Na GEORGE IRON
“Zawadi kwa lipi kaka nililofanya”“Jana umetumia muda wako mwingi sana kuzungumza na Matha nimeyaona mabadiliko leo mabadiliko makubwa nilikuwa na Matha asubuhi ya leo hapa!!” John alizungumza huku tabasamu likichanua katika mdomo wake.
“Aaah!! Amakweli leo nimelala sana”
“Kwa suala hilo nahitaji kukupongeza!!!”
“Usijali wewe ni kaka yangu” Michael alisema huku hasira zikiwa zimemtawala ndani ya nafsi yake pepo wa wivu akaanza kumtafuna taratibu, akaanza kuhisi Matha ni mali yake peke yake.
“Hata kama lakini unastahili zawadi” alisisitiza John. Michael hakupinga zaidi ya kukubali kwa shingo upande hiyo zawadi.
“Matha amekuja??? Muda gani na saa ngapi ameondoka?? Au mtego huu?? Eeh!! Mungu nisaidie” baada ya muda mrefu sana kupita Michael alikumbuka kupiga dua.
Au wananichora hawa kasha wanitoe kafara! Alijiuliza.
****
Hali ya utulivu ilitawala eneo hili la Nyegezi jirani kabisa na chuo kikuu cha mtakatifu Augustino maarufu kama SAUT. Pumzi na mapigo ya moyo ya wawili hawa yalisikika, mmoja akiwa anajiamini na mwingine akiwa ametekwa na uoga. Ilikuwa saa sita na nusu usiku, sauti za ndege wasiojua ubora wa nyimbo zao zilisikika kwa mbali na mara chache kuingiliwa na sauti mbaya za popo. Maumbo yao yalikuwa yanaendana walikuwa wamesimama kama vile kuna jambo flani walikuwa wanazungumza kwa siri kutokana na ukaribu wao.
Majira ya saa saba usiku mmoja alisogea na kujificha mahali na kumwacha mwenzake akivuta sigara na kupuliza moshi hewani. Michael alikuwa ameachwa na John eneo lile, uoga ulipitiliza kipimo hadi akaizoea hali ile kwa kuamini kuwa kama John angekuwa ameamua kumuua angeweza kufanya hivyo mapema na si lazima kutumia mbinu zote hizo. Lakini licha ya kujiaminisha sana, suala la kupewa zawadi eneo kama hili halikuwa la kawaida. Zawadi yangu ni kifo!!! Alijiuliza. Alitamani kumpigia simu Matha lakini akakumbuka alikuwa amepewa onyo kali juu ya kuwasha simu.
“Shika huu waya, nitakuamuru uuvute!!!!” John alimuelekeza Michael kwa sauti ya chini. Michael akatii. John akawasha sigara na kuanza kuvuta. Mara ghafla akamuamuru Michael kuuvuta ule waya hadi kwenye ki-mti kidogo kilichokuwa jirani kabisa na njia hiyo ya uchochoroni baada ya kuufunga waya huo Michael alisikia muziki kwa mbali ukizidi kusogea karibu. Kufumba na kufumbua Michael aliuzuia mdomo wake usiweze kupiga kelele. Pikipiki ilikuwa imeachana na dereva aliyekuwa anaiongoza kama hiyo haitoshi kichwa kilikuwa kinakaribia kuachana na kiwiliwili. John alikuwa ameua kwa kumtegea waya dereva wa pikipiki.
“Panda twende…” John alimwambia Michael ambaye bado alikuwa amezubaa asijue la kufanya. Kwa sauti kali ya John akawa amerejewa na ufahamu akapanda katika pikipiki.
“Bila shaka itakufaa kwa safari za hapa na pale, kifo hiki kinanikumbusha enzi hizo naanza maisha ya ujambazi!!” John alizungumza kwa sauti ya juu ili Michael aweze kumsikia, hakuwa na wasiwasi hata kidogo. Michael hakujibu kitu.
Mnamo saa nane na nusu kila mmoja alikuwa amejichukulia nafasi katika sebule kubwa kabisa. Michael hakuwa na amani lakini John alikuwa mzoefu sana.
“Zawadi yangu!!!!!! Oooops!!! Nilikuwa nimesahau” John alikumbuka zawadi aliyoahidiwa na Matha kupitia Michael.
“Mh!! Hiyo mpaka pakuche tena” alijibu Michael.
“Hapana twende hiyo pikipiki ina mafuta ya kutosha” alitoa hoja John, Michael kwa kumuhofia John akakubali.
