Saturday, December 22, 2012

SITAISAHAU facebook----------------26 THE END

 

MTUNZI: EmmyJohn Pearson

MAWASILIANO: 0654 960040

SEHEMU YA ISHIRINI NA SITA

...
Mayowe yakatawala, akinamama wakiwa wamesahau watoto wao na wanaume nao wakiwasahau wake zao sasa kila mmoja alikuwa akiipigania nafsi yake. Sikuwa katika umoja na akina Jesca tena! Hapa sasa kila mwenye macho hakungoja kuambiwa tazama!!
Makaburi yale mawili yaliendelea kufuka ule moshi wa rangi ya dhahabu.
Wenyeji wa kijiji kile walikuwa katika taharuki kubwa sana huku wakizungumzia juu ya kukasirika kwa mizimu.
Nani sasa aliyeikasirisha? Walijiuliza.
Vilio vilisikika tena kutokea gizani. Watu wakakimbilia huko. Waliporejea ilikuwa taarifa ya mama mmoja aliyekuwa anakimbia ameshambuliwa na kitu kisichofahamika na hatamaniki tena. Amekufa!!
Hali ikatulia kwa muda. Akajitokeza mzee mmoja wa makamo akitembea kwa kutumia mkongojo.
Huyu hakuogopeshwa hata kidogo na hali iliyokuwa inaendelea. Alisimama mbele ya kunndi na kuanza kusema anachokifahamu, alielezea historia fupi ya makaburi ya Kiyeyeu na majanga yanayotokea iwapo wazee wale waliolala katika makaburi yale wakikerwa na jambo. Hapa sasa akafikia kusema kuwa kuna mtu mmoja katika msafara alikuwa ameikasilisha mizimu!!
Ni lazima abaki ili kuwanusuru wenzake. Kama akiendelea mbele basi litatokea balaa kubwa zaidi ya hili. Alizungumza kwa sauti ya juu na kila mmoja aliweza kusikia. Sauti yake na umri wake vilikuwa vitu viwili tofauti!!
“Hivyo kama unajua una lolote la kuikera mizimu hii ni heri ubaki nyuma kuwanusuru wenzako.” Alizungumza kisha akatuachia mtihani wa kuamua aidha kujitokeza ama la!
Maneno yake niliamini kabisa yalikuwa yanamlenga John. Nilijisikia uchungu sana, John alitakiwa kubaki nyuma. Yaani harakati zangu zote hizo zinaishia hapa!! Niliumia sana.
Niliangaza huku na huko. Sikumuona John!! Nilitaka kumuita lakini niliamini kuwa hawezi kunisikia.
Kimya kilitawala akisubiriwa mtu huyo ambaye ameikera mizimu aweze kujitoa kundini. Hakuna aliyejitokeza.
Mzee akaendelea kusubiri!! Bado hakujitokeza mtu yeyote.
Kimya kilikatishwa na sauti ya mwanaume akipiga mayowe. Tukageuka nyuma kumtazama. Alikuwa amejishika shingo yake huku akipiga kelele. Mara damu zikaanza kumtoka puani, masikioni na mdomoni. Badala ya kumsaidia kila mtu akawa anamuogopa!!
Hatimaye akaanguka na kutulia tuli! Alikuwa amekata roho!!

Kina mama wakapiga kelele sana, wanaume wakabaki kushangaa.
Yule mzee wa kimila akaipaza tena sauti yake, “Kama asipojitokeza mtu huyu majanga yataongezeka. Mizimu inakasirika.”
Sasa watu wakaanza kusemezana huku wakisisitizana kuwa mtu huyu ajitokeze ili mizimu itulie. Bado hakuweza kujitokeza mtu yeyote.
Zikaanza kutolewa hirizi miilini mwa watu, lakini yule mzee wa kimila akapinga kuwa hizo ndio tatizo.
Waliokuwa na dawa za kienyeji wakatoa. Bado haikuwa tiba.
Kiza kinene kikatanda kama dalili ya mvua. Mwanga mkali ukamulika bila kutoa kelele. Watu watatu wakasalimia na ardhi.
Ilikuwa radi!! Na walikuwa maiti tayari.
Roho ikaniuma sana, nikajiona mimi ndiye muhusika. Nikatamani John atokezee nimtangaze kuwa ndiye chanzo. Lakini John hakuwepo tena!!

