Friday, November 16, 2012

SITAISAHAU facebook 7


MTUNZI: Emmy John P.

CONTACTS: 0654 960040

SEHEMU YA SABA

ILIPOISHIA

Au nataka kuwa mtakatifu??? Nilijiuliza. Huku nikiamini moja wapo ya dalili za kuwa mtakatifu ni kuyajua yanayokuja kupitia ndoto.

Mh!! Utakatifu gani huu lakini hata kanisani penyewe siendi?? Nilitengua mawazo yangu.

“Dada nakuita jamani!!.” Sauti ya yule muhudumu ilinishtua. Inavyoonekana alikuwa ameniita mara nyingi sana.

Nilikuwa sipo kawaida na niliombea sana wasiitambue hali hii.

Simu yangu ikaita nikaitoa kuitazama alikuwa ni Dokta Davis.

Nikapokea na kuiweka sikioni.

“Samahani nipo saluni.” Nilimsihi.

“Usijali nilikuwa nakutaarifu ukatazame salio katika akaunti yako.”

“Hamna shida.” Nilimjibu na kukata simu.

***ISABELLA katika mtihani mwingine…..Ndoto ya ajabu inayogeuka kuwa kweli.

Je kuna nini hapa??




ENDELEA


Nilipotoka pale saluni nilitaka niende kwanza nyumbani kwangu lakini nikaona kwanza nipitie benki kutazama salio.

“Laki sita elfu sitini na sita na mia sita sitini na sita.” Hichi ndio kiasi kilichokuwa kimeongezeka katika akaunti yangu. Sikushtuka sana safari hii, nilikuwa nimeanza kuizoea pesa hii kubwakubwa.

Sikuwa na haja yoyote ya kutoa pesa kwani bado nilikuwa na pesa nyingi ndani. Niliingia katika bajaji iliyokuwa imenileta nikamuamuru anipeleke Kijiweni, huku ndipo nilikuwa naishi.

Tulipoifikia kona ya kijiweni nilitelemka na kuliendea duka la madawa nikachukua dawa za kutuliza maumivu.

Nilipofika chumbani nikanywa na kujipumzisha kidogo kwa minajiri ya kuoga baada ya dakika kadhaa. Nilikuwa bado nawaza kuhusu kifo cha Basu kwa kung’atwa, lilikuwa jambo la kushangaza sana. Na kilikuwa kifo cha kustaajabisha, kivipi afe kama ndoto yangu ya usiku? Nilijiuliza sana. Sikupata jibu. Nikajitia imani kuwa hizo ni ndoto.


Suala la kwamba ninaandaliwa kuwa mtakatifu lilinisaidia kupungaza hofu.

Lakini utakatifu gani sasa huu wa kuupata bila kwenda kanisani??

Kwani watakatifu wote walikuwa wanaenda kanisani!! Nilijiuliza. Kisha nikaukatisha mgogoro huu wa nafsi kwa kumpigia simu John, nilizungumza naye kidogo akaniambia yupo njiani kuelekea Nyegezi kona kutazama maiti ya Basu.

Aliposema jina hilo nikashtuka lakini hakugundua kwa sababu hakuonyesha wasiwasi na wala hakuuliza swali.

“Basu…Basu amekufa?” Nilijifanya sijui lolote. John akanieleza stori ileile kama mama mnene wa kule saluni aliyosema.

Nikaingia katika fumbo, sikumjua mfumbuzi!!!

Nikapitiwa na usingizi!!!

****


Nilikuwa nautazama sasa umati wa watu ambao sikuelewa ni shughuli gani walikuwa wakiifanya. Sikuwatilia maanani sana na wala sikujua eneo lile ni wapi. Mara nikamuona mtu ambaye ninamfahamu. Nilitamani kumuita lakini niliamini kwa zile hekaheka alizokuwa nazo wala asingeweza kunisikia. Nikapuuzia!!

Sikujua nilikuwa nimejikita katika shughuli gani lakini kuna jambo nilikuwa nafanya.