Mwendo wa dakika kumi tayari walikuwa Buzuluga. Kama kawaida John akamwacha Michael aende mwenyewe. Siku hii hakukaa sana alirejea na bahasha na kumpatia John kisha wakaondoka kurudi nyumbani. Ilikuwa ni nguo ya ndani ya kiume!!
Asubuhi sana aliwasili mtu asiyefahamika machoni pa Michael alikuwa maalum kwa ajili ya kubadilisha namba za pikipiki ile. Zoezi lilifanyika kwa umakini na kufikia jioni John kwa uhuru wote alitoka na pikipiki ile nje akiyapita kama hayaoni magazeti yanayozungumzia kifo cha muendesha bodaboda mitaa ya Nyegezi.
John alifika nyumbani kwa Matha majira ya saa tatu usiku baada ya mizunguko mingi ya kujaribu ubora wa pikipiki ile.
Matha alitegemea ujio huo hivyo chumba kilikuwa kinanukia sana kutokana na maandalizi ya uhakika. John alipokelewa kwa upendo wa hali ya juu sana, mabusu kadhaa ya hapa na pale yalikonga sana nyoyo zao lakini hasahasa John aliyekuwa hana la kusema mbele ya Matha.
“Nakupenda Jo!!”
“Sina la kusema nadhani unajua kuwa nakupenda”
“Asante sana” alisema Matha kinafiki, huku akijua fika ana hatia ya kumsaliti John tena kwa mtu wake wa karibu Michael. Matha alimkaribisha mezani John ili wapate kwa pamoja chakula alichokuwa amekiandaa. Walijumuika kwa pamoja na baada ya hapo wakahamishia mashambulizi kitandani. John alikuwa anampenda sana Matha!!.
Vurugu hizo zilitwaliwa na usingizi baadaye hadi John alipokuja kushtuka alfajiri. Alikuwa na miadi mida ya saa nne hivyo alivaa nguo zake bila hata kuoga kwani hapakuwa na choo wala bafu la ndani kwa ndani katika chumba cha Matha.
“Mh!! Kuoga usioge yaani na Suruali unavaa hiyo hiyo??”
“He! Sasa nitavaa ipi nyingine?? Unaota nini!!”
“Subiri” Matha alisema huku akiinuka kizembezembe, umbo lake zuri lilijihifadhi katika nguo hii ya kulalia John alipatwa na matamanio wakati Matha amegeukia upande wa kabati, John hakujua ni nini anatafuta mawazo yake yote yalikuwa katika maungo ya Matha.
“Mh!! Na wewe kunichungulia tu loh!! Mwanaume huna haya wewe, usiku mzima hujaridhika tu!!” alitania Matha na kumkurupua John aliyezuga kwa kucheka. Matha alimshangaza John kwa kumpatia suruali ambayo ilimkaa na kumpendeza vyema.
“Asante mke wangu!!!” alishukuru John na kisha akahamishia vitu kadhaa kutoka katika suruali aliyoivua na kuvitia katika hii aliyokua ameivaa.
“Umenipatia hadi kiuno” alisifu John huku akijitazama. Matha akajibu kwa tabasamu. Baada ya kujitathmini akambusu Matha katika papi za midomo yake na kuondoka. Pikipiki bado ilikuwa na mafuta ya kutosha. John alipofika nyumbani aliingia moja kwa moja bafuni akaoga kisha akavaa suruali aliyopewa na Matha na juu akaweka shati jingine halafu akachomekea, uchaguzi wa kiatu ukamshinda akaamua kuvaa viatu vya wazi. Tayari ilikuwa saa mbili na nusu asubuhi. Michael alikuwa hajaamka bado, Bruno ndiye aliamka kumfungulia geti John kisha akalala tena hivyo hata wakati (John) alipokuwa anatoka hakuweza kumsikia tena. Wakati huu alitoka na gari ndogo Toyota Corolla. John alikuwa anawahi miadi ya kwenda kuzungumza na wenzake juu ya ‘dili’ la kuvamia mahali.
****
Kituo cha mafuta kilichopo maeneo ya Miti mirefu karibu na shule ya sekondari ya Pamba ndipo John alijijengea mazoea ya kwenda kujaza mafuta hivyo alikuwa anafahamiana na wafanyakazi wengi wa pale. Siku hii pia alikwenda na gari yake hadi katika kituo hicho. Alichangamkiwa na muhudumu ambaye pia alikuwa anamfahamu japo hawakuwa karibu sana.
