Friday, November 2, 2012

HATIA---- 11


MTUNZI: George Iron Mosenya

CONT: 0655 727325


SEHEMU YA KUMI NA MOJA

Kelele za mpiga debe zilimvuta akapanda daladala inayoelekea Nyegezi ikitokea Igoma. Matha alipanda kwa msukumo wa mpiga debe hakuwa amenuia rasmi kwenda huko Nyegezi. Muziki mkubwa ndani ya gari hiyo ulimtia ghadhabu, alitamani kushuka lakini alikuwa siti ya nyuma akahofia kufanya usumbufu.
"Tuache hapo Natta!" abiria mmoja aliyekuwa jirani na Matha alimkumbusha kondakta ambaye naye aligonga bodi dereva akasimamisha. Aliposimama kuanza kushuka Matha naye akaamua kushuka, baada ya kulipa nauli alishangaa hapa na pale na kujiangalia amepungukiwa nini ndipo alipogundua ameacha gazeti ndani ya gari, bila uelekeo maalum Matha alianza kukaza Mwendo.
"Mh! au ile sheli ya Mitimirefu??" swali la ghafla likanasa katika ubongo wake likisubiri jawabu.


****


Minja Meri alikuwa mmoja kati ya wachaga wachache waliokimbia maduka ya wazazi wao na kuamua kupambana kivyao jijini Mwanza, kabla ya kuingia jijini Mwanza Minja aliwahi kuwa dalali mjini Morogoro, muosha magari jijini Mbeya na sasa alikuwa jijini Mwanza akifanya kazi sheli. Kipato cha masaa alichokuwa akiingiza Minja kwa muda anaokuwa kazini hakikumtosheleza kujikimu maisha yake mwenyewe katika chumba chake cha kupanga maeneo ya Mabatini jijini Mwanza. Kwa kulitambua hilo kijana huyu mrefu wa kimo, ngozi yake maji ya kunde na kichwa chake kisichokuwa na nywele huku rangi ya meno na lafudhi ikiuweka hadharani uasilia wake. Minja akawa amebuni mbinu ya kuwa anawachangamkia sana wateja wake, hasahasa wenye magari binafsi na yale ya serikali na wale wenye kawaida ya kuweka lita nyingi za mafuta, tabia yake hiyo iliyojawa na ucheshi akafanikiwa kuwateka matajiri wengi hivyo kwa siku alikuwa hakosi shilingi ya ziada (Bakhshishi) tofauti na malipo yake. Kwa muda mrefu alikuwa amejaribu kwa hali zote kumtia John Mapulu katika himaya yake lakini tabia zake za ajabu ajabu zilimshangaza, mara leo anacheka mara kesho hazungumzi neno. Hata siku hii alipomjazia mafuta katika gari yake bado John hakuzoeleka, kitendo cha kuchanganya pesa za malipo na kikaratasi kidogo japo muhimu cha hospitali kwa Minja ilikuwa kama nafasi yake kubwa kumthibitishia John uaminifu wake hivyo kwa kikaratasi hicho aliamini siku hiyo lazima angepata shilingi kadhaa bila jasho.
Minja hakutaka kumshirikisha mtu yeyote aliamini ilikuwa bahati yake na wala hakulichukulia uzito jambo lililoandikwa na daktari alichoangalia yeye ni maslahi atakayopata. Kwa mbinu hafifu aliweza kuinasa namba ya John Mapulu kutoka kwa mmoja wa mabosi wake, ni baada ya kuomba aazimwe simu ili apige namba yake kwani alikuwa haioni simu yake, bosi akaingia mkenge akampatia. Kitendo cha dakika mbili dalali huyu mstaafu alikuwa ameinakiri namba ya John kichwani mwake. Ilikuwa bahati yake kuwa namba ya John ilikuwa imehifadhiwa kwa jina halisi la ‘John Mapulu’
"We boya kweli, ona simu ipo kwenye soksi unatafuta mfukoni" Minja alishtuliwa na mwenzake wakati anaendelea kuipiga namba yake.
