MTUNZI: George Iron Mosenya
CONT: 0655 727325
SEHEMU YA KUMI NA MBILI
"Hapana hajatoroka wala hajafa.....tatizo ni kwamba baada ya miezi minne atajifungua" alijikakamua na kujibu Mzee Bushir.
"Joyce ni mjamzito!!!!!"
"Ana mimba" alijibu Bushir, John akalegea akakaa chini, hakupenda
kabisa kuisikia taarifa hiyo. Hiyo ndio zawadi alikuwa ameiandaa kwa
ajili ya kumpelekea Michael kwa ukarimu wake na kumrejesha Matha katika
himaya yake, zawadi ya pikipiki pekee ilikuwa haijatosheleza. John
akajikuta katika dimbwi kubwa la mawazo, moyo wake ulijutia kitendo cha
kumficha Joyce kwa muda wote huo. Michael hatanielewa kabisa!!!!
alisema John, Bushir hakuelewa lolote hakuwa akimjua Michael.
Hakuwa na jinsi aliamua kuendelea na zoezi la kusafisha bunduki huku
wote wakiwa kimya sana, kitendo cha Joyce kuwa mjamzito kilimtia uchungu
sana na kuikaribisha shubiri ya hatia kuanza kumshambulia, hakuwa
akimuogopa Michael hata kidogo lakini pia hakutaka kuweka udikteta mbele
ati kisa yeye ni mbabe mbele ya Michael.
*****
Tumbo lake lilikuwa halijachomoza bado, kipande cha limao kilikuwa
pembeni ya kitanda chake. Alikuwa amejilaza huku akilitazama panga boi
lililokuwa linapambana na joto lililokuwa linataka kuingia humo ndani,
bila shaka katika mpambano huo panga boi lilishindwa ndio maana akatumia
leso aliyokuwanayo kujifuta jasho lililopenya katika vinyweleo vyake.
Mawazo yake makuu yalikuwa juu ya kiumbe aliyekuwa amejihifadhi katika
tumbo lake, wazo la pili lilikuwa juu ya utata uliopo katika kiumbe huyo
asiyekuwa na hatia kwa upande wake lakini mama yake alifikiria kwamba
kiumbe huyo naye pia ana hatia kwanini aingie sehemu isiyokuwa salama.
Mwanamama huyu mtarajiwa alisita kumuwazia kiumbe aliyebebwa na tumbo
lake baada ya kusikia hodi mlangoni. Aliuvuta mdomo wake na kumlaani
huyo aliyekuwa anaugonga mlango wake, hakutaka usumbufu wowote ule siku
hiyo alikuwa ameamua kupumzika na kujichukulia maamuzi ya kipekee.
"Ulikuwa umelala nini??" aliulizwa bila hata kusalimiwa
"Wala kwani vipi??"
"Niazime elfu mbili, baba Rozi akija nitakurudishia" ilikuwa sauti ya
upole kabisa ya mama Rozi sauti ile ilielezea waziwazi shida. Matha
Mwakipesile hakujibu kitu aliingia ndani na kurejea na noti ya shilingi
elfu mbili akamkabidhi mama Rozi, akashukuru na kuaga. Wakati anataka
kurejea ndani alimuona mtu kwa mbali chini kabisa, alidhani mwanzoni
kuwa amemfananisha lakini hakuwa amemfananisha.
Mbiombio akashuka
akiwa na kanga moja hakujalisha ni wangapi watamuangalia japo alijijua
kabisa ni kiasi gani ana makalio makubwa na mitikisiko yake ni kanga
hiyo pekee ingeweza kuijibu kuwa ni kiasi gani inaipa shida. Mwendo wa
harakaharaka akaona kama haumsaidii akaamua kukimbia kumuwahi mtu yule,
vijana wavuta bangi na wasiokuwa na kazi walianza kupiga miluzi, Matha
hakujali lolote. Alishawazoea!!!
