Wednesday, December 19, 2012

SITAISAHAU facebook-----------------23

 MTUNZI: Emmy John P.

MAWASILIANO: 0654 960040

SEHEMU YA ISHIRINI NA TATU

...
Nikafadhaishwa baada ya yule Davis ambaye sasa niliamini naenda kummalizia alipogeuka kuwa joka kubwa la kijania. Haraka nikawahi kujitoa lakini nilikuwa nimechelewa sana. Joka lile likawahi kujiviringisha kuanzia kiunoni likawa linapanda juu. Sasa lilikuwa limenifunga hadi kifuani.
Ajabu!! Lilikuwa linawasha sana.nilitamani kujikuna lakini haikuwezekana na mikono ilikuwa imefungwa tayari.
Nililiamuru liniachie lakini halikuiheshimu amri yangu. Nikazidi kuwashwa, nikajaribu kujigalagaza, haikuwezekana. Sasa likaanza kujikaza, muwasho ukaenda likizo, maumivu yakaingia kati. Lilizidi kukaza, mara likaongeza kujiviringisha hadi likaniziba usoni. Kifo kikanukia harufu ya kukera.
Nikabaki jicho moja tu kuona nje!! Viungo vingine vyote vilikuwa vimefunikwa. Sikuwa na ujanja. Jicho langu likamuona John akiwa ameshangaa kama tahira. Nilijaribu kutoa sauti haikutoka, nilikuwa namwomba John kwa mara ya mwisho aweze kuniokoa. Hakuweza kunisikia.
Nikatazama juu nikakutana na mawingu yenye rangi inayoshabihiana na buluu, nikaikumbuka rangi ya mtandao wa kijamii. Ni huku nilikutana na Dokta Davis. Akanipa zawadi ya utajiri, akanipatia kazi nyepesi inayonipatia kipato kikubwa. Nikamuamini sana. Sasa alikuwa amegeuka joka kubwa na lilikuwa linaniua.
Hakika lazima nife!! Jitihada zangu zote hazikuwa na maana tena.
John hakuwa msaada wowote kwangu. Na hakuwepo mwingine wa kunipa msaada.
Nilipofikiria ni nani mwingine wa kunisaidia akili yangu ikaejea kwa mwalimu Nchimbi. Mama yangu mzazi. Nikajaribu kuita sauti haikutoka. Mama naye hakuwa na msaada katika hali hii.
Nikayakumbuka maneno ya mama. Miaka mingi sana nikiwa mdogo aliwahi kunikambia maneno.
“Yupo mtu anakusikia hata usipotoa sauti.” Hili lilikuwa jibu alilonipa baada ya kumuuliza iwapo mabubu na viziwi wanaweza kuzungumza na Mungu. Jibu lake hadi ukubwani halikunitoka.
Nami sasa nilikuwa bubu. Jaribio la mwisho kabisa ni kuzungumza na yule anayesikia wakati wote. Ajuaye unachokiwaza. Kila wakati, mahali popote.
Mungu!
“Eeh! Baba sijui kama nilistahili adhabu hii. Na kama ilikuwa stahili yangu baba. Nichukue kwako sasa. Nimeumia na IMETOSHA.” Nilizungumza katika nafsi yangu. Kisha nikasubiri kuiaga dunia hii chungu.
Nilitua chini kama mzigo mzito, bahati nzuri nilitua katika majani. Sikuumia. Nilipumua kwa fujo sana, nilikuwa nimerejewa na uhai tena.
Nikalishuhudia lile joka likihangaika huku na huko, hatimaye likatoweka.
Maajabu makubwa ambayo sijapata kuyaona na yalikuwa yanastahili kutolea ushuhuda.
Sikuwahi kuwa na imani katika miujiza lakini sasa ilinitokea ili niiamini. John naye alikuwa anashangaa kama awali. Na bado hakuweza kuniona. Sikupoteza muda nikamshika mkono. Tukaanza kuondoka. Sikukiacha kisu changu.
Nilijikuta naifuatilie ile njia tuliyopita awali hadi nikaufikia ule mlango. Nikamtanguliza John nami nikatoka.
Maajabu mengine. Niliwakuta wale waliotangulia wakiwa katika sintofahamu wasijue nini cha kufanya.
Kwa kukadiria muda ilikuwa saa sita mchana. Na tulikuwa katika ulimwengu halisi lakini hatukutambua ni wapi hapo tulipo.
Magu, Bariadi, Sumbawanga, Songea!! Kila mtgu alifanya utabiri wake.