Vile vifo vya radi ya ghafla vilimshtua kidogo yule mzee.
Mara akabadilika sura na kuwa kama aliyekasirika!!
Akatoa amri ya watu kujipanga msitari. Amri ikasikilizwa. Wanaume na wanawake mstari mmoja, mistari ilipopangwa ndipo nilimuona John. Na yeye alikuwa amepanga mstari. Akaanza kupita na kufanya kile anachokijua mwenyewe. Alimfikia John, na yeye akamuona akamshika mkono. Ina maana John anaonekana? Nilijiuliza.
Nikiwa katika hali ya mashaka ya kila kinachoendelea. Mara yule mzee mkongwe alinifikia, alikuwa anatabasamu, mgongo wake uliopinda ulimfanya awe ameinama na kuwa mfupi sana!!
“Shkamoo babu.” Nilimsalimia.
“Marahaba mjukuu wangu.” Alinijibu kwa ukarimu sana.
Kisha akanishika mkono.
Alipofanya hivyo kwa wasafiri wengine hakutumia muda mrefu, lakini kwangu ni kama alitumia sekunde nyingi.
“Unaitwa nani binti.”
“Isabela!!”
“Nani alikwambia unaitwa Isabela.” Aliniuliza huku akinitazama usoni.
“Naitwa Isabela mzee.” Nilitaharuki kutokana na maswali ya mzee huyu.
“Hilo sio jina lako binti.”
“Sio jina langu?”
“Na litakugharimu sana na kuwaumikza wengine katika maisha yako.” Kauli nzito za mzee huyu zilinishangaza.
Isabela sio jina langu? Ni miaka zaidi ya ishirini tangu nipewe jina hilo. Sasa leo ananiambia kuwa hilo sio jina langu? Maajabu haya.
“Hautaendelea na safari hii…kuwaepusha wenzako na mabalaa yasiyowahusu.” Alininong’oneza. Nikahisi ubaridi ukinipenya mwilini, mapigo ya moyo yakapungua kasi. Nikakata tamaa.
Mimi tena? Sio John!! Maajabu haya.
“Kama unao upendo waruhusu wenzako waende zao. Janga lako haliwahusu hata kidogo.” Alinisihi. Nikatikisa kichwa kukubali. Huku nikiamini kwa asilimia kadhaa kuwa tatizo ni John na yule mzee hajui kitu.
Mzee akawatangazia watu kuwa tatizo limekwisha. Na kweli nilipokubali tu waondoke zao. Nilipogeuka makaburini. Ule ukungu haukuwepo tena.
Abiria wakaingia katika basi lile la ziada lililokuja kutuchukua.
Tofauti na mawazo yangu. Kuwa John atazuia basi lisiondoke baada ya yeye pia kuwa mmoja kati ya abiria. Haikuwa hivyo. Basi liliwaka vyema. Na kutoweka!!
Ilikuwa usiku mnene lakini kinyume na taratibu za usafiri Tanzania, basi lile lilisafiri usiku. Hayakusikika malalamiko ya kubanana tena. Kila mmoja alitaka kutoweka eneo lile. Hata madereva na makondakta wote walikuwa waoga.
Nilibaki na yule babu!!! Akina Samson, Jesca, na Jenipher walitaka kubaki na mimi lakini kwa maneno ya yule babu kuwa mzigo wangu hauwahusu. Niliwaruhusu waende zao huku nikiwapatia pesa nyingine ya ziada.
“Nendeni mkautangaze ushuhuda huu popote pale. Msifiche hata moja lililotokea. Hata kama sitafika huko mtakapokuwa. Naamini sisi ni washindi.” Niliwaeleza. Wakalia kwa uchungu. Samson akagoma kabisa kuondoka lakini hatimaye alikubali kuondoka.

