Friday, November 16, 2012

HATIA ----- 13

"Nani Matha au....eeh!! upo Mwanza" alizungumza bila kujiamini, wakati huo yule Matha aliyekuwa anajidai amelewa chakari alikuwa amekaa kitako macho yamemtoka pima.

"Ndio nipo hapa maeneo jirani na nyumba yake dakika sifuri tu nafika ndani, we endelea kulewa si ushalijua jiji mi ntafanyaje??"

Tumekwisha Matha, tumekwisha!!!! alisema Michael huku akitapatapa pale ndani. Matha naye alikuwa wima, kanga ilikuwa imedondoka na alikuwa amesalia uchi lakini hata hakulitambua hilo.

Hatia ikaunda hofu katika mioyo yao!!!


******

Matha hakuonyesha kufurahia ujio wa John pale ndani, alijifanya kuwa amelewa sana ilimradi tu John aweze kuondoka mapema, ujanja wake ukafanikiwa John aliaga na kuondoka huku akiahidi kufika pale asubuhi.
"Na hiyo pikipiki ya nani hapo nje??." John alimuuliza Matha, hakujibiwa lolote Matha akajifanya amesinzia tayari. John akajikongoja akatoka nje, alijaribu kupiga simu ya Michael haikupatikana.
"Hili toto hili na wake za watu, shauri zake!!!" alijisemea John huku akiufungua mlango na kutoka nje.
Michael hakuwa na hali kabisa, mchezo uliokuwa unaendelea ni hatari sana kwa upande wake, hali ya kuwa katika chumba kimoja na John Mapulu ilimchanganya sana, japo alikuwa katika uvungu wa kitanda na John akiwa kitandani huo haukuwa umbali mkubwa sana kati yao, alisikia kila alilozungumza John, hisia alizomueleza Matha.
Hatia ikampa shambulizi kali akajikuta anatokwa machozi kimya kimya ni dhambi aliyokuwa akiifanya na Matha ni usaliti mkubwa sana ni zaidi ya hatia.
John alipotoka na kuhakikisha kweli ametoweka Michael alitoka uvunguni na kuvaa nguo zake vizuri kabla ya kuaga, safari hii hakukubali kutawaliwa kimawazo na Matha. Aliondoka!!!
"Naomba uiache pikipiki!!!" Matha alimwambia Michael, kidogo apinge lakini kwa shingo upande akakubaliana naye.


