Friday, December 14, 2012

SITAISAHAU facebook-------18

 

MTUNZI: Emmy John P.

MAWASILIANO: 0654 960040

SEHEMU YA KUMI NA NANE

...
Ni kama daktari alikuwa haamini ambacho amekiona, katika mwili wangu na alichokuwa akifanya pale ni kunitoa tu katika hofu. Mabadiliko ya mimba yangu yalimfanya achanganyikiwe.
Tulirejea katika chumba chake cha ofisi. Mazungumzo yaliyokuwepo ni juu ya kuitoa mimba ile.
Daktari alikataa kata kata akidai kuwa mimba ikifikisha miezi sita na msichana akijaribu kuitoa basi lazima atapatwa na matatizo na kuna uwezekano wa kufa.
Maelekezo ya daktari yaliyoambatanishwa na neno KUFA yalinipa ahueni ya nafsi kwa sababu nilikuwa nataka kufa. Sikuwa na ujasiri wa kujiua na hakika nilikuwa naogopa kufa. Lakini kufa kwa namna anayoitaja daktari hata hakunipa hofu badala yake nikavutika na kumsihi anisaidie kuitoa ile mimba.
Mazungumzo yalikosa kabisa muafaka. Daktari yule alikuwa mbishi sana hakutaka kushiriki katika utoaji mimba huu. Nilipoona daktari huyu amekuwa na msimamo sana niliamua kutumia njia fulani ambayo hugeuza ukweli kuwa uongo na uongo kuwa ukweli. Nikaangusha mezani shilingi laki mbili. Akazikataa, nikaaga nikatoka. Niliporejea niliziongeza zikafika laki nne. Daktari akazikodolea macho, kisha akatazama kushoto na kulia.
“Umekuja na nani?” akaniuliza.
“Mwenyewe!” nikamjibu. Akatazama tena kushoto na kulia kisha akazikwapua zile pesa akazizamisha katika sehemu zake za siri. Nikakwepesha macho.
Akanifanyia ishara ya mkono. Nikamfuata hadi katika chumba kilichokuwa na harufu kali ya madawa. Akakifunga na funguo tukabaki wawili tu! Kimya.
Daktari alikuwa na hofu. Nililitambua hilo. Sikutaka kuuliza chochote.
“Toa nguo zote.” Aliniamuru. Kauli yake ikanikumbusha kauli ya yule Mnaijeria aliyetaka kunibaka kwa kujifanya ananifanyia tiba ya asili. Huyu sasa alikuwa daktari, nikaamua kucheza pata potea. Kwanza nilikuwa natokwa damu. Sidhani kama angeweza kujaribu kunibaka.
Nikaziondoa zote, wakati huo yeye alikuwa amejikita katika kuchanganya madawa yake ambayo sikuelewa kazi yake ni ipi. Nikabaki kumsubiri.
Njoo hapa!! Aliniamuru huku akinielekezea kitandani.
Geuka hivi!! Nataka kukuchochoma sindano. Nikageuka huku nikiwa katika uoga. Kifo! Nilikuwa naogopa kufa.
Nikahisi kitu cha baridi kikinipapasa. Nikauma meno yangu kungoja uchungu wa sindano. Nilingoja huo uchungu lakini hamna nilichohisi.
“Acha kujikaza wewe sindano itakatikia ndani.” Alinigombeza daktari. Nikashangaa hizo lawama zinatoka wapi wakati mimi hata sijajibana. Alipoona simjibu kitu akanichapa kibao. Nikashtuka.
“Mkubwa hivyo unaogopa sindano alaa!!” alinigombeza. Sikumjibu!!
Nikatega tena aweze kunichoma!! Hali ikawa vile vile.
“Sasa mimi nakuchoma hivyo hivyo.” Alichukua maamuzi yake binafsi.
Nikageuka. Nikayasubiri maumivu!!
Badala ya maumivu nikakumbana nay owe kubwa kutoka kwa daktari. Nilipogeuka na mimi nikiwa na hofu nikamkuta amekaa chini. Mbali na mimi. Alikuwa ana hofu!! Jasho likimtoka.
“Daktari!!.” Nilimuita. Hakunijibu, alikuwa katika mshangao. Alikuwa akinitazama kwa wasiwasi.
