Monday, December 10, 2012

SITAISAHAU facebook-------- 14

 

 

 


MTUNZI: Emmy John P.

MAWASILIANO: 0654 960040


SEHEMU YA KUMI NA NNE

...

ILIPOISHIA

Usiku ukafika nikampigia simu.

“Dada, yaliyonikuta ni makubwa mdogo wako…” nilianza kumuelezea mkasa ulivyokuwa huku nikisita kumshirikisha ukweli kuwa kuna ndoto ikiambatana na hisia ilinishika na nikahisi nafanya mapenzi ndotoni. Nilihofia ataleta ushauri wa kwenda kwa wachungaji feki kuombewa. Sikutaka kabisa kusikia mambo hayo.

Nilipomaliza ukawa wakati wake kunishauri ama kusema lolote.

Kwa sauti tulivu tena iliyojaa unyenyekevu Suzi alianza kunieleza neno kwa neno.

Sasa nikaanza kutetemeka alipoyatamka haya. Nikaketi chini, mapigo ya moyo yakaongezeka. Nikatamani nife kwa muda. Kisha nikakumbuka kuwa nilikuwa naogopa kufa!!! Nikalipuuzia wazo hilo.

Wasiwasi ukazidi. Lakini Suzi alikuwa akiusema ukweli aliouficha moyoni kwa muda mrefu.

**SUZI anamweleza nini Isabela…hadi anapatwa hofu kiasi hicho?

**HIYO MIMBA imeingia vipi? JOHN yupo wapi?


ENDELEA

Suzi aliongea huku akitia msisitizo kwa aliyokuwa anayasema.
Ilikuwa ni historia ambayo sikuwahi kuisikia kamwe lakini sasa Suzi alikuwa ananifumbua macho. Uhusiano wa matukio alivyoupangilia ulinitia katika mashaka.
Wakati nampigia simu wazo langu kuu lilikuwa kuitoa ile mimba ambayo hata sikuwa na uelewa imeingia vipi katika mwili wangu. Nikamdanganya kuwa mpenzi wangu amenipachika lakini hatukuwa na mpango wa kupata mtoto katika kipindi hicho.
“Bela, Bela..usije ukathubutu kuitoa hiyo mimba!!! Usithubutu!!” alinikanya Suzi, hapo ni baada ya kunieleza kuwa kila msichana aliyethubutu kutoa mimba katika ukoo wetu alipoteza kizazi.
Maneno hayo yaliambatana na mifano kadhaa ya ndugu zangu ambao hadi leo hii wanalilia watoto. Umri unakwenda na hakuna dalili ya mimba. Wengine wanaachika na kuolewa tena lakini hakuna mabadiliko. Wanabaki kuwa wapweke na kumshushia lawama Mungu. Kumbe kuna siri mioyoni mwao. Mimba!!
Anti Rozi, mamdogo Sikujua, hao ni baadhi ya ndugu zangu waliokuwa wakinyanyasika kwa kuwa hawazai. Na kama na mimi ningethubutu basi ningekuwa katika mkondo huo. Hapana!! Sipo tayari kudhalilishwa.
Kwa maongezi yale kati yangu na dada Suzi ilimaanisha kuwa sikutakiwa kuitoa ile mimba! Mimba ya gogo! Isabela niende kuzaa gogo. Hapana!
Sasa ni kipi natakiwa kufanya hapa? Nilijiuliza bila kupata majibu.
Suzi akaniaga nikakata simu!!