******


Asubuhi John aliamka akiwa amechelewa kiasi, majira ya saa nne. Simu yake ilikuwa inawakawaka kuonyesha kuwa kuna ujumbe ama simu imepigwa haijapokelewa. Ulikuwa ujumbe wa Matha. Ujumbe uliozidisha hofu ya John juu ya Michael. Matha alikuwa ameuelezea ukarimu wa Michael kwake.
"Tazama ameenda kwenye sherehe, tazama amemrudisha nyumbani na pikipiki, amehakikisha usalama wake upo kabisa, ni mashemeji wachache wanaweza kuwa kama Michael!!!" aliwaza John huku akirudia kuisoma meseji ile.
John alizidi kumchukia kijana aliyempa ujauzito Joyce Keto. "Isingekuwa mimba basi hiyo ndio ilikuwa zawadi ya kipekee kwake" alisema John peke yake.
Mawazo ya John dhidi ya Michael yaliipunguza furaha yake. Siku hiyohiyo jioni baada ya kumtembelea Matha alimtafuta Michael ambaye walikuwa hawajaonana ili waweze kuzungumza.
Kituo cha mafuta maeneo ya mitimirefu ndicho kilimkumbusha kuhusu kijana Minja. Alikumbuka simu yake ya mwisho na mazungumzo kati yao.
"Oyo niaje"
"Poa kaka karibu!!"
"Namuulizia Minja sijui yupo?" aliuliza John
"Yupo kaka yule pale anakuja" alijielezea bwana huyu aliyekuwa na sare za wafanyakazi wa pale sheli huku akielekeza mkono wake kwa Minja, kama vile tayari alikuwa ameitwa Minja alifika pale, mara moja alimtambua John Mapulu.
"Heshima yako mkurugenzi, heshima yako kaka" Minja alianza porojo zake. John hakujibu kitu
"Kulikuwa na nini siku ile kwani, uliponipigia simu" swali lile Minja hakulitegemea ghafla kiasi kile akajiweka sawa kwa kukohoa kidogo kisha akamtazama John, alikuwa amemkazia macho, sura ya Matha akiwa anamsisitiza asimwambie John ikatokeza na kumwambia tena.
"Aaah!! siku zile bosi wangu!! kilikuwa kikaratasi cha mtu mwingine tu nikadhani chako" alijaribu kudanganya.
"Matha Mwakipesile unamfahamu??" aliuliza John kama vile alikuwa akimtuhumu Minja.
"Matha.....Matha......" alijaribu kukumbuka
"Ni wewe uliniambia hilo jina kivipi leo humkumbuki???" aliuliza tena. Kijasho chembamba kikamkumba Minja, mzigo wa kuchukua pesa za Matha ili asiseme lolote ukawa unamzidia na sasa ulikuwa unamwangusha chini.
"Matha ni yule mkeo eeeh!!!" alijifanya kukumbuka Minja. Honi za magari yaliyokuwa yakihitaji kupita ndio ilikatisha maongezi yao, John aliondoa gari, alijaribu kutafuta wapi aweze kupaki lakini hakupata nafasi yoyote.
"Nitakupigia simu!!" alisema kwa sauti ya juu iliyomfikia Minja ambaye alikuwa anatetemeka hovyo. Alikuwa anawaogopa sana watu wenye pesa zao kama John Mapulu.
Njia nzima John alikuwa anamuwaza Minja Meri, alianza kuhisi kuna kitu anafahamu na ameamua kumuingiza mkenge, John alianza kuhisi kuna jambo la maana sana kama sio kitu cha thamani ambacho bwana Minja alikuwa anataka kumtapeli.
Haiwezekani siku ile amesema kuna kitu, leo hii anasema hakuna kitu!!! hapana!!! alisema kwa ghadhabu huku akiupiga kwa ngumi usukani wa gari lake mlio wa honi ukatoka, aliyekuwa na baiskeli mbele yake akapisha njia. John bado hakuwa na uhakika kama aweke kituo kwa Matha au aonane na Michael kwanza. Akaamua aanzie na Michael.


******


Watu hawakuwa wengi sana katika ukumbi wa 'If not why not' Igoma jijini Mwanza, Michael na John walikuwa na masaa mawili tangu wafike pale, baada ya maongezi ya kawaida ya hapa na pale ndipo John alipoleta mezani mada ambayo kwa upande wake ilikuwa ni sawa na kucheza bahati nasibu wakati kwa upande wa Michael ilikuwa ni kama kaa la moto katika kichwa cha mwanadamu.
"Michael mdogo wangu hivi hata wewe si huwa unapenda kwa dhati!" alianza John
"Ndio tena sana tu!!!"
"Sasa kwa mfano, namaanisha ni kwa mfano sawa!!!" alisita John akapiga funda moja la bia yake kisha akaendelea
"Mtu unayempenda unasikia kuwa.....kuwa ni...ni mjamzito" alizungumza kwa kusitasita John, Michael akahisi nguvu zote hakuna mwilini, pombe yake aliyokuwa anaifurahia ikageuka kuwa na ladha ya pilipili, na nyama choma ile iliyopendezesha meza yao ikawa inamzomea, HATIA ikaendelea kumuadhibu na sasa ilikuwa imefikia pabaya zaidi.

Michael sasa kila kitu aliamini kuwa kipo hadharani, sasa afanye nini hilo ndio likawa swali kuu.
"Mbona umeshtuka sana?? au swali limekuja wakati mbaya???" John alimuuliza Michael aliiyekuwa anajaribu kuushinda uoga uliokuwa umemtawala.
"Swali gumu sana kaka, kwani unamaanisha nini hapo???" na yeye Michael akauliza, John akacheka bila kusema lolote akachana pande la nyama akaanza kutafuna na kushushia na bia.
"Wewe ni mwanaume na mimi ni mwanaume, kwa sasa nawahi sehemu, hebu kaa ufikiri halafu unipe ushauri kuwa kwa mtu unayempenda ukigundua kuwa ana mimba unafanya nini???" aliuliza tena kwa sauti tulivu John, Michael akakubali kwa kutikisa kichwa.
John alimpatia nauli Michael kisha akamwacha pale na kuelekea nyumbani kwa Matha, tayari ilikuwa saa tatu usiku.
“Kumbuka kuwa hiyo mimba si ya kwako….” Alisisitiza John. Michael akabaki kumtazama.
John akatoweka!!! Safari ya kwenda kwav mpenzi wake. MATHA!!
Michael akabaki kimya huku akiona kifo chake kikimtongoza!!!