Mara nikamwona tena yule mtu ambaye nilionekana kumfahamu, sasa alikuwa katika mtafaruku. Wenzake wote walikuwa wakimpigia kelele katika namna ya kupingana. Alikuwa peke yake na hakuna aliyemuunga mkono. Mara wenzake wakaanza kumzonga sasa hayakuwa mabishano tena bali ugomvi. Mtu mmoja anachangiwa na watu zaidi ya kumi. Ugomvi ukawa ugomvi. Kuna jambo walikuwa wanalazimisha. Jambo hilo huyo mmoja hakuunga mkono kabisa.


Baada ya kuzidiwa mara yule mtu akawaponyoka. Akaanza kukimbia. Alikuwa anakimbia huku akiangalia nyumba. Nilikuwa natabasamu nikimtazama maana alionekana kuwa na hofu kuu.

Alipogeuka mara ya kwanza lilikuwa kunndi la watu watano wakimfukuza, akazidi kukimbia, alipogeuka tena walikuwa watatu, akajitahidi kujitetea kwa kuendelea kukimbia, wakabaki wawili. Safari hii hakugeuka.

Alipokuja kugeuka sasa alikuwa amekaribia kukamatwa. Lakini cha kutia moyo alikuwa anakabiliwa na mtu mmoja tu. Japo alikuwa amechoka lakini hata huyu aliyekuwa anakabiliana naye alikuwa anahema juu juu. Walikuwa wanatazama kama majogoo yanayofanyiana ubabe.

Mara jogoo lililokuwa linamkimbiza jogoo mwenzake likamrukia yule mkimbizwa. Wakaanguka chini, ugomvi ukazuka.

Wakagalagana hapo chini kwa namna ya kuchekesha. Nami nikawa nacheka.


Mara yule mtu niliyekuwa namfahamu akaangusha vibaya. Halafu yule aliyemuangusha akachomoa kisu kidogo, upesi akamchana nacho mgongoni. Akatoa ukulele wa uchungu na hofu.

Kuchanwa huko kukawa kumemrejesha upya katika ugomvi. Sasa alikuwa na nguvu kamilifu. Yule aliyekuwa na kisu alipojaribu kumchana tena akawa amechelewa mkono wake ukadakwa, kisha kikafanyika kitendo cha sekunde kadhaa tu cha kuikamata shingo ya mwenye kisu na…na….na…


“Mamaaaaa!!!” Nikakurupuka usingizi!!

Nilikuwa nimelala masaa sita. Niliyapikicha macho yangu huku na huko niweze kuangalia vyema mbele.

Ukungu ulikuwa umetanda. Nikajipikicha zaidi nikaweza kuona, na sasa niliweza kusikia. Mlango ulikuwa unagongwa kwa nguvu. Fahamu zikanirejea vizuri, nikauendea bila hata kuulizia nikafungua. Alikuwa ni jirani yangu.

“Kakasirika kweli John dah!! Amegonga mlango, kapiga simu yako hupokei.” Alinieleza huku na yeye akionekana kukasirika.

Nilipiga mwayo mrefu kisha nikamuuliza kuwa alikuja saa ngapi. Akanijibu. Kisha akajieleza shida aliyokuwa nayo nikamsaidia . akaondoka!!!


*****


Sikuweza kuhudhuria msiba uliomuhusu Basu, akili yangu ilikuwa imechoka sana. Baada ya harakati za hapa na pale nilijipikia chakula kisha nilipomaliza nikalala tena.

Mara hii mlango ulipogongwa nilisikia vyema kabisa. Nikasimama na kwenda kumfungulia. Alikuwa John na ilikuwa saa tatu usiku.

John alikuwa amefanya mfano wa hasira usoni, nililitambua hilo na sikuwa na haja ya kumuuliza kwa nini amekasirika.

Baada ya kuzungumza naye dakika kama kumi hivi huku nikijiweka karibu naye. Alilainika na uso wake ukaunda tabasamu.

Tulizungumza mengi na mpenzi wangu huyu wa zamani. Na kama vile tulikuwa tumeambiana kwa pamoja tukageukiana tukakumbatiana kwa nguvu. John alikuwa analia.

Nilijua kuwa anamlilia Jesca, sikutaka kumuuliza najua angelia zaidi. Nilichofanya ni kuzidi kumkumbatia, viatu vikabaki sakafuni, sasa tukawa kitandani. Lugha iliyozungumza ilikuwa lugha ya mapenzi.