“Weka ya elfu thelathini” aliamuru John huku akimkabidhi pesa kijana huyo aliyeonekana kutamani sana mazoea na John lakini ikawa inashindikana, John alikuwa bize sana na simu yake. Baada ya kuhudumiwa John alimpatia kijana huyo shilingi elfu tano kama malipo ya uchangamfu wake (bakhishishi) tangu John anafika hapo.
“Akhsante sana bosi”
“Kwa heri” aliaga John.
John alikuwa wa mwisho kuingia katika mkutano huo wa siri, ulikuwa ni mkutano wa watu sita wakiwa na lengo la kuvamia na kupora katika Supermarket ya Imalaseko jijini Mwanza, mpango ulikuwa umewekwa tayari kabisa kilichokuwa kimebakia ni kutekeleza. Kikao kiliendeshwa kwa sauti za chini sana katika hotel ya Mwanza (New Mwanza Hotel). Wakati kikao kinaendelea simu ya John iliyokuwa katika mlio wa kimya (silent mode) iliita, ilikuwa namba mpya John akapuuzia. Ikaita tena kwa mara ya pili na ya tatu hadi ya nne.
“Naingia uwani dakika sifuri” aliomba ruhusa John.
“Uwahi kurudi” mwenyekiti wa kikao alijibu.
Alipofika chooni simu iliita tena.
“We nani??” aliuliza kwa jazba John
“Samahani bosi….”
“Nimeuliza wewe nani??” aliendelea kusihi
“Bosi ni mimi Minja, wa hapa sheli”
“Tatizo!!”
“Bosi kuna kikadi cha hospitali hapa nadhani kilikuwa katika pesa zako ulizolipia hapa”
“Kikadi gani, sidhani kama ni mimi” alipinga John
“Aaah!! Bosi ni cha kwako, angalia bwana kikipotea hiki itakulazimu kupima upya..??” upande wa pili ulilazimisha uchangamfu ambao haukupokelewa na John. Sauti ilikuwa imemkumbusha John kuwa anayezungumza ni kijana aliyemjazia mafuta kwenye gari asubuhi hiyo
“Mbona sikuelewi”
“Matha Mwakipesile ndio mkeo!!!”
“Ndio kwani nini mbona husomeki jombaa” John alizungumza kwa jazba hakupenda jinsi alivyozungushwa zungushwa.
“Basi kuna kikadi chake hapa cha hospitali….”
“Haya nitakupigia baadaye nipo kwenye kikao” alisema John na kukata simu, alihofia kuwaudhi wenzake waliokuwa wanamsubiri.
Laiti kama angeendeleza mazungumzo japo kidogo tu yangekuwa mengine.
****
Mapigo ya moyo ya Matha yalikuwa yakienda kasi tofauti na siku zote maishani mwake. Kabati la nguo halikuwa na kitu chochote ndani yake, kila kitu kilikuwa shaghalabaghala. Matha alikuwa anatokwa na jasho jingi. Kwa mara ya kwanza tangu aingie katika suala zima la ujambazi alijihisi kutingishika na kushikwa na uoga wa hali ya juu. Kadi iliyokuwa na majibu kwamba yeye ni mjamzito ilikuwa haionekani, kila kona alipojaribu kugusa hapakuwa na chochote, tegemeo la mwisho na aliloliamini zaidi ilikuwa ni katika suruali aliyomzawadia John asubuhi hiyo. Matha alitamani kurudisha muda nyuma lakini muda ulizidi kwenda mbele. Amani ikatoweka, giza likatanda, kizunguzungu kikamtwaa akakaa kitandani, alilazimisha kilio ili kuondoa donge la wasiwasi na karaha kooni, kilio hakikutoka akawa kama anakoroma, akaligundua hilo akanyamaza kimya. Akatamani aizime simu yake bado hakuona tija. Hatia ikaanza kumtafuna, hatia ikaanza kuipasha joto damu ya mlimbwende huyu.
Matha alichukua simu yake na kutaka kumpigia Michael lakini kabla ya kupiga alisita. Hofu ikamkumba Matha, Michael angeweza kukimbia. Nguvu za Hatia ziliendelea kumtafuna kwa kasi Matha aliamua kumpigia simu John japo hakuwa amejiandaa nini cha kumuuliza. Mikono yake ilikuwa inatetemeka wakati simu inaanza kuita, simu iliita bila kupokelewa.
"Tayari amekiona!!" alitahayari Matha, wakati akizipiga tena namba za John. Wakati huu iliita mara mbili kabla ya kukatwa. Wasiwasi ukatanda. Nimelikoroga!! kwa mara ya kwanza Matha alijikuta anamuogopa John. Huku akijitazama kwenye kioo, mikono yake ikiwa imekishika kiuno chake chembamba.