Danganya toto!! aliwaza Minja huku akizuga kujicheka. Kwake ulikuwa ushindi, wakati kwa wenzake ukageuka utani. Muda wake wa mapumziko ulipowadia Minja Meri alibonyeza namba za John Mapulu ambapo walizungumza, Minja alijaribu kuweka ukaribu na heshima za hapa na pale lakini John bado hakuchangamka.
Hawakufikia mustakabali John akatoa ahadi ya kupiga simu baadaye. Minja hakukata tamaa aliendelea kubaki maeneo ya karibu na sheli alikuwa akisubiria simu ya John, alikuwa akihitaji pesa bila jasho. Muda ulisogea bila kupokea simu yoyote, hakutaka kumsumbua John kwa kumpigia simu alisubiri apigiwe kama alivyoahidiwa. Usingizi ulimpitia mara kadhaa alizokuwa amejiegesha katika kiti cha plastiki kilichokuwa mbele ya duka la spea za pikipiki jirani na Sheli. Mara hii alipogutuka kutoka usingizini alikumbana kwa mbali na hisia za kumfahamu mtu aliyekuwa anakuja mbele yake, sura haikuwa ngeni. Hakupata kumbukumbu ni wapi aliwahi kumuona lakini kama kawaida akainuka kwenda kumlaki.
Tabia za kidalali zilikuwa zinamtafuna!
Minja alipandisha juu suruali yake na kuficha kitundu kidogo kilichokuwa kimeishambulia suruali hiyo iliyokuwa mpya miezi mitano iliyopita, bila shaka kitundu hicho kilikuja kuhitimisha uchakavu wa suruali ile. Baada ya kujiweka sawa kabisa kwa ujasiri wa hali ya juu alichanganya miguu yake hadi akawa ameiziba njia aliyotaka kupita mwanadada huyu mrefu wa haja, mweupe wa rangi' uzuri wake haukukamilika kutokana na kukosa tabasamu, japo simanzi iliyomtawala usoni haikuficha uzuri wake.
"Sista....sista..nakusalimia" Minja alinyanyua mkono wake na kutaka kumsalimia Matha. Matha hakutoa mkono wake, akamkazia jicho lililojaa chuki bwana Minja.
"Shimboni..." alisalimia kikwao katika hali ya utani, bado Matha aliyekuwa amesimama akimshangaa hakujibu lolote. Wala hakuruhusu tabasamu!!
"Yesu na Maria naumbuliwa mie leo" alijaribu karata ya mwisho ya utani! akafanikiwa Matha akajenga tabasamu hafifu, Minja akaviona vishimo vilivyozama katika mashavu ya Matha. Akausikia moyo wake unadunda, akaelewa alikuwa ameanza kumtamani yule binti.
"We mkorofi wewe mwone meno yake..." Matha aliongea huku akijizuia kucheka.
"Meno yangu ya dhahabu, usimwambie mtu yeyote wataniteka" Minja alimnong'oneza Matha huku akitazama kushoto na kulia kama vile kuna watu wanafatilia mazungumzo yao. Safari hii Matha akalipuka na kicheko kikubwa lakini cha kistaarabu meno yake meupe yakammulika Minja. Ile kujizuia kucheka mabega yakawa yanatikisika, na maungo mengine yakaiga mfano wa mabega. Akapendeza!!!
Minja akawa amefanikiwa kuujenga urafiki.
"Ehe! unajua ni kama nimewahi kukuona vile mahali fulani...kwema utokeapo lakini?"
"Kwema sana aisee!!...naingia hapa sheli mara moja" Matha alijibu huku akianza kuondoka.
"Sheli ndio mimi, kwani una tatizo gani…gari ipo wapi tujaze mafuta upesi" Minja aliwahi kumzuia Matha kwa kumdaka mkono asiondoke! wakati huo akiendelea kuvuta kumbukumbu ni wapi amewahi kumuona
"Ehee! tena we nimewahi kukuona hapahapa sheli nimekumbuka tayari, ni dada nani vile waitwa" Minja alimweleza Matha. Matha akavutiwa na uchangamfu wa Minja akamuona ni mtu sahihi wa kuweza kumuuliza.
