Sunday, April 7, 2013

RIWAYA: PAINFUL TRUTH (UKWELI WENYE KUUMA)----------3

MTUNZI: Nyemo Chilongani

MAWASILIANO: 0718 06 92 69

SEHEMU YA TATU


“Nitachagua wa kumuoa hapo baadae. Ila hata Happy nae anafaa sana. Mmh! Wazazi watanielewa vipi kama nikimuoa? Kwanza hawamjui hata mara moja, wataweza kuniunga mkono katika maamuzi yangu? Mmh! Huo nao uamuzi mgumu” Wayne alijisemea wakati ndege ikiwa imekwishafika katika ardhi ya Morocco tayari kwa kuendelea na safari ya kuingia Ulaya na kisha kuelekea Marekani.


Jina la Brown Michael Ryn lilikuwa jina kubwa miongoni mwa matajiri ambao walikuwa wakipatikana nchini Marekani. Mzee huyu alikuwa akimiliki miladi mikubwa nchini Marekani pamoja na mingine iliyokuwa katika mataifa makubwa kama Uingereza, Urusi na Ufaransa.
Huyu ndiye alikuwa mwasisi wa shirika la ndege la American Airways, ndiye alikuwa akimiliki kiwanda kikubwa cha kutengeneza makaratasi cha Brown Paper Company Limited, huyu ndiye ambaye alikuwa akiimiliki kampuni kubwa ya kutengeneza magazeti ya Independent ambayo yalikuwa yakitoka mara mbili kwa wiki nchini Marekani.
Tofauti na vitega uchumi hivyo, pia alikuwa na kampuni nyingi pamoja na visima vya mafuta nchini Qatar. Jina lake lillikuwa kubwa na kila siku alikuwa akiingiza kiasi kikubwa cha fedha katika maisha yake.
Mpaka inafika mwaka huo wa 1990, Bwana Brown alikuwa ameingiza kiasi cha dola bilioni sabini katika mwaka huo na kumfanya kuwa tajiri namba kumi na nane duniani. Maisha yake siku zote yalikuwa yametawaliwa na fedha, alikuwa akithamini sana fedha kuliko kitu kingine chochote kile.
Miaka ya nyuma katika kipindi ambacho alikuwa na umri mdogo, alikuwa kijana masikini ambaye alifiwa na wazazi wake na kuachwa akiwa hana kitu. Mchezo wa kamari wa Pluto Game ndio ambao ulimpatia fedha kiasi cha dola elfu themanini ambazo akazifanyia biashara ambayo ikaanza kumuingizia fedha.
Maisha yake yakabadilika na kumfanya kuongeza jitihada kwa kila biashara ambayo alikuwa akiifanya. Ni ndani ya mwaka mmoja tu, akafanikiwa kumiliki hisa ya asilimia arobaini katika kampuni ya kutengeneza magari ya Mc Lloyd.
Alipofikisha miaka ishirini na mbili akaamua kumuoa mwanamke mzuri, Ruth ambaye aliishi nae kwa miaka minne na kuachana nae. Hapo ndipo alipoamua kutulia ila baada ya miaka miwili akamuoa mwanamke mmoja ambaye alikuwa akiitwa Lydia.
Huyu ndiye ambaye alikuwa amedumu nae katika ndoa mpaka kumpatia watoto wawili, Wayne na msichana Esther. Watoto hawa ndio ambao walikuwa kila kitu katika maisha yake, aliwathamini kuliko hata alivyozithamini biashara zake.
Kijana wake, Wayne alionekana kuwa tofauti sana na watoto wa matajiri wengine. Yeye alikuwa akiishi maisha ya peke yake, kamwe hakuwahi kuchangamana na watoto wa matajiri. Maisha yake yalikuwa mitaani pamoja na watoto weusi ambako alikuwa akikaa nao na jioni kurudi nyumbani.
Maisha yake yalikuwa yakimkasirisha baba yake, kila siku alikuwa akimkaripia na hata kumpiga lakini Wayne hakuonekana kubadilika. Bwana Brown akaonekana kuchoka, akaamua kumuacha Wayne kuishi maisha ambayo alikuwa akitaka kuishi.
Hata Wayne alipoamua kumleta mchumba wake, Luciana, Bwana Brown akaonekana kukasirika. Kamwe hakutaka mtoto wake awe katika uhusiano na msichana yeyote wa kimasikini, alihitaji kijana wake awe katika uhusiano na msichana yeyote kutoka katika familia ya kitajiri.
