HATIA--06
Na George Iron
Geti dogo lilifunguliwa kidogo, baada ya kuhakikisha aliyetegemewa kuingia ndiye alikuwa mlangoni lilifunguliwa zaidi.
“Mheshimiwa Mapulu!!!! Karibu nyumbani…..kama ndoto vile” sauti nzito ya kiume ilimlaki John aliyejibu kwa tabasamu hafifu.
“Matha yupo au na yeye alikamatwa??” John aliuliza wakati huo ilikuwa yapata saa kumi adhuhuri.
“Matha yupo lakini anakamuliwa na mshkaji mwingine” Alijibiwa kwa njia ya utani akaling’amua hilo akatoa kicheko kidogo.
“Dogo langu hili, linaitwa Michael Msombe
muite Dabo M,ukishindwa kabisa muite Dabo” John alimtambulisha Michael
kama mtu ambaye anamfahamu siku nyingi sana. Jina lake likageuka na kuwa
Dabo.
“Mambo vipi bro!!!” alisalimia Michael MsombePoa Dabo naitwa Bruno…karibu sana”
“Asante sana” alijibu na geti likafungwa.
Haikuwa nyumba iliyotangaza umasikini hata kidogo lakini ilionyesha
matumizi mabaya ya pesa kwa samani zisizokuwa na shughuli maalumu
kulundikana pale ndani, usiku ule hakuona mtu yeyote zaidi ya Bruno
akahisi huenda wamelala wengine lakini haikuwa hivyo hadi panapambazuka
hali ilikuwa hivyohivyo.
Michael alishangaa lakini hakuuliza.
Asubuhi yule John wa selo aliyekuwa akishindia kapensi kafupi
kalikochakaa na wakati mwingine kumwacha uchi wakati akigombania vyakula
walivyoletewa mahabusu wengine hakuwa yule tena alikuwa ameng’ara ndani
ya nguo ya kulalia rangi nyeupe kabisa mkononi alikuwa na kikombe
kikubwa kilichoongezwa uzito na maziwa yaliyokuwa ndani yake. John
alikuwa tofauti sana hata rangi yake ilikuwa si ile iliyochafuka na
kukosa maji ya kuoga walipokuwa selo.
“Michael kuna mtu yeyote aliyekuwa anafahamu uwepo wako ndani ya selo??.”
“Mh!!!! Hapana sidhani” alijibu baada ya kujaribu kufikiri
“Una uhakika kuwa hujawahi kuja kusalimiwa???”
“Hakuwahi kuja mtu yeyote pale kaka, we ulikuwa shahidi” aliendelea
kusisitiza. John alitikisa kichwa ishara ya kukubali kisha akaifuata
rimoti na kuitazama luninga kuubwa bapa iliyokuwa inamtazama kisha
akaminya kitufe ikawaka, hakujishughuisha kuangalia ni chaneli ipi
iliyokuwa inaupiga mziki wa zook, akajiondokea.
“Michael!!! Una uhakika na unalosema???” aliuliza tena macho yake mekundu yakiwa yanautazama mdomo wa Michael.
Swali hilo likamshtua Michael kwa nini lilikuwa likiulizwa sana, safari hii akachelewa kidogo kujibu
“Siku ile nilimpa namba za msichana mmoja yule afande sijui kama
alipiga ama la lakini hakuwahi hata kuja pale mahabusu.” alijibu kwa
sauti iliyokuwa na hofu
“Nipe namba ya huyo msichana na kuwa
makini sana wakati mwingine unapojibu swali sawa!!!” alifoka kidogo John
na Michael akakubali bila kuzungumza chochote. Baada ya kumtajia
akaondoka, jambo la kushangaza ni kwamba John akuuliza mara mbilimbili
na wala hakuandika hiyo namba mahali popote pale, ni kama alikuwa
ameipuuzia hata Michael aliamini hivyo.
Siku hiyo ilipita huku
Michael akipewa nguo za kubadilisha ambazo zilimkaa sawa kwenye mwili
wake, japokuwa alikuwa na mawazo sana hakusita kukiri kwamba aliifurahia
hali ya kuwa huru.
****
Majibu ya askari aliyekuwa na wasiwasi mkubwa machoni mwake
yalimkera na kumshangaza sana Joyce Keto, alishindwa kuelewa kwamba ni
kweli aliyezungumza naye kwenye simu alikuwa ni askari ama ni mtu
alimletea utani. Kwa ghadhabu aliondoka kituoni pale.
Kwa nini
nisimpigie simu huyo aliyejifanya askari!!! Alijiuliza Joyce huku
akitembea kwa ghadhabu hakuwa na uhakika kama alikuwa akiyumba yumba ama
la alichotambua ni kuwa alikuwa akisonga mbele. Moja kwa moja katika
duka lililokuwa linauza vocha.
