Thursday, April 4, 2013

RIWAYA: MREMBO ALIYEPOTEA-------- 4

SEHEMU YA NNE

...
Tatizo la kutokuweza kupata mtoto liliendelea sana kumsumbua John Mapunda. Pesa nyingi alizokuwa akizipata kupitia kazi yake ya kusimamia shughuli za urembo hazikuweza kumpa furaha ya nyumba kabisa. Toka alipofunga ndoa na mkewe Janet miaka mitatu iliyopita alizidi kukosa furaha ndani ya nyumba kutokana tatizo la mkewe kutokushika ujauzito. Mwanzoni alijihisi pengine tatizo litakuwa upande wake lakini haikuwa hivyo. Kila hospitali aliyokuwa akiongozana pamoja na mkwewe kujua nani ana tatizo jibu lilikuja pale pale kuwa mkewe John, Janet ni mgumba na kamwe hawezi kupata mtoto. Furaha ya nyumba ikaanza kubadilika siku baada ya siku ndani ya miaka mitatu. John akawa ni mtu wa kulewa na kutembea na wasichana ovyo.
Maisha yake yote sasa akawa ameyahamishia kwenye wanawake. Mwanzoni alifanya kama siri kutembea na wanawake tofauti lakini mwishowe alijionesha dhahiri kutembea na kila mwanamke amtakaye mbele ya mkewe. Hali ile ya John kubadilika kulimuumiza sana mkewe janet. Janet alijihisi ni mtu mkosaji duniani, alijutia ndoa waliyofungishwa kanisani miaka mitatu iliyopita. Uzuri aliokuwa nao Janet na unyenyekevu ilikuwa jibu tosha kwa aliyemuona. Kuimba kwaya kanisani ndio kazi aliyokuwa ameichagua katika maisha yake ya kumtolea Mungu kupitia kipaji alichokuwa nacho. Janet hakuwa na kazi ya maana zaidi ya kujiendesha kwa biashara za mikononi ambapo alikuwa akikopesha kinamama wenzake nguo za watoto na kulipwa baada ya wiki mbili hadi tatu. Kuimba kwake kwaya kulimfanya ajiepushe na mengi japo siri kubwa alimganda moyoni kuwa hana uwezo wa kushika ujauzito. Janet alifanya kila njia kuhakikisha anamuweka mumewe John katika hali ya kutokujisikia tofauti kwa kutopata watoto na akiamini kuwa ipo siku Mungu atawashushia Baraka na watapata mtoto wa maisha, Alihangaika sana kwenda kwenye semina mbali mbali za maombezi na kuombewa sana lakini bado hakuwa na dalili yeyote ya kuondoka ugumba wake. Siku, wiki, Miezi, miaka ilizidi kukatika bila mafanikio yeyote kwa Janet. Kipindi hiki sasa John ndio akaamua kuzidisha ule umalaya aliokuwa akiifanya mwanzo. Kwake kutembea na wanawake hata watatu kwa siku na kuwahonga lilikuwa ni jambo dogo sana. Ushauri aliokuwa akipata kutoka kwa baadhi ya marafiki zake juu ya tabia yake hiyo alikuwa akiupuuzia na hata mwingine kuuweka kichwani japokuwa alikuwa mzito sana katika kuufanyia kazi. Taratibu John akaanza kubadilika. Sasa akawa anatembea na mwanamke mmoja tu. Nusu ya mshahara wake akawa anagawana na mwanamke huyo. Hakuwa mwingine bali alikuwa ni Angel. John alijivunia sana kumpata Angel katika maisha yake na akiamini kuwa atamfanya nyumba ndogo na kumuahidi kuwa endapo atamzailia mtoto basi nusu ya mali zake zitakuwa mikononi mwa Angel . John alifanya siri kubwa kutembea na Angel na hata makutano yao mara nyingi yalikuwa ni hotel maarufu pale kariakoo ya Royal Image mtaa wa Livingsotne na hakutaka kabisa kwenda kwa Angel kwani aliamini angefuatiliwa na mkewe hivyo kungemletea matatizo Angel na mkewe Janet. Angel ambaye alizoea kutembea na wanaume wengi sasa akawa ameachana nao baada ya kumpata John na kumpa kila alichokitaka, na hata pesa za kuhama alipokuwa akikaa zamani ni John pekee ndio alizozitoa. Angel hakupenda kabisa kumshirikisha wala kumjulisha mdogo wake Alice juu ya kutembea na john na ahadi walizoahidiana. Hata kipindi walichokuwa wakitoka wote katika matembezi ya pamoja Alice alikuwa akimuona tu John akiwa karibu na Angel lakini hakujua ndani yao kuna kitu gani. Ilimchukuwa wiki chache tu Angel kunasa mimba ya John na hata John mwenyewe alipopewa taarifa juu ya kushika hiyo mimba hakuamini mpaka alipokutana naye hotelini wanapokutana na kumkimbiza hospitali nakugundua kuwa kweli Angel ni mjamzito wa wiki chache. Furaha ya ajabu ilimtanda John, siri kubwa alikuwa nayo na hakutaka hata rafiki wala mkewe Janet wajue mpaka Angel atakapojifungua.
