Thursday, December 20, 2012

SITAISAHAU facebook------------------24

 

MTUNZI: Emmy John P.

MAWASILIANO: 0654 960040

... SEHEMU YA ISHIRINI NA NNE

Nilimchukua Jenipher, Jesca na Samson. Kikawekwa kikao cha dharula. Mada kuu ikiwa tunatoka vipi.
Nilimpatia Jenipher na Jesca baadhi ya nguo. Wakajihifadhi.
Mazungumzo yalikuwa marefu sana na pambazuko lilikuwa linakaribia. Mengi yalizungumzwa na sasa tukawa tumefikia katika maamuzi mawili. Kubwa kabisa likawa kukimbilia ubalozini kupata msaada.
Wazo la kupata simu tuweze kufanya mawasiliano nyumbani pia lilitujia vichwani!! Lakini hatukulitilia sana maanani katika nchi za kigeni. Tulitaka tufike kwanza Tanzania ndipo tufanye mawasiliano.

Ubalozini!! Hiyo ndio ikawa mada.
Lakini swali likaja kwa John ambaye bado alikuwa na alama 666 na hakuwa akionekana. Lakini kama hiyo haitoshi, tukapata hofu ya usumbufu wa maswali mengi kutoka kwa chombo husika kitakachokuwa kinahusika na mambo ya uhamiaji.
Kwa jinsi tulivyokuwa wengi tuliamini kuwa itatuwia ngumu sana kupata msaada upesi. Pia ubalozi wa Tanzania katika nchi ya Zambia ulikuwa una makao yake Lusaka. Mji mkuu wa Zambia.
Hilo lilikuwa gumu sana. Tulikuwa tunahitaji pesa. Pesa!!
Kama tukipata pesa tunaweza kupanda mabasi yatakayotufikisha Mbeya. Hapo sasa tutakuwa katika ardhi salama ambayo tunaweza kupata msaada.
Pesa tutaitoa wapi? Hilo likawa swali.
Tukakubaliana kuingia katika mapambano ugenini. Mimi, Jesca, Jenipher na Samson. Tukafunga mjadala.
Asubuhi ikazidi kujongea. Hapa sasa nikachukua maamuzi. Nikatembelea kundi moja baada ya jingine. Nikawapatia chakula kidogo kidogo nilichonunua kwa kutumia pesa niliyopewa na kaka yule wa kitanzania. Huku katika kila kundi nikiwapa moyo kuwa tumekaribia kuondoka kurejea nyumbani.
Siku iliyofuata kila mtu alikaa kwa tahadhari bila kuzungumza na raia wa Zambia.

*****

Majira ya saa nne asubuhi nilikuwa katika ofisi ya yule mwanaume wa kitanzania aliyeahidi kunisaidia niweze kufia Mbeya. Nilimkuta akiwa amebanana kulingana na majukumu. Nikatulia mpaka alipomaliza. Nikaingia.
Alinichangamkia sana. Akamkabidhi mwenzake ofisi akanipeleka mgahawani. Chai ya maziwa na chapatti nzito kabisa.
Mazungumzo yakiendelea!!!

Akanielezea mpango wake huku akinisihi niwe mvumilivu katika safari maana patakuwa na tatizo la kuhamishwa siti na wakati mwingine kukosa kabisa pa kukaa maa nitasafiri kama ‘staff’. Hilo halikuniumiza kichwa sana, maana niliamini naweza kusimama cha msingi nia yangu kutimia. Kilichoniumiza kichwa ni hawa wenzangu. Itakuwaje!!
Nilimshukuru yule bwana. Akanipatia namba yake ya simu. Ni hapo nilimtambusa jina lake aliitwa Saidi.
“Ukinipigia simu we niite Side boy.” Aliniambia wakati ananiaga.
Alinipatia kiasi kingine cha pesa.
Nilishukuru kwa kuzaliwa mwanamke maana bila hivyo sidhani kama ningepata msaada.
Jioni ilipofika. Jesca hakuwa ameambulia lolote. Na Sam hadi wakati huo hakuwa amerejea. Tukajipa moyo kuwa huenda amefanikiwa kupata kibarua chochote huko alipo. Ikafika giza nab ado Sam hakuwa amerejea. Hofu ikaanza kutuingia na kuamini kuwa Sam anaweza kuwa aliongea Kiswahili na kugundulika kuwa ni mtanzania asiyekuwa na uhalali wa kuishi Zambia.
Hatukujua kuwa ni wapi tuanzie kumtafuta. Kama tukisema twende polisi na sisi tutakuwa matatani. Tatizo jipya!!
Jesca na Jenipher wakawa wananisikiliza mimi.
Kimya kikatanda!! Makundi mengine hayakujua nini kinaendelea.

