MTUNZI: Emmy John P.
CONT: 0654 960040
4
Nilikuwa makini katika kulikanyaga lile zulia jekundu, sikutaka kuonekana mshamba katika hilo. Nilijilazimisha kutembea mwendo wa kilimbwende wakati niliamini kuwa iwapo nitathubutu kuingia katika mashindano ya ulimbwende basi nitashika nafasi ya mwisho ama sitapata walau kigezo cha kusimama jukwaani kama mlimbwende. Maana nilikuwa cha ufupi na nilikuwa na dalili ya kuwa kibonge.Niliongozwa hadi katika chumba kikubwa sana, kila kitu pale ndani kilikuwa cheupe kasoro ngozi yangu ambayo ilifanya kama uchafu pale ndani. Sikujali!!!
“Utalala hapa ndani…na hawa watakuhudumia.” Nilipewa wakinamama wawili kwa ajili ya kunihudumia. Umri wao sidhani kama unatofauti sana na wa mwalimu Nchimbi yule mama yangu mzazi. Lakini matabasamu yao ni kama walikuwa na miaka kumi na nane.
Ungekuwa wewe ungejisikiaje. Mwenzako nilijisikia kama malkia.
Nilipata huduma zote za msingi hadi nilipopitiwa na usingizi na kuamka siku iliyofuata. Baada ya kuwa nimeoga na kupewa nguo nyingine nyeupe tena nilikaribishwa kifungua kinywa.
Ilikuwa kufuru nyingine tena niliyoweza kuishuhudia. Meza ilikuwa imesheheni kila aia ya makorokoro. Kazi kwako mlaji kujihudumia. Kiaibuaibu nikajinyima kula nilivyovitamani nikala nilivyovizoea. Na ushamba pia ulichangia. Kuna vyakula sikuelewa kama vinaliwa kwa kijiko ama uma, harufu yake nzuri ikabaki kunisurubu. Nikaogopa kujaribu!!!
Majira ya saa tano asubuhi niliongozwa tena kuelekea katika ile gari ya milango sita. Nikaingia humo kwa namna ileile kama malkia. Safari yetu ikaishia katika sehemu nyingine ya kifahari. Sikuwa naielewa nchi ya Zambia hivyo sikujua lolote.
“Mukuba Hotels.” Hilo ndilo neno nililoweza kulisoma baada ya kuunyanyua uso wangu juu. Sikujua maana ya Mukuba. Lakini bila shaka zilikuwa lugha za huko kwao. Hii hoteli ama jumba la kifal me!! Nilijiuliza.
Tuliingia hadi ndani huku mimi nikiwa mfuata mkia nisiyejua lolote linaloendelea mbele. Baada ya kukatiza kona kadha wa kadha sasa tukakutana na mlango ulioandika kwa maandishi yenye rangi ya dhahabu!! Dr. Davis. Moyo wangu ukapiga kwa nguvu. Paa!!
Ina maana Davis anaishi hapa? Nilitamani kuuliza ila nikasita.
Nikiwa nasubiri ajitokeze mtu kwa ajili ya kubisha hodi ili tuweze kuingia ndani maana sikuona mahali pameandikwa ‘PULL/PUSH’ mara mlango ule wa vioo ulianza kufunguka wenyewe.tukaingia ndani.
Sasa tulikuwa watu watatu pekee!! Wale wawili baada ya kuingia ndani pamoja nami wakatoka nje. Bila kusema neno!!
Sasa nikabaki peke yangu.
Kiti cha kuzunguka kilichokuwa kimegeuziwa ukutani kikazungushwa taratibu. Vazi la suti likanisabahi, kisha uso ukanyanyuka.
“You are most welcome!!” Alinikaribisha. Kisha akatabasamu. Alikuwa anafanana na Davis lakini sikutaka kuamini. Labda ndugu yake au au au…
“Ndo mimi mbona unashangaa.” Aliniwahi. Ni kama alijua nilichokuwa nawaza. Alikuwa ni Davis. Sauti yake ilikuwa ileile.
Nikachukua nafasi. Bila kusema lolote alibonyeza kitufe mara kikashuka mfano wa kitrei cha kuwekea vyombo.
“Unatumia kinywaji gani.” Aliniuliza mimi nikiwa bado nashangaa.
“Aaaah!! Chochote.” Nilijiumauma.
Akabonyeza vitufe kadhaa, kikaondoka na kurejea tena baada ya dakika tano.
Maajabu ya nane ya dunia. Kile kitrei kilikuwa na glasi mbili za juisi. Akatwaa moja akanipatia. Sijawahi kuona tangu nizaliwe!!
“Asante.” Nilimshukuru. Hakujibu.
Dokta Davis aliyekuja Tanzania hakufanana hata kidogo na huyu. Huyu alinuka pesa tena pesa nyingi.
