Tuesday, November 27, 2012

SITAISAHAU facebook

MTUNZI: Emmy John P.

CONTACTS: 0654 960040



SEHEMU YA TISA


                                                                                           ILIPOISHIA

Pasipokutegemea John alisukumwa chini, akapinduka, lakini yule bwana alijaribu kukimbia tayari mguu wake ulikuwa umekamatwa.

John alipogeuka ile alama ya kuchanwa na kisu ikaonekana. Nikabaki kama zoba siwezi kupiga kelele wala kutoa msaada wowote.

Huyu naye akageuzwa shingo, kisha ghafla pakawa giza sikuweza kuona mbele. Lakini nilihisi kama napoteza fahamu hivi.

Macho yalipopatra ujasiri na kufunguka nilikuwa nimezungukwa na watu wenye nguo nyeupe.

Kila jicho likinitazama mimi.

Hofu mpya ikaanza.

***ISABELA katika mtihani mwingine!!!!


ENDELEA


******

Watu hawa walitabasamu vizuri lakini sikujua kwa nini wanatabasamu.

“Pole sana!!.” Mmoja wao aliniambia.

“Nini kwani…eeh!! Hapa ni wapi.”

“Hospitali ulipoteza fahamu.” Mwanaume aliniambia.

Sasa akili ilianza kuunganika upya nikawatambua kuwa wale ni madaktari. Kilichonisibu nikashindwa kukielewa vyema. Nikavuta kumbukumbuku nikakumbuka kuwa ni ndoto. Ndoto nyingine ya maajabu. Ndoto iliyonifanya nizimie dah!! Hii ilikuwa hatari zaidi ya kawaida.

Nikatamani kumshirikisha mtu yeyote kati ya wale madaktari lakini nikaamini kuwa hawataelewa.

Mtu sahihi wa kumueleza ni John. Huu ni wakati muafaka wa kumueleza kila kitu kinachotokea. Ni John pekee ambaye anaweza kunielewa juu ya shida hii. Sikuona mtu mwingine wa kumueleza.

Nilipumzika kwa masaa kadhaa kisha John akaruhusiwa kuondoka na mimi. Ni yeye aliyenileta pale hospitali baada ya kugundua kuwa nilikuwa nimezimia.

Ilikuwa ni tukio la kawaida mtu kuzimia lakini lilikuwa si la kawaida kwa sababu aliyezimia ni Isabela. Mtu mwenye heshima zake pale chuoni. Kila mtu alitaka kujua nini kimenisibu. Nashukuru John alikuwa akiwajibu kwa niaba yangu.

Sasa tulikuwa chumbani. John alinikorogea uji wa ulezi akatia maziwa na pilipili manga. Alijua kuwa ninaupenda sana uji wa aina hiyo.

Nilipomaliza kunywa kikombe cha kwanza. Nilitaka kuanzisha ile mada juu ya nini kilinitokea ndotoni.

Maajabu!! Nilipomuita naye aliniita ndani ya sekunde hiyo hiyo. Tukajikuta tunacheka.

“Nani sasa aitike ya mwenzake.”

“Ladies first.” John alidakia. Basi sikuwa na ujanja mimi nikaitika nimsikilize John anasema nini.

“CR (Class representative) wa PR (Public relation)….”

“Amekufa??.” Niliuliza hata kabla John hajamaliza kunieleza. Tayari picha ilianza kuja kichwani.

“Yeah! Umejuaje kwani?.” Aliniuliza.

“Ni yule alikuwa ndugu yako au sio..”

“Ni yeye Michael ndio jina lake. Binamu yangu.” Alisema kwa masikitiko makubwa sana John kisha akainama. Hapakuwa na haja ya kuuliza kama alikuwa anajizuia kutoa machozi.

“Pole John.” Nilimwambia kwa sauti ya chinichini.

“Wamemnyonga binamu yangu wameona kumuua Jesca haitoshi aaah!!.” Alilalamika mwisho akashindwa kuendelea akaanza kulia kwa sauti ya juu. Nikawa katika hali mbili ghafla. Kwanza hofu kubwa kwani alichozungumza John sasa kilitaka kuwa kile ambacho nilikiota. Pili nikawa katika kumbembeleza Michael kwa juhudi zote. Huku nafsi ikiniambia ninambembeleza muuaji.

Lakini muuaji gani huyu sasa asiyejitambua kuwa ameua? Nilijiuliza.

Nikahisi kuchanganyikiwa.

“Isabela.” Aliniita.

“Bee!!.”