*****

Matha aliufungua mlango taratibu, John akaingia ndani bila kuvua viatu, Matha alivyoufunga mlango John akamkumbatia ishara ya kumjulia hali.
"Vipi unaumwa??" aliuliza Matha. John hakujibu, akamtazama Matha usoni.
"He!! vipi wewe??"
"Hata siumwi ila kuna tatizo nadhani"
"Usinambie kuwa umechezwa machale kuwa tukienda kuiba tutakamatwa? maana na wewe kwa hayo machale" alidakia Matha huku akimfungua John vishikizo vya shati lake.
"Matha hakuna kitu chako chochote kimepotea humu ndani??"
"Mbona wauliza hivyo kuna nini??"
"Kuna kitu umepoteza??" alirudia swali lake.
"Hapana sidhani!!!"
"Mimi nadhani na kuna mjinga mmoja anataka kutuchezea!!"
"Nani huyo??? na ni kitu gani??" Matha aliuliza kwa umakini mkubwa, sura ya kikatili ilikuwa imemuingia tayari.
"Anajiita sijui Minja sijui nani ni wa pale sheli Mitimirefu" Alijieleza awezavyo John, Matha moyo ukamshtuka kwa hofu kuu baada ya kusikia hilo jina Minja, kwa kuwa alizijua mbinu za John, hakutaka kukutanisha macho naye hivyo akainama chini. Alimfahamu fika Minja Meri, ni huyuhuyu aliyekuwa anaijua siri ya ujauzito wake, lakini haikuwa siri kiasi cha hatari iliyopo, aliamini kuwa Minja alichukulia kama kamchezo flani tu kati ya mtu na mpenzi wake. Hofu ikazidi kumtanda Matha alipomfikiria John, aliijua fika ghadhabu yake ikipanda juu ya mtu hatua ya chini kabisa ni kutesa hadi kuua kama si kuua mara moja.
"Vipi unamfahamu huyo jamaa"
"Jina sio geni sana!!" alijibu Matha akiwa bado na ameinama
"Utakuwa unamfahamu, ni bwege mmoja hivi, kesho nitakupitia ukamuone, anadhani mimi bwege, yaani asiposema kitu kesho namuua!!!" aliapiza John huku akiuma meno yake, Matha akatambua John yupo katika hasira kali juu ya Minja.
Taratibu akamsogelea na kuanza kumpepea kwa kutumia shati alilokuwa amemvua, jasho lilikuwa linamtoka. Matha alifanikiwa kuishusha jazba ya John, tatizo likabaki kwake ni nani wa kuishusha presha iliyokuwa inazidi kumpanda, hofu iliyokuwa ikimtawala. Ni nani wa kumsaidia kuibeba hatia hii, kama Minja atakutana na John katika faragha lazima atausema ukweli, na hata akisema bado atauwawa je itakuwaje kwa yeye Matha atakayesalia duniani kumkabili John, na vipi juu ya kijana Michael. Hayo yote yalimuumiza na kumkera Matha.
"Hata nikiitoa kwa sasa haina maana tena!!!" aliwaza Matha. John aliaga akaondoka na kuahidi kufika siku inayofuata muda wowote kwa ajili ya kwenda kwa Minja. Kuondoka kwa John kidogo kulimpa nafuu Matha, akaondoa nguo zake zote ili kukabiliana na joto, Matha alitamani sana iwe ndoto lakini hii ilikuwa hali halisi.
John atatuua!!!!
Wazo la kuuliwa na John, Matha hakutaka kulilazia damu kwani alimjua nje ndani. Baada ya kufikiria sana alipata wazo, wazo la kuonana na Michael ili waweke mipango sawa.