*****
Akiwa amewakera wenzake katika kikao hicho cha watu wachache japo chenye mpango wa kuumiza wengi John Mapulu hakuumizwa sana na hilo ila ile hali ya kupigiwa simu na Matha kisha hakuzipokea ndio ilimtia mawazo. Kengere za tahadhari zilipiga masikioni mwake, huenda Matha yupo matatani, ama ana shida ya msingi sana. Akafikiria kuomba ruhusa tena lakini nyuso zilizojaa chuki zilikuwa zikimtazama yeye, akahairisha! lakini kwa kujificha akatuma ujumbe.
'Nipo kwenye kikao honey! kuna nini?' baada ya kutuma ujumbe ule akahifadhi simu yake, punde wakati akijiweka sawa kuendelea na kikao akaisikia simu yake inatoa mlio, akaichomoa tena.
"Message sending failed" alijilaumu John kwani alikuwa hana salio kwenye simu yake hivyo ujumbe haukufika, kwa ujasiri akaomba ruhusa.
"Dakika moja ni 'waifu' sijui kuna nini" alijieleza John. Hakuna aliyemjibu. Alijua wamekasirika lakini hakujali, alimpenda sana Matha. Alipofika chooni akambip Matha. Punde akapigiwa.
"Yes sweet heart nambie"
"Kwani vipi?...kwema huko, nimekukumbuka wewe" alijiumauma Matha.
"Huku poa tu sijui hapo nyumbani"
"Poa tu upo kwenye kikao eeh!...nimekusumbua" alijishaua huku sauti yake ikitawaliwa na mawimbi mawimbi ya hofu
"Hujanisumbua hata kidogo" alijibu John
"Haya endelea na kikao mume wangu" Matha alitoa neno hilo ambalo lilimlegeza John akauhisi upendo wa Matha ulioanza kupotea ukirejea kwa kasi.
"Asante 'waifu' ehe! unatoka saa ngapi leo ulisema?"
“N’taenda baadaye mjini mpenzi wangu kuna mahitaji nitafuata supermarket"
Suala la Matha kuelekea mjini likaifungua akili ya John akakumbuka kitu, ilikuwa ni simu aliyopigiwa kutoka sheli. Upuuzi wa kimaamuzi alioufanya haustahili kusamehewa. John Mapulu akamgusia suala hilo Matha 'mkewe'
"Tena afadhali pitia hapo sheli hapo kuna jamaa mmoja mchaga hivi anafanya hapo kazi amesema sijui kuna kidude gani nimempa kimakosa hebu kaanga.. . . . ." kabla hajamalizia kuongea simu ilikatwa na kuzimwa, mwenyekiti wa kikao alikuwa amemfuata John huko huko chooni, kwa hasira akaitwaa simu na kuizimisha, John akasonya kwa ghadhabu lakini hakufanya lolote zaidi ya kurejea kwenye kikao.
Matha alikuwa anatetemeka tangu anaongea na John neno la kwanza kwenye simu, alikuwa anajaribu kuzichanga karata zake aweze kufahamu kama John alikuwa anafahamu juu ya uwepo wa kikaratasi kinachoonyesha majibu yake siku alipoenda kupima ujauzito. Hofu ilikuwa imetanda lakini aliamua kujaribu. John hajui lolote! ndio mshangao alioupata Matha baada ya kuisikia sauti ya John ikiwa tulivu na iliyojaa mahaba.
"Sheli...kidude. . . Mchaga hivi vitu vinahusiana kweli na hicho kikaratasi" alijiuliza Matha baada ya mawasiliano kukatika. Alikodolea macho simu yake huwenda John atampigia, hakupigiwa, akaamua kupiga tena, simu ikawa haipatikani. Sentensi isiyonyooka na isiyomaliziwa kutoka kwa John ilimuacha Matha katika jitimai la nafsi. Hakuelewa John alimaanisha nini.
Matha hakuelewa kama John alimaanisha hicho kikadi alichokuwa akikiwaza yeye ama la! . Akili ya Matha ilikumbwa na zizimo, muda ulikuwa unasogea bila maamuzi sahihi kupita katika halmashauri ya ubongo wake.
Aliingia bafuni akaoga akavaa nguo zake alizokuwa amevaa siku iliyopita. Kama vile mtu anavyoitwa na wachawi usiku wa manane kutokea usingizini ndivyo Matha alivyotoka chumbani kwake na kuanza kutelemsha ngazi hadi akafika chini.
Sheli!! lilimjia hilo wazo ghafla baada ya kugundua hakuwa na mahali rasmi pa kwenda.