"Hivi nanii? hapa kuna....." Matha akakatishwa na mlio mkubwa wa simu ya kichina ya Minja. Minja akataka kusogea pembeni aweze kuipokea simu, ikawa zamu ya Matha kuingiza utani akamdaka Minja mkono.
"Hauondoki na wewe!! chagua simu au mimi" Minja akainama chini kama aliyekuwa anafikiria jambo kwa sekunde kadhaa akapata maamuzi
"Fimbo ya mbali haiui nyoka! huenda huyu ndo riziki yangu" alijifikiria na kisha akakata simu na kuizima. Ikapiga kelele wakati inazima, akatumia viganja vyake kuiziba spika.
"Nimekuchagua wewe mama naniii" Matha akalipokea jibu hilo kwa kicheko hafifu.
"Naitwa Matha"
"Matha MWAKIPESILE yeah!" alimalizia Minja kwa sauti yenye mshangao. Matha macho yakamtoka alishindwa kupiga kelele, hakuweza kucheka wala kulia, sura yake ikawa kama aliyeshtuka kutoka usingizini.
"Umenijuaje?" aliuliza
"Nilikwambia nakufahamu..sasa nimekumbuka vizuri" alijibu Minja.
"Ndio umenijuaje kwani?" alihoji tena Matha wakiwa bado wamesimama
"Nikikwambia jingine ...we mke wa mzee John Mapulu" alisema Minja kisha akacheka huku akimkimbia Matha kiutani, Matha naye akamkimbilia. Minja akasimama. Hofu kubwa ikamzunguka Matha hakumfahamu mtu huyu lakini yeye alimtambua. Wapita njia wakawa wanaosha macho yao kufurahia mchezo huu wa Matha na Minja.
"Mungu mkubwa sana nilikuwa nakusubiri wewe, na niliyemzimia simu ni mumeo..nina bahati mie" alizungumza Minja, Matha akahisi nguvu zikipungua mwilini, ujasiri ukaaga mwili wake Hatia ikachukua nafasi yake.
Mambo yameharibika??? akajiuliza
"Hebu tukae basi!!" Matha alizungumza huku akitupia macho yake huku na huko kuangalia wapi pa kukaa. Minja alitambua msako huo, akamshika Matha mkono hadi kwenye kimgahawa fulani wakakaa, Minja alikuwa ametawaliwa na tamaa na ujivuni alitamani kila mtu amwone jinsi alivyokuwa anatembea huku amemshika Matha mkono. Alitamani sana kuwa na uwezo wa kumiliki mtoto mzuri kama yule lakini hakujua upande wa pili wa Matha kuwa ni mtu hatari sana.
"Ujue mzee wetu asubuhi amesahau kitu cha msingi sana, nilimpigia simu lakini hatukuelewana.
"Kitu gani"
"Kwanza naitwa Minja wa Meri" alijitambulisha bila kuwa ameulizwa na yeyote. Alifanya hivyo baada ya kugundua kuwa hakuna atakayemuuliza hapo baadaye.
"Haya!! haya ehee!!" alikubali harakaharaka Matha, hakulitilia maanani jina la Minja kwa wakati ule.
Muhudumu akafika na kuwasikiliza, wote wakaagiza maji ya matunda, wote walichagua mchanganyiko wa embe na parachichi.
Mlipaji alikuwa ni Matha!!!!
"Hongereni sana maana dah!! ujue mtu akikuangalia hawezi kuamini mh!! watu mmeumbwa mkakubali kuumbika" Minja alizungumza huku akiupima urembo wa Matha kwa macho yake. Tabia za kidalali zikaendelea kumtafuna Minja. Maneno mengi!!!. Akili ya Matha ikagutuka hakika alikuwa akimuhitaji sana Minja, hapakuwa na kingine cha kupewa hongera zaidi ya huo ujauzito, tena kwa mtu kama yule wasiyefahamiana.
Noti nyekundu nne tayari zilikuwa halali ya Minja baada ya mazungumzo hayo na kumkabidhi Matha kile alichokuwa anakitafuta.
"Sitaki John ajue sawa!!! nilikuwa nimemfanyia kama 'surprise' hivyo usimwambie kitu chochote kile" Matha alidanganya, Minja akauingia mkenge.
"Usiwe na shaka bosi wangu!!!" alitii.