“Nitahakikisha namfahamu huyo muuaji…kitambulisho chake kilidondoka na polisi wamedai wanafanya upelelezi.” John alitoa kauli nyingine. Kauli ambayo ilinishtua upya. Niliona kitambulisho kwenye ndoto. Lakini mwenye hicho kitambulisho alikuwa ni John mwenyewe na muuaji ni John.

Ina maana John anaapa kujitafuta mwenyewe ama!!

Nilichanganyikiwa!!!

Nilitamani kumweleza John juu ya ile ndoto lakini sasa hamu yote ilikuwa imetoweka. Sikuwa na haja ya kumweleza, ataniamini vipi. Kwamba ni yeye aliyemuua binamu yake kwa kumnyonga na kuwa hicho kitambulisho ni cha kwake.

Hapana hawezi kuniamini hata kidogo!! John ataniona mjinga na ataidharau ndoto yangu.

Nikaghairi kumweleza. Siri hiyo ikajikita na kuanza kuutesa moyo wangu. Mateso makali.

Baada ya maziko hayo. Sasa chuo kilikuwa kimesimamia kidete juu ya upelelezi juu ya vifo mfululizo vya wanafunzi katika chuo cha mtakatifu Augustino. Kitambulisho kilichookotwa eneo la tukio kilikuwa kimeamsha hamasa ya kumjua muuaji. Polisi walikuwa makini sana katika hili na walikuwa watulivu wakiendelea na upelelezi kimya kimya.

Alipotoka msibani John alikuwa na jingine jipya. Alikuwa amepoteza kitambulisho cha chuo.

“Yaani sijui hata kimepoteaje. Maana kilikuwa kwenye Wallet yangu. Sasa ah!!” Alinieleza John. Sasa ndoto ikawa imekamilika kabisa.

Ni John alikuwa muuaji. Lakini muuaji wa ndotoni.

Ndani ya siku saba nilikuwa nimekonda sana. Uzito ulikuwa umepungua. Ni serikali ya ubongo wangu pekee iliyojua ni nini kinanisibu.

Si John wala mtu mwingine aliyejua nini kinanisibu.

Nilikuwa nawaza juu ya usalama wa John. Niliona kama anaenda kukutana na hatia kubwa sana ambayo hawezi kuikwepa. Lakini kosa lile alilifanya katika ndoto yangu mimi pekee!!!

Kivipi niwe na hofu!!

Nilijifariji kuwa ile ilikuwa ni ndoto tu lakini hapana bado nilikuwa hoi bin taabani

Suala la kupoteza kitambulisho chake lilinipagawisha.kimawazo.


****


Hakuna ambaye hakujua kuwa sikuwa na tabia ya kunywa pombe baada ya kuanza rasmi kuwa muelimishaji rika la vijana. Nilikuwa nahamasisha sana kuhusu jambo hili na kuipinga vikali pombe.

Wataalamu wa mambo walikiri kuwa pombe husaidia kupunguza mawazo sana. Sasa Isabella mimi nilikuwa na mawazo. Tena mawazo makali yaliokuwa yakishambulia ubongo wangu.

Kitambulisho!!!

Hiki ndio kiliniua kabisa. Hamu ya kula, raha ya kuwa na pesa zote hazikuwa na maana tena.

Siku hii nikaamua kwenda kugida pombe. Lakini kwa siri kubwa kabisa nikaamua kwenda mbali na chuo. Mbali na John.

Mbali ya kila jicho linalonifahamu kwa ukaribu.

Mkolani!!!! Nikajichimbia huko. Nikatafuta baa safi kabisa, nikajiweka sehemu ambayo si rahisi kugonganisha macho na watu.

Moja, mbili, tatu…nikaanza kuhesabu idadi ya chupa zinazokuwa tupu mbele yangu. Ni siku nyingi nilikuwa sijapata kinywaji hichi. Basi ilikuwa burudani.

“Dada mna vyumba hapa?.”

Nilimuuliza muhudumu mmoja. Akakiri kuwa vyumba vipo. Nikamwomba anifanyie Booking.

“Standard, Suite ama Deluxe.” Aliniuliza. Swali hilo likanikumbusha wakati tunampeleka dokta Davis kuchagua hoteli ya kulala.

Alijibu vipi vileeee.

“Deluxe.” Nilimwambia kwa kujifanya nimefikiria sana.

Sikuwa na muda wa kuulizia bei. Pesa ilikuwepo ya kutosha.

Baada ya kusikia kichwa kinachemka sasa nikahamishia makazi chumbani. Elfu sabini ilinitoka kwa malipo ya chumba.

Hata sikujuta!!

Mashambulizi ya kunywa pombe yaliendelea kwa fujo. Kitanda cha sita kwa sita kikinisubiri iwapo nitapitiwa na usingizi.

