Mbona unaonekana kama umechanganyikiwa?”
“Ni lazima tufunge harusi haraka iwezekanavyo. Huo ni uamuzi ambao nimejiwekea. Najua ni uamuzi ulioamuliwa kwa haraka sana. Haina jinsi mpenzi. Wiki ijayo ni lazima tufunge ndoa” Wayne alimwambia Kristen.
Ni kweli. Ulikuwa ni uamuzi wa haraka sana, Wayne alionekana kuchanganyikiwa. Taarifa za ujauzito ambazo alikuwa amepewa zilionekana kumchanganganya kupita kawaida. Siku mbili zilizofuata, wakasafiri na kurudi tena nchini Marekani ambako huko mipango ya harusi ikaanza kufanyika.
Kila kitu kilikuwa kimepangwa kwa haraka haraka sana hali ambayo ilikuwa ikimshangaza kila mtu. Vyombo vya habari vikaanza kutangaza harusi kubwa ambayo ilitarajiwa kufanyika wiki ijayo. Kila mtu akawa na hamu ya kuiangalia harusi hiyo kwenye televisheni.
“Ni bora nioe ili nimsahau Happy. Haiwezekani kuzaa na msichana wa Kiafrika” Wayne alisema.
Kitu walichokifanya ni kuanza safari ya kuelekea Elmon, mji mdogo uliokuwa pembeni mwa jiji la New York kwa ajili ya kuwaona babu na bibi wa mchumba wake, Kristen kwa ajili ya kuwapa taarifa kile ambacho kilikuwa kinataka kutokea.
Ndani ya gari walikuwa wawili tu, Wayne na Kristen. Wayne ndiye ambaye alikuwa ameshikilia usukani, alikuwa akiendesha kwa mwendo wa kasi sana kwani alihitaji wafike katika mji huo haraka iwezekanavyo.
Bado kichwa chake hakikuwa sawa, muda wote alikuwa akimfikiria Happy na ujauzito ule ambao alikuwa nao. Mara kwa mara alikuwa akipiga usukani ule kuonyesha ni kwa jinsi gani alikuwa amechanganyikiwa.
“Happy.....haiwezekani...” Wayne alijikuta akisema kwa sauti kubwa iliyosikiwa na Kristen.
“Umesemaje?” Kristen aliuliza.
“Nini?” Wayne nae aliuliza.
“Nimekusikia umeongea kitu”
“Kitu gani?” Wayne aliuliza.
Bado Wayne alikuwa akiendesha gari kwa mwendo wa kasi hadi kutokukiona kibao ambacho kilimtaka kuendesha gari kwa mwendo wa taratibu kutokana na matengenezo ya barabara. Ghafla, mbele yake akaona gari kubwa likichimba barabara ile huku mainjiania wakitoa malelekezo kwa dereva wa gari lile kubwa la kutengeneza barabara.
Kutokana na mwendo mkali ambao walikuwa nao, ikawa ngumu kufunga breki na gari kusimama. Gari lao ambalo lilikuwa katika mwendo wa kasi likalivamia gari lile kubwa lililokuwa likitengeneza barabara.
Mlio mkubwa ukasikika, Kristen akarushwa kutoka ndani ya gari mpaka nje na kukibamiza kichwa chake katika chuma kikubwa cha gari lile lililokuwa likitengeneza barabara ile. Na Wayne akarushwa mpaka nje, akaburuzika katika marabara ile, sehemu kubwa ya ngozi yake tumboni ikabaki barabarani.
Ilikuwa ni ajali kubwa ambayo wala haikuwa na moyo kuitazama. Gari lao lilikuwa limebondeka, milango ya mbele haikuwa ikionekana kabisa, yaani gari lilikuwa limebaki nusu tu kuanzia milango ya nyuma.

Je nini kitaendelea?
Je huo ndio mwisho wa Kristen na Wayne?
Je nini kitaendelea katika maisha ya Happy?
Itaendelea.

No comments:

Post a Comment

Recent Posts