*****

Michael alishindia nyumbani akitathmini juu ya mauaji aliyoyafanya John, lakini mauaji hayo hayakuwa ya kumuweka kitandani kubwa zaidi ilikuwa juu ya Matha na mimba aliyonayo. Maswali na hofu kuu ilikuwa dhidi ya John iwapo akigundua itakuwaje. Je ataniua kikatili zaidi ya yule bodaboda?? au atanipiga risasi?? Alijiuliza Michael bila kupata majibu sahihi. Simu yake ya mkononi ndio ilimkatisha kupata jibu sahihi, alikuwa ni Matha, Michael aliitazama sana simu ile kabla ya kuamua kuipokea, aliamini ilikuwa ni kero nyingine tena.
"Michael nahitaji kuonana na wewe kuna jambo hapa haliendi sawa!" aliongea huku akitweta Matha
"Nini tena??" aliuliza kwa utulivu
"Nahitaji kukuona" sauti hii sasa iliamrisha, Michael akashtuka
"Sawa muda gani??"
"Saa mbili usiku we utajua jinsi ya kufika nitakuwa SHETHEMBAA SHETHEMBA BAR Mecco"
"Haya nitakuja" alijibu na kukata simu.
Hakuwa na hamu ya kuwa karibu na Matha tena kutokana na hatari iliyopo lakini hakuwa na ujanja aliitii amri, tayari ilikuwa saa kumi na mbili jioni. Michael akajikokota hadi sebuleni akaliendea jokofu na kujitwalia maji ya kunywa yaliyokuwa kwenye kopo dogo, wakati anayafungua akasikia injini za gari zikiunguruma nje, alikuwa ni John amerejea, akahairisha kunywa maji akaliendea geti na kufungua.
"Usifungue nahitaji kutoka na wewe, vaa viatu twende maeneo kidogo" sauti ya amri ya John ilimzuia Michael. Kama vile roboti akatii amri akaingia ndani na kuvaa viatu kisha akarejea baada ya kuwa amemuaga Bruno aliyebaki ndani.
Mwendo haukuwa mrefu sana, injini ikazimwa mbele ya maandishi 'WELCOME CHEERS PUB" wakatafuta mahali tulivu wakakaa, muhudumu akawasikiliza haja zao na kuwapatia huduma.
"Michael nimepata safari ya dharula, nadhani nitaondoka kwa wiki kama mbili hivi" alianza kuzungumza John kisha akaendelea, "Ishi vizuri na Matha na Bruno sawa, wasikilize wanachokueleza na wala usilete ubishi" Michael akakubali kwa kichwa.
"Nakuachia jukumu kubwa moja, chunguza sana mienendo ya Matha halafu nikirejea utanipa taarifa rasmi japo naamini hakuna baya analofanya nyuma yangu, zawadi nitakayokuletea itakufanya utabasamu maisha yako yote!!!"
Michael akawa msikilizaji hadi mambo ya msingi yalipoisha, pombe alizokunywa zikamsahaulisha kuwa alikuwa na ahadi na Matha, majira ya saa tatu kasoro alijongea kwenda haja ndogo, mezani akimwacha John akiendelea kupata mvinyo wake. Baada ya dakika kadhaa alirejea.
"We dogo hapa kwa wasukuma utarogwa!!!!"
"Nirogwe na nani na kwa nini??"
"Wake za watu ni sumu" alisema John huku akimpa Michael simu yake. Upande wa ujumbe ulikuwa wazi yaani kuna ujumbe umesomwa.
"Nimekwambia tuonane umepuuzia ngoja sasa bwege akigundua kuwa una mahusiano na mimi utakoma, usinipigie simu" Michael alitetemeka dhahiri, pombe ikayeyuka, aliogopa kumtazama John aliyekuwa hoi kwa kicheko.
"Cheki unavyokodoa macho!!!! ndo unaachwa hivyo" alitania John
Michael hakusema lolote, licha ya kwamba jina lilikuwa halijahifadhiwa kama Matha lakini bado aliogopa. Akajichekesha kidogo na kujidai hakuna anachoogopa. John naye akaacha kucheka.
Wakaendelea kunywa hadi usiku wa manane ndipo wakarudi nyumbani, wakalala sebuleni, siku iliyofuata John akasafiri, alimtaarifu Matha kwa njia ya simu.