Hatukuendelea kukaa pale. Tukaanza safari kuelekea tunapoelekea bila kutambua ni wapi.
Baada ya kilometa takribani sita tukaingia kijijini.
Mimi nikiwa na upande wa kanga pekee. Wenzangu wakiwa na nguo zilizochakaa sana. Tukakiona kijiji. Baadaye tukaanza kukutana na watu.
Kila mtu akiwa na lake la kufanya. Hakuna aliyetuuliza swali. Walikuwa weusi sana, wengine walifanana na nyani huku wanawake wengi wakiwa na maziwa makubwa.
Ni wapi sasa hapa? Nilijiuliza.
Tulitamani sana kuzungumza na watu hawa lakini hawakuwa wakarimu.
Njaa iliuvunja uamuzi wetu wa kusubiri watuanze. Njaa ilituuma na hatukuwa na chochote cha kuweka tumboni.
“Ha…habari..”
“Nkesuu…” asijui kama aliniuliza ama alinijibu salamu.
Lugha ya wapi hii!! Niliwahi kusikia mahali, ni wapi vile. Niliumiza kichwa. Kila mmoja alikuwa ananitazama mimi kama mwokozi katika mapambano haya.
“Me come great…” nilizungumza kiingereza kibovu ili nipate kujua wanazungumza lugha gani na ni watu wa wapi. Hakunijibu akanikazia jicho kwa shari. Ni hapo nikapata jawabu sura hizi nimewahi kuziona wapi. Ni kwenye basi. Siku ya safari yangu kuelekea Ndolla Zambia kwa Dokta Davis kusaini mkataba ule ulionifikisha hapa nilipo.
“Sam…it’s either Congo or Ndolla….(Sam ni aidha Kongo ama Ndolla)” nilimnong’oneza yule msukuma.
“Ndolla??”
“Yes! Ndolla Zambia..” nikamjibu. Akashangaa. Yule bwana tuliyemuuliza akawa amesonya na kutoweka.
Watu hawa sio wazuri hata kidogo. Wameathiriwa na vita za wao kwa wao. Wakitugundua ni hatari. Naamuru!! Hakuna mtu kuzungumza na mgeni yeyote, I WILL!!! Nilitoa tamko kama amiri jeshi mkuu wa mapambano hayo.
Kila mmoja akanielewa.
Safari ikaendelea, tulikuwa tumechoka lakini tuliuhitaji sana ukombozi, tulihitaji uhuru wetu.
NDOLLA TOWN 40 KM AHEAD. Kilisoma hivyo kibao kigumu cha chuma. Nikajipongeza katika nafsi yangu kwa kuwa na kumbukumbu nzuri.
Jesca alikuwa mtu wa mawazo mazito. Hakuwa akiongea na ule urembo wake wa enzi zile haukuwa na nafasi hapa. Pia ugomvi wetu wa kumuwania John kimapenzi haukupewa nafasi pia. Kila mmoja alitazama anajikomboa vipi.
Tulitembea kimafungu mafungu. Jumla tulikuwa watgu ishirini na moja lakini, tulikuwa kama hatufahamiani. Kila mmoja na lake. Likitokea la kuzungumza nilikuwa nachukua nafasi hiyo.
Tulipoufikia mto, kila mmoja aliyatumia maji anavyoweza, wengi walikunywa na wachache walioga. Pumziko la dakika ishirini kisha tukaendelea mbele. Tukaufikia mti wa maembe. Hapa sasa kila mtu alikula kulingana na ukubwa wa tumbo lake. Angekuwa mjinga ambaye angeacha kubeba akiba ya maembe matamu ya Zambia.
Sasa kasi ikaongezeka na mazungumzo yakaibuka. Njaa kitu kibaya sana.
Mimi na John tulikuwa tumeambatana. Ile hali ya yeye kutoniona iliniumiza sana lakini sikuwa na namna.
Kilometa zikazidi kukatika, tulitembea hadi usiku, kwa kukadiria tulitumia masaa yanayozidi kumi. Kuzikamilisha zile kilometa.
Mji wa Ndolla ukatukaribisha. Ulikuwa mara yangu ya pili kuja katika mji huu na mara ya kwanza kufika nikiwa katika matatizo.
Nilijipongeza tena kwa tabia yangu niliyoionyesha siku ya kwanza. Tabia ya kushangaa shangaa. Hivyo kuna baadhi ya vitu nilivikumbuka. Hadi tukaipata stendi.
Kama nilivyoamuru kila mmoja alijitenga kama hatujuani. Kanga yangu ikiwa imefungwa vyema. Ni hiyo pekee ilikuwa ngao yangu. Nikaingia katika stendi ile ambayo ilikuwa inazidiwa hadhi na stendi ya Ubungo jijini Dar es salaam katika nchi yangu ya Tanzania.
