Saturday, December 8, 2012

SITAISAHAU facebook


MTUNZI: Emmy John P.

MAWASILIANO: 0654 960040


SEHEMU YA KUMI NA MOJA


ILIPOISHIA


Nikataka kwenda kumuangaza nje. Lakini sikuona maana hiyo nikataka kumuita, mdomo ukawa mzito sana. Nikageuka huku na huko. Hola!! Nikageuka tena. Hakuna kitu.

Nikajisonya!! Kisha nikaguna mwenyewe kuwa ninamtafuta mtu gizani.

Mpuuzi kweli mimi!!! Nikasogea ukutani nikaanza kupapasa. Nikakipata kiwashio, nikabonyeza. Waaa!! Pakapendeza.

Nikageuka. Waaaa!!! Mdomo wazi, mtu anakula chakula.

Pwaaaa!! Nikaachia kikopo na glasi.

Osmani!!!

Osmani anakula chakula nilichopika mimi.

“Kaa hapo sahivi jamaa si amelala au.” Aliniambia kwa sauti isiyosikika vizuri, alikuwa na pande la nyama mdomoni.

Puuuu!! Nikaanguka. Lakini fahamu zipo pamoja nami. Namtazama Osmani. ***OSMANI ni nani katika simulizi hii ya kushangaza….simulizi iliyoanzishwa na kukutana na mwanaume facebook…kanitajirisha sasa nipo katika mabalaa.


ENDELEA.

“John!!!! John!!!” Nilianza kuita kwa sauti ya juu sana. Osman alinitazama akacheka huku akijiziba mdomo. Nikaita tena. Hakuna John aliyetokea kunisaidia.
“Amelala wewe acha kelele.” Alinionya Osman ambaye sasa alikuwa amemaliza kula na alikuwa anakunywa maji. Nikamshangaa. Alikuwa ananijibu bila wasiwasi wowote.
“Unajua nini Isabela. Tulia tuzungumze, mbona haya mambo madogo tu!!.” Aliendelea kuzungumza Osmani. Kidogo nikatulia sasa, akafanya tabasamu kisha akaendelea kuongea.
“Nimefuata kitu kimoja tu hapa!! Kimoja tu.”
“Nini?.” Niliweza kumuuliza sasa. Nikijilazimisha kuwa jasiri.
“Kitambulisho changu.” Alinieleza huku akiwa amenikazia macho. Sauti yake ilisikika vyema kabisa. Hakuwa katika kutania hata kidogo.
“Kitambulisho? Kitambulisho gani?.” Nilihoji. Bado nilikuwa chini.
“Kile nilichokupa siku ile. Pale wapi sijui. Unapajua wewe.”
“Sina kitambulisho cha mtu.” Nilijibu kwa jeuri.
Kama vile jibu lile lilikuwa sawa na kumtukana aliruka akanifikia, kiganja chake kikanyooka akanitandika kofi moja. Maumivu yakapenya hadi mahali machozi yalipojihifadhi, yakatoka kwa fujo huku kilio nacho kikisindikiza.
“Sasa nadhani unaweza kuniambia. Kitambulisho kipo wapi.”
“Nilikichoma moto.” Nilijibu huku kigugumizi kikinitawala na kilio cha kwikwi.
Yule bwana akakodoa macho baada ya kuisikia taarifa hiyo.
“Umefanyaje?” aliniuliza, sikumjibu. Nilikua natetemeka sana, nilianza kumuogopa sana Osmani, kwanza niliwaza kile kitambulisho ni cha John iweje aseme chake? na kwanini siku ile alinipa akasema nilikidondosha? Mhh!! Ushirikina!! Nilianza kuamini kwenye imani hizo ambazo nilikuwa siziamini kabisa hapo kabla.
Wanafunzi wa SAUT wanaanza kuniroga, wananionea wivu!! nilihisi
“ Isabella Isabella!!alinishtua John kutoka kwenye mawazo niliyokua nayo, nilipoangalia kwenye kiti alipo kaa Osmani nikapigwa na butwaa! Osman hakuwepo, Kheeee!! Nikashangaa, John akafikiri nimemuitikia yeye akatoka kutoka kwenye mlango wa chumbani alikosimama akanifuata. Uso wake ulikuwa umetawaliwa na uzembe wa usingizini. Bila shaka alikuwa ametoka kuamka.
“Vipi baby mbona upo mezani? nilishangaa chumbani sikuoni, chooni haukuwepo kulikoni mpenzi au njaa”? Aliniuliza John kwa sauti ya kukwaruza kwaruza. Bado nilikuwa nimekaa chini palepale nilipoanguka baada ya kumshuhudia Osmani akiwa ndani ya chumba changu. Nilishindwa nianze kumjibu vipi John.
Mdomo ulikuwa mzito. Pepo la usingizi lililokuwa linamkabili John lilizidi kutwaa nafasi. Akaonekana kushindwa kuvumilia. Akajivutavuta kuelekea chumbani. Mh!! Nibaki peke yangu hapana!!! Nilikata shauri. Hata taa sikukumbuka kuzima nikatimua mbio. Nikamfuata John. Sasa nilikuwa katika wasiwasi mkubwa hii haikuwa ndoto tena!!!
Nilichokiona ni kweli kilikuwa kimetokea.
Nilifika chumbani na kumkuta John naye akimalizia kujifunika shuka. Nikaingia kwenye shuka kwa fujo. Hakuligundua hili vurumai labda kwa sababu ya usingizi mzito. Nikamkumbatia John huku nikitetemeka.
Hayawi hayawi hatimaye yakawa!! Asubuhi ikafika.
John wangu akaamka wa kwanza. Kuamka kwake kukanifanya na mimi kuukatisha usingizi wangu usiokuwa na ladha kabisa.
“Hivi jana ilikuwa ndoto eeh!!.” Alianzisha mazungumzo John.
“Umeamkaje mpenzi jamani.” Nikamkatisha kwa salamu, maana hatukuwa tumesalimiana. Akanijibu kisha akaendelea kuzungumza.
“Jana si nikaota aisee. Dah!! Ndoto nyingine nazo!! Ila kuota pesa ni dalili za utajiri.”
“Ndoto gani tena. Nikamuuliza.”
“Eti amekuja mgeni sijui ilikuwa nyumba gani. Umezungumza naye, alipotoka eti akakuachia wewe Cheque mezani sijui milioni ngapi huko. Nilipotokea si wivu ukawa umenizidi. Nikawa mkali. Akawa kama anahairisha kukupatia. Mi nikaondoka, baadaye nikawa nachungulia mh!! Akaiweka sijui chini ya sahani ile. Ulipotoka kumsindikiza nikawahi kufunua nikakuta amekuandikia kiujumbe hata sikukielewa. Sasa nikawa nakusubiri unieleze yule ni nani. Mara kuku wako haoo wakawika kumekucha tayari!!!” Alimalizia kwa kicheko kirefu John. Nami nikaungana naye. Tukacheka.
“Una wivu we mwanaume!!.” Nilimweleza.
“Ah!! Ndoto tu hizo.” Alifunga mjadala.

