Thursday, April 4, 2013

RIWAYA: WASALIMIE KUZIMU-------------------3

 

MTUNZI: Hussein Wamaywa

SIMU: 0755 697335


SEHEMU YA TATU


Alivunga kwa hili na lile kabla hayajashusha pumzi ndefu na kusema “Oke, hayo tuyaache yashamwagika hayazoleki tena. Vipi kuhusu Saadan, anasema bado anakupenda licha ya yote yaliyotokea yuko tayari pia kukuoa na kuwalea watoto wako iwapo utakubali kwenda kuishi nae Oman. Unasemaje Nasra mwanangu?”
Nasra akaachia tabasamu dogo, akageuka na kumtazama Saadan, alikuwa kijana mzuri sana ingawa kwake hakuwa na mvuto kama ule aliokuwa nao Promota Halfan.
“Naweza nikakubali baba ikiwa tu atanitekelezea masuala fulani fulani”
“Good!” Alwatan Dafu akaruka kwa furaha “Masuala gani?”
“Moja nataka umfutie kesi Promota Halfan! Najua unahusika!”
“What?”
“Eeeh! Hilo la kwanza la pili baada ya kumfutia kesi nataka umuombe radhi kwa kumpiga na kumdhalilisha siku ile ya fainali pale Diamond Jubilee. Aidha nataka umuheshimu na umuhakikishie kuwa hutambughudhi tena na tena umtambue kama mkweo aliyepita na baba wa watoto wangu!”
“Mpuuzi!” Alwatan Dafu akanguruma, sharubu zikicheza cheza kwa hasira. Mikono pia ikimcheza cheza. Akaendelea kuongea povu likimtoka mdomoni.
“Nasema mpuuzi!! Una wazimu… una wazimu… unawazimu! Sababu ulizotoa sijui masharti hakuna zima hata moja. Nasema utaolewa tu, upende usipende!”
“Bila kutimiza hayo siolewi!” Alikuwa Nasra kwa kiburi.
“Huwezi kunichezea kama umejizaa mwenyewe sasa utanitambua! Hasira zikamzidi Alwatan Dafu akakunja mikono ya kanzu na kumjongelea mwanae huku akitetemeka kwa hasira.
Akamuinua pale kitandani na kumtandika vibao viwili vya nguvu. Nasra akaanza kulia, watoto wake pia wakaanza kulia! Hii haikumfanya Alwatan Dafu asimuinue zaidi na kumkunja vizuri kwa kutumia “Blouse” yake. Mkono wake wenye nguvu ukitua katika shingo la Nasra, Sadaan akamwahi na kumzuia.
Nasra akapata nafasi ya kuinuka, akawaifadhi wanae vizuri pasipo kukijali kilio chao halafu akamfuata baba yake, akipiga kelele zilizochanganyikana na kilio.
“Saadan! Muache, muache aniue, father kill me, kill me please! Maisha gani haya! Nilishachoka muache aniue ndio niue tu!!” akajitahidi kumnasua lakini Saadan akawa imara.
“Saadan!” Dafu akafoka akitweta “Acha nimfundishe hawezi kuniendesha anavyotaka. Hajakauka huyu kwamba nitashindwa kumkunja, mimi ni baba yale lazima aniheshimu, asikilize ninataka nini niache nimtandike!” povu zilizidi kutoka katika madomo wa Alwatan Dafu.
“Saadan, leave him! Mwache aniue!” Nasra anaendelea kupiga kelele akimfuata baba yake. Hamad! Alwatan Dafu akaponyoka mikononi mwa Saadan na kumfuata Nasra.
Nasra nae akamfuata!
Wakakutana katikati. Alwatan Dafu alimdunda Nasra kama ngoma! Makelele ya Saadan ndiyo yaliyowaita walinzi na wahudumu wa hospitali ile ambao walifika wanamundoa Alwatan Dafu toka katika shingo ya Nasra.
Huku akikohoa na kushika shingo lake kwa maumivu, Nasra aliendelea kumfuata baba yake na kuomba watu waliomshika mzee wake wamuache amuue.
Mama Nasra ambaye alikuwa amerudi hima kufuatia makelele yaliyopigwa na Saadan alishangaa kuikuta hali aliyoikuta, akamvuta Nasra na kumshika kwa nguvu.