Alilipita hilo kundi kama vile
upepo na kuendelea mbele, akiwa hajategemea tukio kama hilo kumtokea
Matha alihisi kuguswa na mkono wa mtu, kuna bwana alikuwa amemshika
Matha makalio. Miluzi ikazidi kwa sababu ya tukio hilo, hasira ikamkumba
Matha. Yule mwanaume akaleweshwa sifa na ile miluzi akaanza kukimbia
kumfuata Matha ili amshike tena na kujizolea sifa zisizokuwa na tija.
Macho makali na maangavu yakamtoka Matha akahisi kudhalilishwa na mtu
dhaifu sana, akauvua urembo wake akauvaa umafia aliofunzwa na John
Mapulu, Matha akauvaa ukichaa wake akaudaka ule mkono kwa kutumia mkono
wake wa kushoto. Mkono wa kuume ukatamani nao kufanya walau kazi kidogo,
Matha akauruhusu, ngumi moja imara ilitosha kuuchana chana mdomo wa
mtumiaji huyu wa madawa ya kulevya ambaye shibe kwake ni hadimu sana,
damu ilibakia katika mkono wa Matha wala haikumshtua alishayazoea
matukio hayo. Mzuka wa mapambano tayari ulikuwa umempanda. Akamuona yule
kiumbe alifaa sana kwa kushushia mzuka huo. Mwanamke huyu jasiri
alifanya kitendocha ghafla lakini cha maajabu. Alijitupa hewani kwa
mzunguko wa teke la Vandame, teke la kwanza likamkosa lakini like la
pili likatua sawia shingoni. Akatua chini kama mzigo. Tendo alilolifanya
Matha mwanamke wa kawaida hawezi kulifanya lakini MATHA si mwanamke wa
kawaida!!!
Alipomaliza kumuadabisha kelele hazikuwa kwake tena bali
alikuwa akizomewa yule aliyeadhibiwa, Matha alikuwa amempoteza machoni
mtu aliyekuwa anamfuatilia lakini alijipa moyo kuwa atakuwa ameingia
stendi.
Akaamua kuingia hapo ndani, kwa macho makali kabisa ya
kijambazi aliangaza haraka haraka ndani ya dakika tatu tayari alikuwa
amemtia machoni.
"Michael!!!!" aliita Matha, bado alikuwa na ari ya
kijambazi. Michael aligeuka na kukutanisha macho yake na Matha, alitaka
kukimbia pasipo sababu Matha akaligundua hilo akamdaka mkono, Michael
hakutegemea Matha huyu ambaye huwa anamsukuma anavyotaka wakiwa
kitandani anaweza kuwa imara kiasi hiki, hakuweza kuutoa mkono wake
katika mkono mmoja wa Matha.
"Unaenda wapi Michael"
Michael
hakujibu, Matha akamkokota hadi pembeni kidogo ambapo waliweza kusikiana
wao wawili tu. Matha akamtazama Michael machoni kisha akamwachia
"Naomba unipe dakika mbili tu nizungumze ukimaliza endelea na safari
yako, safari ya kumkimbia mwanao, safari kafiri ya kuyakimbia
majukumu!!! Michael samahani kama nakulazimisha, kuwa huru wewe ondoka
lakini kamwe sitakiua kiumbe ndani ya tumbo langu, nipo radhi John aniue
lakini si mimi kuua, nilitegemea muunganiko huu wa damu ndio ungetupa
akili ya kutanua penzi letu lakini kwako haikuwa hivyo, ni wapi sasa
waelekea??? sitaki kujua jibu la swali lako, kwani najua ni wapi
unaelekea, unatokea katika uanaume wako kamili na kuukimbilia ushoga kwa
ufahari mkubwa.
Nenda Michael, nadhani umenichoka na unatamani
kuolewa gerezani, nenda Michael nenda!!!" alishindwa kuendelea
kuzungumza Matha donge la hasira lililokuwa limemkaba kooni likapasuka
na kuleta sayansi ya ajabu kuliko zote duniani, uchungu wa moyoni
unaosikika kooni na kifuani kisha kutokea machoni kama machozi na
kujihifadhi tena mwilini kama majonzi makubwa. Kwa haraka haraka akaanza
kuondoka, mkono wake ukawa unamsaidia kuyafuta machozi kwa nguvu zote,
machozi yakakaribisha kamasi nyepesi hasira kali ikamfumba macho Matha
barabara mbovu ikamkaribisha kipofu huyu wa muda akajikwaa na kuisalimia
ardhi kwa heshima zote, kichwa, kidevu, mikono, miguu na tumbo vyote
vikaibusu barabara!!!! Matha hakupata hata nafasi ya kupiga kelele
akatulia tuli.
