Tuesday, November 6, 2012

SITAISAHAU facebook


MTUNZI: Emmy John P.

CONTC: 0654 960040


SEHEMU YA SITA

ILIPOISHIA

Sasa na mimi nikaanza kuhaha, kana kwamba niliyoyawaza ni sahihi. Upesi nikanunua muda wa maongezi nikampigia tena rafiki yake John. Nikamsihi anieleze nini kimetokea.

Bila kusita akaanza kunieleza. Mwishowe nikapata jibu kamili. John hakuwa ameathirika na UKIMWI bali mshtuko. Joyce aliyeanguka wakati wa kuaga mwili wa marehemu viwanja vya

Raila Odinga na yeye amefariki.

Cha ajabu na kushtua hakuna ugonjwa wowote uliohusika katika kifo hicho. Nilifadhaika nikakaa chini, sikukumbuka hata kuaga tayari nilikuwa nimekata simu.

Mbona hivi vifo vinakuja mfululizo kiasi hichi?? Nilijiuliza na hakuwepo timamu yeyote wa kunijibu.


***UTATA…….Vifo hivi vinasababishwa na nini???

*** Isabella anahusika vipi??



ENDELEA...


Jesca naye kama ilivyokuwa kwa aliyetangulia aliagwa na wanafunzi uwanja uleule wa Raila Odinga. Halikuwa jambo la kushangaza bali lilimezwa na huzuni. Haikuwa mara ya kwanza vifo kutokea katika maisha ya chuo, lakini hichi kifo cha Jesca kilikuwa cha ghafla mno. Iliuma sana!!!
****
Wiki mbili zilikatika tangu Jesca aache simanzi kubwa katika chuo cha Mtakatifu Agustino. Nilikuwa karibu sana na John nikimfariji kwa kumpoteza mpenzi wake. John kwa kiasi kikubwa sana alifurahia ukaribu wangu kwake. Kiasi kikubwa upweke ukawa unatoweka.
USIKU WA MANANE
Kila kona ya jijini Mwanza ilikuwa imetulia, upepo ulikuwa unavuma kiasi cha kuyumbisha miti midogomidogo iliyoota pembezoni mwa barabara. Magari machache yalikuwa yakiipa usumbufu barabara ya lami ambayo ilikuwa katika mapumziko baada ya suluba ya mchana.
Gari dogo aina ya Corolla ilipata hitirafu ambayo ilionekana kuwasumbua vichwa abiria waliokuwa ndani yake. Kila mmoja alionekana kumsukumia mwenzake mzigo wa kutafuta suluhu ya ya gari hilo. Wale abiria watatu wote walikuwa wanafunzi wa chuo cha mtakatifu Augustino.
Baada ya muda wa kujadiliana hatimaye mwanafunzi mmoja aliyetambulika kwa jina la Joseph alivua shati lake akaweka pembeni akaingia katika ufundi. Wenzake wawili walitulia wakimtazama.