Nilijiuliza maswali mengi sana bila kupata majibu. Samson amefanya jambo gani la kitofauti hadi wakati huu hajarejea.
Au amerejea tena katika kijiji cha Dokta Davis. Niliwaza peke yangu bila kumshirikisha mtu yeyote hisia zangu.
Saa nne usiku nilikuwa nimepitiwa usingizi.
Nilisikia kama natikiswa nikadhani ni Jesca amejigeza lakini nilikuwa naendelea kubughuziwa. Japokwa nilikuwa nimelala chini niliutamani usingizi.
Nilijikaza nikafumbua macho.
Usingizi ukakatika palepale. Alikuwa ni Sam!!
“Bella!! Bella!!” alinong’oneza. Nikamtazama usoni nikahisi kuna nhali ya tahadhari. Nikajipa utulivu wa lazima.
Akanishika mkono akaninyanyua. Akanivuta pembeni kidogo.
“Ulikuwa wapi Sam.”
“Bwana Mkubwa!!.”
“Kafanyaje…ndio nani?” nilitaharuki.
“Sio mtu ni sehemu inaitwa hivyo.”
“Pamekuwaje…”
“Nimekutana na mtu!! Aah!! Nimemuona mtu….amepata madini.”
Bado sikuweza kumuelewa Sam anamaana gani. Nikamuomba anielezee kwa kirefu.
Akanieleza juu ya mgodi wa Bwana Mkubwa ambao upon je kidogo ya mji wa Ndolla. Mgodi huu alipoutaja tu! Sikuwa na swali lolote. Nilikumbuka somo la Historia kidato cha pili hadi cha tatu. Mgodi huo ukanikumbusha madini hadimu ya Risasi (Copper) ambayo hupatikana kwa wingi katika nchi ya Zambia. Hasahasa Ndolla.
Sam akaendelea kunielewesha. Na sasa akanigusia juu ya bwana ambaye amepata madini hayo siku hiyo.
“Kwa hiyo ulikuwa huko.”
Akanijibu kwa kutikisa kichwa juu na chini akimaanisha kuwa ni kweli alienda ‘Bwana Mkubwa’.

Samson alikuwa amekuja na habari ambayo mwanzoni nilikuwa ninapingana nayo lakini hatimaye kulingana na shida tuliyokuwanayo nikaamua kukubaliana naye. Wizi!
Samson alinihakikishia huyo bwana ana pesa nyingi sana. Amefuatilia nyendo zake hadi alipofanikisha kuyauza yale madini.
“Alinipa lifti kwenye gari yake. Nilijifanya sijui lolote lile. Aliponishusha mjini nikamfatilia na kumuona aliyauza.”
“Sasa tunampata wapi?”
“Yupo anakunywa pombe sasa hivi. Ni hapo pekee pa kumkamatia.” Alinisisitiza.
“Nzuri zaidi ni mtanzania…” alinisisimua kwa kauli hiyo. Nikamwomba Mungu huyo bwana asiwe na tabia za kitanzania bali awe mbongo.
Nilitulia kwa dakika chache kisha nikamuamsha Jesca. Hakunisikia. Nikapekua huku na huko. Nikachukua mafuta. Nikaenda bafu za kulipia nikaoga. Nikajipaka mafuta. Nikavaa kanga moja.
Samson akawa kioo changu akakiri kuwa kwa namna ile lazima anitamani.
Samson akaniongoza hadi nikafika eneo la tukio.

Jirani na bwana huyu palikuwa na kiti kipweke ambacho hakikuwa na mlevi aliyekikalia. Nilikitoa upweke nikajiweka juu yake.
Haraka akafika muhudumu wa kizambia, mweusi na mbaya kumtazama. Nikaagiza soda.
Meza yangu haikuwa mbali sana na yule bwana ambaye Samson alinielekezea. Nilikunywa soda taratibu huku nikiisoma akili ya yule bwana aliyepata bahati ya kupata madini Bwana mkubwa.
“Yaani wahudumu wengine nao….ona sasa.” Nilizungumza kwa hasira. Kama najiongelesha. Sauti ikamfikia mlengwa ambaye ni yule bwana anayekunywa pombe.
Akajileta mtegoni.
Akasogeza kiti karibu nami.
“Wewe ni mtanzania kumbe..ama unaibiaibia Kiswahili. Nimefurahi kukusikia ukisema Kiswahili.”
Nikatabasamu, nikalegeza jicho kimaksudi.
“Yeah! Mtanzania halisi…..na wewe je?”
“Mimi ndio orijino kabisa.” Alijibu. Nikacheka tena.
“Dah!! Miezi miwili sijarudi nyumbani aisee. Maisha haya.” Nililalamika.
“Aaah! Mimi kila wiki huwa naenda aisee.”
Maongezi yakawa maongezi. Kama bahati alinipendelea vile. Yule bwana alikuwa na tabia za kibongo. Akaniingizia mada za mapenzi.
Sasa nane usiku tukawa tunatafuta chumba kwa ajili ya kutimiziana haja. Yeye akinitaka kimwili na mimi nikimtaka kipesa.