Wazo hilo likapitishwa na asubuhi ya siku iliyofuata Matha akafanya ugeni wa ghafla nyumbani kwa John. John hakuutegemea.
"Mambo vipi Michael....darasani tafadhali" aliamuru Matha, John na Bruno wakavutiwa na amri ile wakamchukulia Matha kuwa ni mwanamke wa shoka. Michael alighairi kuendelea kunywa chai akamfuata Matha katika chumba cha mafunzo.
"Nakupenda sana Mic" Matha aliyeonekana mwanamke wa shoka mwenye amri sasa alikuwa amelegeza macho na kumwangukia Michael begani.
"Matha hali sio nzuri huyu jamaa amegundua kitu"
"Kitu gani???" aliuliza Matha huku akisimama imara na kumkazia macho Michael. Michael alimueleza swali zito alilopewa na John ili alifanyie tafakari.
"Kwa hiyo nani atakuwa amemwambia??" aliuliza Matha japo hakutegemea jibu lolote kutoka kwa Michael
"Au Minja amemwambia kilichopo katika kile kikaratasi"
"Minja ndo nani???" aliuliza Michael, ikawa zamu ya Matha kuelezea juu ya huyo Minja na wasiwasi wake juu yake.
"Atakuwa ni huyo hakuna mwingine!!!" alisema Michael huku akikaa kitako.
"Tukamtafute baadae" alitoa wazo Matha likakubaliwa na Michael. Hakuna mazoezi yoyote waliyofanya wawili hawa, Matha alikuwa anakwanguliwa na makali ya Hatia wakati Michael alikuwa kama mfu tayari. Matha alijaribu kumtia moyo Michael lakini ilikuwa sawa na bure hata yeye alilitambua hilo.
"Sasa tukishamuona tunamwambia nini?"
"Mbele kwa mbele itafahamika" alijibu Matha kisha akaendelea, "Akileta upuuzi atanijua mimi ni nani" Michael akawa kimya hakujazia neno.
Baada ya masaa mawili walitoka katika chumba cha mazoezi, Matha aliaga akaondoka Michael akaingia chumbani kwake. Hakuna ambaye aliwagundua kuwa walikuwa katika matatizo makubwa.

****


Minja Meri akiwa bado hajausahau ujio wa John Mapulu siku iliyopita. Siku iliyofuata akiwa kazini amehudumia magari mengi, lilikuja gari dogo aina ya Toyota Vitara, vioo vyake vilikuwa vimewekewa utando mweusi 'tinted' hivyo ilikuwa ni vigumu kuwaona walioko ndani.
"Ya shilingi ngapi bosi wangu???" Minja alimuuliza dereva ambaye alikuwa ameshusha kioo.
"Elfu ishirini....chukua pesa dirisha lile pale" alielekeza dereva, Minja kwa nidhamu akaelekea alipoelekezwa.
"Mambo vipi Minja??....sikia pesa hii hapa...unatoka kazini saa ngapi??" Minja alikutana na sura yenye uchangamfu ya Matha. Kwa kuwa walionekana kuwa na haraka naye Minja alijibu upesi.
"Ndio natoka sasa hivi hapa namalizia tu hizi gari mbili tatu, kuna ishu halafu nataka..."
"Poa nakuja muda si mrefu" Matha alimkatisha.
Baada ya kujizungusha kwa dakika kadhaa Matha alimpitia Minja wakaondoka eneo lile wakati huu alikuwa alikuwa anaendesha mwenyewe hivyo kwenye gari walikuwa wawili tu.
"Jana akaja mume wako bwana lakini hatukuweza kuzungumza vizuri....mh!!" Minja akaanza simulizi zake, Matha akawa kimya akijitwalia pointi mbili tatu.
"Minja unaipenda sana kazi ya sheli?" Matha alituliza swali hilo kwa Minja, walikuwa maeneo ya Mkuyuni tayari mezani pakiwa na vinywaji baridi.
Nitafanyaje sasa dadangu!!!" Minja hakuwa amejibu swali, lakini Matha alielewa.
"Nahitaji kukusaidia" alizungumza akasita kisha akaendelea, "nataka ufanye kazi nyingine tofauti na hii"
"Nitafurahi sana dadangu" alidakia.
"Unalipwa au unapata shilingi ngapi kwa siku??"
"Inategemea kuna siku napata elfu kumi siku nyingine hadi kumi na tano"
"Na una familia??"
"Naishi peke yangu maisha magumu sana!" alivutia kwake Minja.
"Pole sana!!" alisema Matha huku akimkazia jicho Minja.
Hisia za Minja zikaangukia katika mapenzi akaanza kuhisi kuwa Matha alikuwa amempenda tayari. Walipomaliza maongezi Matha alimkabidhi Minja shilingi laki moja na kumsihi asirejee tena kufanya kazi eneo lile. Minja alikuwa dhaifu katika pesa alipozipokea na amri aliifuata kama alivyotakiwa. Hakujua kuwa alikuwa kipofu anayepelekwa njia yenye miiba mikali, Minja akajihesabia kuwa ametoka kimaisha kwa kupendwa na mtoto mrembo sana tena mke wa tajiri.
Siku iliyofuata hakwenda kazini!!!
Na hata John alivyomchukua Matha jioni kwa ajili ya kwenda kumtambua na kumuadabisha Minja hawakumkuta. Matha akatabasamu ndani ya nafsi, kwake yeye ulikuwa ushindi wa chee!!! John akazikuza hasira zake juu ya Minja.
"Boya amekimbia ngoja!!!"
"Achana naye mjinga tu!!!" alidakia Matha
"Simuachi kirahisi hivyo......." alijibu John kisha akapiga kite cha hasira na kuondoa gari. Matha akazishusha pumzi zake na kumbusu John katika papi za midomo yake. Akawa amempumbaza!!!. ikabaki kazi ya kumtafutia kazi Minja Meri ambaye amebeba siri nzito bila kujijua kuwa ushahidi wake unahitajika ili dunia ipokee damu itakayomwagika.