*******


Mazingira yalikuwa yamebadilika sana japo ni miezi mitano tu tangu afike pale kwa mara ya mwisho, mabadiliko yalikuwa makubwa mno, ni yeye alituma pesa kwa ajili ya marekebisho hayo lakini hakutegemea kama ingekuwa kiasi hicho. Geti lilikuwa kubwa jeusi la kisasa, katika mitaa yote ya Lincon, Maree, Maruku na Uhasibu palikuwa na nyumba mbalimbali lakini hii ilikuwa na ulinzi mkubwa zaidi pia ilikuwa nzuri sana.
Barabara ya Ginery iliyokuwa lami tupu hadi maeneo ya uhasibu ilimpa raha sana John kuliendesha gari aina ya Landcruiser Prado alilotokanalo Mwanza, ulikuwa ni mwendo mkali sana lakini alifika Singida bila wasiwasi wowote.
Honi mbili alizopiga zilimsukuma mlinzi hadi nje, akalifanyia usahili wa macho gari lile, likawa geni machoni mwake.
"Shida!!!" aliuliza kwa amri yule mlinzi, sauti yake ilikuwa ya kujiamini sana.
"Mgeni wa mzee Bushir!!!" alijibu John huku akijiamini
"Mna 'pointment' " aliuliza tena kwa kiingereza cha kubahatisha lakini bado alizungumza kwa amri kama vile askari polisi.
"Mwambie John Mapulu"
"Nani??"
"John Mapulu!!!!" alirudia kwa utulivu. Simu ikanyanyuliwa na kubonyezwa namba kadhaa. Baada ya maelezo mafupi akairudisha mahali pake na kufungua geti, John akaingiza gari. Jumba lile lilikuwa limependeza sana na lilimvutia John akaridhika na kiasi cha pesa walichotoa kulikarabati.
"Comrade John Mapulu!!!! Mapulu ze great" akiwa bado nje analitathmini jengo hilo, mzee Bushir akawa amefika na kumlaki John. Wakakumbatiana kwa sekunde kadhaa; lakini Bushir mzee huyu wa kiarabu hakuwa na furaha sana.
"Vipi malaria au?? mbona hivyo??"
"Hapana ni unyonge tu, si unajua tena mama yako ameenda kwao kusalimia" alidanganya, John akaridhika.
"Vipi mgeni wangu naye mzima?? au naye malaria" aliuliza John.
"Mzima yule" alijibu kana kwamba hakulitaka swali hilo. Wakaongozana hadi ndani ambako hawakukaa sana , jokofu halikuwa na vilevi hivyo wakaamua kuhamishia maongezi yao Bar ya uhasibu iliyokuwa maeneo ya jirani.
"Sam Mayuni bado yupo??" John alimuuliza Bushir wakati wakikatiza maeneo jirani na chuo cha uhasibu Singida T.I.A.
"Yupo, aende wapi yule??" alijibu.
Pale bar, nyama choma na bia zilitawala maongezi yao lakini kuna mada ambayo mara kwa mara mzee Bushir alikuwa anaikwepa ni mada kuhusu mgeni wa John. Yote walizungumza lakini walipofikia mada juu ya Joyce Keto mzee Bushir alilegea sana.
"Kwani vipi mbona kila unavyomzungumzia unaguna???" John aliuliza akiwa na mashaka kidogo
"Aah!! hapana hapana kitu" alijitahidi kujibu Mzee Bushir bila kujua kwamba alikuwa akijiumauma. John akapandisha mabega juu, akabetua midomo kisha akakata pande la nyama akalitupia mdomoni na kushushia na Kilimanjaro baridi.
Waliendelea kupiga pombe huku wakisimuliana mikasa mbalimbali iliyowahi kuwasibu katika shughuli zao hizo haramu, kwa jinsi walivyokuwa wakisimuliana ni kama vile suala la kwenda jela kwao kilikuwa kitu cha kawaida.
"Hivi Dulla yupo???" John alimuuliza Bushir
"Ah!! Dullah alipigwa condemn" alijibu Bushir. Ndugu msomaji 'Condemn" maana yake ni kuhukumiwa kunyongwa.
John alisikitika kidogo kisha akaendelea kula nyama.
"Ulisikia kuhusu Soja.....dah!!! msela wetu yule wamemuua vibaya sana, wamemvisha tairi wakamtia moto....halafu nilikuwa naye kwenye ule msala pale Kariakoo sokoni...unadhani napatamani Dar tena???" John alisimulia ikawa zamu ya mzee Bushir kusikitika.
Majira ya saa nane usiku wakaanza kujikongoja kurejea nyumbani, kwa kuwa hawakuja na gari lao walijikokota kilevilevi hadi wakafika nyumbani, kila mmoja akalala hoi. Asubuhi wote waliamka mapema 'hangover' haikuwa kikwazo kwa wawili hawa kupanga mipango yao. Kilichokuwa kimemleta John katika mji huo ni silaha na funguo kwa ajili ya tukio walilotegemea kulifanya la kuiba katika supermarket
"Bushir jana usiku nimeota mambo ya kiajabu ajabu lakini nimekumbuka asubuhi kuwa haikuwa ndoto bali ukweli mtupu"
"Nini tena" aliuliza kwa hamu ya kujua jambo
"Joyce Keto na Minja"
"Minja??? ndo nani huyo"
"Lofa mmoja anauza mafuta huko mwanza"
"Mafuta ya kusafishia bunduki!!! kafanyaje" aliendelea kuwa gizani mzee Bushir
"Petroli...nimekumbuka niliwahi kuzungumza naye kwenye simu aliniambia mambo ya ajabu ajabu hata hayana msingi ila nashangaa eti namkumbuka"
"Ushaanza ule ujuaji wako wa kuhisihisi wewe..machale yalikuaga zamani ushachoka wewe!!" alisema Bushir wakati huo walikuwa chumba cha silaha wakisafisha Bunduki. John hakuendelea kuzungumza.
"Anaweza kuwa 'Informer' yule" alijisemea John, mzee Bushir akasikia. Msomaji, INFORMER ni askari aliyestaafu ambaye anajichanganya na watu waovu huku akijidai ni mwenzao kumbe anatoa taarifa kwa polisi walio kazini.
"Unamuacha anaishi hadi leo???" alishangaa Bushir.
“Nikirudi Mwanza namchukua mateka, kama ni informer namuua kwa mkono wangu!!!” aliapa John, kwa kusema hivyo na Bushir naye akasita kuendelea na zoezi lile.
"Hata mimi kuna mjinga namsaka, yaani zingekuwa enzi zangu kabla ya huu uzee ningekuwa nimemkamata tayari na kumtoa uhai"
“Nani tena huyo”
“Fala mmoja alikuwa mlinzi hapa!!!”
“Akaiba???”aliuliza John
"Bora angeiba, ame......" alisita kuzungumza akamtazama John machoni, John akasita kuendelea na zoezi la kusafisha bunduki. Bushir akaendelea, "Alimbaka Joy!!!" alimalizia kwa sauti ya chini. John akajikuta yuko wima, laiti kama angekuwa mchina nywele zake zingesimama.
"Joyce Keto alibakwa?????" alihoji John, ni kama hakuelewa nini Bushir anazungumza. Bushir akaanza kusumbuliwa na hatia, hatia ya kubakwa kwa Joyce. Aliamini itamuwia ngumu sana John.
"Joyce yupo wapi sasa????" aliuliza John baada ya kufanikiwa kuituliza hasira yake. Bushir hakujibu kitu akawa anatetemeka midomo. John aliliona hilo, mapigo ya moyo yakaamua kuongeza mwendo kumaanisha kwamba John alikuwa anaogopa kusikia jibu kutoka kwa Bushir.

