Sunday, December 9, 2012

SITAISAHAU facebook .....13


MTUNZI: Emmy John P.

MAWASILIANO: 0654 960040

SEHEMU YA KUMI NA TATU 

 

ILIPOISHIA

Nikaufikia mlango nikataka kuufungua, roho ikawa inasita.

Niligundua kuwa nilikuwa natetemeka sana!! nikakishusha kitasa. Mara nikasikia vishindo vikisogea kwa kasi pale mlangoni. Mawazo yangu yakaenda moja kwa moja kwa kiumbe ambacho kimemtia majeraha yule bwana niliyepishana naye. Mbio! Nikatimua.

Nyuma vishindo vikaendelea kunifuata kimyakimya.

Ilikuwa vyema kwamba nililiacha geti wazi. Nikapenya na kuzidi kukimbia. Sasa mdomo ulifunguka nikaanza kupiga kelele kama chizi. Huku ninazidi kukimbia!!!

Nilipoweza kugeuza shingo kutazama nyuma. Kweli kilikuwa kiumbe cha ajabu!! Kiwiliwili kile kilikuwa kimevaa nguo za dada yanu. Suzi. Lakini usoni hakuwa Suzi. Huyu naye alikuwa ameumuka uso wake. Alikuwa anatisha. Nikiwa nimejikita mawazo yangu katika kumtathimini yule kiumbe anayenikimbiza mchana kweupe mara nikajikwaa.

Yule kiumbe naye akawa ananikaribia!!!