“Mama niache! Niache baba akaniue, ndio nataka anitoe roho niepukane na hili balaa. Inakuwaje anifanye na kunigeuza vile apendavyo, vile atakavyo? Vile ajisikiavyo? Mie mwanasesere? Mie mtoto wa bandia? Niache mama, niache!
Mie ni binadamu kamili kama wengine. Mwenye uhuru, mwenye haki, mwenye uwezo wa kuamua! Vipi ayaingilie mamuzi yangu? Vipi auingilie utashi wangu, vipi aninyanyase? Niache akaniue nitoweke!”
“Hasira hazisaidii mwanangu!”
“Potelea mbali!” Nasra akataka aondoke tena lakini karipio la nguvu toka kwa mama yake aliyemvuta kwa nguvu ndio lililomrudisha.
“Mimi kama mama yako nasema acha, acha kabisa!” akafoka. Nasra akamsikiliza mama yake akarudi na kumkumbatia akiongeza kasi ya kilio.
“Mama! Nakupenda mama! Lakini roho inaniuma mama. Moyo wa subira sasa unaambulia zilizooza baada ya mbivu, uvumilivu wake umeuponza. Roho inauma mamaaah!”
Akazidisha kilio mara dufu. Mama yake akamfariji kwa kumkumbatia huku akumpigapiga mgongoni kwa vikofi vidogo vya upendo. Akamwambia.
“Najua! Najua kama inauma! Vuta subira zaidi itapoa na utasahahu!”
Walinzi waliomshika Alwatan Dafu sasa waliweza kumdhibiti vizuri na kupata ahueni baada ya mama Nasra kumdhibiti Nasra.
Alwatan Dafu akapozwa kiutu uzima hata akakubali kutoka nje. Saadan akampakia kwenye gari waliyokuja nayo na kuondoka. Alipomfikisha kwake, akamtaka apumzike kwa muda halafu yeye akarudi hospitali alikolazwa Nasra lengo lake lilikuwa moja tu kusikia Nasra anasema nini.
Naam! Toka atoke Oman, karibuni miezi miwili nyuma alikuwa hajabahatika kupata nafasi ya kuongea na Nasra kwa tuo. Kila alipokuwa akijiandaa kuongea nae yalitokea haya na yale ambayo yaliharibu na pengine kuvuruga maandalizi hayo.
Hakika! Alimkuta Nasra akijiandaa kupumzika, mama yake nae alikuwa pembeni akamsalimu na kumsalimia Nasra kisha akaketi pembeni yao kabla ya hajaanza kuwaangalia mmoja baada ya mwingine kwa zamu.
“Samahani mama,” Akaanza kwa upole na heshima na kuendelea
“Inawezekana pengine nafanya makosa kukuita hivyo pasi ya idhini yako wala ya Nasra. Lakini madhali umemzaa Nasra ambaye tunakaribia kulinganalingana, sioni kwa nini usiwe mama yangu, sioni! Hata hivyo natanguliza radhi za dhati kama muono wangu ni opofu!” akatua kuvuta pumzi.
“Bila samahani Saadan, wewe ni mwanangu kwa kila hali kuwa huru sijui unasemaje?” akajibiwa
“Unajua nilikuja huku Afrika na hususani hapa Tanzania kwa ajili ya kumuoa Nasra. Na haki ya nani nilimpenda Nasra toka nilipomuona mara ya kwanza katika picha.
Na siku nilipokuja kumtia machoni ‘live’ kwa mara ya kwanza pale jukwaani Diamond Jubilee, upendo wangu kwake ukaongezeka mara dufu mpaka sasa ninampenda kuliko tafsiri halisi ya neno hilo…”
“Saadan!!” Nasra akaingilia kwa karaha “Natumai hukuja hapa kumueleza mama yangu jinsi unavyonipenda sawa?” Saadan alipokubali kwa kutikisa kichwa Nasra akahitimisha kwa kusema “Basi mashairi achana nayo, mueleze lililokuleta!”
“Usihamaki Nasra! Ninachofanya ni kujenga msingi wa mazungumzo na labda maelezo yangu ili aweze kunielewa vizuri au ni makosa kufanya hivyo?”
“Yeah! Inawezekana!” Alikuwa Nasra tena