Nilikuwa siijui tena thamani ya kuwa na mavazi na aibu ya kuwa uchi. Nilitapatapa hivyohivyo pale ndani. Daktari akiwa bado ananishangaa.
“Vaa nguo!” aliniamuru kwa sauti ya chinichini. Nikaziendea nguo zangu na kuzivaa.
Kisha nikamfuata hadi ofisini!
“Chukua pesa zako!!” alinikabidhi pesa zile. Nilisita kuzichukua akanisihi nizichukue. Nikatii!!
Nini kimetokea daktari? Nilimuuliza. Hakunijibu bali alisikitika.
Kisha akaanza kunielezea juu ya nini alichokiona. Ilikuwa ni alama ya maajabu katika mwili wangu sehemu za makalio. Mwili wangu ulikuwa umetoboka na matundu hayoyaliweza kuonyesha alama ya ‘666’.
Mungu wangu!! Nikashangaa, daktari yeye akawa ni wa kusikitika tu!
“Usipokuwa mkweli utakufa wewe na familia yako nzima kama wenzako.”
“Wenzangu? Wapi”
“Mnaomtumikia”
“Nani?” nilihoji kwa hofu.
“Mmiliki wa hiyo alama. Kwani siku wanakuwekea hawakukuambia.” Alinihoji kwa utulivu mkubwa.
Nikawa kama mwendawazimu na sikuwa na lolote ninalojua kuhusu hiyo alama katika makalio yangu.
“Daktari sijui lolote mbona.”
“Haya shauri zako, atakufa mama, baba, mdogo wako, dada, shangazi, mjomba, wifi, na marafiki ikibidi kisha watakumalizia wewe tena kwa uchungu mkubwa.” Daktari alinieleza haya kama simulizi ya kawaida huku akinitajia orodha ya watakaokufa. Kwa lugha nyepesi alikuwa kama babu anayemsimulia mjukuu simulizi ya kutisha. Nikatetemeka sana!! Vifo!!
“Sasa daktari jamani mimi ninakuficha nini. Mimi sijui kitu.” Nilishindwa kuendelea kuongea nikaanza kulia. Nililia sana maana nilikuwa nimekata tamaa. Mbaya zaidi nilikuwa nimepigwa chapa ya 666.
“Ndio maana nimejishangaa sana, iweje leo nikubali kuchukua rushwa, nikubali kutoa mimba msichana. Ama kweli kila mwenye alama hii hatakataliwa na dunia kwa lolote.” Daktari alinong’ona kama anasema mwenyewe vile. Nilisikia kila kitu.
Sasa nilikuwa nimechanganyikiwa!
“Nitakusaidia.” Alinyanyua uso daktari akanieleza huku akinitazama vyema usoni.
Nilifarijika sana kusikia maneno yale. Kisha akaendelea, “Lakini uwe mkweli kwa kila kitu. Ukijaribu tu kuficha lolote lile. Nasema ukijaribu kuficha lolote lile. Wewe, marafiki na ukoo wako wote utatokomea. Mimi nakueleza haya kama mzee wako, katika kipindi changu cha miaka ishirini ya udaktari nakutana na matukio mengi. Lakini hili ni la tatu katika maisha yangu. Wenzako wawili, mmoja miaka saba imepita na mwingine mwaka juzi, nilitaka kuwasaidia lakini wakaleta ujanja ujan ja. Tuliwazika!! Aah!! Hatukuwazika insearch labda niseme tuliyafukia mabaki yao.” Alimaliza kunielezea kisha akashusha pumzi kali sana.
Macho yangu nilihisi kama yanajilazimisha kutazama mbele. Machozi yalikuwa yamezidi. Mapigo ya moyo yalikuwa juu, sasa nikaanza kuamini niliyokuwa nayatazama katika filamu za kinaijeria. Kumbe uchawi upo? Hakika uchawi upo!!
“Kesho njoo!!” alinipa ahadi hiyo.
“Kwa hiyo sitatokwa damu tena?” niliuliza swali la kijinga.
“Kwani mimi ndiye niliyekuwekea” Daktari naye akanipa jibu la kijinga kama nilivyotegemea.
“Usimwambie mtu yeyote kuhusu maongezi haya.” alinionya
Nikaaga! Kiguu na njia hadi nikaipata taksi.