Michael akaliona tukio lile, begi lake dogo
likamponyoka lakini hakujua kama limeanguka akaanza kutimua mbio, Matha
alikuwa ametulia tuli
*******
Joyce Keto alikuwa amejikita katika kucheza game katika kompyuta ndogo
iliyokuwa chumbani kwake, tayari alikuwa ameyazoea maisha ya kufugwa,
miezi kadhaa aliyokuwa amekaa hapo bila kuwasiliana na upande wa pili wa
dunia ulikuwa umetosha kumbadilisha, alipata kila alichokitaka katika
nyumba ile aliishi na familia ile kama yupo nyumbani kwao, japo alipata
tabu sana siku za mwanzo kuzoea lakini baada ya kipindi hicho kirefu
alizoea.
"Da Joy baba anakuita!!!" aliitwa na mtoto wa bwana Bushir aliyeitwa Davda alikuwa na asili ya kihindi.
Joyce Keto hakujibu kitu aliendelea kucheza game kisha baada ya dakika kadhaa aliinuka na kuelekea katika wito.
"We!! Davda yupo wapi mheshimiwa" aliuliza Joyce. Davda akamweleza akatoweka kuelekea katika wito.
"Neh neh papa!!!" Joyce alizungumza akimwambia Bushir, Bushir
akajilazimisha kucheka. John akajua kuwa Bushir alikuwa na utani na
Joyce.
"Shkamoo bosi!!!" alimsalimia mgeni aliyekuwa na Bushir. John
Mapulu naye hakujibu bali alicheka japo si kicheko halisi, Joyce
akachukua nafasi katika kiti kilichokuwa wazi, akaiunganisha miguu yake
katika staili ya kukunja nne, kinguo kifupi alichokuwa amevaa kikayaweka
mapaja yake wazi, kwa Bushir lilikuwa jambo la kawaida lakini kwa John
moyo ulighafirika akahisi anaingizwa majaribuni.
"Mambo vipi Joy....unanikumbuka???"
"Hapana tangu nizaliwe ndo nakuona mara ya kwanza hata ndotoni sijawahi
kukutana nawe" alijibu Joy, John akacheka. Hakika Joy asingeweza
kumkumbuka John kwani kwa sasa alikuwa ana afya tele tofauti na awali
alipokuwa ametoroka rumande.
"Naomba niwaache kidogo!!" aliaga Bushir
"Naitwa John.......John Mapulu" alijitambulisha
"Mara ya mwisho nilikuona ukiwa unamtesa bwana mmoja kule Mwanza ni
nani yule??" aliuliza Joyce huku akilamba kipande cha limao. John hakuwa
na la kujibu.
"Mimi!!!!!"
"Ndio wewe John, japo umebadilika, nilikuwa nimekusahau lakini sio jina lako kamwe sijalisahau"
John alijaribu kupambana na wasiwasi uliomkumba kwa kupiga funda kubwa la juisi iliyokuwa mezani, akafanikiwa.
"Utajua siku nyingine" akajibu kwa amri, Joyce Keto akanywea.
"Unamfahamu aliyenibaka" aliuliza Joyce
John akashindwa tena kujibu, Bushir alikuwa amesahau kumwambia John
kuwa tukio la kubakwa alilofanyiwa Joyce liliathiri akili yake na
kumfanya kuonekana kama kiumbe wa ajabu asiyeogopa kitu.
"Nitampata!!!!" alijibu John swali ambalo hakuwa ameulizwa
"Ukimpata utanipa na mimi nimtese kama mlivyomfanya yule wa Mwanza"
alizungumza Joyce akikumbuka tukio la kumuona John akimuadabisha mateka
wake jijini Mwanza.
"Usijali!!!!"
“Yule mjomba wetu mzima…”
“Mjomba? Yupi?”