ENDELEA


Maajabu yule kiumbe aliponifikia na yeye hakuwa akizungumza lolote kama yule. Ishara za vidole zikawa zinanielekeza jambo fulani. Sikuelewa lolote!! Cheni yake shingoni ikanifungua akili kuwa yule alikuwa ni dada yangu!! Lakini sasa amekuwaje.
Sikupata jibu umati ukawa umetuzunguka! Kila mtu akitaka kuhoji na kufahamu nini kimetokea. Suzi aliwashangaza wengi sana. Alikuwa amevimba na hakuweza kuzungumza lolote.
Kwa ishara hizohizo sasa akaanza kuwaelekeza washangaa ji wengine wakamfuata. Baadhi wakiwa na silaha mikononi. Wanawake wakiwa nyuma nyuma…..na baada ya kuifikia nyumba kila mtu akawa anaogopa kuingia ndani ya nyumba yangu. Nyumba ambayo niliizindua kwa mbwembwe za hali ya juu. Nilifadhaika.
Mwanaume mmoja aliyekuwa ameshikilia kisu tayari kwa lolote litakalokuja mbele yake aliingia ndani. Sisi tukabaki kushuhudia nini kitatokea. Suzi ambaye bado sura yake ilikuwa imeumuka alikuwa amejiweka mbali kabisa huku akionekana kutawaliwa na uoga.
“Mbona hamna kitu!!” Alizungumza yule mwanaume baada ya kutoka. Mmoja baada ya mwingine wakaanza kuingia katika nyumba yangu. Hakuna madhara waliyopata.
Suzi alikimbizwa hospitali. Baada ya siku tatu aliweza kuzungumza.
Kumbe yule mwanaume ambaye nilikutana naye siku ya tukio akiwa ameumuka usoni alikuwa ni kiongozi wa kiroho katika kanisa analolifahamu Suzi maana yeye ndiye alimleta kwa ajili ya kumfanyia maombi mama yangu mzazi.
Wakiwa katika maombi mara akaanza kiongozi wa kiroho kulalamika huku akiwa chini anagalagala hovyo. Hakuwa akinena kwa lugha lakini alikuwa akilia kwa kabila la kwao huku akimlaani paka aliyekuwa amemkaba koo huku akimshambulia.
Suzi alikuwa anashangaa tu mtu huyo akilia na kuomba msaada. Baadaye alitulia. Huo mda aliotulia tuli ndio ambao Suzi aliutumia kumsogelea. Dhahama ikahamia kwake!!
Sasa aliweza kumuona paka mkubwa rangi nyeusi!! Paka akamkwaruza kadri alivyoweza. Suzi alikimbilia chumbani lakini bado hakumkwepa paka huyu.
Wakati nafika na kuufungua mlango ndio wakati huo ambao paka alipotea na kumwacha Suzi ambaye alitimka mbio na kunikuta mimi nikiwa nimeanza kukimbia tayari.
Sasa alikuwa ameweza kuongea.
“Ajabu paka huyu hajamdhuru mgonjwa.” Suzi alishangaa. Nami nikashangaa zaidi. Paka hakuwa amemjeruhi mama hata kidogo!.
Simulizi hiyo ya Suzi iliniogopesha sana. nikamualika rafiki yangu Maria aishi nasi kwa muda. Wiki ya kwanza tangu afike pale. Mambo yalikuwa vizuri tu. Hapakuwa na mauzauza na michubuko katika paji la uso wa Suzi ilikuwa inafifia.
Jioni moja nilikuwa najisomea kwa maandalizi ya mitihani iliyokuwa imekaribia. Suzi ambaye hatukuwa tunasoma darasa moja alinikatisha kidogo. Akaleta maongezi yanayohusiana na imani za kishirikina juu ya kupote kwa John. Nilitega sikio nikamsikiliza kwa makini hadi akayamaliza maongezi yake.
“Ujue nini Bela hapa kuna mtu hawapendi anakufanyizieni” alizungumza huku akiwa amenikazia macho binti huyu wa kisukuma.
Kimya nikawa namsikiliza!!
“Na hapa ukilemaa wanampoteza na mama.” Alitamka maneno yaliyonishtua. Sasa hapo nikamtilia maanani. Ushauri wake wa mwisho akanisihi niende kwa mganga wa jadi kabla mama hajachukuliwa.
Kwa kuwa aliweka neno mama sikuwa na ujanja. Siku mbili baadaye nikaingia kwa mganga wa jadi kwa mara ya pili.
Mara anikwangue kiganja mara anikwangue kichwani mzee huyu!! Mimi kimyaa namsikiliza atasema nini. Akaomba pesa akapewa.
Akatoa masharti yake!! Hayakuwa magumu sana. tukatii na kuondoka.
Alituomba turejee baada ya wiki moja. Tuliporejea tukakuta matanga. Mganga mjanja mjanja hakuwa nasi tena duniani. Alikuwa amekufa!! Kifo cha ghafla. Siku moja baada ya sisi kuondoka pale.

Taarifa ile kila mmoja kati yangu na huyo rafiki yangu tulipokea kimshtuko. Hasahasa mimi. Nilijiuliza kwa nini? Sikupata jibu.
Maisha yakaendelea!!