Kadri siku zilivyokuwa zinasonga ghafla mawasiliano ya John na Angel yakakatika ghafla. Na ni Angel pekee ndio aliyoyavunja mahusiano hayo kwa haraka baada ya hali kumzidia juu ya ugonjwa wa ukimwi uliokuwa ukimsumbua. Hakutaka kuiona hata simu ya John ikiita kwani aliamini angekosa cha kujieleza kutokana na kuwa hoi kitandani. Kutokana na kuendelea kukaa kimya kukamuharibu kabisa John kisaikolojia, ule utendaji wa kazi ukaanza kupungua kazini kwao. Siku zote alijiona kama msaliti asiye na bahati hapa duniani. John hakujua aanzie wapi kumtafuta kipenzi chake Angel. Alitembea usiku kumbi zote walizokuwa wakitembea wote bila kupata jibu haswa alipokuwa akiishi. Wazo likamjia kumtafuta rafiki yake wazamani sana na Angel ambaye alijulikana kwa jina la Miriamu. Alifanikiwa kuonana na Miriam kwenye mawindo yake usiku wa manane..
“Miriam bora nimekuona mambo rafiki?”
“Safi tu!!, niambie sasa, leo shosti wako hayupo twende wote tukalale basi?”
“Hapana Miriam!!, yani nipo hapa kujua tu anapoishi huyo Angel?, na kuhusu kulala na wewe haitawezekana ila nitakupa hela yako ya siku unayoingiza hapa!!”
“Daahh!!, sijui nianzie wapi kukueleza John, yaan nina muda mrefu sijui hata Angel yupo wapi na anafanya kazi gani kwa sasa kwani tangu kipindi kile unakuja kumchukuwa sijamuona tena na wala kwake nimepasahau kidogo”
John alizidi kunyong’onyea baada ya kuambiwa maneno hayo na Miriam.., akilli ilizidi kumchanganya hadi akaiona dunia chungu.
“Lakini Miriam alipokuwa akiishi zamani si unapakumbuka?”
“Ndio napakumbuka lakini si sana?”
“Basi mie nipeleke tu mpaka hapo halafu nitajua cha kufanya”
John aliingia kwenye gari na Miriam kisha safari ikaanza mpaka nyumba ya zamani alipokuwa akikaa Angel napo alipofika tu hakufanikiwa kupata jibu sahihi sehemu alipoamia kutokana na Angel pamoja na mdogo wake Alice kuwa viburi na wenye dharau kwa majirani wenzake. Sasa Shati la John likawa kama limetoka kufuliwa linasubiri kuanikwa. Mwili wote ulikuwa umetapakaa majasho japokuwa alikuwa akiendesha gari tena ndani yake mlikuwa na kipupwe.
..hatua tatu mbele na moja nyuma ndizo zilikuwa zimemtawala John huku akiutoa mikono wake mmoja nakuurusha juu mithili ya mchungaji akiwa madhabahuni akihubuiri. Akiwa bado nje ya ile nyumba aliyekuwa akiishi Angel zamani mara Miriam naye akashuka ndani ya gari na kumfuata John alipo..
“Mbona sikuelewi?, umeambiwaje?”
