MTUNZI: Emmy John P.
MAWASILIANO: 0654 960040
... SEHEMU YA KUMI NA TANO
Zilipita siku nne, kila siku nilikuwa napitia barua pepe yangu kutazama kama kuna majibu yoyote kutoka kwa Dokta Davis lakini mambo yalikuwa tofauti Davis hakupiga simu wala hakujibu ujumbe niliomtumia. Nilijiuliza je? Nimpigie simu ama niendelee kuvuta subira. Hali hiyo ya kungoja sana ikanitia mashaka, kumpigia simu pia nikasita kwa kukumbwa na maswali mengi. Kama hajaisoma ile e-mail itakuwaje? Na kama ameisoma pia nilitegemea maswali mchanganyiko ambayo yangeweza kunitia katika majaribu ya kumweleza Davis juu ya ile mimba ya kimaajabu! Jambo ambalo sikutaka kabisa litokee. Nikaendelea kuwa kimya!
Siku zikasonga mbele. Amani finyu moyoni! Maria sasa akawa kama ndugu yangu, tuliendelea kuishi wote.
***
Zilipokatika siku saba za kuikamilisha wiki moja, ustahimilivu ukanishinda, mateso ya nafsi yakanikita. Ujasiri ukaikimbia subira. Nikaamua kujaribu kupeleleza, kwanini? Davis hadi sasa hajasema neno. Sijui kwanini nilikuwa namuogopa Davis kwa kipindi hicho. Lakini sikuweza kumpigia simu.
Nifanyeje? Nilijiuliza!
Facebook! Jina hilo likanivamia kama jinamizi linalotisha lakini lenye msaada.
Kwanini naogopa? Nilijiuliza.
Ilikuwa saa moja usiku, nikiwa kitandani. Mkononi glasi ya juisi, kompyuta yangu ndogo ikiwa inamalizia hatua za kuwaka. Ilipomaliza, nikaingia katika mtandao. Tangu nitingwe na kazi niliyopewa na kampuni ya Dokta Davis na matatizo yaliyokuja baadaye nilikuwa nimeususa kabisa mtandao wa kijamii wa facebook, kwanza jina langu tayari lilikuwa kubwa pale chuoni hivyo nilikuwa napata usumbufu mtandaoni, pili sikuwa na muda kuingia kule mara kwa mara. Lakini siku hii nililazimika kuingia mtandaoni.
Nia kubwa ikiwa kutazama akaunti ya Dokta, ni lini mara ya mwisho kuandika kitu mtandaoni. Kama ningejua hilo ningeweza kuhusisha hofu yangu ya kwamba aidha kuna jambo baya limemkumba Davis.
Mdomo ukabaki wazi, nikapumbazwa na picha iliyokuwa katika akaunti yangu! Nikaitazama kwa makini! Haikuwa ndoto! Alikuwa yeye! Sasa ni lini ameiweka hapa? Nilijiuliza!
Nikataka kumuita Maria, nikagundua hatakuwa na la kunisaidia. Kwanza ye mwenyewe hana hulka na mtandao huu!
Nikabaki kuishangaa picha ya John! Alikuwa anatabasamu!
John alizipata wapi namba zangu za siri za facebook? Nilijiuliza bila kupata majibu.
Mh! Au hii picha niliweka mwenyewe? Lini sasa? Nikajiuliza.
Kwa hili sikushtuka sana. Nikajipa moyo kuwa huenda niliwahi kuiweka hii picha ya John bila kujitambua kutokana na kukolea katika penzi. Penzi la John ambaye hadi wakati huu hakuwa akifahamika ni wapi alipo. Nikiwa nimeamua kumpuuzia John na hiyo picha sasa nikaamua kuendelea na kile kilichonifanya niingie mtandaoni.
Nikataka kuifungua akaunti ya Dokta Davis niweze kuikagua.
Hata kabla sijaanza kuikagua akaunti ya Doka, nikakutana na kitu kingine cha kushangaza, hapa sasa nilijikuta naitupa laptop na kuruka mbali nayo kama nimepigwa shoti ya umeme. Ama nimeona kitu cha kushtua sana.
Ilikuwa picha nyingine, hii ilikuwa ina ujumbe juu yake 'In love with the guy!' marafiki zangu walikuwa wameishambulia kwa maoni, wengi wao wakisifia picha hiyo, huyu kwenye picha naye alikuwa anatabasamu, tofauti ya picha hizi ni kwamba John alikuwa amevaa fulana yake, lakini huyu mwingine alikuwa kifua wazi.
Kwa mtazamo wangu hii picha haikuwa
Ilikuwa picha mbovu, isiyokuwa na mvuto. Hasa hasa kwangu ambaye hadi kumsifia mvulana amependeza lazima nichunguze vitu vingi, sasa kati ya hizo sifa huyu hakuwanayo hata moja.
Huyu hakuwa mwingine alikuwa ni yule mganga wa kinaijeria. Kamwe nisingeweza kumsahau maana nilimuona kwenye mwanga huku lile tukio la kujaribu kunibaka kasha akatulia tuli kitandani na lenyewe lilikuwa limenasa katika kichwa change.
Tatizo!!
Bado nilikuwa wima natetemeka huku nikiiogopa ile laptop.
Nani ameingia kwenye akaunti yangu na kufanya haya?
Ujanja wa mtu muoga ni kukimbia shari. Palepale nikaitumia kanuni ile. Nikatimua mbio nikapishana na Maria alikuwa amekamata glasi iliyokuwa na juisi nikamsukuama yeye na glasi yake. Yeye akawahi kujizuia lakini glasi ikasambaratika vipande. Nikamsikia akitoa yowe la hofu!