Hapakuwa na mauzauza tena. Na kizuri zaidi hatimaye mama alizinduka kutoka katika usingizi ule wa kifo. Suzi akajivutia kwake kwamba ni maombi yamemwamsha, mimi sikuwa na lolote la kusema.
Mama hakuwa na kumbukumbu yoyote ile, alibaki kushangaa shangaa tu. Kwetu ilikuwa siku ya furaha sana. furaha iliyopitiliza. Sasa mama aliweza kula peke yake na hakuhitaji msaada tena. Walau furaha yangu ikarejea huku nikisahau kuhusu imani za kishirikina na kuamini mama alikuwa katika ugonjwa wa kawaida tu!!
Sasa vipi kuhusu John na ile ndoto niliyoiota? Nilijiuliza. Maana mama alikuwa amezinduka lakini John bado hakuonekana. Chuo kilishindwa kusema lolote maana mwanafunzi wa chuo kikuu anachukuliwa kama mtu mzima hakuna anayemlinda, hakuna uzio uliowekwa kumzuia asitoke, hivyo maisha ya mwanafunzi wa chuo yapo mikononi mwa msomaji mwenyewe. Chuo kitasema nini kuhusu kutoweka kwa John!! Ajabu ni kwamba hakutoweka katika mazingira yoyote yanayoelezeka bali ni ghafla tu akagundulika kuwa hayupo chuo
Nami nikaichukulia ile taarifa kma ilivyo. Kwanza upendo wangu kwa John ulikuwa umepoa sana. nilikuwa nimeanza kuhisi kuwa huyu si mtu mzuri kwangu.
****
Baada ya siku tatu. Mama akiandamana na dada yangu Suzi walirejea Makambako. Kama kawaida pesa ilikuwepo. Kwa nini sasa mama yangu asipate jambo la kukumbukwa maishani. Na Suzi naye apate la kujitambia kwa walokole wenzake. Nikawapandisha ndege. Sasa nikabaki kuishi peke yangu tena!! Sikuwa na uoga mkubwa japo sikumruhusu rafiki yangu huyu kuondoka. Tukaendelea kuishi wote.
Usiku huu ambao mama yangu alikuwa ametoweka nilikumbwa na hisia ama jambo la ajabu katika mwili wangu.
Kichwa kilikuwa kinauma, nilijaribu kumeza dawa lakini hazikunisaidia sana zaidi ya kuniweka katika majaribu ya kupitiwa na usingizi.
“Maria!! Mi nalala shosti.” Nilimwambia rafiki yangu. Alikuwa amejikita katika kuangalia filamu. Hivyo hakuitilia maanani sana taarifa yangu.
Mguu na njia nikakivamia kitanda nikaanza kuutafuta usingizi. Mara hizo hisia za kuumwa kichwa zikatoweka. Nikawa katika hisia nyingine zinazokera. Nikaanza kumkumbuka sana John . nikaukumbuka usiku ule mimi na yeye katika hoteli ya kifahari. Nikakumbuka pia jinsi nilivyoanza kuishi naye kama mchumba wangu. Mara nikayakumbuka mapenzi yake.
Ni hapa sasa nikaanza kuhangaika!! Nilikuwa namuhitaji John.
Nilikuwa nahitaji awe nami kitandani!! Lakini hakuwepo.
Nilitaka kujilazimisha kuamka niweze kukabiliana na hisia hizi lakini sikuweza. Nikahisi macho mazito sana!!
Mara likawa giza nene!! Kisha ndani ya sekunde kadhaa nikajihisi kama nina mikono ya ziada najipapasa. Mh!! Nikataka kufumbua macho bado yalikuwa mazito.
*****
Nilikuwa nimejilaza na kanga niliyokuwa nimeivaa wakati naandaa chakula. Ile mikono ya ziada nikawa naisikia kabisa ikiiondoa bila idhini ya akili yangu!! Nikajilazimisha kuamka. Sikuweza. Sasa nilikuwa sina nguo mwilini.
Kisha ile hali ya kumkumbuka John ikazidi. Nikawa katika kuhitaji huduma fulani hivi ambayo ni John pekee aliweza kunitimizia.
Sikuchukua muda mrefu nikapata kile ninachokitamani. Lakini lilikuwa kama gogo limeniangukia kifuani. Nikaanza kupalangana kulitoa. Pumzi zikazidi kuniishia lile gogo halikutoka kifuani kwangu. Sijui kama zilikuwa dalili za kufa ama vipi.
Jamani nakufaaa! Nilipiga mayowe. Sijui kama sauti ilikuwa inatoka ama la! Hofu ya kifo ikanitawala.

“He!! We naye unalala uchi? Kulikoni leo?” Niliisikia sauti ikiniuliza. Nikadhani bado nina lile gogo kifuani. Nikanyanyuka kwa nguvu sana. Maria alikuwa akitazamana nami uso kwa uso. Alinishangaa nami nikamshangaa.
“Unaota wewe!”
“Kwani kuna nini?” Nilimuuliza huku nikijishangaa kweli nipo kitandani, uchi kabisa. Halikuwepo lile gogo pale kitandani.
Wasiwasi ukatanda!
“Kweli ni ndoto..ndoto mbaya.” Nilimuunga mkono Maria.