John alijaribu kujizuia asihamakinike lakini alishindwa kujizuia kwa hilo, Bushir akaliona hilo. Hofu ikamtanda akamuogopa John kama kiumbe cha ajabu kisichofaa kuishi na mwanadamu. John alikuwa ameiva kwa hofu kuu iliyochanganyika na hasira.
"Kwa hiyo Joyce ametoroka ama ame.."
"Hapana hajatoroka wala hajafa.....tatizo ni kwamba baada ya miezi minne atajifungua" alijikakamua na kujibu Mzee Bushir.
"Joyce ni mjamzito!!!!!"
"Ana mimba" alijibu Bushir, John akalegea akakaa chini, hakupenda kabisa kuisikia taarifa hiyo. Hiyo ndio zawadi alikuwa ameiandaa kwa ajili ya kumpelekea Michael kwa ukarimu wake na kumrejesha Matha katika himaya yake, zawadi ya pikipiki pekee ilikuwa haijatosheleza. John akajikuta katika dimbwi kubwa la mawazo, moyo wake ulijutia kitendo cha kumficha Joyce kwa muda wote huo. Michael hatanielewa kabisa!!!! alisema John, Bushir hakuelewa lolote hakuwa akimjua Michael.
Hakuwa na jinsi aliamua kuendelea na zoezi la kusafisha bunduki huku wote wakiwa kimya sana, kitendo cha Joyce kuwa mjamzito kilimtia uchungu sana na kuikaribisha shubiri ya hatia kuanza kumshambulia, hakuwa akimuogopa Michael hata kidogo lakini pia hakutaka kuweka udikteta mbele ati kisa yeye ni mbabe mbele ya Michael.

*****

***MATHA amecheza karata sahihi...amemuwahi MINJA kabla hajafikisha ile kadi kwa JOHN MAPULU....kumbuka MINJA hajui siri iliyojificha katiaka kadi hii.........

***JOHN MAPULU anapewa taarifa kuwa JOYCE KETO ni mjamzito.......anajisikia yu HATIANI kwa rafiki yake mpenzi......JE NI NANI AMEMPACHIKA MIMBA JOYCE!!!!

HATIA INAZIDI KUTAPAKAA......

Itaendelea

No comments:

Post a Comment

Recent Posts