“Hapana Miriam, ni kwamba hawajui alipohamia Angel, na mie lazima nimpate leo leo sirudi kwangu”
Miriam hakuwa na roho ya huruma toka aanze kujijihusisha na biashara hii ya ukahaba, kwake kumdai mwanaume hadharani au kumkunja shati na kutaka kumpiga kwa kudai pesa kwake ni jambo la kawaida sana. Na sasa Miriam alikuwa ameshamvumilia John vya kutosha, lile giza lililokuwa linazidi kufunika ndilo lillikuwa linampa hasira zaidi Miriam na sasa alitamani pesa zote zote na alitaka achukue pesa kwa John aliohadiwa na vile vile arudi tena mawindoni kutafuta zingine.
“Haya mie msaada wangu umeishia hapa John, nipe changu nitambae?”
Bado sura ya John ilikuwa katika majonzi na kuchanganyikiwa kwa kile ambacho hakiamini juu ya mpenzi wake Angel anapoishi. Hakutaka kusikia maneno tena ya Miriam kwakuwa dhahiri alishaonesha kuchukizwa na kuchelewesha hivyo John alichukuwa mkono wake wa kulia nakuingiza ndani ya suruali yake kisha akachomoa shilingi elfu thelathini nakumpatia Miriam. Miriam alizipokea kisha akajigeuza kwa jicho la dharau na kuondoka zake. Ilimchukuwa nusu saa nzima John kuzubaa pale na majirani wale waliokuwa wakiishi na Angel zamani kwa kuwabembeleza kisha akaingia ndani ya gari nakuondoka zake. Ramani ambayo alibembeleza baadhi ya majirani wakampa sasa ilikuwa imehamia kichwani mwa John. Hofu yake ilikuwa juu ya mimba ambayo alimwachia Angel na aliamini sasa inazidi kukuwa. Alijipa moyo hata kama Angel atakuwa amepata bwana mwingine lakini yupo tayari kumlipia mtoto gharama zote ili mradi damu yake aliyoitafuta kwa miaka mingi isipotee bure. Dakika ishirini ndani ya gari zilimtosha John kutoka lile eneo la Tabata bima alipokuwa akiishi Angel zamani mpaka eneo jipya. Nyumba kubwa yenye uzio wa matofali huku ikilembwa kwa geti lenye kila aina ya urembo ndilo lilizuzua macho ya John. Kabla hajashuka kwenye gari john aliangalia kwanza saa yake lakini tayari ilikuwa inamuonesha imetimia saa tano za usiku, haraka haraka akashuka nakuongoza mpaka eneo la geti nakuanza kugonga. Hakukuwa na mlinzi yeyote, John alitumia dakika tano nzima kugonga bila ya majibu yeyote, ile hali ya hofu na uwoga vikaanza kumtawala nakujihisi huenda amedanganywa na wale majirani ama yeye mwenyewe amekosea ramani. Lakini kwa upande mwingine akawa anajipa moyo kuwa huenda Angel wake na mdogo wake wamelala kwakuwa usiku umeshaingia na tena mida inayoyoma. Ile hali ya kugonga taratibu alioanza nayo John sasa ikawa imebadilika, alichukuwa kipande cha jiwe na kugonga kwa nguvu lakini bado haikusaidia chochote, na sasa akawa ameshikilia geti la upande wa kuingilia huku akisukuma kwa ndani napo bado geti halikufunguka. Akili ikamjia kwenda pembeni yake ambapo kulikuwa na bar ambayo bado ilikuwa haijafugwa watu wanakunywa, moja kwa moja akamfuata muhudumu mkuu pale.
“Samahani Anti?”
“Bila samahani kaka!!”
“Eti nilikuwa naulizia hawa wanaoishi nyumba hiyo hapo wapo?”
John aliuliza kwa sauti ya uwoga na kutokujiamnini na anachouliza huku akionesha kutetemeka mwili wote.
“Unaulizia hao wadada weupe?”
John aliitikia kwa kichwa moja kwa moja na kwa haraka haraka.
“Mida ya asubuhi nilimuona yule mdogo akipita kashikilia mfuko mkubwa kama ametoka sokoni asubuhi ila huyo mkubwa hajaonekana muda kidogo anakaribu mwezi, kwani umeshawagongea hapo getini kwao?”