Hapo ndipo alipoanza mipango yake ya chini chini kuhakikisha kwamba Wayne anaingia katika uhusiano na msichana yeyote kutoka katika familia ya kitajiri. Akafanikiwa kumuunganisha Wayne na msichana Kristen ambaye alikuwa ametoka katika familia ya kitajiri.
Wayne na Kristen wakaanza kuzoeana na hatimae kuanzisha uhusiano ambao ulionekana kuwafurahisha wazazi wao. Mipango ya harusi ikaanza kufanyika taratibu. Kila tarehe ya harusi ilipokuwa ikikaribia, harusi ilikuwa ikihahirishwa kwa sababu ambazo hazikujulikana vizuri.
Wayne akaonekana kukasirika, na hapo ndipo alipoamua kuomba muda wa kupumzika kwenda katika nchi yoyote abayo ilikuwa na vivutio vizuri. Hapo ndipo alipoisoma Tanzania katika ramani ya dunia na kuamua kuja nchini Tanzania.
Akatamani kuziona mbuga za wanyama ambazo zilikuwa zikitangazwa sana pamoja na mlima mrefu kuliko milima yote barani Afrika. Akasafiri tena akiwa peke yake, japokuwa baba yake alikuwa akimtaka atumie ndege ya kukodi lakini akaonekana kukataa kabisa.
Kwa sasa alikuwa ndani ya ndege kurudi nchini Marekani. Kichwa chake wala hakikutulia kwa mawazo, wasichana wawili ambao walikuwa kichwani mwake walionekana kumchanganya kupita kawaida.
Ndege ikaanza kupaa kutoka katika uwanja wa ndege wa Morocco na kuingia katika nchi za Ulaya. Kitu ambacho alikuwa akikitaka Wayne ni kufika nchini Marekani haraka iwezekanavyo ili apate kujua ni kitu gani alitakiwa kukifanya kwa wakati huo ambao mchumba wake alikuwa katika matatizo makubwa.
Kutoka nchini Morocco mpaka nchini Marekani, alitumia masaa ishirini na mbili na ndipo ndehe ikaanza kutua katika uwanja wa ndege jiji New York. Mara baada ya ndege kusimama, abiria wakaanza kuteremka na kuanza kupiga hatua kuelekea ndani ya jengo la uwanja huo wa ndege ambako baada ya mizigo yao kuchunguzwa, wakaichukua na kutoka nje.
Gari aina ya BMW ilikuwa ikimsubiri nje, alipoifikia, akaingia ndani ya hiyo gari na kisha safari ya kuelekea Eastchester kuanza huku ikiwa imetimia saa tano asubuhi. Ndani ya gari Wayne hakuonekana kuwa na furaha, muda wote alikuwa akimfikiria Kristen.
Gari likasimama nje ya jengo kubwa lililojengwa katika eneo kubwa lililokuwa na ukubwa wa mita mia moja na ishirini kwa urefu na upana wa mita sabini. Geti likajifungua na gari kuingizwa ndani. Wayne akateremka na kuanza kuelekea ndani ya nyumba hiyo.
Wazazi wake hawakuwepo, ni wafanyakazi wa ndani tu ndio ambao walikuwa wakizunguka zunguka ndani ya nyumba ile. Alipoulizia mahali walipokuwa, aliambiwa kwamba walikuwa katika hospitali ya St’ Mathew ambako mchumba wake, Kristen alikuwa amelazwa.
Wayne akatoka ndani ya nyumba ile, akaanza kuelekea katika sehemu za kupakia magari na kisha kulichukua gari lake aina ya Aston Martin na kuanza safari ya kuelekea katika hospitali hiyo ambayo ilikuwa kusini mwa jiji la New York karibu kabisa na bandari ya Hamilton.
Mawazo juu ya Happy yakafutika, Kristen ndiye ambaye alikuwa akimfikiria sana kwa wakati huo. Aliendesha gari kwa mwendo wa kasi, shida yake ilikuwa ni kutaka kufika hospitalini haraka iwezekanavyo. Ni ndani ya dakika thelathini tu, akawa analipaki gari lake katika eneo la hospitali hiyo.