Wakati John anaingia kuoga, mimi niliamka na kuanza usafi wa hapa na pale. Nikiisaili nyumba yangu. Sasa nilikuwa sebuleni. Nilipofika pale palikuwa kawaida tu!!
Hivi kumbe jana nilikuwa naota!! Nilijisemea.
Nikaanza kutoa vyombo mezani. Tayari kwa kuviosha na ambavyo havijatumika nivirudishe mahala pake. Ni hapo ndipo nilipopatwa na mshtuko mwingine mkubwa. Chini ya sahani moja palikuwa na karatasi. Karatasi ya rangi ya kijani kibichi. Hili jani ama karatasi? Nilijiuliza. Nikajikaza nikausogeza mkono nikalishika.
Lilikuwa karatasi!! Nikalinyanyua kwa uoga mkubwa. Bado liliendelea kuwa karatasi. Mkono wa pili nao ukajisogeza ukalipakata.
Kisha nikaligeuza.
Maandishi!!! Ya rangi nyeupe. Kiswahili sanifu, maneno machache.
AFE AMA UKUBALIANE NAMI.
Nani sasa? Nikajiuliza.
UTAMFAHAMU HIVI KARIBUNI.. Maandishi yale yalimalizia kama yanayojibu swali langu. Mwisho zikawekwa alama ambazo nilihisi kuwa ni namba za simu. +666666666. Simu ya wapi hii!! Nilitafakari.
Nikahisi wazimu unataka kunipanda. Akili zikasogeleana niliposikia John akiufunga mlango wa bafuni. Nikatwaa kile kikaratasi nikakificha kabatini.
Sikutaka John agundue kitu chochote. Maana kugundua kwake kungesababisha nimueleze pia juu ya kitambulisho, pia juu ya mauaji aliyoyafanya ndotoni na sasa yametokea kweli. Haukuwa wakati muafaka wa kumueleza.

******

Jina langu Isabella lilizidi kukua katika chuo cha mtakatifu Augustino, wasichana wengi walitamani sana wawe kama mimi maana hakuna kitu ambacho nilikua sina, takataka zote za urembo nilikua nazo, cha ajabu mimi Isabella sikuonekana kuwa karibu na msichana yeyote yule, hata rafiki yangu Happy nilimsahau, hela kitu kingine bwana nilisahau mema yote aliyonitendea Happy maana maisha yalivyokua yananipiga mtu wa kwanza kumfuata alikua yeye lakini kwa wakati ule nilimsahau kabisa
Mtu wa jirani yangu alikua John nilisahau kabisa kuwa John aliniacha kwa ajili ya umasikini wangu, sikufikiria kabisa kuwa anaweza kuwa yupo nami kisa ya pesa nilizokua nazimiliki,pesa za kutotolea jasho zaidi ya kuwaelimisha tu watu kidogo. kweli mapenzi ni kipofu