“Karibu Ndolla Zambia, hii ni ofisi yangu ndogo ya huku, nyingine ipo Lusaka, Accra na kubwa zaidi ipo Washington.” Alinielezea kwa sauti iliyojaa ujivuni. Lakini alikuwa amechangamka!!
Nilikuwa makini kumsikiliza.
“Isabela…. .”
“Abee!!.” Niliitika.
“Kampuni yangu imeamua kufanya kazi na wewe.”
“Nashukuru sana Dokta.” Nilishukuru, hakujali hilo akaendelea
“Unauchukia umasikini?.”
“Nauchukia kuliko niavyoweza kujielezea.” Nilisisitiza.
“Na….anyway..unaenda sana kanisani.”
“Aaah!! Kiukweli ni mara chache chache.”
“Kwa nini?.”
“Aaah!! Mambo huwa yanakuwa mengi sana.”
“Ok!! Achana na hayo…Isabella kazi uliyopata hapa ni kazi nyepesi na kila mwezi itakuingizia shilingi milioni sita laki sita na elfu sitini na sita kila mwezi.” Alizungumza Dokta bila wasiwasi, alimanusura nipoteze fahamu. Mwili ukawa wa baridi. Nikajaribu kujishtua huenda ninaota, haikuwa hivyo. Hali ile ilikuwa halisi.
Nilikuwa Zambia na nilitangaziwa dau hilo kubwa.
“Unawazungumziaje wanaume kwa ujumla?.” Davis hakujali ule mshtuko wangu akanitupia swali jingine, bila shaka milioni sita kwake si lolote si chochote.
“Aaah!! Kiaje labda” Nilimuuliza huku nikifinya finya mikono yangu.
“Vyovyote vile lakini hasahasa katika kazi ya mapenzi.”
“Viumbe waongo, wasiokuwa na huruma, wanyanyasaji na…”
Nilishindwa kuongea nilikuwa nimemkumbuka John, mwanaume aliyeamua kuachana nami kisa sina pesa. Sasa hapa nazungumzia juu ya kupata pesa.
“Labda ukiambiwa uwape adhabu utatoa adhabu gani kwao.”
“Dah!! Sijui watoweke duniani…aaah!! Sijui ila nawachukia wanaume wenye tabia hii.” Nilimjibu huku nikilegeza koo kwa kugida funda mbili za juisi ile. Ilikuwa tamu sana. sijui tunda gani lile!!!
“Safi sana…kumbe kazi utaiweza kabisa lakini lazima kwanza ubadili kwanza mawazo yako hayo ya kuombea wanaume watoweke. Lengo la kampuni yangu mimi ni kuwabadili wanaume kuacha na mfumo huo wa unyanyasaji na pia kuwafunza wanawake kuepukana na vishawishi vya wanaume wadanganyifu. Tunaamini kuwa utaweza kutuwakilisha vyema katika nchi yako. Ukimuelimisha msichana mmoja kwa siku basi ujue umeielimisha jamii kubwa sana.” Aliongea kwa umakini mkubwa huku akiwa amenikazia macho. Nilikwepesha kutazamana naye.
“Nitaweza hata usitie shaka.” Niliikubali kazi. Zikaangushwa karatasi nne mezani nikasaini mkataba mnono.
“Baadaye kidogo pesa ya utangulizi itaingizwa katika akaunti yako.” Alimaliza Dokta.
Tunaweza kuzunguka zunguka kidogo uitazame ofisi yangu. Lilikua ombi la Dokta nikakubaliana nalo.
Tulizunguka kona tofauti tofauti. Nilikuwa nikimtazama Davis kwa kuibia ibia na yeye pia alifanya hivyo. Yale mawazo ya kumfanya awe mpenzi wangu yakawa yananisumbua akili nilitamani kumwambia lakini mdomo ukawa mzito.
Laiti kama nikiwa naye!! Hata hii ofisi pia itakuwa mali yangu!! Niliwaza.
*****
Ulikuwa usiku wa kipekee sana kwangu, ndio kwanza nilikuwa nimerejea jijini Mwanza, kwa usafiri bora wa ndege. Kwa mara ya kwanza katika maisha yangu. Sijui niseme mara ya pili!! Maana mama alinihadithia kuwa nilipokuwa mtoto niliwahi kupanda ndege!!!
Baada ya kushuka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere bila kuwa na wa kunipokea sasa hapa Mwanza nilihitaji mtu fulani ajue kuwa nimekuja na ndege!! Huyo mtu ni nani kama sio John!!!
Nilimwomba John afike kunipokea. Nilifanya hayo makusudi ili kumkomoa kwa ubaya alionifanyia. Ubaya wa kuniacha na kuwa na mahusiano na msichana mwingine.