Kwa haraka sana akateremka na kuanza kupiga hatua kuelekea ndani ya jengo la hospitali hiyo, sehemu ya kwanza kwenda ilikuwa mapokezi, akamulizia mgonjwa wake. Dada wa mapokezi akachukua kipanya cha kompyuta na kuanza kukipeleka huku na kule huku macho yake yakiwa katika kioo cha monita ya kompyuta.
Akaliandika jina la ‘Kristen’ na kisha kompyuta yenyewe kuanza kutafuta. Wayne alikuwa kimya akimwangalia yule dada wa mapokezi kwa jinsi alivyokuwa akicheza na kompyuta yake. Ni ndani ya sekunde kumi na tano tu, akaonekana kukipata kile alichokuwa akikitafuta.
“Yupo chumba namba 108 katika ghorfa ya sita” Dada yule alimwambia Wayne.
Wayne hakutaka kupoteza muda wake, alichokifanya ni kupanda lifti na kisha kuanza kuelekea katika ghorofa hiyo ambayo alikuwa ameelekezwa. Bado kichwa chake hakikutulia kabisa, mawazo juu ya Kristen yalikuwa yakimtesa kupita kawaida.
Alipofika katika ghorofa hiyo akateremka na kisha kuanza kupiga hatua kukitafuta chumba hicho. Alipokifikia, akakishika kitasa na kuanza kuufungua mlango. Kwa kuwa muda wa kuona wagonjwa ulikuwa umefika, akaruhusiwa kuingia.
Macho yake yakatua kitandani, Kristen alikuwa kimya kitandani pale huku mashine ya Oksijen ikiwa imefunika pua na mdomo wake. Wayne akajikuta akiishiwa na nguvu, akaanza kupiga hatua kuelekea katika kitanda kile.
Japokuwa pembeni ya kitanda kile walikuwepo wazazi wake pamoja na wazazi wa Kristen lakini yeye wala hakuonekana kuwaona, mtu aliyekuwa akimuona kwa wakati huo alikuwa Kristen tu. Alipokifikia kitanda kile, akapiga magoti chini, akauchukua mkono wa Kristen na kuubusu.
“Usiniache mpenzi...” Wayne alisema.
Machozi yakaanza kumtoka na kutiririka mashavuni mwake, hali ambayo alikuwa nayo Kristen ilionekana kumuumiza kupita kawaida. Katika maisha yake, ugonjwa wa pumu ndio ambao alikuwa akiuchukia kuliko ugonjwa wowote kwa kuwa ulikuwa ukimkosesha amani kupita kawaida.
“Lakini kwa nini mimi? Mbona maisha yangu ya uhusiano hayana furaha kabisa? Mbona kila siku ni mimi tu. Nani ameichukua furaha yangu?” Wayne alikuwa akijiuliza.
Akashikwa bega lake kwa nyuma, alipoyageuza macho yake, alikuwa baba yake, Bwana Brown. Wayne akasimama na kisha kumkumbatia baba yake huku akilia tu. Mama yake, Bi Lydia nae akawasogelea na kisha kuwakumbatia. Wote walionekana kuumizwa na hali ile ambayo alikuwa nayo Kristen, kila siku sala zao zilikuwa ni kutaka Kristen apone kabisa ugonjwa ule.
Wazazi wa Kristen ambao walikuwa pembeni nao wakawasogelea na kuwakumbatia. Wote walionekana kuumizwa na hali ambayo alikuwa nayo Kristen, kwao waliona kwamba muda wowote ule msichana yule angepoteza uhai wake.
Walihangaika katika kila hospitali huku wakijitahidi kutumia kila aina ya dawa ambayo waliambiwa watumie lakini wala hali ya Kristen haikubadilika, kila siku alikuwa vile vile. Wote wakakata tamaa na maisha ya Kristen, sala zao ambazo kila siku walikuwa wakisali zikaonekana kukosa majibu kutoka kwa Mungu wao.
Kristen akakaa katika hospitali ile kwa muda wa wiki mbili, akaruhusiwa kurudi nyumbani huku akionekana kuwa mzima wa afya. Hatua hiyo ikaonekana kuwa ya furaha kwa Wayne ambaye alionekana kumthamini sana katika maisha yake.
Miezi mitano ikapita. Kitu alichokipanga pamoja nae ilikuwa ni kusafiri kuelekea nchini Tanzania huku sababu yake kubwa ikiwa ni kutaka kumuonyeshea mbuga mbalimbali za wanyama pamoja na kuuona mlima mkubwa kuliko wote barani Afrika.