Njia nzima nilikuwa nawaza na kuwazua. Zile ndoto zangu za kumjengea mama nyumba nzuri, wadogo zangu kusoma shule za kimataifa, mimi kuwa maarufu zaidi chuoni, ndoto za kwamba nataka kuwa mtakatifu! Zote zilikuwa zimekufa. Sasa nilikuwa nahangahika huku na huko huku nikisurubika na mateso ya nafsi.
Swali likajengeka katika kichwa changu. Dokta Davius linizuia nisimueleze mtu kuhusu mambo haya. Sasa daktari ananisihi nisifiche kitu. Hapa sasa nimuamini nani? Nilijiuliza.
“Kata kushoto!!” nilimuelekeza dereva.
Mawazo yangu yakawa yameishia hapo.
Maria aliniona kuanzia mbali. Akanikimbilia, akafika akanikumbatia.
“Da Bela jamani. Mbona mnyonge hivyo!.”
“Nimemkumbuka sana John.” Nilidanganya, huku siri kubwa nikiwa nayo mwenyewe.
Maria akaniongoza hadi ndani. Nikajibweteka kwenye sofa sebuleni. Maria akaniletea maji ya matunda niliyokuwa nayapenda, nikayagida kwa fujo kisha nikagundua kuwa nilikuwa na njaa. Chakula kilikuwa tayari!! Maria akanihudumia. Sasa niliweza kupumzika!! Sikutaka kwenda chumbani. Nililala sebuleni.
Kila baada ya masaa kadhaa nilikuwa naamka na kubadilisha pedi na nguo ya ndani kisha kuoga. Hali hii japo ilikuwa haijatimiza hata mwezi kwangu ilikuwa mateso makubwa. Sasa sikuweza kwenda kwa marafiki wala nisingeweza kwenda. Nilijihisi ninanuka, japo Maria hakuwa ameniambia hata siku moja lakini nilijijua mwenyewew kuwa sikuwa kawaida hata kidogo.

Siku hii ikamaliza bila tatizo!!
Asubuhi ya siku iliyofuata niliwahi sana kuamka. Badala ya kumuomba Mungu anijalie uzima na aniepushe na matatizo haya mimi niliwekeza imani yangu yote iliyosalia kwa daktari yule ambaye hadi sasa sikuwa namfahamu jina lake.
Saa nne kamili asubuhi. Nilikuwa katika mlango wa kuingia ofisini kwake. Japo kulikuwa na watu kadhaa waliohitaji kuonana naye. Mimi nilipewa kipaumbele, nikawapita nikaingia ndani.
Ahaaa!! Binti! Vipi kwema? Alinichangamkia sana.
Nikamjibu salamu yake. Nikakaa kitako kumsikiliza.

“Ngoja niwaondoe hawa watu hapo nje. Wewe nitakupigia simu uje mahali.” Alininong’oneza. Nikamuelewa nikampatia namba yangu ya simu kisha nikaaga.
****

