Saturday, October 27, 2012

HATIA---08



“Matha Mwakipesile ndo wewe eeh!!!.”
“Ndio ni mimi dokta vipi malaria nini??.” alifanya utabiri usiokuwa sahihi.
“Hapana hauna Malaria mwanangu..”
“Mh!! Nini sasa hichi Mungu wangu.”
“U mjamzito Matha!!!....mwezi mmoja.”
“Dokta!!! Be serious!!!”
“Ninamaanisha, vipi kwani hukutegemea au??.”
“Yaani siamini maana ni wakati muafaka hii zawadi imekuja.” alijibu kwa uchangamfu Matha. Akaaga akaondoka!!!
Alimanusra apate ajali njiani kwa papara alizokuwa nazo katika kuendesha gari kwa mwendo kasi ili awahi mahali. Hakuwa akienda kwa John lakini alikuwa akielekea kwa Michael aliamini kwa namna kubwa sana yeye ndiye muhusika wa hiyo mimba maana hawakuwahi kutumia kinga hata siku moja. Sijui walikuwa wakijiamini vipi!!!!
Matha alikuwa na furaha tele kwani ni mwaka wa nne tangu awe na uhusiano na John Mapulu bila dalili zozote za kupata mtoto. Tangu amtoe usichana wake walipokutana katika msiba wa mama yake mzazi na Matha, uhusiano uliokomaa na kudumu kwa miaka hiyo tele, miaka iliyomhamisha Matha kutoka shuleni na kuingia rasmi katika ujambazi. Akiwa kama kipenzi cha John hakumjua mwanaume mwingine hadi anapoingia kati Michael Msombe.
“Kumbe John hazai!!!” alisema kwa sauti ya chini kama vile kuna mtu pembeni yake alikuwa anamsikiliza.
“Mbona sasa amekuwa mbinafsi kiasi hicho??? Kwa nini hakunambia kuwa ana matatizo, nimejihisi mpweke na kumlaani mama yangu kwa kunizaa mgumba!!! Namchukia John. Kama alinipenda kwa nini ameificha siri hii??” alilalama Matha bila kupata msaada wowote. Breki za gari yake zikafanya kazi yake alipolikaribia geti kisha injini ikazimwa baada ya gari kuwa limeingia maeneo ya Mecco ndani ya nyumba ya John aliyoishi na Bruno!!! John hakuwepo!!! Lakini Michael alikuwepo.
“Michael!!!!.”
“Nambie mpenzi wangu.” Kwa mara ya kwanza Michael akamwita Matha jina hilo kwa kujiamini. Matha akambusu shingoni kimahaba, wakati huo walikuwa katika chumba chao cha mafunzo ya kutumia bunduki.
“Michael asante sana!!!!.”
“Asante kwa lipi huishiwi visa wewe mke wa bosi!!”
“Ah!! Sitaki mie hilo jina utaniudhi sasa hivi!!!” alilalamika kwa sauti ya chini Matha.
“Basi samahani kipetito” Michael alimwambia Matha huku akichukua kichwa chake na kukilaza mapajani mwa Matha.
“Michael nina ujauzito.” kama vile aliyepigwa shoti alijikuta akiruka kutoka mapajani mwa Matha na kusimama mlangoni kama anayetaka kukimbia. Matha akaubetua mdomo wake.
“Matha unasemaaje??.”
“Kwani ulikuwa unatumia kinga wakati tunafanya??.” Swali la Matha likamfadhaisha Michael akawa kama anayetaka kulia lakini chozi lilikuwa mbali sana, sura yake ikawa kama amepigwa ngumi.
“Michael nimekwambia nina mimba yako!!!”
“Sasa Matha hapo mimi nafanyaje unadhani??” alizungumza kwa upole Michael.
“Nakusikiliza wewe!!!.”
“Una uhakika kuwa ni ya kwangu???.”
“Asilimia zote!!!! John hana uwezo wa kuzalisha” alijibu Matha kwa ujasiri
“Fikiria kwa makini halafu utaniambia tunafanya nini???” alisema Matha kisha akambusu Michael katika papi za mdomo na kumwacha solemba. Mara akarejea na kumkuta Michael akiwa bado amesimama
“Katika mawazo yako yote sahau kuhusu kufanya arbotion, I won’t!!!”