“Ndio, nimepiga hodi sana lakini hakuna majibu yeyote ya mtu kuitika ama kufungua”
“Basi watakuwa wamelala kajaribu kuwagongea tena”
Akili ya john sasa ikawa tofauti naya mwanzo lile wazo la kuambiwa akawagongee tena lilimkaa na sasa akili yake ikajazwa kuwa aende akaruke tu ukuta aingie ndani labda akigonga kwenye madirisha yao watasikia nakumfungulia. Ilimchukua dakika mbili yu tayari John akawa amesharuka ndani ya ukuta wa ndani anapioshi Angel. Woga wote ulimfutika ghafla huku akituna macho yake kuangaza hapa na pale mule ndani ya geti. Giza tororo lililokuwa limeanza kugubikwa ndani ya nyumba hii bado halikumsababishia John kuwa muoga, hakukuwa na taa ya aina yeyote iliowashwa, akili za John bado zillimtuma kuwa Angel na Alice watakuwa wamelala ndani, alichungulia chumba kimoja baada ya kingine kupitia madirishani napo haikusaidia chochote kujua kinachoendelea ndani. Wazo la kuvunja na kuufungua mlango ndilo lililomtawala halmashauri ya kichwa chake na sasa akawa ameshikilia kitasa ambacho hakikuwa kimefungwa kwa funguo yeyote. John alifanikiwa kuingia ndani na kuwasha taa za sebuleni na nje. Hatua kumi zilimtosha sana kufungua chumba kimoja bila kuambulia chochote na sasa akawa amebakiza chumba cha mwisho mbele ya macho yake. Akashusha pumzi yake kwanza aliokuwa akihema juu juu na kisha akatoa tabasamu kwa furaha huku akiamini atakuwa amemfanyia ‘surprise’ mpenzi wake Angel. Kitendo cha kufungua tu mlango na kuwasha taa mule chumbani hakuaamini alichokiona. Wote wawili, Alice na Angel walikuwa wapo chini na hawaongei na Angel alionesha kubadilika rangi ya mwili nakuwa mweusi sana huku matapishi na mikojo vikitapakaa pembeni na kuweka mfereji.
Hofu kubwa iliendelea kujengeka mwilini mwa John, na sasa akawa anatetemeka huku akijihisi mkojo wa moto unatoka kupitia suruali yake alioukuwa amevaa. Midomo yake ilionesha kabisa kukosa ushirikiano kwani lipsi zote za juu na chini zilikuwa zikimtetemeka huku zikiyasukuma meno yake kugongana yenyewe mithili ya vyombo vikipitiwa na panya kabatini tena wale panya sugu wa usiku wanaokimbizana ovyo.
“Oooohh my God!! Oohh my God!! nini tena hiki? Mkosi gani tena huu?”
John hakujua aanzie wapi na wala amalizie wapi kwani alitoa mkono wake nakuingiza mfukoni kwa dhumuni la kutoa simu apige polisi lakini alivyoitoa tu simu napo akachanganyikiwa nakusahau asijue ni mtu gani alikuwa akitaka kumpigia akairudisha tena mfukoni. Alirudi tena mpaka mlangoni hatua mbili tena akarudi pale pale walipokuwa wamelala Angel na Alice. Machozi ya kiutuuzima yakawa yameshatawala sura yake huku mashavu yakionesha dhahiri kupokea rundo la machozi na kuyatelezesha kupitia kidevuni mwake mpaka kwenye shati lake la ofisini. Akili aliokuwa nayo John ni kuinama mpaka chini na kwa kutumia kichwa chake moja kwa moja nakukiinamisha kifuani kwa Angel lakini mawasiliano kati ya kichwa cha John na kifua cha Angel hayakuwa sahihi kwani hakuweza kuusikia muungurumo wowote kuonesha kuwa mapigo ya moyo ya Angel yapo sawa.
“Angel my love?, Angel? Angel? Angeeeeeeeeeel??? amka jamani, amka unione mumeo nimekuja?? nimekuja kukufanyia ‘suprise’ mke wangu! pliiz Angel japo fungua macho basi nikuone, rudisha furaha yangu kipenzi”
John bado hakutaka kuamini kama Angel kapoteza maisha, alimtingisha sana bila kuambulia chochote na sasa alichokifanya aliinuka nakuvua shati lake nakubakiwa kifua wazi kilichojaa nywele za kiume sambamba nakulowana na jasho kisha akainamisha kichwa chake kwa angel kwa mara ya pili tena kusikilizia mapigo ya moyo napo hali ikawa kama ile ile ya mwanzo. Akili ikamganda mithili ya barafu linapokutana na ubaridi asijue nini cha kufanya ikabidi aamie pembeni yake alipokuwa amelala Alice nakuanzaa kumuasha kwa kumtikisa ama alivyofanya kwa Angel.