Baada ya dakika kadhaa mwanafunzi mmoja alibanwa haja ndogo. Taratibu akajivuta kichakani. Sijui kwanini aliamua kukitafuta kichaka cha mbali wakati usiku ulikuwa mnene na hapakuwa na watu wakipita hovyo. Alikifikia kichaka taratibu akaanza kuifungua zipu yake tayari kwa kukidhi haja yake ya wakati huo.
Ghafla aliiachia suruali yake na kutazama mbele katika namna ya kukodoa huku akiwa na hofu kuu. Alikuwa akitetemeka huku akifanya namna ya kushtua kama anatisha kitu kibaya kinachomkabili. Nilitamani sana kujua ni nini hicho mbele yake lakini nikaendelea kuwa mtazamaji wa filamu hiyo ya ajabu.
Kisha kama aliyesukumwa akaanguka chini. Akawa anajaribu kupambana kwa kujirusha huku na huko. Alikanyagakanyaga lakini hakufua dafu. Alirusha mikono hewani, bado alionekana kukabwa ipasavyo.
Ghafla nikajiona kuwa mtu wa ajabu sana, kwa nini nashuhudia jambo hili na sitoi msaada wowote. Nikataka kupiga kelele. Lakini koo lilikuwa limekauka.
Kwanza ni filamu!! Nilijiambia tena.
Mara yule kijana akatulia tuli. Nami hapo nikashtuka!!!!
Ndoto!! Ndoto mbaya.
Nilikuwa nimeung’ata kwa meno upande wa kitanda. Nilikuwa natokwa jasho na nilikuwa naunguruma kama mbwa mwenye ghadhabu anayejiandaa kubweka.
Nilihisi kama maumivu kwa mbali katika bega langu.
Taharuki!! Kamwe sijawahi kuota ndoto kama hii!! Mbaya sana.
Nilitazama saa ilikuwa saa tisa usiku. Giza nene nikiwa peke yangu kitandani.
Nilisimama nikafanya ishara ya msalaba. Nilikuwa natetemeka. Na nilivyokuwa muoga wa filamu za kutisha, basi nilikuwa sikamatiki kwa hofu.
Nilikuwa nimebanwa na mkojo lakini nilipaogopa sana chooni. Nikaamua kurejea kitandani. Mkojo ukazidi kunibana. Sasa nikajiona kuwa bwege, nina choo ndani halafu naogopa kukitumia.
Ni ujinga kujikojolea kitandani wakati kuna choo ndani ya nyumba!!!
Nikaiuweka uoga kando nikaenda bafuni. Nikachuchumaa niweze kukojoa, nikahisi maumivu kiunoni.
Mh!! Nimelala vibaya ama!! Nilijiuliza huku nikijilazimisha kuchuchumaa.
Nilipochuchumaa ndipo nikagundua kuwa nanukia marashi yasiyokuwa ndani ya chumba changu. Hilo pia nikalipuuzia.
Nikamaliza haja zangu nikarejea kitandani. Nikajidhihaki kwa hofu ya kijinga niliyoiruhusu initawale.
Usingizi ukanipitia. Sikuota tena!!!!
Asubuhi majira ya saa mbili nikashtuka usingizini. Ilikuwa siku ya jumamosi, nikaamka kuwahi saluni kutengeneza nywele.
Kabla ya kufika saluni nilipita hotelini nikapata kifungua kinywa.