“Nisaidie Tigo ya mia tano!!”
alisema Joy na mwenye duka akampatia baada ya kuwa ameisugua. Bila ya
kujua ni mara ngapi alikuwa ameingiza ile vocha bila kuwa na umakini
aishtushwa na ujumbe uliomtaarifu kuwa namba yake ilikuwa imefungiwa
kutokana na kuingiza namba zisizokuwa sahihi, Joy alitamani kulia,
aliitazama simu yake kwa jicho la hasira kama ni yenyewe ilikuwa
imefanya makosa hayo ili kumkomesha. Kwa mwendo wa kukata tamaa akaanza
kuondoka lakini akasita tena na kurejea dukani.
“Makao makuu ya tigo ni wapi, samahani lakini!!!”
“Bila samahani malkia!!....” alizungumza kwa lafudhi ya kichaga na
kisha akamuelekeza Joy wapi ambapo kampuni hiyo ya simu imeweka makao
yake.
“Asante sana….kwaheeri!!!” aliaga. Mwanzoni wazo lake
lilikuwa kuondoka moja kwa moja na kuelekea hapo alipoelekezwa lakini
njaa ilimkatisha kufanya hivyo, jicho lake liliangaza huku na huko kisha
akajifikiria kwa muda pesa aliyokuwa nayo ilimruhusu kula wapi jibu
likapatikana kuwa alitakiwa kula chakula cha bei poa sana ili mambo
yaende sawia. Mama Fredi mgahawa jipatie chakula safi hapa.
Maandishi hayo yaliyoandikwa kwa mkaa yalimfanya Joyce atabasamu kisha
akajiambia “Mahali sahihi pa Joyce kupata chakula chake kwa siku ya
leo.” akanyata na kuingia kwa mtindo wa kuinama hadi akapata nafasi
yake. Bila hata kutaja ni chakula gani alikuwa anahitaji alishangaa
mbele yake ukiwekwa wali uliochanganywa na maharage, nyama moja, mchicha
na kipande kidogo cha bilinganya, hakutaka kuhoji aliamini huo ndio
utaratibu wa mgahawa wa mama huyo aliyekuwa muongeaji sana. Huenda hata
ndio sababu ya kuvuta wateja wengi sana katika genge lake.
Baada ya
kujiridhisha nafsi yake na chakula hicho kilichomgharimu shilingi elfu
moja Joyce Keto alinawa mikono yake na kuondoka.
“Ngoja niandae
mahali pa kulala kwanza maana dalili zote zinaonyesha kuwa nitalala
Mwanza, na huu ugeni nisije nikapata tabu baadaye.” alijishauri na
kukubali ushauri huo akaanza kuhangaika huku na huko hadi alipopata
nyumba ya kulala wageni iliyomgharimu shilingi elfu kumi ikiwa na choo
na bafu ndani.
Hakudumu sana katika chumba hicho baada ya kukizoea
kwa dakika kadhaa wazo la kurejea tena Tigo lilimrudia, lakini kabla ya
yote alijiweka maliwatoni na kuupasha mwili wake kwa maji baridi nguvu
zikamrejea na uchangamfu ukachukua nafasi yake. Kosa dogo alilofanya
Joyce liligeuka kuwa kubwa, ni baada ya kujiegesha kitandani na usingizi
kumpitia. Alikuja kushtuka jioni ya saa kumi na moja.
Tayari huduma alizotaraji kuzipata tigo hazikuwezekana palikuwa pamefungwa tayari.
“Hee!! Saa kumi na moja.” alipayuka kwa nguvu akiwa pale kitandani
lakini hakuwepo wa kumjibu hoja yake iliyokuja kwa mtindo wa kushtukiza.
Alisimama kama anayetaka kuondoka ili awahi kitu lakini alirejea kivivu
pale kitandani hakuwa na pa kwenda. Alijilaza pale alipotoka na
kumkaribisha tena jinamizi wa usingizi lakini kabla hajachukua kiti na
kuketi simu yake ya mkononi iliita. Ilikuwa namba mpya!! Mh!! Atakuwa
mama yake Michael ama…sasa kwa nini atumie namba mpya…au!!!” alijiuliza
bila kupata majibu, simu ikakatika!! Mara ikaanza kuita tena
“Hallo!! Mambo vipi dada Joy” upande wa pili ulianza kubwabwaja
“Poa nani mwenzangu samahani nilipoteza….”
Mimi Fredrick, haunifahamu lakini” ilimkatisha sauti ile baada ya kueelewa kuwa alitaka kujitetea kwa kudanganya.
“Wa wapi wewe??”
“Mwanza nimepewa namba yako na Michael yupo matatizoni, umeenda kumwangalia polisi???” iliuliza sauti ile kwa utulivu
“Nimeenda lakini sijamkuta….”
“Wamekwambiaje kwani??”