*****


Usiku mzima Minja alikuwa akitafakari juu ya ukarimu aliotendewa na Matha, fikra zake bado zilikuwa bado katika mapenzi.
"Hivi nini kimemvutia kwangu mtoto mzuri kama yule jamani halafu kesho ananiletea jibu kama nimepata kazi ama la!!" Minja alijiuliza kwa sauti ya chini kama vile pembeni yake kuna mtu atampa jibu.
"Nikishakuwanaye najua hata haka kajumba nitahama...mbona akina Mussa watakoma" aliwakumbuka rafiki zake waliokuwa wanaishi maisha ya kufanana.
"Lakini kuhudumiwa na mwanamke mh!!!" aliendelea kuwaza. Usingizi ukampitia hatimaye. Asubuhi nayo ikachukua nafasi tena, Minja alikuwa amedamka mapema sana, tabasamu lilimtawala muda wote. Mara kwa mara alimfikiria Juma, huyu alikuwa ni jirani yake aliyekuwa anaishi nyumba ya vyumba viwili tena umeme na maji vilikuwepo, pia alimkumbuka mkewe Juma alivyokuwa mrembo aliyemtamanisha kila siku alipomtia machoni, dharau za mwanadada huyu aliyeitwa Husna zilikuwa zinamkera sana Minja lakini hakuwa na la kufanya. Minja aliamini kuwa karibu na Matha ndio kutawafunga mdomo wavimba macho wote mtaani, hisia za mapenzi zikamezwa na hisia za majivuno Minja akawa na ndoto ya kupata jina upesi upesi mtaani. Subira ikashindwa kutulia katika moyo wake, mguu na njia Minja akitembea mwondoko tofauti kabisa akaamua kwenda kumtangazia rafiki yake jambo hilo. Kwa kawaida huwa anatembea kwa miguu na kupita mikato ya hapa na pale hadi kufika nyumbani kwa Rashid, lakini siku hiyo aliamua kupanda gari la kukodi aina ya 'taksi'. Alifanya hivyo ili akajitwalie sifa mbele ya familia hiyo ya kimaskini maeneo ya Mbugani.
"Elfu tatu!!!"
"Twende!!!" alijibu kwa sauti iliyojaa ujivuni, Minja. Dereva akawasha injini gari likaondoka kwa mwendo wa kawaida hadi nyumbani kwa bwana Rashid, kabla ya kushuka kwa mbali kabisa aliwaona watoto wawili wa mzee Rashid wakikimbizana aliyetangulia alikuwa na hindi la kuchemshwa huku wa nyuma akiwa uchi na kilio kikimtawala. Rashid alikuwa akiwaangalia hakuwa na la kufanya bila shaka alikwishazoea maisha hayo.
"Hebu twende pale mara moja!!!, nitakuongezea malipo" Minja alimwamrisha dereva naye akatii bila kutia neno. Alisimamisha gari mahali ambapo palikuwa na duka kubwa kwa kiasi chake, Minja akatelemka na kuingia pale alitoa noti ya shilingi elfu kumi akanunua mikate na soda za kopo kisha akarejea garini.
"Simama mlangoni kabisa!!!" alielekeza Minja.
Kadri gari lilivyokuwa linasogea ndivyo watoto na mzee Rashid akishirikiana na mkewe walilikaribisha kwa macho yenye mshangao sana, haikuwa kawaida kabisa kupokea ugeni wa namna hiyo kwenye kibanda hicho cha mlinzi asiyekuwa na vyeti aliyeajiriwa kulinda duka la mtu binafsi.
Minja alishuka kwa madaha yote, akamwita yule dereva nje na kumlipa pesa yake umati wote umtazame, kisha akashusha mifuko ya mikate na vinywaji alivyokuja navyo. Heshima yake kwa siku hiyo ikawa juu sana, alifanikiwa kuwateka maskini wenzake.