Sikuchoka kusubiria. Japo alichukua muda sana. Baada ya masaa mawili na nusu. Aliniita odisini kwake. Nikaenda upesi nikamkuta akiwa pamoja na mwanaume ambaye laiti kama ningekutana naye wakati ule ambao nilikuwa na jeuri ya pesa sidhani kama alikuwa na hadhi ya kupokea salamu yangu. Nilimsalimia kwa kuwa tu alikuwa pamoja na daktari.
Nilipomsalimia badala ya kunijibu, akanikonyeza!! Nikataka kusonya nikasita.
Kwa ncha za macho yangu nikamtazama mwanaume huyu, kuanzia mavazi yalivyochoka, amechakaa nywele zake na hata ngozi ilikuwa imepauka. Nikaamini hata akili yake haiku sawa. Nilipokumbuka jambo hili la akili kutokuwa sawasawa nikaamini atakuwa ni mgonjwa wa akili. Na daktari huyu alikuwa katika kumpa tiba. Kimoyomoyo nikamsamehe kwa kosa la jinai alilofanya la kunikonyeza.
“Binti..kama nilivyokueleza jana!! Usisite kuusema ukweli wote. Ukificha haitakusaidia kitu zaidi ya kuuangamiza ukoo wako wote.” Alinieleza kwa utulivu. Yule tahira akacheka.
“Sawa daktari.” Nilimjibu. Tahira akacheka tena!! Akaanza kunikera.
“R.I.P mtu wako niliyekwambia ndio huyu.” Sasa daktari hakuwa akizungumza na mimi, bali alikuwa akisemezana na yule tahira. Nikashtushwa na hali ile, ina maana ananikabidhi mimi kwa yule chizi au alikuwa anamtania. Niliomba iwe hivyo lakini haikuwa. Alimaanisha.
Sasa tahira akanivagaa akanishika mikono. Nikajitoa mikononi mwake akacheka!!
“Nenda naye ofisini kwake huyo akakupe maelekezo. Anaitwa R.I.P”
“Na yeye anaitwa nani.” Yule mtu niliyedhani ni tahira sasa aliuliza.
“Jitambulishe binti.” Tahira alinieleza huku akinishika makalio. Kidogo nimtukane. Nikasita baada ya kuona daktari hakushtushwa na jambo hilo.

Nitafanya nini sasa!! Nikaanza kufuata uelekeo alionipeleka. Mara kwa mara alikuwa anacheka. Tulipishana na watu wengi lakini hakuna aliyemshangaa. Huyu sio tahira!! Nililazimika kuamini

Mlango ukafunguliwa nikaingia ndani!! Ofisi yake ilikuwa na hewa nzito sana ya madawa lakini yeye aliifurahia.
Karibu ukae…aaah!! Usikae kwanza hebu njoo huku.” Akanivuta kwa nguvu, nikamfuata. Akafungua kabati moja kwa fujo.
Mungu wangu!! Maiti!! Nikaruka pembeni, akacheka!!
“Binti hawa nao walikuwa wajing wajinga tazama….njoo..njoo” akaniita. Nikasogea. Akavuta kabati jingine likafunguka.
Maiti ya mwanamke. Akamgeuza. Alikuwa na alama ya 666 katika makalio yake. Maiti huyu nilikiri kuwa kabla ya kuwa hivi alikuwa mrembo sana.
Sijui nini kilimuua maskini!!
Akanipeleka katika kabati jingine akavuta tena. Akatoka motto mdogo. Hana kichwa nay eye ana alama ya 666..R.I.P kazi yake ilikuwa kucheka tu kama tahira. Wakati mimi nilikuwa katika hofu kuu.
Sasa nilikuwa nimechanganyikiwa. Maiti karibia tano zilikuwa pamoja nasi, waziwazi. Amani ikatoweka moyoni.
“Na wewe ukificha neno lolote tu!! Utakufa na vizazi vyote vitakavyofuata.” Aliongea bila kucheka sasa.
Nilikuwa natetemeka.
“Hata huyo uliyemkalia na yeye nadhani ni walewale..hebu funua.”
“Wapi?” nilimuuliza, likiwa neno langu la kwanza hapo ndani.
Akanionyesha kwa kidole. Ni pale nilipokuwa nimekaa. Nikafunua nikiwa natetemeka.
“Mamaaa!!” nikapiga kelele. Kumbe nilikuwa nimekaa juu ya maiti. R.I.P akacheka sana!!
Zile dharau zangu zikawa zimeishia hapa!! Nikamuheshimu!!!

*** ISABELA ndani ya chumba cha kuhifadhi maiti…je kuna msaada gani hapa!!!

***Nini hatma ya mimba yake!!!!

No comments:

Post a Comment

Recent Posts