*****
Suala la Matha kumkumbusha Michael kuwa sahau kuhusu kitu kinaitwa utoaji mimba lilimchanganya zaidi Michael. Kila alipofikiria kuhusu tatizo la John la kutokuwa na uwezo wa kuzaa Michael alizidi kuchanganyikiwa kwani aliamini kuwa endapo John ataigundua mimba aliyonayo mpenzi wake (Matha) basi mshukiwa wa kwanza kabisa ni yeye (Michael) hilo halikuwa na kipingamizi chochote.
“Na ikiwa hivyo basi nimekwisha mie!!!” Michael alisema kwa sauti ya chini huku kijasho kikipenya katika vinyweleo vya mwili wake kutokea kichwani na kuweka michirizi katika mashavu yake.
Michael hakutafakari na kupata jawabu lolote la maana akaingia chumbani kwake akajiegesha kitandani. Akapitiwa na usingizi!!!
Majira ya saa mbili usiku ndipo alishtuka, mang’amung’amu ya usingizi yalikuwa yakimyumbisha alikuwa akiyapikicha macho yake ili aweze kuona mbele vizuri wakati huo alikuwa anauendea mlango wa chumba chake aweze kuufungua na kutoka nje kiu kilikuwa kimemshika. Alipoufungua mlango ni kama alikuwa amemfungulia mtu ambaye bado alikuwa hajaomba kufunguliwa, Michael alikurupuka kama aliyekuwa amekabwa na jinamizi kisha ghafla akawa ameachiwa. Alikuwa ni John!!
“Vipi dogo….” John aliuliza
“Ahh!! Ni usingizi tu kaka vipi…aah!! Nilikuwa nimelala si unajua” alijibu pasipo kujiamini kijana huyu.
“Jiandae tutoke!!!..nakupa kama dakika kumi na tano fanya fasta” John alimuamuru Michael. Wasiwasi ukamuandama Michael, hakujua huo mtoko ulikuwa wa kwenda wapi. John hakuwa katika mavazi ya kikazi, bali alikuwa ameitundika suti yake nyeusi iliyombana kiasi na kuonyesha kifua chake kilivyoachana katikati, kwa ndani alikuwa na shati jeupe, kiatu cheusi chini kilihitimisha kumfananisha John na bwana harusi na wala si jambazi mzoefu. Hivi tutakuwa tunaenda wapi?? Alijiuliza Michael.
Hakuwa na wa kumpa jibu akaghairi kuliendea jokofu ili apate maji akapiga hatua kadhaa bafuni ili aweze kuoga, hata hivyo ubaridi wa maji ulimsababisha ajijengee hoja kwamba alikuwa msafi na kuhalalisha maamuzi ya kuacha kuoga. Badala yake akanawa uso kujitoa ile ladha ya usingizi usoni mwake, kisha akaliendea sanduku lake lililozuia zipu isijifunge kutokana na wingi wa nguo akatwaa jinsi ya bluu na fulana nyeupe akazitua katika mwili wake baada ya kuwa ametanguliza singlendi nyeupe kwa ndani, kisha akamalizia na raba iliyotawaliwa na weusi kiasi kikubwa na weupe ukichukua nafasi ndogo. Miwani aliyoivaa ilikuwa imempendeza sana kwani ilirandana na kiatu lakini usiku haukuwa wakati muafaka wa kuvaa miwani hiyo, baada ya kugundua hilo aliivua na kuirejesha mahali pake. Marashi!! Alikumbuka wakati anataka kutoka, haraka haraka alirejea na kupulizia kwa chati, aliporidhika akatoka na kuelekea sebuleni.
Hakuwa na haja ya kujitazama kwenye kioo, alikuwa amependeza!!
“Umejiandaa fasta sikutegemea maana nimekushtua sana!!!”
“Nimekacha kuoga!!! Ndo maana nimewahi” alijibu Michael huku akikaa katika ncha ya sofa.