Maria, Maria njoo!! Nilimuita wakati huo tayari nikiwa sebuleni.
Maria kwa hofu akanifuata. Nikamkumbatia. Mapigo yake ya moyo yalikuwa juu sana. Lakini yangu yalikuwa juu zaidi. Kila mmoja alikuwa katika kuogopa.
Sikuweza kuzungumza chochote. Nikamvuta Maria tukaelekea chumbani. Nia yangu kumueleza kila kitu kilichonisibu hadi nikatimua mbio. Tulifika chumbani, ajabu Maria alikuwa anatetemeka kuliko mimi muhusika.
Tulitulia kitandani, nikaisogeza laptop nikaanza kumuelekeza Maria, kile nilichokiona. Hasahasa picha ya yule mganga. Lakini sikumweleza lolote juu ya mimi kumfahamu.
“Jamani Bela…wame’HUCK’ akaunti yako..mbona haka kamchezo ka kawaida tu!.” Alinieleza. Ni kweli jambo hilo nilikuwa nalifahamu. Lakini huyu mganga amejuaje kuwa mimi naitwa Isabela hapa facebook? Nilijiuliza.
Ok! Kama ni kweli ameingilia akaunti yangu na kunidhalilisha hivi. Naapa atakiona cha mtemakuni. Nilimuapia Maria. Wakati huo sikumbuki kuwa palikuwa pia na picha ya John.
****
Sikuwa katika utani. Nilikuwa nimekerwa na kitendo cha yule mganga kunifanyia huu upumbavu. Kesho yake pesa ikaongea nikawapa pesa nzuri maaskari. Nikawapa na ushahidi. Ndani ya Defender kwenda kumkamata yule mganga. Lile jaribio la kutaka kunibaka lilikuwa moja kati ya mambo yaliyonitia hasira.
Niliikumbuka vyema njia na tulifika bila usumbufu.
“Mzee alitutoka. Ni wiki sasa imekatika.” Mke wa mganga alitueleza kwa huzuni kuu. Moyo ukawa wa moto ghafla. Mganga amekufa!! Mbona tarehe ya ile picha na kifo cha huyu mganga vinashangaza sasa. Tarehe aliyoweka ile picha tayari alikuwa marehemu.
Ewe! Mwenyezi Mungu nichukue mimi Isabela, dunia imenishinda!!! Nilisali kimoyomoyo. Mauzauza yalikuwa yamenizidi nguvu.
Nilirejea nyumbani nikiwa mwingi wa mawazo. Sikumueleza lolote Maria. Nilimpita akiwa anajisomea. Zaidi ya salamu sikusema neno. Moja kwa moja chumbani nikajinyoosha kitandani nikaanza kulia.
Nikiwa bado sijasinzia vizuri. Simu yangu iliita. Alikuwa ni rafiki yake na John.
Kidogo nisipokee. Lakini alipopiga tena na tena nikaamua kupokea.
“Mambo vipi shemu?”
“Poa!” nilimjibu kwa kujilazimisha.
“Sijakuelewa kabisa shem! Una matatizo gani?” aliniuliza.
“Kwa nini mbona niko poa sema nimechoka tu.”
“Umechoka ndo unaandika mambo gani sasa haya kwenye facebook?” alizungumza kwa hasira kidogo. Nikakaa kitako, usingizi hakuna tena!!!
“Nimeandika nini kwani eeh!! Hebu ngoja.” Nikamkatia simu.
Haraka haraka nikafungua simu yangu sehemu ya mtandao. Jasho lilikuwa linanitiririka. Sijui ni kipi kilikuwa kimeandikwa. Na ni nani ameandika kama ambaye ameiingilia akaunti yangu tayari alikuwa ni marehemu.
“1986-201..REST IN PEACE ISABELLA” Ilisomeka hivyo katika akaunti yangu.
Karibia kila mtu alikuwa anauliza kulikoni nimeandika hivyo.
Lakini bora ningekuwa nimeandika mimi! Mimi hata sijaandika. Nikaanza kulia nikajigalagaza kitandani, nikavua nguo zangu. Nikavuruga nywele zangu. Nikalia kama motto.
“nimekukosea nini Mungu wangu eeeh!! Nimekosa nini sasa!!” nililaumu sana, uchungu ukanikaba kooni. Ukasafiri hadi moyoni, ukanisurubu kila upande. Suluba nisiyoelewa chanzo chake. Suluba kamilifu.
Naelekea kuchnganyikiwa? Nilijiuliza. Lakini nikajicheka. Tangu lini mwendawazimu anautambua wazimu wake? Huenda mimi ni kichaa tayari.
Munkari ya kusoma ikapotea na mitihani ilikuwa karibu kabisa.
Liwalo na liwe!!
Nilitamani sasa kwenda kwa viongozi wa kiroho waweze kunishauri na kuniombea kama inawezekana lakini tatizo lilikuwa katika kuwaeleza kuanzia mwanzo. Zile ndoto za John anaua na mengine yote. Niliogopa kuaibika.
Nikakaa kimya na siri yangu, mateso pia yakabaki kuwa yangu!!!
Nilipowaza mitihani, wazo la kuwa nina mimba pia likajileta pia katika orodha.
NANI ameingia na kufanya haya katika akaunti ya Isabela.
NINI HATMA YAKE??
Na atafanya nini na hiyo mimba!!!!
No comments:
Post a Comment