“Yule ambaye mlikuja naye siku zile kunichukua ….” Joyce alikuwa
akimaanisha Bruno. John akaishia kucheka bila kujibu. Joyce naye
akafanya tabasamu!!!
Hawakuzungumza zaidi!!
*****
Hofu aliyokuwa ameipata Michael ingeweza kumletea uwendawazimu kichwani
kama tu asingekuwa jasiri wa kukubaliana na hali, jambo zuri ni kwamba
walikuwa jirani sana na kituo kikubwa cha mabasi hivyo usafiri wa kukodi
halikuwa jambo lenye usumbufu sana.
Ndani ya dakika mbili Michael
alikuwa amepata wasaidizi wa kutosha wengine walikuwa kazi yao ni kulia
wengine walimgusagusa Matha Mwakipesile kama vile walikuwa wanampima
homa kwa njia ya hisia za mkono. Matha hakutikisika, baada ya
ushirikiano mkubwa Matha alikuwa ndani ya 'Taksi' safari ya kuelekea
hospitali ya mkoa ya Bugando!!! Hakuwa akijitambua kwa lolote, fahamu
zilikuwa zimeuacha mwili kwa muda.
Wazo la Michael kutoroka likawa limeishia pale.
******
Umati wa watu katika jumba la kifahari alilokuwa anaishi John na Bruno
kabla ya ujio wa Michael ulimshangaza kila mtu, ulikuwa ni msiba wa aina
yake, watu wote walikuwa wamevaa sare sare, wanaume walikuwa wamevaa
suti nyeusi huku akina mama wakiwa na mavazi yao ya vitambaa vyeupe,
kila mmoja alipendeza. Katika kundi la wanawake wale ni mwanamke mmoja
tu aliyemshtua Michael, huyu kwa kila kitu alifanana na Joyce Keto,
msichana ambaye kwa namna kubwa sana alikuwa amechangia yeye kuwa katika
janga hili lililotawaliwa na Hatia.
"Ametoka wapi??? au
nimemfananisha" alijiuliza Michael wakati huo akijipenyeza katika kundi
la wanaume na kuingia katika kundi la akina mama, lengo likiwa
kuhakikisha kuwa aidha yule ni Joyce ama la!!.
"Mambo vipi dada!!"
alimsalimia, yule mwanamke aligeuka na kuanza kumshangaa, wakati wakiwa
bado wanashangaana Michael alihisi kuguswa begani, mwanzo alipuuzia
hadi pale Joyce alipomwambia kuwa anaitwa. Alipogeuka alikutana na sura
ya Matha ikiwa inatabasamu kinafiki.
"Mamaaaaaaaaaaaaaaaa!!!!!! " alilipuka kwa kelele kubwa Michael.
"Vipi kaka nini???" Michael aliulizwa na mtu aliyekuwa pembeni yake.
"Ah!! ni ndoto kaka dah!!!" Michael alijibu huku akiyapikichapikicha
macho yake ili aweze kuipata nuru mbele yake, nuru iliyokuwa imemezwa na
usingizi, usingizi ulioambatana na ndoto, ndoto ya ajabu, ndoto ya kifo
cha Matha na marejeo ya Joyce Keto. Ah!! ni ndoto tu Matha hawezi
kufa!! aliwaza Michael na kupuuzia alichokiota. Pia alijenga tabasamu
baada ya kuyakumbuka maneno ya mama yake aliwahi kumwambia ukimwota mtu
amekufa, huyo hafi.
"Lakini Joyce hivi atakuwa wapi yule binti!!!"
alijiuliza, hakuwepo wa kujibu. Majira ya saa kumi na moja jioni majibu
kutoka chumba cha uangalizi alichokuwa Matha yalitolewa. Hakuwepo mtu
mwingine wa kuyapokea zaidi ya Michael ambaye ndiye alimleta.
Majibu
hayakuwa ya kufurahisha sana, kwani maombi ya Michael yalikuwa juu ya
mimba alitamani sana itoke lakini wala jambo hilo hakulisikia kutoka kwa
daktari.
"Jitahidi sana, hakikisha anapata pumziko la kutosha na matunda ale mara kwa mara."