****

Haikuwa ndoto kama nilivyodhani na kujiaminisha kuwa ile kanga ilitoka bahati mbaya katika mwili wangu. Kichefuchefu na kukosa hamu ya kula kukanikimbiza hospitali.
Mimba!!! Yalikuwa majibu.
Sijui kama akili iliniruka nikamkunja daktari ama ni mizimu ilifanya hivyo. Sijui!!
Daktari akatapatapa akanitoa na kunituliza. Huku akisisitiza kuwa ninayo mimba.
Maajabu haya!! Nimeipatia wapi hiyo mimba.
Mimi ni muelimishaji wa mambo ya kimapenzi jinsi ya kujilinda na magonjwa ya zinaa na mimba zisizotegemewa. Sasa nina mimba ya maajabu!!
Nimshirikishe Maria? Nilijiuliza. Nikasita. Maria alikuwa mropokaji sana angeweza kunisambazia habari hiyo na heshima yangu ikashuka.
Nikimueleza mama atanilaani!! Maana alikuwa akiniamini sana. bora basi angekuwepo John ningesema ni ya kwake.
Sasa hapa namsingizia nani?
Hapana sina mimba mimi!! Nilijikataa penye ukweli.
Nikaenda hospitali nyingine. Jibu lilikuwa MIMBA.
Akili ikahama, na nikaanza kuamini kumbe ule mtihani wa mama kupoteza fhamu ulikuwa mdogo sana. kumbe tatizo likikukumba wewe ndio utaugundua uzito wake.
Nikimbilie wapi Isabela mimi!!! Nilitaharuki.

Hisia zangu zikaenda kwenye lile gogo usiku ule. Nikajiona nimedhalilishwa kupewa mimba na gogo. Tena ndotoni!! Chumbani kwangu.
Eeh!! Mungu nionee huruma mja wako. Nilikumbuka kumshirikisha sasa Mungu.

*****

Dada yangu Suzi. Alikuwa ni mlokole lakini licha ya hayo yote alikuwa jasiri katika kutunza siri. Hili lilifahamika kwetu sote tangu tukiwa wadogo. Alitunza siri nyingi sana kifuani mwake. Siri za baba, siri za mama, zote alizibeba bila kuzitoa.
Nikamuona mlokole huyu ni mtu sahihi katika kumueleza linalonisibu.
Nikampigia simu tukapanga wakati tulivu kabisa wa kuzungumza.
Tukapendekeza iwe usiku. Mumewe akiwa ameingia kazini.

Usiku ukafika nikampigia simu.
“Dada, yaliyonikuta ni makubwa mdogo wako…” nilianza kumuelezea mkasa ulivyokuwa huku nikisita kumshirikisha ukweli kuwa kuna ndoto ikiambatana na hisia ilinishika na nikahisi nafanya mapenzi ndotoni. Nilihofia ataleta ushauri wa kwenda kwa wachungaji feki kuombewa. Sikutaka kabisa kusikia mambo hayo.
Nilipomaliza ukawa wakati wake kunishauri ama kusema lolote.
Kwa sauti tulivu tena iliyojaa unyenyekevu Suzi alianza kunieleza neno kwa neno.
Sasa nikaanza kutetemeka alipoyatamka haya. Nikaketi chini, mapigo ya moyo yakaongezeka. Nikatamani nife kwa muda. Kisha nikakumbuka kuwa nilikuwa naogopa kufa!!! Nikalipuuzia wazo hilo.
Wasiwasi ukazidi. Lakini Suzi alikuwa akiusema ukweli aliouficha moyoni kwa muda mrefu.

**SUZI anamweleza nini Isabela…hadi anapatwa hofu kiasi hicho?

**HIYO MIMBA imeingia vipi? JOHN yupo wapi?

ITAENDELEA!!

No comments:

Post a Comment

Recent Posts