****

Mama weeeeeeeeeeee!!!nilishtuka kutoka kwenye ndoto mbaya, ndoto iliyonitoa jasho jingi nililowa utafikiri nilijimwagia maji, Niliota nimeenda kwetu Makambako, siku hiyo tulienda kupamba ukumbi wa sherehe na mama yangu Mwalimu Nchimbi, tulimaliza saa tano usiku, hatukupata gari la kuturudisha nyumbani tukaanza kutembea kwa mguu, mara tukashangaa nyuma vijana wawili wanatukimbiza. Tuliamini kuwa walikuwa vibaka. Mama akaanza kukimbia na mimi nikafuata nyuma huku tukipiga makelele ya kuomba msaada, hatukupata msaada tukazidi kukimbia kwa juhudi zote na sasa kila mmoja akaanza kuchoka. Mama akasema maneno fulani ya kukata tamaa huku akimkabidhi Mungu madaraka ya kuamua kitakachotokea kwetu. Mimi sikuwa na neno la kuongezea nikiwa nimekata tamaa niligeuka nyuma kutazama vijana haoa watatuua kwa silaha gani. Badala ya kutilia maanani silaha zao kali walizobeba, macho yangu yakatua kwenye sura zao. Osmani!! Alikuwa anatabasamu. John!! Yeye alikuwa amekunja sura kwa ghadhabu. John wangu!!
Niliendelea kutulia nikitegemea maswali kutoka kwa viumbe hawa wasioonyesha huruma hata kidogo. Sikuulizwa swali.
Mara wakagawana majukumu. John akamwendea mama na Osmani akanifata mimi. Alikuwa ameshikilia kitu mfano wa mkia, aliponifikia akanitandika nao mikononi. Maumivu yakapenya nikatokwa na yowe kubwa sana nikaanza kugalagala. Akaniacha pale akamfuata mama. Wakasaidiana na John kumnyanyua mama halafu wakaanza kukimbia naye huku wakimburuza. Nilipiga kelele nikiwasihi wamuache mama yangu. Lakini hakuna walichobadilisha walizidi kukimbilia na kupotelea gizani. Nilipiga mayowe sana lakini hakutokea mtu wa kunisaidia. Nilipoanza kujigalagaza kwa kukata tamaa ndipo nikakutana na ardhi ya ajabu, ardhi inayonesanesa. He!! Ardhi ya wapi hii? Nilijiuliza huku nikijilazimisha kufumbua macho yangu, macho yalikuwa mazito sana kufumbuka. Nikajilazimisha hadi yakafumbuka. Nikakutana na giza nene, nikaanza kupapasa huku na huko, nikakutana na vitu vingine viwili vinabonyea nilipojilazimisha zaidi kuvitazama ndipo nikakutana na mito miwili katika kitanda changu. Na ile ardhi ndio hichi kitanda changu cha sita kwa sita. Ndoto!!!
Nikawasha taa lakini nikahisi maumivu makali katika mikono yangu, Kheee!nikashtuka kukuta mikono yangu imevimba na ina alama ya kama michirizi hivi, hofu ikanitanda mhh!! ina maana ilikua ya kweli ama? Kama ni kweli kwa hiyo John amempeleka wapi mama yangu? Wamempeleka wapi mwalimu Nchimbi!! Nikaendelea kutahamaki. Hali hii sasa ilikuwa ya hatari kupita zote. Gusa popote katika maisha yangu ila chunga usimguse mama yangu.
Kama hii ni kweli John lazima anieleze ni wapi wamempeleka!! Nilijiapiza.
Uwiii!!! simu yangu iko wapi nimpigie mama kama yupo salama, nilijisemesha mwenyewe huku nikiomba kisiwe kimetokea chochote kama ilivyo kwenye ndoto, nikapata simu yangu nikajaribu kumpigia hapatikani!! Nikaogopa kukubaliana na ukweli huo.
Mungu wangu mama hapatikani ana nini jamani? nilijiuliza hivyo huku nikisahau kuwa huo ulikua usiku na inawezekana akawa kazima simu..ilikua kama saa tisa za usiku..nikampigia baba naye akawa hapatikani, hofu ikanizidi nilitamani nipae nifike nyumbani nijue nini kimejili, lakini huo uwezo sikua nao..ghafla nikapitiwa na usingizi.
Bila kujua hatma ya mama!!!

Nilishtuka kutoka usingizini baada ya simu yangu kuita kwa mda mrefu, kuangalia jina ni la mdogo wangu, usingizi wote ukaniisha nikakumbuka ile ndoto ya usiku, hofu ikanitanda nikawaza au mdogo wangu alikua ananipigia kunipa habari za msiba wa mama? mara simu ikakatika.
Nikampigia mdogo wangu!!! Nijue kulikoni, wakati huo natetemeka mwili mzima. Jasho likinitoka. Sikutaka kuamini hii ndoto.
Kwa hili nilichanganyikiwa kuliko vipindi vyote nilivyowahi kuchanganyikiwa!!

*Tumepafikia sasa patamu Isabella anaapa kuwa kama John amemgusa mama yake lazima adili naye kikamilifu.
ITAENDELEA

No comments:

Post a Comment

Recent Posts