Saturday, December 8, 2012

SITAISAHAU facebook

MTUNZI: Emmy John P.

MAWASILIANO: 0654 960040


SEHEMU YA KUMI NA MBILI


Nikawasha taa lakini nikahisi maumivu makali katika mikono yangu, Kheee!nikashtuka kukuta mikono yangu imevimba na ina alama ya kama michirizi hivi, hofu ikanitanda mhh!! ina maana ilikua ya kweeli ama? Kama ni kweli kwa hiyo John amempeleka wapi mama yangu? Wamempeleka wapi mwalimu Nchimbi!! Nikaendelea kutahamaki. Hali hii sasa ilikuwa ya hatari kupita zote. Gusa popote katika maisha yangu ila chunga usimguse mama yangu.

Kama hii ni kweli John lazima anieleze ni wapi wamempeleka!! Nilijiapiza.

Uwiii!!! simu yangu iko wapi nimpigie mama kama yupo salama, nilijisemesha mwenyewe huku nikiomba kisiwe kimetokea chochote kama ilivyo kwenye ndoto, nikapata simu yangu nikajaribu kumpigia hapatikani!! Nikaogopa kukubaliana na ukweli huo.

Mungu wangu mama hapatikani ana nini jamani? nilijiuliza hivyo huku nikisahau kuwa huo ulikua usiku na inawezekana akawa kazima simu..ilikua kama saa tisa za usiku..nikampigia baba naye akawa hapatikani, hofu ikanizidi nilitamani nipae nifike nyumbani nijue nini kimejili, lakini huo uwezo sikua nao..ghafla nikapitiwa na usingizi.

Bila kujua hatma ya mama!!!


Nilishtuka kutoka usingizini baada ya simu yangu kuita kwa mda mrefu, kuangalia jina ni la mdogo wangu, usingizi wote ukaniisha nikakumbuka ile ndoto ya usiku, hofu ikanitanda nikawaza au mdogo wangu alikua ananipigia kunipa habari za msiba wa mama? mara simu ikakatika.

Nikampigia mdogo wangu!!! Nijue kulikoni, wakati huo natetemeka mwili mzima. Jasho likinitoka. Sikutaka kuamini hii ndoto.

Kwa hili nilichanganyikiwa kuliko vipindi vyote nilivyowahi kuchanganyikiwa!!


*Tumepafikia sasa patamu Isabella anaapa kuwa kama John amemgusa mama yake lazima adili naye kikamilifu.

ITAENDELEA……Siri imekaribia kufichuka.

Simu ikaita. Mara ya kwanza haikupokelewa!!!
Nikazidi kutetemeka!!!
Mara ya pili simu ikapokelewa.
“Dada..shkamoo.”
Alinisalimia. Sikuweza kumjibu. Nikamuulizia mama. Akasita kunijibu. Nikamsikia akihema juu juu. Wasiwasi wangu ukazidi.
“We Helena!!” nilimuita katika simu.
“Abee!!” aliniitikia.
“Si nimekuuliza kama mama ni mzima.”
“Yeah! Ni mzima. Ila ana homa.”
“Naweza kuongea naye sasa hivi?.” Nilimuuliza hakujibu swali lile akazalisha mengine. Nikaanza kuiamini ndoto yangu!!!
“Niambie mama ana nini?” sasa nilimkaripia.
“Mama ana homa kali amelala!!.”
Nikakata simu. Nikasimama wima. Hofu kuu!!

Nifanye nini sasa!! Nilijiuliza. Kisha nikaamua kwa ujasiri kumtafuta John. Nikabonyeza namba zake. Nikawa nasikiliza huku nikitawaliwa na uoga.
Simu yake haikuwa hewani. Wasiwasi ukazidi.
Ina maana John ndio ameenda Makambako kwa mwalimu Nchimbi!! Nilijiuliza. Sikupata jawabu. Hakuwepo wa kunijibu vilevile.
Ilikuwa lazima nifanye kitu. Hapakuwa na muda wa kujilaza tena!!!
Nikaufunga mlango nikatoweka!!
Teksi niliyochukua ikanifikisha nyumbani kwa John. Nilikuwa nimeamua kuitoa siri yote ilimradi kuokoa maisha ya mama. Nilijiuliza John atanifikiriaje kwa haya mashairi ambayo naenda kumuimbia. Litakalokuwa na liwe!! Nilijitia imani.
Kama nilivyopiga simu ya John bila kupokelewa ndivyo ilivyokuwa katika mlango wake. Mlango haukufunguliwa na yeyote. Nilibaki katika mshangao hadi alipofika jirani yake na kunitaarifu kuwa hata yeye hajui John alipoenda, ni masaa kadhaa yalikuwa yamepita.
Nilikubaliana naye. Nikatoweka, moyoni nikiwa nazidi kuifuga hofu.
John hapatikani nyumbani kwake masaa yamepita, mama yangu ana homa kali. Matukio haya yanayowiana yalinitia mashaka. Mama yangu amekufa! Niliwaza huku nikiichukia hali iliyonikumba. Sikujua ni uelekeo upi natakiwa kwenda, nilisimama chini ya mti nikaanza kuwapigia simu rafiki zake John, wote wakakiri kuonana na John lakini masaa kadhaa yaliyopita. Hakuna aliyemuona muda mfupi uliopita.
“Hakuwa na safari yoyote?” Nilimuuliza mmoja wao. Akapinga hoja hiyo. Nikazidi kuumia.