Hofu kuu ilinitawala baada ya kuwa peke yangu tena. Bado nilikuwa nimeishikilia simu na nilikuwa natetemeka sana. Ni kama dunia ilikuwa imenigeukia na kunizomea baada ya kuwa imenivua nguo zote. Dunia ilikuwa inanionea. Haikuwa inanitendea haki hata kidogo.
Nililitazama tumbo langu dogo kisha nikafumba macho na kujenga picha jinsi litakavyokuwa siku za usoni. Tumbo kubwa kabisa na kila mmoja ataliona. Aibu kubwa!
Kama hiyo haitoshi itafikia kipindi nitaugulia uchungu na hatimaye nitajifungua. Mtoto wa nani huyu? Nilijiuliza bila kupata jawabu sahihi.
Mawazo yakaniumiza kichwa nikameza dawa za kutuliza maumivu. Nikasinzia!
Asubuhi nikashtuka kutoka usingizini. Tatizo lilelile haikuwa ndoto, nilikuwa na mimba. Nikawaza na kuwazua bado hapakupatikana jibu sahihi. Nikajaribu kupuuzia lakini suala hili liliniumiza kichwa.
Sasa nikakumbuka kuwa nilikuwa na pesa za kutosha katika akaunti yangu. Sasa kwa nini niendelee kuhangaika kiasi hiki. Ina maana pesa haiwezi kutatua tatizo hili.
Nikafikiria kugawana pesa zangu na mganga mwingine wa jadi. Lakini huyu sikutaka awe anatokea hapa Tanzania. Nilihitaji mganga mwingine kabisa kutoka nje ya nchi.
Sikumshirikisha Maria, maana angegundua kuwa nina mimba. Hili nililiepuka sana.
Kimya kimya nikampata mganga. Alijitambulisha kuwa anatokea Naijeria. Huyu alikuwa ananifaa.
Nikamfungia safari! Alikuwa amejiundia ofisi yake nje kidogo ya jiji la Mwanza, maeneo ya Shamaliwa kata ya Igoma.
Nyumba yake ilikuwa nzuri sana, tofauti na wale waganga waliotangulia ambao walikuwa wakiishi katika vibanda vya nyasi huku wakiwa mabingwa wa kuomba kuku na mbuzi kama njia ya kutibu tatizo.
Huyu alikuwa katika nyumba nzuri sana. Huenda na tiba yake ilikuwa nzuri.
Nilipokelewa vyema na kuandikisha jina langu getini. Nikafikishwa ofisini kwake. Na penyewe palivutia sana.
Alikuwa anaye mkarimani wa kumsaidia kuweza kuwasiliana na wateja wasiojua kiingereza. Mimi sikuhitaji mfasiri nilikuwa najua kiingereza hivyo tulizungumza moja kwa moja.
Alinisikiliza kwa makini, miwani yake machoni. Kisha akaanza naye kunipa maelekezo.
Alitoa maelekezo mengi. Mwisho akaniambia nirejee usiku wa saa mbili aweze kunipatia tiba. Wakati huo ilikuwa saa kumi na moja jioni.