"Hamna shaka dokta" alikubali Michael. Saa moja usiku Michael
aliruhusiwa kumchukua mgonjwa wake, pesa ya ziada aliyobaki nayo mfukoni
alilipia matibabu na usafiri wa kurudi nyumbani, safari nzima walikuwa
kimya hadi wakafika nyumbani kwa Matha, Michael akamsaidia Matha kupanda
ngazi taratibu hadi wakafika chumbani. Siku mbili mfululizo Michael
alikuwa anashindia nyumbani kwa Matha akimuuguza, Bruno hakuwa akifahamu
ni wapi huwa anaenda na wala hakujali sana kwani ni mtoto wa kiume.
Furaha ya Matha ilirejea tena kutokana na upendo wa Michael.
Maisha yakaendelea!!!
Haikuwa kawaida ya Michael kulala nyumbani kwa Matha, nafsi haikumvusha
hadi kuufikia ujasiri huo. Lakini siku hii ya ijumaa tulivu kabisa
Michael alijikuta akifanya mambo kinyume na matakwa yake.
Ilianzia kwenye sherehe ya siku ya kuzaliwa ya Matha, Michael pamoja na Bruno walikuwa wamealikwa.
Bruno aliaga mapema na kuondoka kwani haukuwa utaratibu wake kukaa
maeneo ya watu wengi kwa muda mrefu, kwa kuwa Michael alikuja na
pikipiki yake hakuwa na wasiwasi wowote muda wowote angeweza kurejea.
Kadri muda ulivyokuwa unaenda ndivyo Matha alizidi kunywa pombe hadi
akawa hoi kabisa. Michael alikuwa amelewa kiasi cha kawaida sana, kwa
pamoja waliondoka majira ya saa tano usiku kurejea nyumbani. Michael
alitegemea kumfikisha Matha na kuondoka zake kuelekea nyumbani lakini
haikuwa hivyo. Matha alimletea vurugu za kilevilevi hadi wakaoga wote,
kama hiyo haitoshi wakaingia kitandani wote. Michael hakuweza kujizuia
zaidi akakiri kuzidiwa maarifa akasalimu amri. Saa saba usiku simu ya
Michael iliita, hawakuwa wamelala wawili hawa.
"Ni John!!!!"
alihamaki Michael, Matha hakusema neno. Zilikuwa ni siku nne tangu
aondoke na kuahidi kurejea baada ya wiki mbili.
"Niambie kaka mkubwa!!" alianza kuzungumza baada ya kupokea simu.
"Poa dogo, nishakukataza mambo ya wake za watu shauri zako hapo najua upo na mke wa mtu!!!" sauti ya John ilijibu.
"Hamna nipo kwa mwanangu mmoja hivi kanipiga pombe hatari"
"Haya bwana mi naenda kwa shemeji yako hivyo, si nilikuwa nimesahau
kama leo ndo 'birthday' yake!!...yaani najua atakuwa amenuna huyo"
"Nani Matha au....eeh!! upo Mwanza" alizungumza bila kujiamini, wakati
huo yule Matha aliyekuwa anajidai amelewa chakari alikuwa amekaa kitako
macho yamemtoka pima.
"Ndio nipo hapa maeneo jirani na nyumba yake
dakika sifuri tu nafika ndani, we endelea kulewa si ushalijua jiji mi
ntafanyaje??"
Tumekwisha Matha, tumekwisha!!!! alisema Michael huku
akitapatapa pale ndani. Matha naye alikuwa wima, kanga ilikuwa
imedondoka na alikuwa amesalia uchi lakini hata hakulitambua hilo.
Hatia ikaunda hofu katika mioyo yao!!!
******
Katika chumba ambacho MICHAEL yupo na mpenzi wa mtu hatari
kabisa....mpenzi wa JOHN MAPULU......huyu kiumbe asiyekuwa na huruma yu
jirani kuingia.
MICHAEL na MATHA chumbani.....je? JOHN akiwafumania
kitatokea nini...je!! ndio kifo cha MICHAEL...ama wote MICHAEL na
MATHA!!!!!
ITAENDELEA
No comments:
Post a Comment