****

Niliwakuta wateja wawili tu hapo saluni, hivyo mahesabu yangu yalikuwa sawa, sikuwa nimechelewa sana.
Nilisubiri kidogo zamu yangu ikafika. Baada ya mimi kuanza kuhudumiwa walimiminika wateja wa kutosha.
Kila mmoja na haja yake.
Saluni huwa ni eneo zuri sana kwa wale wabahili wa kununua magazeti ya udaku, kujipatia habari nyingi burebure tena kwa uhakika kwa sababu hata nafasi ya kuuliza maswali huwa inapatikana.
Penye wengi pana mengi. Na sasa tulikuwa wengi pale saluni. Mara kimya kikatawala alipoingia mwanamke mnene. Sikuwa namjua jina lakini haikuwa mara ya kwanza kumwona.
Baada ya kimya hicho ambacho uswahilini kinaitwa ‘jini kapita’ wote tulilipuka na vicheko.
Hata yule mama mnene na yeye alilipuka kwa kicheko kikubwa. Kisha tena akauvaa uso wake wa awali.
“Mnacheka wakati watu tuna msiba” Alikoroma, nusu akimaanisha na nusu ukionekana dhahiri kuwa ni utani.
Wengine wakacheka na wengine wakakaa kumsikiliza.
“Halafu mjue sitanii jamani.” Alikazia kisha akaendelea, “Basu ametutoka.”
“Basu? Basu ndio nani?.” Mwanamke moja aliuliza.
Nami nikapatwa na kihoro cha kuuliza. Nikajizuia lakini sikuweza.
“Basu huyu wa BBA (Bachelor of Business Administration).” Niliuliza.
Mama yule mnene kumbe na yeye alikuwa mwanafunzi. Akaiunga mkono kauli yangu.
Basu alikuwa amekufa!!!
Nini kimemuua jamani, si juzi tu alikuwa anacheza mpira kwenye haya mashindano ya FAWASCO? Niliuliza. Msomaji mashindano ya FAWASCO ni mashindano ya michezo mbalimbali huwa yanafanyika chuoni SAUT
Yule mama mnene akashusha pumzi kabla ya kujibu kwa sauti ya kunong’oneza.
“Ameng’atwa shingoni huko Nyegezi Kona. Amekutwa kwenye mawe huko.”
“Niniiii!!!!.” Kila mmoja wetu alishtuka kwa namna yake. Wahudumu walisimamisha walichokuwa wanafanya wote wakamgeukia mama mnene. Hakuna kauli aliyobadilisha alimaanisha alichokisema.
Mapigo yangu ya moyo yalikuwa yanaenda kasi. Ile mashine kichwani ikageuka mzigo. Nikahisi kizunguzungu.
Alichokizungumza yule mama kilifanana na hali fulani halisi, ilikuwa ni hali gani na kwa nini nilikuwa natetemeka? Nilijiuliza. Sikupata jawabu. Nikafumba macho nikakumbuka saa nane usiku!!!!
NDOTO!!! NDOTO YA KUTISHA!! Ndoto iliyonipelekea kushituka nikiwa na maumivu makali. Na si maumivu tu. Nilikuwa nimekiuma kitanda kwa nguvu sana. Na…na …..na nilikuwa nakoroma kwa hasira. Kama Mbwa!!! Nilikuwa kama mbwa!!!
Hiki nini!! Nilitaharuki kwa hofu. Sikusema kitu chochote, niliulazimisha utulivu!!! Lakini moyoni hapakuwa na amani.
Inamaana nimekiota kifo cha Basu? Nilijiuliza. Bado sikupata jibu.
Nilivuta kumbukumbu ya sura ya Basu, nikamfananisha na yule mhanga wa kwenye ndoto.
Hofu!!! Alikuwa mtu mmoja.
Nikapiga ukulele wa hofu.
“He Mungu wangu nimemuunguza dada wa watu.” Yule muhudumu alipiga kelele huku akizima mashine.
Hakugundua kuwa nilikuwa dunia nyingine kabisa tofauti na hiyo aliyokuwa anadhania.
Alinimwagia maji akaniosha nywele. Sikujali ubora wa kazi, nilikuwa nimehamakinika. Akili ilimuwaza Basu.
Kama amekufa kifo cha kufanana na kwenye ndoto maana yake nini?
Au nataka kuwa mtakatifu??? Nilijiuliza. Huku nikiamini moja wapo ya dalili za kuwa mtakatifu ni kuyajua yanayokuja kupitia ndoto.
Mh!! Utakatifu gani huu lakini hata kanisani penyewe siendi?? Nilitengua mawazo yangu.

“Dada nakuita jamani!!.” Sauti ya yule muhudumu ilinishtua. Inavyoonekana alikuwa ameniita mara nyingi sana.
Nilikuwa sipo kawaida na niliombea sana wasiitambue hali hii.
Simu yangu ikaita nikaitoa kuitazama alikuwa ni Dokta Davis.
Nikapokea na kuiweka sikioni.

“Samahani nipo saluni.” Nilimsihi.

“Usijali nilikuwa nakutaarifu ukatazame salio katika akaunti yako.”

“Hamna shida.” Nilimjibu na kukata simu.

***ISABELLA katika mtihani mwingine…..Ndoto ya ajabu inayogeuka kuwa kweli.
Je kuna nini hapa??

ITAENDELEA

No comments:

Post a Comment

Recent Posts