Nilirejea nyumbani kwangu nikiwa nimekata tamaa sana. sikuweza kulala wakati jina la mama likinishambulia kichwa changu.
Nilijaribu mara kwa mara kupiga simu ya John. Hali ikawa ileile.

Hatimaye nikafikia maamuzi binafsi. Nikaamua kurejea Makambako nikashuhudie tatizo gani limemsibu mama yangu.
Kama ilivyokuwa awali nikazungumza tena na kiongozi wa darasa kwa ajili ya kunitetea kwa lolote litakalotokea mimi nikiwa safarini.
Nikampatia kiasi kikubwa cha pesa ili kumshawishi zaidi. Akashawishika.

****


Ndege ndogo ya shirika la serikali ilitua katika uwanja mdogo wa ndege Iringa mjini uliojulikana kwa jina la Nduli. Nilitamani kushuka upesi upesi lakini ulikuwepo utaratibu wa kushuka.
Hali ile ua kupanda ndege kama wengine wanavyofanya kwenye magari ilinifanya niamini kuwa pesa ndio kila kitu. Wachache wangeweza kuamini kuwa nilikuwa jijini Mwanza masaa yaliyopita kisha nikawa jijini Dar na sasa mjini Iringa.
Kitendo cha kusubiri basi kuelekea Makambako na chenyewe nilikiona ni cha kupoteza muda. Nikakodi gari aina ya Noah.
“Mwendo mkali tafadhali!” nilimsihi.
Safari ikaanza.

Hali ya mama ilikuwa mbaya zaidi ya homa aliyonielezea mdogo wangu kwenye simu. Ule muda waliokuwa wanashangaa nimefika vipi Iringa mimi niliutumia kumshangaa mama jinsi alivyokuwa anatokwa jasho huku akitetemeka. Alitokwa na vipele vya baridi na kuacha maswali kama anahisi baridi ama la! Maana wakati huo pia jasho lilimiminika.
“Mmeenda hospitali?.” Niliuliza swali langu la kwanza. Hakuna aliyenijibu. Nikawatazama nikingojea majibu.
Dada yangu akanijibu kuwa walikuwa na mpango huo. Nikatambua anamaanisha nini.
Upesi nikamwagiza mdogo wangu akaenda kuchukua teksi na baada ya muda kidogo mama alikuwa katika machela za akikimbizwa katika wodi ya wagonjwa mahututi. Hospitali ya Ilembula.

Madaktari walipima vipimo vyote. Kama nilivyotegemea. Mama hakuwa na ugonjwa wowote. Lakini ajabu!! Alikuwa amezimia. Mama hakuwa akiongea.

Baada ya siku nne tukashauriwa kumrejesha mama nyumbani.
Hatukuwa na ujanja tukarejea na mzigo wetu, akawa anahudumiwa chakula kwa njia za mipira. Wakati dada na mdogo wangu wakijiuliza nini kimemsibu mama, nilibaki na siri nzito sana. niliamini kabisa tatizo hili la mama linahusiana kabisa na ile ndoto.
Kwa hiyo John ni mchawi!!! Nilijiuliza.
Kama ni mchawi basi huyu napambana naye kishirikina. Dawa ya moto ni moto!! Nilijiapiza lakini sikuweza kumshirikisha yeyote kati ya dada ama mdogo wangu. Imani zao za kilokole zilipingana na matendo haya.
Nikaamua kufanya kimya kimya!! Ilimradi kuokoa maisha ya mama.

Kwa mara ya kwanza nikaingia katika kibanda kidogo cha mganga wa jadi. Nje nikalisoma bango akiwa anajisifia kuwa yeye ni bingwa katika Nyanja tofauti tofauti.
Nilijielezea tatizo langu. Akasema hilo ni tatizo dogo sana. akazungumza lugha alizozijua yeye. Akafoka sana hatimaye akaanza kucheka kama tahira vile. Mwisho akanipatia dawa na maelekezo.

Nikatimiza yote aliyohitaji lakini hakuna kilichobadilika.
Siku zilizidi kusogea, na kipindi cha mitihani kikajongea zaidi. Nikawa katika mitihani mingi kwa wakati mmoja.