“Alice?, Alice? amkeni jamani nini tatizo?”
John alijihisi kuchanganyikiwa zaidi kwa kutikujibiwa na mtu yeyote wala kuonesha mshtuko wa aina yeyote, alichokifanya hapo alilichukuwa lile shati lake aliokuwa amelivua hapo mwanzo nakuanza kuwa pepea kwa nguvu zote mithili ya feni. Ndani ya dakika takribani tano John akashangaa Alice akijikunja kunja mithili ya mtu anayesumbuliwa na ndoto usingizini, akazidisha zaidi kupuliza kwa kutumia lile shati lake huku akihamishia na kwa Angel haraka haraka. Taratibu Alice akaonesha matumaini, akayafungua macho yake nakumtazama John kwa tabasamu huku akioneshawa kutokwa na ufahamu juu ya kilichomfanya azimie. Mshangao ambao alikuwa akiendelea nao sasa ukawa umefika pembeni yake ambapo ulikuwepo mwili wa Angel akiwa bado hajazinduka.
”Dada ni kweli umekufa dada? nani sasa nitaishi naye dada yangu? Maisha yangu yatakuwaje na umeniacha bila mtetezi wa maisha yangu Dada? kwanini kila mikosi ni mimi tu dada yangu?, Dada Angel amka basi japo uniage mara ya mwisho amka Dada yangu John wako amekuja kukuona Dada? nitaishi na nani tena mie Alice?”
Muda wote John alikuwa kashikwa na butwaa na asielewe cha kufanya zaidi ya kuendelea kumshangaa Alice alivyokuwa amezinduka toka usingizini nakumlilia Dada yake Angel. Akili ya kiutu uzima ikaanza kumtawala John katika halmashauri ya kichwa chake nakutambua kuwa zile damu alizokutana nazo pindi akiingia zilikuwa zikitoka kwa Angel na si kwa Alice. Macho yake yakaanza kuufata ule mchiriziko wa zile damu ulipotokea mpaka kwenye gauni alilokuwa amelivaa Angel.
“Angel umemuua mtoto wangu? Kwanini umekufa na mtoto wangu Angel? kwanini jamani?, nini kimekusibu si ungeniambia hata kwa simu?, ona sasa nani tena atakayenizalia na mke wangu matatizo yake unayajua Angel, mke wangu hawezi kuzaa na wewe ndio ulikuwa mtetezi wangu kwa hiki kiumbe?, nitakuwa mgeni wa nani tena John mimi?”
Nyumba nzima ikageuka vilio lakini havikuwa vilio vya makelele sana bali vilikuwa vilio vya chini chini ambavyo vilikuwa vikitolewa na Alice na John huku kila mmoja akioneka kumlalamikia Angel ambaye tayari alikuwa amefariki. Vilio hivyo vilifungua ukurasa upya ndani ya sura za John na Alice kwani sura zao zikawa zimefunikwa kwa machozi na kwikwi za hapa na pale. Kuna kipindi John alijitahidi kujikaza kiume lakini uzalendo ukawa unamshinda nakujikuta akitoka sauti kubwa. Sasa Alice akawa amedondoka chini kwa mara ya pili hali iliyomfanya Johna kuzidi kuchanganyikiwa akijua tayari na Alice amekufa. Alichukuwa mkono wake nakuulaza kwenye kifua cha Alice lakini mapigo yake ya moyo yakawa kama ya yamegoma kudunda. Ule mkojo uliokuwa ukimchuruzika John kidogo kupitia suruali yake kwa uoga sasa ukawa umeongeza kasi nakuwa mwingi sana hali iliyofanya suruali yake yote kulowana na lile kojo. Alijikaza kiume na kisha akamnyanyua Angel kwa kumbeba mithili ya wacheza mieleka kisha akaongoza mpaka kwenye gari lake nje nakumuhifadhi halafu akarudi tena ndani kumchukuwa Alice naye akampakazia kwenye gari lake nakuelekea hospitali ya Amana.
“Mungu nisidie nifike salama, Eeeh Baba niongoze ningoze Baba” OOohhh!!”

ITAENDELEA

No comments:

Post a Comment

Recent Posts