Kristen hakutaka kupinga, kwake, matembezi ndio yalikuwa moja ya maisha yake. Akamkubalia mpenzi wake kwa moyo mmoja kusafiri nae kuelekea nchini Tanzania. Moyoni hakujua kwamba Wayne alitamani sana kuelekea nchini Tanzania kwa sababu moja tu, kumuona Happy ambaye tayari alikwishaanza kurudi kichwani mwake kwa kasi ya ajabu.
Siku tatu zilizofuata walikuwa ndani ya ndege ya Amerian Airlines wakianza safari ya kuelekea nchini Tanzania. Ndani ya ndege walikuwa wakiongea mengi lakini mudaa wote Wayne alikuwa katika mawazo mazito juu ya Happy.
Walichukua masaa ishirini na saba, ndege ikaanza kutua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwl Julius Kambarage Nyerere. Wakateremka na kisha kukata tiketi ya ndege ya siku hiyo ya shirika la Precious kwa ajili ya safari ya kuelekea jijini Arusha ambako huko wangetembelea sehemu mbalimbali za mbuga za wanyama na pia kusafiri mpaka Kilimanjaro ambako wangeupanda mlima Kilimanjaro.
Ndani ya saa moja, ndege ya shirika la Precious ilikuwa ikitua katia uwanja wa ndege wa KIA ambako wakachukua teksi iliyowapeleka mpaka Arusha mjini ndani ya hoteli ya nyota tano ya Chui Chui.
Kila mmoja akaonekana kuwa na furaha, walitembea sehemu mbalimbali wakiwa pamoja huku wakinunua vinyago vingi kwa ajili ya kurudi navyo nchini Marekani. Katika vipindi vyote hivyo, Wayne alikuwa na mawazo ya kuonana na Happy tu.
Asubuhi iliyofuata, saa moja akaamka na kuanza kuvaa nguo zake. Kitu alichokuwa akikitaka ni kuondoka na kuelekea kwa shangazi yake Happy ambapo angemuulizia Happy na kuonana nae. Hata kabla Kristen hajaamka, Wayne akaamka na kuanza safari ya kuelekea huko huku akihakikisha kwamba Kristen hakumuona katika kipindi ambacho aliondoka.
Njia nzima Wayne alikuwa na mawazo juu ya Happy. Aliukumbuka uzuri ambao alikuwa nao msichana huyo, kwake alionekana kuwa msichana wa ajabu ambaye hakustahili hata siku moja kukaa nchini Tanzania.
Alifika katika nyumba hiyo, Bi Selina alikuwa nje akifagia uwanja wa nyumba hiyo kwa kutumia ufagia mkubwa. Uso wa Wayne ukajaa tabasamu, kitendo cha kumuona Bi Selina kwake kikaonekana kumfariji kupita kawaida. Wakasalimiana kwa furaha hadi kukumbatiana.
“Aliondoka kuelekea nyumbani kwao” Bi Selina alimwambia Wayne.
“Siwezi kumuona kwa siku ya leo?” Wayne aliuliza huku akionekana kuwa na kiu ya kutaka kumuona Happy.
“Inawezekana. Inabidi tuondoke hata asubuhi hii. Ni mwendo wa dakika ishirini tu hadi kufika kwao kwa daladala” Bi Selina alimwambia.
Hakukuwa na kitu cha kusubiri, alichokifanya Bi Selina ni kujiandaa na kisha kuanza safari ya kueleka, Machame, Kilimanjaro. Ingawa ndani ya gari walikuwa wakiongea lakini Wayne alionekana kuwa na mawazo. Kitu cha kwanza alikuwa akimfiria Happy lakini kitu cha pili alikuwa akifikiria kuhusu Kristen katika kipindi ambacho angeamka na kumkosa kitandani.
“Nitahitaji kumuona tu ili mladi kiu yangu ikatike na hata ikiwezekana nifanye nae tena” Wayne alikuwa akijisemea moyoni katika kipindi ambacho safari ilikuwa ikiendelea.


Je nini kitaendelea?
Je Wayne ataweza kumuona Happy?
Je nini kitatokea baada ya wawili hawa kuonana?
Itaendelea.
 


No comments:

Post a Comment

Recent Posts