Alilipia chumba cha bei ghali sana. Nilimshuhudia wakati anauacha mkoba wake mapokezi. Nikagundua mchezo unataka kuharibika.
Nikajipa moyo. Nikaenda hadi chumbani!!
Hapakuwa na jipya huko. Mzee huyu mwenye matamanio. Alinivagaa na kuanza kunisumbua huku na huko. Sikuwa na hisia hata kidogo. Niliwaza pesa tu.
Nilipomtazama umri wake nikagundua huyu hana lolote la kuweza kunishinda. Akili ya maajabu ikanivaa, nikajikuta nimevamiwa na wazo kuwa kama nisipokuwa makini naweza kutumika kimwili na nisipate chochote kile.
Nikaamua kutumia nafasi moja tu kusawazisha mambo haya!!!
Pata potea!!

“Mh!! Hauna kinga?” nilimuuliza baada ya kuwa nimempelekesha akalegea kabisa macho yake na nikajua kuwa alikuwa anahitaji mwili wangu.
Ni hapa nilikuwa napahitaji.
“Sina mpenzi wangu…njooo tu hivyo hivyo” akajibu. Nikamtukania mama yake kimoyomoyo kwa ujinga aliozaa.
Nikasimama. Nikamtazama kwa jicho la kimapenzi huku moyo wa chuki ukimtusi. Ubongo unaohitaji pesa nao ukifanya kazi kwa bidii kubwa.
“Ngoja niende kuchukua mpenzi wangu, naogopa mimba mwenzako, ujue nimeolewa eeh!!” nilimlaghai. Akaingia mkenge. Nikachukua upande wangu wa kanga, nikashusha ngazi mpaka mapokezi.
Nikamkuta mwanadada mweupe akiwa ameuchapa usingizi.
“Nipatie mkoba wa mzee!!” nilimwambia huku nikiwa nimetega mkono!! Moyo ukiwa hauamini kama nitafanikiwa.
“Mmm. Hapana mwambie aje mwenyewe dada, hajaturuhusu kumkabidhi yeyote zaidi yake.” Alinipinga yule dada kwa kingereza chake kibovu kisha akaendelea kuuchapa usingizi. Nilitamani sana kumrukia nimkabe. Lakini alikuwa ametenganishwa na nondo. Nisingeweza hata kumgusa.
Niliondoka pale nikiwa nimetaharuki sana, mpango ulikuwa unakaribia kushindikana sasa, na asubuhi inayofuata nilitakiwa kusafiri kuelekea Mbeya.
Nikapanda hadi juu kule chumbani nikaufungua mlango kwa ghadhabu kubwa.
Yule bwana akashtuka.
“Ndio ujinga gani huu huku Zambia I hate such embarrassment!!” nililalamika.
“Nini tena mamito.” Aliniita kimapenzi akiwa amelegea.
“Yaani hadi kuchukua kinga I need to go with you!!”
“He!! Wamekunyima?” aliponiuliza swali hilo, nikajikuta Napata nafasi ya mwisho.
“Fanya hivi naomba umpigie umwambie anipe!! No discussion!!” niliwaka, zile hasira za kutaka kuikosa pesa ile zilikuwa zimenipanda.
Mbongo akachukua simu akainyanyua. Nikaomba mizimu yote asije akasemam maneno mengi kwenye simu.
“Halo!! Chumba namba 12….mpe huyo dada nilichomuagiza…na muache mambo ya kipumbavu” akakoroma kwa kiingereza kilichonyooka. Kisha akakata simu kwa hasira.
Sikusema neno!! Nikafungua mlango, nikatoka.
Nikiwa nimeukunja uso kwa ghadhabu nikafika mapokezi. Yule dada usingizi ulikuwa umekatika!! Tukatazamana!!
Yeye anaogopa na mimi naogopa!!!

***Je? ISABELA ataichukua hiyo pochi anayoamini kuwa ina pesa??
***Vipi safari itawezekanika????

No comments:

Post a Comment

Recent Posts