Chumba hakikuwa na mbu hata mmoja. Nani kakudanganya raha ni mpaka uende ulaya?

Hata Mwanza kuna raha, sehemu yoyote kuna raha.

Cha muhimu hizo raha jipe mwenyewe!!!

Isabella nilikuwa najipa raha mwenyewe.

Muhudumu wa kike alikuwa bize kila mara kuja kunitazama kama nimemaliza pombe alete nyingine ama labda nahitaji kutafuna kuku akachome ama afanye lost ni mimi tu!!!. Na hiyo ndio ilikuwa kazi yake kwa ujira wa elfu ishirini niliyompa.

Ni kweli nilikuwa nimelewa lakini bado nilikuwa ninao uwezo wa kuona. Safari hii mlango ulipofunguliwa aliingia mwanaume, huyu hakuwa na mavazi kama ya yule muhudumu.

Alijitambulisha kwa jina sikuweza kusikia. Akataja wadhifa wake, ulikuwa wadhifa mkubwa lakini hata hivyo pia sikuweza kusikia vyema.

Macho yalikuwa yameanza kupoteza nuru. Nikaingia gizani.


Saa nne asubuhi ndipo niliamka.

“Dada mchemsho tuweke nini na nini?.” Aliniuliza yule dada niliyemlipa usiku uliopita. Hakika alifanya kazi yake ipasavyo.

“Leta supu ya mbuzi..supu ya mbuzi unanielewa.” Nilimwambia. Akanielewa akaondoka.

Hangover ilikuwa inacheza na kichwa changu. Na sikuwa na mawazo yoyote.

Baada ya kunywa supu niliyoipenda kabisa nilijisafisha na kubadilisha nguo. Nikalipia bili zote, kisha yule dada nikamwongeza pesa nikaondoka.

Nilipotoka nje niliangaza hapa na pale nikaona teksi, nikaipungia mkono.

“Nipeleke mjini.”

“Elfu nane.”

Akanitamkia sikumjibu. Nikaingia garini. Akaondoa.

Hapakuwa na foleni. Dakika ishirini nikawa nimefika.

Nikatoa pesa yake na kumpatia.

Nikaanza kuondoka baada ya kuwa nimemweleza kuwa hiyo elfu mbili abaki nayo. Nilikuwa nimetoa noti ya shilingi elfu kumi.

Sasa nilikuwa naondoka kabla hajaniita tena.

“Umedondosha kikadi chako.” Aliniambia. Nilipogeuka. Nilitazama chini, ni kweli nilikuwa nimedondosha kitu. Nikajongea na kukiokota.

“Asante!!” nilimshukuru. Sasa nilimtazama usoni kwa mara ya kwanza.

Nilitaka kumuita jina lake kwa sababu nilihisi ninalijua jina hilo. Hata sura mbona nilikuwa nimewahi kuiona hapo kabla? Lakini kabla sijajua anaitwa nani. Teksi ilipigiwa honi ikapisha njia ikaondoka zake.


“Ah!! Huenda aliwahi kunibeba hapo kabla.” Nilijipa moyo.

Nikafungua pochi yangu na kuhifadhi hicho nilichookota.


“Mungu wangu!!!!” nilipiga kelele kwa nguvu sana. Nilikuwa nimesimama wima.

Kwa kuwa halikuwa eneo la watu wengi nilipata sekunde kumi za kuhakikisha nilichokiona.

Hakika kilikuwa chenyewe.


Kilikuwa kitambulisho cha chuo ni heri kingekuwa changu.

Kitambulisho cha John mikononi mwangu. Kitambulisho kinachoaminika kupotea, msibani huko Iringa , kitambulisho nilichokiona ndotoni.

Kitambulisho cha muuaji!!!

Ewe dunia funguka unimeze!!! Ni sala niliyoiomba kimyakimya.

Nilikuwa nimezizima siwezi kwenda mbele wala kurudi nyuma.

Harufu ya kifo!!!!


***NI jambo juu ya jambo…….ISABELA ISABELA ISABELA.

Lakini je ungekuwa wewe ungefanya nini sasa….John unampenda, John umeota akiwa anaua, kweli mtu kafa. Huyu mtu ni binamu wa John. John anapoteza kitambulisho. Na ndotoni muuaji anadondosha kitambulisho. Sasa unamiliki kitambulisho hicho.

John na muuaji wa ndotoni wanafanana….Kabla ya kujua Isabela mimi nilifanya nini…Je WEWE UNGEFANYA NINI HAPO.

Pagumu!!!!!


ITAENDELEA.

No comments:

Post a Comment

Recent Posts