Nilibaki na mzee yule tukizungumza. Alinieleza juu ya jina langu. Akadai kuwa hakuwa akijua nilikuwa naitwa nani lakini Isabela halikuwa jina langu.
“Rejea nyumbani ukalitafute jina lako. Jina lako limepotea ama limefichwa. Na ukiendelea kuamini kuwa wewe ni Isabela basi maisha yako yatakuwa ya tabu sana. Utawatesa wenzako nawe utateseka sana.” Alinieleza yule babu.
“Unaweza kwenda kupumzika nyumbani kwangu. Kesho upatafute nyumbani kwenu. Ukalitafute jina lako.”
Tuliongozana na yule mzee hadi nyumbani kwake. Hapo tulipokelewa na mbwa wengi sana waliomlaki bwana huyu kwa furaha.
Wahehe na mbwa!! Niliwaza.


******

Nililala katika mkeka. Ni kama nililala kwa sekunde kadhaa hatimaye pakapambazuka.
Mzee akaniamsha, akanisihi sana nihakikishe Napata jina langu halisi na hapo nitaendelea na maisha yangu vizuri.
“Jina langu ni nani?” nilijiuliza kwa sauti akanisikia.
“|Hata mimi silijui lakini ni lazima ulipate ili kuzikwepa laana za ukoo wako. Fuatilia historia yako vyema mwanzo hadi mwisho. Historia ya kweli ipo kwa mama…kamuulize mama yako. Wewe ni nani? Lakini nakukumbusha kuwa wewe sio Isabela”
Mzee alinisindikiza hadi njia ya mabasi.
“Usizungumze na mtu yeyote, kwa usalama wako na abiria wenzako.” Alifanya kunisemesha kwa sauti hafifu. Nikamsikia na kumwelewa.

Basi likapita. Nikapanda!! Mzee alinilipia nauli huku akichukua fursa ya kuzungumza na kondakta.
Safari ya kurejea Makambako. Safari ya kwenda kulitafuta jina langu. Jina lililopotea.
Kaka aliyekuwa pembeni yangu alikuwa anaongea maneno mengi sana. Lakini sikuwa namjibu chochote.
Hatimaye tukaifikia Makambako!! Nikashuka garini nikaikanyaga ardhi ya Makambako kwa huzuni sana!! Hatua kwa hatua nikaanza kuelekea nyumbani.

*****
Mwanamke wa makamo ambaye sasa mvi zilikikaribia kichwa chake chote alikuwa anafagia uwanja. Alikuwa akiimba nyimbo anazozijua yeye huku akionekana kuzifurahia. Nilimtazama kwa makini. Nikatamani ningekuwa nimekuja kwa mazuri huenda ningemshtua kisha tukacheka wote. Lakini nilikuwa nimekuja kwa mengine magumu sana.
Huyu alikuwa ni mwalimu Nchimbi. Mama yangu mzazi.

Nikanyemelea. Akashtuka akageuka.
“Belaaa….Belaaa mwanangu.” Akautupa ufagio, akanikimbilia, akanikumbatia kwa nguvu. Joto lake likaupenya mwili wangu ulio dfhaifu. Nikaamini kuwa nilikuwa nimemkumbuka sana. Chozi likanitoka. Nikamkumbatia kwa nguvu zaidi.

“Karibu mwanangu…mbaya wewe..yaani kimya kimya au uliongea na Suzi..wabaya sana nyie.” Alilalamika nikajilazimisha kutabasamu.
Tuliingia ndani. Tukafanya mazungumzo ya hapa na pale. Hadi tulipokatishwa na nyimbo nyingine kutoka kwa mlevi. Huyu alikuwa baba yangu mzazi. Asubuhi sana alikuwa anatokea kilabuni.
Sijui alilala huko? Nilimuuliza mama./
“Hamna sema ameamkia huko.”
“We Helena wewe…Aaah!! Suzy..inaq maana haunioni uje kunipokea…si ku hizi hamsalimii watu!!” alizungumza kilevi. Macho yake hayakumwezesha kujua iwapo mimi ni Isabela.
Akapita akiacha nyuma harufu ya pombe kali. Akaingia chumbani.
Baada ya kelele za hapa na pale akasikika akikoroma!!!