Uamuzi wa mwisho niliofikia ni kuondoka na mama akiwa mgonjwa hivyo hivyo. Pia nikaondoka na dada yangu kwa ajili ya kumuhudumia.
Nyumbani akabaki mdogo wangu pamoja na baba.


****

Nilikuwa na pesa na zilizidi kuongezeka lakini ajabu nilikuwa nakonda sana. si ugonjwa wa mama pekee ulionifanya kuwa hivyo bali ile ndoto ya John akishirikiana na Osmani kumchukua mama yangu katika namna ya kuumiza. Walikuwa wanambuluza chini. Sasa mama yupo hoi kitandani. Ajitambui. Na yeye John hajulikani alipo. Maajabu!!
AFE AMA UKUBALIANE NA MIMI!! Niliukumbuka ujumbe huo, niliotumiwa siku chache kabla mambo hayajaharibika. Nikaanza kujiuliza ni kitu gani kilimaanishwa. Kisha nikaikumbuka ile namba +6666666. Haraka nikakimbia chumbani, nikachukua simu nikaingiza zile namba. Simu ikaita lakini haikupokelewa. Nikajaribu tena na tena hali ikabaki kuwa kama ilivyo.

Wiki moja ilipita. Nilikuwa najilazimisha kwenda chuo. Na siku hii pia nilikuwa nimeenda.
Lakini hali ya pale chuoni niliona kama hainifariji kabisa. Nikaamua kurejea nyumbani majira ya mchana walau nimuone mama yangu!!
Nilipofika getini kabla ya kugonga nilisita. Kwa mbali nilisikia vurumai ikitokea ndani. Na hakuwepo mtu zaidi ya dada yangu pale ndani.
Au mama ameshtuka!! Nilijipa imani. Lakini haikudumu kwa muda mrefu. Mlango ukafunguliwa nikamwona mwanaume.
Ina maana Suzi ameanza kuingiza wanaume hapa ndani!! Nilikisia kwa mashaka. Kisha nikaamua kuulinda ushahidi. Nikafungua geti nikutane na yule mwanaume nimuhoji. Tayari nilikuwa nimekasirika.

Kwa mwendo wa upesi nikaingia ndani. Hatua za harakaharaka sasa nikawa naklabiliana na yule mwanaume. Tofauti na mategemeo yangu kuwa atashtuka. Aliunyanyua uso wake akanitazama. Nilitaka kukimbia lakini mwili ukawa dhaifu. Sijui kama alikuwa anajaribu kutabasamu au alikuwa anazomea. Uso wake ulikuwa umevimba sana na ulikuwa umechubuka. Ni kama alikuwa amekwanguliwa.
Mwanaume huyu wa ajabu akasimama wima akajaribu kuongea akashindwa akanielekeza kwa vitendo kama ananizuia vile kuingia nyumbani kwangu.
Kuna nini sasa!! Nilijiuliza.
Akazidi kunisisitiza kwa vitendo nisiingie. Hakuweza kutoa sauti.
Kabla hata sijajua nimjibu vipi kwa ishara alinyanyua miguu yake akaliendea geti akatoweka.
Akaniacha nikiwa katikati ya kuingia ndani ama kurejea getini. Hali yake usoni ilinitia mashaka sana, nilihisi na mimi nikiingia nitatoka kama yeye. Uoga ukatanda!!
Bado sikujua nifanye nini. Sikukumbuka hata kumpigia simu Suzi ambaye ni dada yangu. Nikaanza kunyata kuusogelea mlango, kisha nikaghairi nikaliendea geti nikalifungua likawa wazi kabisa.
Nikaufikia mlango nikataka kuufungua, roho ikawa inasita.
Niligundua kuwa nilikuwa natetemeka sana!! nikakishusha kitasa. Mara nikasikia vishindo vikisogea kwa kasi pale mlangoni. Mawazo yangu yakaenda moja kwa moja kwa kiumbe ambacho kimemtia majeraha yule bwana niliyepishana naye. Mbio! Nikatimua.
Nyuma vishindo vikaendelea kunifuata kimyakimya.
Ilikuwa vyema kwamba nililiacha geti wazi. Nikapenya na kuzidi kukimbia. Sasa mdomo ulifunguka nikaanza kupiga kelele kama chizi. Huku ninazidi kukimbia!!!
Nilipoweza kugeuza shingo kutazama nyuma. Kweli kilikuwa kiumbe cha ajabu!! Kiwiliwili kile kilikuwa kimevaa nguo za dada yanu. Suzi. Lakini usoni hakuwa Suzi. Huyu naye alikuwa ameumuka uso wake. Alikuwa anatisha. Nikiwa nimejikita mawazo yangu katika kumtathimini yule kiumbe anayenikimbiza mchana kweupe mara nikajikwaa.
Yule kiumbe naye akawa ananikaribia!!!


ITAENDELEA

No comments:

Post a Comment

Recent Posts