Mtoto wa mwisho wa Rashid akamlilia Minja waondoke naye. Minja akambeba juu juu akampatia noti ya shilingi elfu tano. Kilio kikaishia pale.
Minja na Rashid wakatoka!!!! Rashid hakuisha kujichekesha kila mara mbele ya bosi wake wa siku hiyo. Kwa mwendo uleule wa kuchukua teksi Minja na Rashid walipotea mbele ya eneo hilo la kimaskini na kutua maeneo ya Nyegezi wakatafuta mgahawa mzuri wakakaa na kuanza kunywa taratibu. Kisha maongezi yakaingilia kati, Minja akamueleza kila kitu Rashid juu ya zali/bahati iliyomwangukia kupendwa na mke wa tajiri.
Maelezo ya Minja si tu kwamba yalimpa wivu uliokithiri Rashid lakini pia yalimuweka katika kizungumkuti, hakuelewa kama alikuwa sahihi ama la!!
"Umesema John Mapulu ndio mume wa huyo binti!!!!"
"Ndio lakini huwezi kumjua" alijibu Minja huku akipiga funda kubwa la bia.
"John Mapulu!!!" Rashid alifanya tafakari ya miaka miwili nyuma katika kazi yake ya ulinzi aliamini kuwa huyu mtu anayezungumziwa na swahiba wake aliwahi kuwa bosi wake tena si mara moja kwani aliwahi kupumzishwa na kurejeshwa tena, na baadaye bosi wake alitoweka katika mazingira ya ajabu hivyo akapewa chake na kuachishwa kazi. Hawezi kuwa amesahau zama hizo kwani alikuwa analipwa vizuri sana na familia yake ilikuwa inaneemeka na kazi ya baba yao, lakini baada ya kuachishwa kazi mambo yakawa magumu.
"Namfahamu lakini mbona...."
"Wewe humjui nakwambia cha msingi nipe ushauri!!!" aliingilia kati Minja. Rashid akakaa kimya kwa sekunde kadhaa akiikodolea macho sahani iliyokuwa imesheheni nyama ambazo ni kama zilikuwa zimekosa mlaji.
"Minja hapa kuna namna!!!"
"Namna gani, unadhani nimetumia juju" aliuliza Minja.
"Hapana sivyo!!! ila huyo John huyo John Mapulu namfahamu hana uwezo wa kuzaa iweje useme mkewe ana ujauzito?" aliuliza kwa sauti ya chini Rashid, macho yakamtoka Minja akabakia na pande la nyama mdomoni bila kutafuna, kauli ile ilikuwa imefungua akili yake kwa kiasi kikubwa.
Akatulia hivyo kwa sekunde kadhaa bila kusema lolote. Kisha akatikisa kichwa kumaanisha kuwa ametambua jambo. Akili yake ilifanya kazi harakaharaka tamaa ya pesa ya kichaga ikamwingia, ikamtuma kumchenga Rashid ili aweze kula peke yake.
"Ah!! wanawake wa mjini hao, hebu achana naye" alisema Minja. Rashid akaafiki, baada ya nusu saa wakaagana. Safari hii kila mmoja aliondoka kivyake.


****

***MINJA anahisi MATHA amempenda kimapenzi kwa wema aliotendewa......hajui kama anaingia HATIANI bila kujua......eeh! Mungu muepushe na janga hili.
***RASHID anajua kitu kuhusu John Mapulu!!! Na amemueleza MINJA je? Minja atatumia siri hjii kama chambo???
***HATIA ya mimba ya Joyce inamtesa na kumsulubisha JOHN MAPULU!!!!

HATIA INAZIDI KUSAMBAA....
TAFADHALI...

No comments:

Post a Comment

Recent Posts