“Nasra hebu muache mwenzio aongee kwanza!” Mama Nasra akaingilia. Nasra akanyamaza kwa shingo upande.
“Naomba msamaha tena endapo nimekosea ninachotaka kusema ni kwamba toka nimefika hapa nimeshuhudia vingi na mengi, lakini sijapata nafasi moja muhimu nayo ni kuongea na Nasra.
Nilipofika hapa siku moja kabla ya shindano, niliambiwa nisiongee na Nasra kwani naweza kumchanganya kiasi cha kumfanya afanye vibaya. Niliheshimu.
Mashindano yakafanyika, akafanya vizuri lakini yaliyotokea ukingoni mwa shindano sote tunafahamu na kwa vile Nasra alipoteza fahamu kwa siku kadhaa, kila wakati nimekuwa nikifika hapa na kukosa nafasi ya kuongea nae na hali ya kuwa ni nusu mfu!
Sikukata tamaa nimesubiri kwa mapenzi mazito na uvumilivu mkubwa mpaka leo hii muumba alipoleta Baraka zake. Lakini mara nyingine tena yametokea ya kutokea ambayo sote tumeyaona. Ingawa Alwatani Dafu ananipa matumaini lakini mimi siyo mtoto wa kudanganywa na pipi.
Ndiyo sababu nikatangulia kuomba radhi mama, naomba uniruhusu niongee na Nasra faragha ili nijue msimamo wake kwangu ukoje! Ili niweze kujua kama nastahili kusuka au kunyoa! Ni hilo tu.”
Mama Nasra akamgeukia mwanae na kumtazama kama anayemuuliza “Unasemaje’. Nasra akabetua mabega na midomo kama nayesema sitaki au sijui. Mama Nasra akatabasamu na kumgeukia Saadan!
“Bila samahani mwanangu. Ninaweza tu kukupa nafasi nzuri ya kuongea na Nasra, usifadhaike. Usijali, usijali hata kidogo” akamjibu akachukua baadhi ya nepi za watoto na kwenda kuzifua nje.
Nasra akamuangalia Saadan na kuketi vizuri kitandani. Akamnyanyua mtoto wake mmoja aliyekuwa analia na kumnyonyesha halafu akamuuliza Saadan kwa kiingereza.
“Enhe! Unataka kuongea nini na mimi?”
“Mengi tu Nasra!” Saadan akajibu kwa kiingereza pia na kuendelea “Nadhani ingekuwa vizuri kama tungeanza kwa kuongelea habari za ndoa yetu. Sio siri mimi ninakupenda sana, tena sana sijui wewe kwangu?”
“Una maana gani Saadan?”
“Unataka kuniambia kwamba hujui kilichonitoa Oman kunileta hapa?
“Naweza kusikia, kwamba umekuja kufunga ndoa na mimi si ndo hivyo?”
“Yah! Uko sahihi”
“Lakini tayari umemkuta Nasra akiwa mjamzito na mbaya zaidi kajifungua Diamond Jubilee mbele ya halaiki ya watu tena watoto mapacha! Hufikirii kwamba huyu Nasra unayetaka kumuoa leo alikuwa Malaya, mshenzi wa tabia na kiruka njia ambaye anaweza kukuambukiza hata Ukimwi?”
Saadan akatulia tuli pasipo kujibu. Nasra akaendelea
“Haya, umeshuhudia ugomvi baina ya Nasra na baba yake. Hivi hufikirii kama Nasra anaweza kuwa mbishi na kupigana na baba yake mzazi, aliyemzaa, akamlea na kumosomesha; vipi baba wa Saadan! Atamsalimisha kweli? Na kama hatomsalimisha, huo ukoo wa Saadan utamuelewaje Nasra?” Akatulia tena, bado Saadan alikuwa kimya.
“Hiyo tisa! Kumi nina watoto hawa tena mapacha, hawa bado wanahitaji uangalizi wa karibu wa mimi mama yao, hasa ukizingatia uduni na udhaifu wa afya zao. Utawaeleza nini wanaukoo wenu ambao watahoji juu ya watoto hawa?!
Naomba ufikirie vizuri uamuzi wako Saadan, mie nafikiri sifa zangu chafu zinanifanya nikose sifa za kuwa mke mwema kwako. Najua unanipenda, tena unanipenda sana! Hilo nalifahamu fika.