"Sheli gani sasa??" lilikuwa swali lililofuata. Hakika lilikuwa swali gumu sana kwa maana sheli zilikuwa nyingi mno. Matha aliweka kituo kisichokuwa rasmi katika banda linalouza magazeti, akawa kama anasoma vichwa vya magazeti mbalimbali kwa umakini mkubwa sana lakini hakuna alichokielewa, mawazo yake hayakuwa hapo.
"Naomba KIU" Matha alitoa pesa na kumlipa muuzaji akapewa gazeti alilohitaji. Macho yake yakakutana na sheli upande wake wa kushoto alipogeuka. Bila kujiuliza mara mbilimbili akawa ameamua kuifuata baada ya kuhakikisha upande wa kushoto na kulia mwa barabara usalama ulikuwepo. Pale sheli palikuwa na mgahawa, Matha akapenyeza hadi karibu na huo mgahawa, walipita watu kadhaa akaishia kubadilishana nao salamu, mara aanze yeye ama wao, hakuongeza neno.
Niulize mchaga au? huu ni upuuzi!! Matha akajifanyia mahojiano mafupi na kugundua alikuwa anajidanganya. Alipiga hatua kadhaa kuuacha mgahawa kwa ghadhabu lakini mara upepo ukavumia usawa wa pua yake, harufu nzuri ya chai ya maziwa, donati, sambusa, chapati na mayai ya kukaangwa mchanganyiko na eggchop vyote vikaungana na kupenya katika pua yake. Minyoo ikashtuka usingizini, tumbo likaunguruma Njaa!! Matha akabadili uelekeo akaurejea mlango wa mgahawa, akachukua nafasi yake.
"Maziwa ya moto, donati na egg chop" aliagiza kwa utulivu Matha huku macho yake yakizipitia kurasa za gazeti alilonunua, simulizi ya Beka Mfaume ya WIVU ambayo siku zote ilikuwa inateka akili yake leo hii alikuwa anaiona kama makala mbovu ya siasa za ughaibuni tena iliyoandikwa katika lugha ya kigeni.
Chai ilipoletwa ukawa mwisho wa kusoma gazeti. Tumbo lake ambalo halikuwa na chochote tangu kupambazuke lilikuwa linafurahia maziwa ya moto yaliyopenya katika kinywa kisichopatwa na ladha yoyote. Mfululizo wa matukio yasiyokuwa katika mtiririko maalum uliisumbua akili yake hatimaye akaiona sura ya Michael, akajutia kukutana naye lakini akajilaumu kwani yeye ndiye alimwendesha hadi akafikia kuwa mpenzi wake wa siri. Hakujua alitumia muda gani kufikiri lakini alipokumbuka tena kupeleka kikombe cha maziwa mdomoni yalikuwa yamepoa hakuendelea kunywa.
Akalipa akaondoka!!
Kelele za mpiga debe zilimvuta akapanda daladala inayoelekea Nyegezi ikitokea Igoma. Matha alipanda kwa msukumo wa mpiga debe hakuwa amenuia rasmi kwenda huko Nyegezi.
Muziki mkubwa ndani ya gari hiyo ulimtia ghadhabu, alitamani kushuka lakini alikuwa siti ya nyuma akahofia kufanya usumbufu.
"Tuache hapo Natta!" abiria mmoja aliyekuwa jirani na Matha alimkumbusha kondakta ambaye naye aligonga bodi dereva akasimamisha. Aliposimama kuanza kushuka Matha naye akaamua kushuka, baada ya kulipa nauli alishangaa hapa na pale na kujiangalia amepungukiwa nini ndipo alipogundua ameacha gazeti ndani ya gari, bila uelekeo maalum Matha alianza kukaza Mwendo.
"Mh! au ile sheli ya Mitimirefu??" swali la ghafla likanasa katika ubongo wake likisubiri jawabu.
****MATHA amesahau kikadi kinachoonyesha majibu yake kuwa YU MJAMZITO.......katika Suruali aliyompatia JOHN MAPULU.......
***JOHN MAPULU bila kutambua anakitoa kikaratasi kile pamoja na pesa anazolipia sheli.....Anapigiwa simu kukumbushiwa juu ya alichosahau!!!
***MATHA naye anahaha kujitoa katika HATIA hii.....hatia ya usaliti......
***JE NANI ATAMUWAHI MWENZAKE????....na vipi ikifahamika...USALAMA WA MICHAEL UPO WAPI???
HATIA HATIA HATIA!!!!
No comments:
Post a Comment