Saa mbili nilikuwa kwa mganga tena. Sasa alinipeleka mahali anapotolea tiba.
“Una mimba ya jinni..jini la hatari..na ukilitoa kwa njia ya kuzaa.UTAKUFA! hakika UTAKUFA!” Alizungumza kwa msisitizo. Nikatetemeka kusikia suala la kufa.
“Hongera umewahi sana..bado halijakomaa. Sasa unatakiwa ulitoe sasa hivi. Linatakiwa kutoka.”
“Nitoe!.” Nilijikuta najibu huku ninatetemeka. Akacheka.
“Vua nguo zako zote.” Alitoa maelekezo.
Nikasita, akacheka tena. Kisha akanitazama.
“Toa nguo zako!!.” Aliamuru kwa kiingereza chake chenye lafudhi ya Afrika magharibi. Alikuwa mweuzi tii.
Nikasalimu amri, mtaalamu huyu ndiye aliyekuwa ameshika mpini nami mikono yangu kwenye makali. Yeye mshindi.
Nikasaula moja baada ya nyingine. Nikaacha chupi. Akakoroma huku akitetemeka. Nikaiondoa na hiyo iliyobaki. Sasa nijizibe wapi? Juu ama chini nikakosa maamuzi.
Nikabaki katika mfadhaiko!.
“Lala hapo kitandani!” aliamuru. Nikajilaza kitanda cha futi sita kwa sita chenye shuka jeupe kabisa.
Mara taa ikazimwa. Giza likatawala. Kimya nacho kikatanda. Sauti ya mganga pekee akiunguruma kwa sauti ya chini ndiyo ilisikika. Mimi hofu tupu!
Mara kitandani tukawa wawili. Mikono ikinipapasa. Tiba gani hii! Nilishangaa lakini sikuuliza.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida nikapatwa na kiu kikali sana ghafla. Kiu kilichokausha koo langu kabisa.
“Thirsty….” Nilinong’ona, mganga hakujibu. Nikajaribu tena kunong’ona sauti haikutoka. Lakini sikuwa katika uhitaji wa maji ya kunywa. Kuna kitu cha ziada nilikuwa nahitaji, sijui ni kitu gani sijui!! Lakini nilikuwa nahitaji.
Mikono niliendelea kunipapasa. Sasa hakuwa anaunguruma tena lakini alikuwa anahema juu juu sana. Huku napapaswa huku nahisi kiu cha ajabu.
Mara yule mganga akafika kifuani akaendelea kunishambulia. Kuja kutanabai alikuwa yu uchi! Hofu ya kubakwa ikanikumba. Nikajaribu kupiga kelele. Sauti haikutoka. Nikajaribu kumsukuma, alikuwa mzito kupita kiasi. Alikuwa na uzito kama lile gogo la usiku ule. Gogo lililonitia mimba. Kiu kikanifadhaisha na sasa sikuweza kujizuia zaidi nilitakiwa kupata kinywaji. Lakini sio maji wala soda.
Mganga akazidi kunikumbatia. Nikafanya jaribio la kumn’gata ili asitimize kitendo chake cha kunibaka. Maajabu!! Ile ladha ya chimvichumvi la jasho ikanipendeza, nikaitamani na nikazidi kumng’ata, damu! Damu ikaanza kumtoka, sikutaka hata tone moja linipite kando. Alijirusha rusha lakini sikubanduka. Hadi pale kiu kiliponiisha.
Wakati kiu kinaisha na yeye alikuwa ametulia tuli!
Nimekunywa damu!! Nilighafilika. Nikasimama wima huku nikiwa siamini kabisa kilichotokea pale ndani. Nikatapatapa katika giza mara nikabonyeza bila kutarajia kitufe. Taa ikawaka!
Macho yangu ana kwa ana na dude kubwa jeusi. Asili yake Naijeria likiwa limetulia kitandani. Shuka nyeupe sana bila hata tone la damu.
Dude lile lilikuwa uchi wa mnyama. Lilitia kinyaa kulitazama maungo yake.
Nikajifuta midomo nikaitazama. Hapakuwa na damu!! Na sikuwa na kiu tena. Kumbukumbu za kumshambulia yule mganga wa jadi zilikuwepo akilini na pia tukio la kumnyonya shingoni lilikuwa linaishi katika akili yangu. Sasa mbona hakuna damu. Mbona mashuka hayajachafuka.
Nikavaa nguo zangu huku nikiziona dalili za kufa mbele yangu.
Nikamtikisa yule daktari pale kitandani. Hakuamka. Na alidumu hivyo hadi nilipotoka. Hatua kwa hatua. Hadi nikatoka nje, hofu ikiwa inaniadhibu.
Sikusimama sana barabarani nikapata taksi.
“Nyegezi kona.”
“Nyegezi?” aliniuliza. Nikakubali.
Akawasha gari tukaondoka. Sikutaka kuzungumza lolote. Nilikuwa najiuliza ni kipi kinanitokea mfululizo kiasi hicho.
Simu yangu ikaita. Nikaitoa nikiamini ni Maria. Hakuwa yeye alikuwa Dokta Davis.
Nikachelewa kupokea. Ikawa imekatika.
Nikategemea atapiga tena! Hakupiga badala yake akatuma ujumbe.,
“Nakutakia usiku mwema!” sikumjibu.

****

Amani ikatoweka kabisa moyoni mwangu. Sikuyafurahia maisha yangu ya chuo. Sikuifurahia tena kazi niliyopewa na dokta Davis na kampuni yake.
Nikiwa nimejaribu kwa waganga na kushindwa kupata msaada wowote. Na sikuwa nikiamini sana ulokole na imani za uponyaji sasa niliamua LIWALO NA LIWE. Nitailea mimba yangu hadi nitakapojifungua.
Lakini nitakuwa na amani sana iwapo sitakuwa nachangamana na makundi ya watu. Na ili nisichangamane basi nilitakiwa kuiachia kazi niliyokuwa nimeipata. Kazi yenye kipato kizuri kabisa.
Nikatokwa na machozi nilipofikiria kuandika barua ya kuacha kazi!! Roho iliniuma sana.
“Na chozi langu likuangukie wewe uliyeniletea makwazo haya!!” nilitamka hayo wakati naweka nukta ya mwisho ya barua ile ya kumweleza Davis na kampuni yangu nia ya kuachana na kazi yao.
Sikuweza kuwaelezea kuwa nilikuwa na mimba. Niliwaambia shule imenibana sana na utendaji wangu kimasomo ulikuwa umeshuka sana.
Nikaituma kwa njia ya barua pepe kwenda kwa Dokta Davis.
Barua ikawa imefika!
Nikayasubiri majibu.
Zile milioni milioni ziliniuma sana kuziacha ziende mbali nami.
Lakini sikuwa na ujanja. Laana zangu kwa mbaya wangu!!

****


ISABELA ameamua kuachana na kazi iliyokuwa inamuingizia kipato kikubwa.
Je? Barua yake itakubaliwa?

Nini hatma ya MIMBA YAKE!!!

ITAENDELEA.
See More

No comments:

Post a Comment

Recent Posts