Na tena ninashukuru mno kwa msaada wako wa hali na mali ulioutoa kwangu toka pale jukwaani mpaka hapa Aga Khan hospiatal! Kitendo cha kujitolea kuwasaidia wanangu wasiokuhusu ndewe wala sikio, kinanifanya nikose cha kukulipa zaidi ya kusema Asante, Mungu atakulipa zaidi!” Nasra akahitimisha.
Saadan akatabasamu na kusema “Nasra mimi ndiye ninakwenda kuishi na wewe siyo baba, mama, kaka, dada, ndugu na wala wanaukoo wangu. Mimi nina akili, uelewa na ufahamu mzuri siwezi kukulaumu kwa yaliyotokea kwa vile tayari nimeshajua ulikuwa ukiishi maisha ya namna gani. Siwezi kukulaumu kabisa.
Shukrani zako nimezipokea, lakini sio kweli kwamba huna cha kunilipa. Upendo wako kwangu ni malipo tosha, malipo yatakayouacha Moyo wangu ukiwa umesuuzika vilivyo.
Bila shaka pia, baba na mama washakwambia kuwa mimi nipo tayari kuishi na wewe na watoto wako tena nitawalea kwa upendo na mapenzi yote kama baba yao mzazi, kama baba aliyefundwa vyema kulea. Tafadhali Nasra nipokee tuishi pamoja!”
“Maneno yako mazuri na hayachoshi masikioni Saadan, lakini ingawa sina hakika, najijua fika kwamba mimi ni mcheshi. Yeah! Wazazi marafiki na jamaa wananiambia hivyo, hata waalimu waliniambia hivyo hivyo.
Nina hakika ukaidi wako wa kujitia kunijali mimi kuliko ndugu zako, utawafanya ndugu zako wajenge nidhamu ya woga wakijitia kuuheshimu uamuzi wako wa kuoa msichana Malaya mwenye watoto wawili wasio wako.
Lakini chuki zao kwangu hazitajificha, zitaonekana dhahiri bin shahiri! Kitu kinachonifanya niishi pasipo ushirikiano wa kati yangu na wanaukoo wenzako.
Na mimi siwezi kuishi kwa amani wakati fika sielewani na wifi, sielewani na shemeji na baba mkwe au mama mkwe siwezi! Nahitaji kila mtu anizoee, tutaniane, tucheke na kufurahi ndio maana nikakwambia ufikirie uamuzi wako tena, fikiria tafadhali!”
“Niufikirie vipi Nasra? Inatosha kusema ninakupenda na kukuhitaji kuliko unavyoweza kufikiria. Sijui kwa nini unashindwa kunielewa, ndugu zangu sio wakatili kama unavyowafikiria na labda watakuchukia si unaweza kuniambia?”
“No! utakuwa mwanzo wa kukuchonganisha na ndugu zako. Hiki ni kitu kingine ambacho sikipendi daima dumu nitataka kuona mkiishi kwa upendo, amani, furaha, kama mlivyokuwa mkiishi baada ya mimi kufika!”

Saadan akamtazama Nasra na kuyafikia majibu yake, zilikuwa hoja za uhakika ambazo zingemgharimu muda mwingi kuziweka sawa ili kuondoa mashaka kwa Nasra, akajikuta akishusha pumzi za kukata tamaa na kusema.
“Sasa unataka kuniambia nini? Kwamba hunipendi na hutaki kuolewa na mimi?”
Ikawa zamu ya Nasra kumtazama Saadan kwa muda kabla hajayarudisha macho chini, kwa ujumla Saadan alikuwa amekata tamaa. Akaachia tabasamu dogo na kumuonea huruma.
“Sikiliza Saadan! Nikikwambia nakupenda, upendo kama huo ulionao wewe kwangu ninakuongopea! Baba wa watoto hawa ndiye haswa aliyeushika moyo wangu. Hata hivyo juhudi zako zimenifanya nigundue ni namna gani unavyonipenda.


***SAADAN anaelezea hisia zake zote kwa NASRA lakini NASRA anamuwaza baba wa watoto wake…..
****Mzee Dafu analazimisha mwanaye aolewe na SADAAN nini kitajiri..

ITAENDELEA

No comments:

Post a Comment

Recent Posts