“Twende zetu, huyu Bruno sijui atakuwa wapi muda huu??”
“Hata sijui maana tangu nimelala dah!! Wewe wakati unakuja pale ndo na mimi nilikua naamka, masaa kama manne hivi nilikuwa mfu”
“Shwari…tutampigia simu.” alijibu John huku akitangulia na Michael aliyetawaliwa na walakini akimfuata kwa nyuma hadi kwenye gari. Michael hakuingia kwanza alifungua geti gari ikatoka kisha akafunga ndipo akalifuata gari na kupanda.
“Aaah!! Tafadhali bwana mdogo yaani mi nimekuwa dereva wako!!!” alizungumza John kimasikhara baada ya Michael kukaa siti ya nyuma, haikuwa mara ya kwanza Michael kumsikia John akisema hivyo, mara moja akahamia siti ya mbele. Kabla hajakaa John aliondosha pakiti ya sigara iliyokuwa imebakiwa na sigara tatu ndani yake, hiyo ilimaanisha kuwa sigara takribani kumi na saba zilikuwa zimezama na kutoka katika mapafu ya John. Alipenda sana sigara bwana John!! Michael bila kuomba alitwaa naye sigara moja akaiwasha na kuanza kupuliza moshi ndani na nje. Na yeye tayari alikuwa ameathirika japo sio sana na utumwa huu wa sigara.
John alikuwa makini na usukani, kutokea pale Mecco alipinda kushoto kuifuata hoteli na bar ya Cheers kisha akakata kulia akiipita stendi ya Mecco na kuifuata barabara iendayo Nyakato sokoni, hapakuwa na masumbufu ya foleni za hapa na pale hivyo waliwahi sana kufika, baada ya kufika Nyakato sokoni gari ilikata kushoto baada ya kuwa imeingia barabara kuu ya Mwanza maarufu kama Nyerere road, gari liliondoka kwa mwendo mkali lakini salama kuelekea Igoma, NDAMA HOTELS ndipo kilikuwa kituo cha mwisho ambacho John alisimamisha gari lao dogo aina ya corolla. Wakati huo Michael alikuwa anamalizia kipisi kidogo cha sigara ya mwisho wakati wanashuka garini. John hakuwa katika hali ya uchangamfu hali hii ilizidi kumtia mashaka Michael.
“Vipi ina maana amegundua kinachoendelea ama kuna jambo gani linaendelea hapa??” alijiuliza Michael wakati huo John alikuwa akiangaza ni wapi wanaweza kukaa kwa utulivu. Walipata mahali palipokuwa na utulivu walioutaka wakaketi.
“Karibuni!! Karibuni sana” sauti ya muhudumu wa kike aliyetawaliwa na tabasamu bandia usoni maalum kwa ajili ya kazi aliwalaki wawili hawa.
“Asante sana…tutakuita tukikuhitaji!!!” alijibu John bila kumuangalia binti huyu usoni. Binti hakujibu kitu bali tabasamu lake liliyeyuka ghafla akaanza kuondoka.
“Hey!!....Mimi niletee Kilimanjaro, iwe ya moto tafadhali” aliamuru Michael
“Naomba 1800….” Alijibu yule dada ambaye sasa lile tabasamu lililopotea ghafla baada ya kuambiwa ataitwa baadaye sasa lilikuwa limerejea maradufu. Michael hakujibu akamtazama John aliyekuwa ameinama, muhudumu akailewa maana hiyo akamsogelea John bila shaka ni yeye alikuwa na jukumu la kulipia bili.
“Na mimi niletee Castle lite baridi, leta mbili kabisa.” John aliagiza huku akitoa noti ya shilingi elfu kumi na kumkabidhi yule binti, akaondoka kwa furaha!! Bila shaka walipokea posho kutokana na idadi ya wateja walioweza kuwahudumia kwa siku.