Nilijikaza sana na sasa nikaamua kumueleza mama kilichonileta pale nyumbani.
“Mama hivi hili jina la Isabela ni nani alinitungia.”
“Mbona wauliza hivyo mwanangu.”
“Nipe jibu mama..ama ukoo wangu ni upi.”
“We mtoto umekuwaje lakini.”
“Nijibu mama.”
“Mbona kila kitu kipo wazi..ukoo wako ni huu wa baba yako, na jina hilo ni mimi na baba yako tulikupatia.” Alinijibu.
Niliondoka sebuleni nikaenda chumba cha wasichana nikajinyoosha. Nikapitiwa na na usingizi.

Nilikuja kushtuka nikiwa na njaa kali.
Nikaliendea jiko.
Nikajihudumia vilivyokuwepo, kisha nikareje chumbani.
Majibu ya mama yalikuwa hayajaniridhisha hata kidogo.
Nitamuuliza baba pia!! Huenda kuna kitu anajua.
Kwa nini aliniita Isabela.
Nikasinzia huku nikiwa nimejiahidi hivyo kichwani mwangu.

*****

Asubuhi na mapema nilikuwa wa kwanza kuamka. Nilihitaji kumuwahi baba akiwa katika akili zake vyema kabisa.
Kabla hajalewa!!
Niliwahi na kujifanya naosha vyombo.
Hatimaye nikasikia mlango wa chumbani unafunguliwa. Baba akatoka.
“Aaah!! Bela mwanangu…lini tena umetuvamia wewe…umemaliza mitihani lakini.”
“Nimemaliza..shkamoo baba….”
`aliijibu salamu. Tukabadilishana mawazo na hatimaye kama kawaida yake akaniomba pesa.
“baba kabla ya hilo…nahitaji kukuuliza kitu.”
Alinisikiliza kwa makini, nikamueleza kile nilichomueleza mama. Baba alionekana kushtushwa na habari hiyo. Alijaribu kujiweka sawa lakini nilikuwa nimemsoma.
“Fanya hivi…nipatie hiyo pesa nikirejea tutaongea ni stori ndefu kidogo..si unataka kujua maana ya Isabela na kwanini tulikuita hivyo..nifanyie kwanza nienda kupata supu kidogo.” Alijaribu kukwepesha mada.
Niliheshimu maamuzi yake. Nikaingia ndani nikarejea na pesa kidogo nikampatia. Akatoweka.
Moyoni nilipata matumaini makubwa sana!! Niliyaamini yale maneno ya yule mzee.
Sasa mimi ni nani kama sio Isabela? Na kuna siri gani inazunguka hapa. Nilijiuliza. Wa kunijibu alikuwa ni baba.

Nilisubiri sana. Hadi pale ilipokuja taarifa kuwa baba amekutwa mtaroni. Hana jedraha lakini haijafahamika bado kama anapumua ama amekufa!!
Hii ilikuwa ni habari ya kushtua sana.
Mimi na mama tukakimbia kuelekea hospitali ambayo tulielezwa kuwa amelazwa.
Bahati mbaya zilikuwa mbio za kuwahi upepo.
Baba yangu hatukuwa naye tena!! Kifo cha utata. Hakuwa amelewa. Alikutwa na ile pesa niliyompa.

Hakika mimi sio Isabela, na kuna siri mzee wangu amekufa nayo!! Nilizungumza na nafsi yangu.
Jina langu ni nani sasa? Na kwa nini waliniita Isabela?


***Najua wengi watafadhaishwa na hili……lakini hakuna jinsi lazima iwe hivi.
***ISABELA katika wakati mwingine mgumu…amehakikishiwa kuwa Isabela si jina lake. Na hicho ndio chanzo ncha matatizo.
***JINA lake hasa ni nani? Na kama baba amekufa na siri hiyo atafanya nini kujikomboa na kuwakomboa wengine???
***JOHN, BASU, DAVIS, OSMAN…nini hatma yao viumbe hawa???

KWA HAPA uwanjani SITAISAHAU facebook inaishia hapa.

No comments:

Post a Comment

Recent Posts