John alikuwa mtulivu kama aliyesafiri kwenda ulimwengu wa mbali. Nikaitoa shati yake akawa amebakiwa na singlendi. Nikataka kuitoa na ile.

“Ngoja nikaoge kwanza baby…” aliniambia kwa sauti nzito yenye kutamanisha.

Nikatulia nikamtazama naye akanitazama.

“Twende wote pliiz.” Nilimsihi. Hakujibu chochote nikajua kuwa maana yake ni kwamba twende.


Nikaziondoa nguo zangu, nikajivika upande wa kanga.


“He!! Sa na hiyo singlendi waipeleka bafuni kufanyaje tena!!!” Nilimuuliza John baada ya kumuona akiingia na ile singlendi bafuni.

“Si haujataka kunivua sa mi ntafanyaje?.” Aliniuliza kitoto. Nikatabasamu, nikamwendea, akakimbilia upande mwingine wa chumba nikamfata tukawa kama tunagombana. Japo hatukutumia nguvu sana!!!

“ukiweza kunivua nakubeba mgongoni!!” Alinipa motisha nikazidisha juhudi. Nikaitoa nikawa mshindi.

Mshindi kubebwa mgongoni!! Ikumbukwe hiyo.

Mimi ndiye mshindi, mgongo mali yangu.

John akachuchumaa nikawa nyuma yake.

Ile nataka kupanda mgongoni nikaona kitu cha ajabu.

Kovu!!! Kovu bichi!!! Kovu katika mgongo. Kovu la kuchanwa na kisu

“Mamaaaaa!!” nikapiga kelele. John akasimama. Tayari nilikuwa katika kona ya chumba nikiwa natetemeka sana!!!

“Sabe sabe!! Umekuwaje…” aliniuliza huku akinisogelea. Nikawa namkimbia, lakini wakati huu haukuwa mchezo tena nilikuwa katika hofu ya ukweli. Nilikuwa namuogopa John.

John alinisihi niache utani!!! Lakini sikuwa natania. Nilikuwa katika kumaanisha.

Hali ilikuwa tete. John alikuwa ananitisha.

Nikiwa katika kumkimbia John. Sasa aligundua kuwa kuna jambo limenisibu. Akanifata kwa kasi. Akanivagaa. Nikajilazimisha kujitoa mikononi mwake huku nikipiga kelele. Ghafla akaninasa vibao viwili.

Sasa hapo ndio nikachanganyikiwa mwenzenu na kuamini kuwa dunia imefika mwisho. Nililia huku nikimtaja mwalimu Nchimbi.

Lakini cha ajabu na kukera huyo mwalimu Nchimbi hata hakuwa akinisikia.

Iliniuma. John akaniongeza vibao vingine viwili. Sasa yale maumivu akili ikasogeleana.

“John una damu!! Una damu!!” nilipayuka

“Damu??” aliniuliza.

“Mgongoni umekuwaje wewe.”

“Mgongoni pamekuwaje kwani…alilalamika huku akijipapasa”

Maajabu mengine jamani!. Mkono wake haukuwa na damu. Akanigeukia.

Nikatamani kuiaga dunia niende likizo mbinguni. Hakuwa na kovu.

Mgongo laini kabisa wa kiume ukatazama nami. Nikaruka mita kadhaa.

Akapoteza uelekeo kuniona naruka vile nikataka kukimbia nje.

Akanidaka kanga yangu. Kanga ikateleza ikauacha mwili.


Shanga nane za rangi tofauti zilizokishika vyema kiuno changu ndio pekee zilizosalia katika mwili wangu. Sasa John alikuwa amebaki na kanga mkononi mimi nikiwa nina shanga kiunoni. Nusu nilikuwa nje na nusu nilikuwa ndani.

Swali likavamia kichwa changu.

Nikimbie na shanga kiunoni kwenda nje ama nirudi chumbani kwa John huyu wa maajabu!!! John niliyemuhisi kuwa sasa ni ………….

Nikabaki katika kizungumkuti.


JE ISABELA ATAKIMBIA NA SHANGA KIUNONI KWENDA NJE AMA ATARUDI KWA JOHN ANAYETISHA??

NINI KINATOKEA HAPA!!!!!!!


ITAENDELEA!!!

No comments:

Post a Comment

Recent Posts