Nilizunguka hapa na pale. Nikaiona ofisi ya magari amabyo nilikuwa naitaka.
“Mambo vi wewe…inakuwaje…mishemishe vipi…oya acha kuzingua…” maneno haya yalikuwa yanazungumzwa katika ofisi hizi.
Nikainama chini jicho langu la kulia likatangulia kumwaga chozi la kushoto nalo kwa uchungu likamwaga chozi. Nikajiinamia chini nikalia kwa uchungu mkubwa. Uchungu wa kuikumbuka nchi yangu Tanzania. Kilio hichohichoi kwa namna ya kipekee kilikuwa kilio cha furaha. Ndio lazima nifurahi. Sasa ningeweza kumvuta mtu na kuzungumza naye Kiswahili.
Ni hivyo nilifanya. Mwanaume kipande cha mtu akavutika kunisikiliza. Kwanza sikutaka kumuelezea kuwa tupo wengi. Niliitetea nafsi yangu. Nilikuwa natetemeka kwa baridi. Akanipatia sweta zito nikajistiri. Nikajielezea kuwa nimepotezana na bwana aliyenileta Zambia.
“Umesema wewe mwenyeji wa Makambako.”
“Ndio kaka.”
“Makambako sehemu gani hiyo?”
“Ni karibia na stendi kuu. Hapa Magegele …..”
“Alaa Magegele napafahamu sana huko…kabla ya kuhamia huku nilikuwa naenda na mabasi ya Dodoma Mbeya…sasa hapo Magegele kuna mgahawa tulikuwa tunakula tulimzoea sana yule mama kiukweli..hata wewe nikutajia lazima utakuwa unamjua..”
“Mama Kesho.” Niliwahi kumjibu. Akacheka sana, hakuna mtu wa Makambako ambaye hakumjua mama huyu. Alikuwa mkarimu sana.
Tulizungumza mambo mengi usiku ule. Alizungumza nami kwa ukarimu. Ni nani alikwambia kuwa watanzania sio wakarimu.
Kuna tofauti kubwa kati ya mtanzania na mbongo!! Mtanzania ana utu lakini mbongo anajifanya mjanja mjanja. Huyu bwana alikuwa mtanzania haswaa.
Upesi nikapata chakula. Kisha akaingia ndani akatoka na nguo. Zilikuwa za kike.
Akanieleza abiria huwa wanasahau nguo zao na kamwe hawarudi tena kuzichukua. Nikamshukuru. Akanipatia na kiasi cha pesa. Akaniomba nirejee majira ya saa tano asubuhi aweze kunifanyia utaratibu wa kunisafirisha kurejea Mbeya kisha Makambako Iringa.
Ilikuwa bahati ya kipekee sana kupata msaada huu. Lakini hapo hapo ilikuwa bahati mbaya sana maana nisingeweza kusafiri peke yangu. Na yule bwana sikumueleza tupo wengi zaidi ya kikosi cha timu ya mpira wa miguu.
Ubarikiwe sana!! Nilimpa Baraka hizo.
Kisha nikiwa na mavazi kamili sasa. Nikapiga hatua kwa hatua. Kigiza giza kikanifanya nionekane kama kivuli. Mkono mmoja mfukoni kuzilinda Kwacha (Pesa halali kwa matumizi ya Zambia) nilizopewa, mkono mwingine ukiwa umeshika kiroba cha nguo nilizopewa na yule bwana. Isabela nikiwa na raba nyepesi miguuni. Nikatoweka huku nikiamini nina mzigo mkubwa wa kuwaokoa rafiki zangu ambao walinitazama kwa jicho la huruma.
Nilijihesabu kama mshindi wa vita ya 666. Lakini bado nilikuwa na vita nyingine ya kurejea nyumbani.
Mshindi akifia ugenini huyo ni mshindwa lakini akirejea nyumbani hata kama amejeruhiwa vipi bado ataitwa mshindi.
Mapambano yameanza rasmi!!! Nilikiri huku nikiwa nayatamani hayo mapambano ambayo niliamini hayawezi kuwa magumu kushinda vita ya joka kuu la msituni.



***HAYA SASA KAMANDA ISABELA OPARESHENI UKOMBOZI imefikia Ndolla Zambia. Nini kitaendelea katia nchi hii ya kigeni??

*** Je Davis amekufa?? Vipi kuhusu chata ya 666 katika shingo la John!!!!

No comments:

Post a Comment

Recent Posts