Ni kweli John alikuwa amenitenda vile lakini John bado alikuwa moyoni mwangu. Nilikuwa nampenda sana John. Walikuwepo wanaume wengi lakini nafasi ya John bado nilikuwa sijaona wa kumrithisha.
John aliposikia nakuja na ndege hakusita kunikubalia. Labda ili athibitishe kwamba kweli nimekuja na ndege ama la. John alinipokea huku akinipapatikia, niliifurahia hali hiyo. Tulichukua taksi iliyotufikisha katika hoteli yenye hadhi ya juu ya La kairo jijini Mwanza tukajipatia chumba. Chumba cha bei ya juu kabisa!! Sikuwa na wasiwasi kuhusu pesa!!
Wakati huo John tayari alikuwa amemdanganya mpenzi wake wa wakati huo Jesca kuwa hatarejea chuoni siku hiyo kwa kuwa kuna rafiki yake anaumwa. Ameenda kumsalimia.
Usiku majira ya saa nne, tayari tulikuwa tumelia sana baada ya kukumbushiana yaliyopita. John akaniomba msamaha nami sikusita kumsamehe. Kilichofuata hapo ni kurejesha hisia za zamani na kuanza kushambuliana, kila mmoja akijitahidi kuamsha hisia za mwenzake, baadaye kidogo. Vita!!!
Vita ya miili. Kila mmoja akitamani kuibuka mshindi, hapakuwa na mwamuzi. Wakati vita hiyo ikiendelea ikaanza kusikia kama sauti ikiniongelesha kwa kabila kama kihehe vile, lakini sikuweza kuielewa lakini niliwahi kuisikia mahali. Ni kweli niliwahi kuisikia mahali, lakini sasa sikuwa nakumbuka ni wapi. John alikuwa bize, huenda alikuwa akifurahia peke yake. Nilitamani kumwambia John azisikilize zile sauti lakini hakuweza kunisikia alikuwa ulimwengu mwingine.
John alipokoma, na sauti zile nazo zikatoweka. Ni kama vile zilikuwa kando ya dirisha zikitusemesha ama zikinisemesha.
“John walikuwa wanasemaje?.”
“Nani?. Hao wahudumu ama.?” Aliuliza kwa utafiti.
“Hapana!!!anyway acha ilivyo.” Nilimaliza mjadala.
John hakuuliza zaidi.
Nilielekea bafuni kujisafisha, kisha nikarejea tena pale kitandani. John alikuwa amesinzia. Sikuwa na hamu naye tena bali nilizitafakari zile sauti zilikuwa zikisema nini.
Lakini kama John , hajazisikia basi hakuna sauti yoyote!!! Nilijipa moyo.
Asubuhi John alikuwa wa kwanza kuamka. Aliingia aliwatoni akajisafisha na kuniamsha. Nami nikafanya kama alivyofanya kisha tukaondoka. John akaelekea alipopajua nami nikaelekea chuoni.
Zile sauti nilizozisikia usiku ule sikuzikumbuka tena. Nilichokumbuka ni kwamba mimi na John tulikumbushia enzi.
******
Sikuweza kujua ilikuwa ni saa ngapi, lakini niliamini ilikuwa ni usiku tena usiku sana. Kuna sauti zilikuwa zimezungumza nami, tena kwa lugha ninayoielewa, zilikuwa sauti zenye furaha sana.
Nikiwa bado natafakari sauti hizo zilizungumza nini na mimi. Mara simu yangu iliita. Alikuwa ni rafiki yangu wa darasani. Nikajiuliza kulikoni. Nikaipokea simu.
“Isabella, Isabella….Jenipher jamani. Jenipher!!”
“Amekuwaje tena. Eh!! Nambie.”
“Jenipher yupo hoi hospitali hapa.” Alijitahidi kuongea bila taharuki lakini alisikika akitetemeka. Baada ya pale hata kabla sijamjibu, simu yake ilikatika.
Nilipojaribu kumpigia hakupatikana. Nikajilazimisha kulala, huku nikiamini kuwa lile ni tatizo la kawaida tu
Asubuhi palipopambazuka, taarifa ilikuwa nyingine, taarifa ya kushtua nafsi!! Jenipher msichana aliyekuwa akiishi na huyo rafiki aliyenipigia usiku uliopita.alikuwa amefariki baada ya jitihada za madaktari kugonga mwamba.
Ilikuwa habari ya kusikitisha sana kwani kilikuwa kifo cha ghafla mno.
Sikuzikumbuka zile sauti za usiku ule zilikuwa zinasema nini na mimi.
Sasa nikawa nawaza juu ya msiba huo!! Msiba wa ghafla!!
***Sauti gani zinazomsumbua Isabela??
Na ni kitu gani zinamueleza???
ISABELA amesaini mkataba……Je? Atatimiza malengo yake anayowaza kila siku.
ITAENDELEA......
No comments:
Post a Comment