“Michael unamuonaje huyu binti!!!.”
“Kivipi yaani.”
“Muonekano wake tu!! Ni mrembo eeh!!.”
“Kiasi chake, namaanisha yupo katikati!!” alijibu Michael huku akimtazama John na kulazimisha tabasamu ambalo halikujibiwa na John.
“Wasichana wana mambo sana…..” kauli hiyo ikamgutua Michael kimawazo.
“Kwanini wasema hivyo….” Aliuliza huku akijiweka sawa kwenye kiti chake, viwiko vya mikono yake vikiegemea mezani
“Unajua unaweza kumpenda sana mtu halafu asitambue upendo wako, akatumia upendo huo kukuadhibu……lakini bado unaendelea kumpenda” alianza kujieleza John
“Yeah!! Hiyo inawezekana lakini sijaelewa maana ya kauli yako ” aliuliza kwa hofu Michael wakati huu alitoa mikono yake mezani na kuifunga kifuani kwake
“Michael si unajua kuwa wewe ni rafiki yangu sana?”
“Naelewa hilo na ni kaka yangu pia kwani kuna nini??” Michael aliuliza huku akijutia kuuliza vile kwani hakutaka kusikia jibu litakalotoka, hatia iliusaga moyo wake, aliamini kwa maongezi hayo John kuna kitu alikuwa kama hajakigundua basi alikuwa amekihisi kati ya yeye (Michael) na Matha. Mapigo ya moyo yakaanza kwenda kasi, fulana yake iliyombana ilimwezesha mtu ambaye hata kama si mchunguzi wa masuala ya afya kuligundua hili.
“Shiit!!! Nimeacha mguu wangu ndani ya gari!!!” John alijisonya baada ya kugundua amesahau bunduki yake garini, haukuwa utaratibu wake kutembea bila silaha. Lakini hakujisumbua kusimama na kuifuata. Kauli hiyo ilizidi kumtetemesha Michael.
Ina maana ndio amekuja kunifichulia maovu yangu na kuniua hapahapa!!!! Mungu wangu, lakini nilimwambia Matha kila siku kuwa ananitia matatani ona sasa!!! Aah!! Ona sasa Matha!! Aliwaza Michael kwa uchungu na kuzitupa lawama kwa Matha kabla John hajaendelea kuzungumza
“Eeeh!! Umeuliza kuwa nina maana gani, ujue Michael kuna wakati unafika lazima kila ukweli uwe wazi na uamuzi ufanyike mara moja, na uamuzi mgumu ni ule unaomuumiza aliyeuamua!!!” John aliendelea Michael akawa kimya, alikuwa amekodoa macho funda la mate alilotaka kumeza ni kama lilikuwa linataka kumshinda, koromeo lilionekana kuwa dogo lakini akajilazimisha likapita.
“Michael nakupenda sana lakini………” hakuweza kuendelea John muhudumu akawa amefika na vinywaji, akawafungulia , Michael akapiga mafunda mawili kulainisha koo lake, John hakupiga funda lolote bali alitia kiasi fulani kwenye glasi yake, wakati muhudumu huyu anaondoka kupisha faragha ya Michael na John, muhudumu wa kiume kutoka jikoni naye akafika kuwasikiliza.
Paja la mbuzi, weka pilipili, tenganisha sahani, ndizi nne zikaushe vizuri, mwambie huyu aongeze bia. Ni baadhi ya maneno mengi waliyozungumza na hatimaye mada ikawa imesahaulika!!! John hakuendelea na maelezo. Simu aliyopigiwa na Bruno ikawa imeingilia kati.

*******

Je!! Siri imefichuka???
Nini hatma ya Michael na Matha.

ITAENDELEA

No comments:

Post a Comment

Recent Posts