“Wamesema tu hayupo mi nikaondoka zangu”
“Dah!! Hata sisi wametwambia hivyo..wewe upo wapi sasa maana sisi wenyewe wageni hapa Mwanza”
“Mimi pia mgeni lakini nipo hapa Mitimirefu sehemu inaitwa Resting
house, ukishuka tu hapa kituoni unapaona nadhani panafahamika”
alijieleza Joy huku akiwa na furaha ya kupata wenzake katika vita moja.
“Haya kama tukiweza tutafika, kwa lolote lile tufahamishane sawa!”
“Msijali nitapenda sana mkija” alisisitiza Joy. Simu ikakatwa.
Baada ya saa zima akiwa anafanya tafakari mbili tatu
alishtushwa na mlango wa chumba chake kugongwa kwa utaratibu maalum.
“Nani tena muda huu!!!” alijiuliza huku akiuendea mlango na kuufungua.
“Una vitu vingine zaidi ya huo mkoba mezani??” lilikuwa swali kutoka kwa sura hizi mbili ngeni kabisa machoni mwa Joy.
“Nyie ni akina nani??” aliuliza lakini hakujibiwa.
“Tuondoke haraka eneo hili” aliambiwa
“Twende wapi…nyie ni akina nani???”
“Ndugu zake Michael, chukua vyako tuondoke”. Joyce akatii amri na
kukusanya vilivyo vyake na kuanza kuondoka hadi kwenye gari ndogo aina
ya corolla safari ya kuelekea asipopajua ikaanza.
“Shem ujue nini
yaani hii hali inashangaza sana mh!! Kumbe kweli anayekwenda jela si
lazima awe na hatia…” baada ya kimya alikuwa ni John ambaye alikwa
anajulikana kwa jina la Fredrick aliyeuvunja ukimya pale ndani. Mh!!
Nimekuwa shem tayari!! Alijiuliza Joyce na kumalizia kwa tabasamu la
kulazimisha bila kusema lolote.
Baada ya mwendo kidogo John
alitoa pipi na kuwagawia wote waliokuwa pale ndani, ni Joyce pekee
aliyekurupuka na kuibugia pipi ile, baada ya sekunde kadhaa usingizi
mkali ulianza kuyafumba macho yake alijaribu kupambana bila mafanikio
kuidhibiti hali ile, dhahiri alionekana kutambua janja hiyo iliyokuwa
imechezwa dhidi yake lakini haukuwepo ujanja wowote ule Joyce akapitiwa
na jinamizi la usingizi mkali sana.
Alikuwa amewekewa dawa za usingizi katika pipi!!!.
Alikuja kushtuka masaa manne baadaye na kujikuta katika chumba kikubwa
cha haja ambacho kilikuwa na hewa safi sana yenye ubaridi bila shaka
palikuwa na kiyoyozi.
Joyce alijinyoosha nyoosha huku akiyapikicha
macho yake ili kujiweka sawa. Hapa ni wapi?? Alijiuliza, lakini kabla ya
kupata jibu alisikia mlango ukifunguliwa kisha akaingia John ambaye
alijitambulisha kwa Joy kama Fredrick.
“Mambo vipi Joy naitwa John….jisikie huru upo nyumbani” John alijitambulisha kwa Joy ambaye bado alikuwa anashangaa.
“Nimefikaje hapa….hapa ni wapi??” aliuliza Joyce, John ambaye alikuwa
amevaa pensi pamoja na fulana kubwa iliouzidi mwili wake huku miguuni
mwake akiwa na raba nyeupe.
“Hapa ndio nyumbani kwetu karibu sana” alisema John huku akiachia tabasamu hafifu.
*****
Michael Msombe alikuwa ametekwa na sinema aliyokuwa anaangalia
katika luninga kubwa iliyokuwa sebuleni, hakupatwa na ukiwa wowote kwa
kuondoka John na Bruno. Mdadi ulikuwa umemshika pale jambazi kuu
lilipokuwa likipigwa na nyota wa filamu hiyo ambaye alikuwa ni Jackie
Chan, Michael alikuwa ni kama amezama na kuwa mmoja wa wahusika wa
filamu hiyo hadi pale aliposhtuliwa na kikohozi cha kujilazimisha kutoka
katika upande wa mlango wa kuingilia.
Macho yake yalihama kutoka katika luninga na kuelekea pale mlangoni.
Alikuwa ni msichana ambaye hakuna mwanaume ambaye angesita kumuita
mrembo, nguo fupi aliyokuwa amevaa iliyaruhusu mapaja yake meupe
kuchungulia nje, wepesi wa kitambaa cha nguo hiyo ulionyesha mchoro wa
chupi aliyokuwa amevaa ikiwa katika mfumo wa bikini, kinguo cha juu
saizi ya mtoto wa miaka minne kilihalalisha nusu ya tumbo lake kuwa
nje. Matiti yake kifuani yalikuwa na uwezo wa kukinyanyua kinguo hicho
kwa umbali mdogo sana huku ule mchomo wa mbele ukionekana kumaanisha
kamwe hajawahi kunyonyesha.
Sauti ya Michael ilipotea kabisa akajaribu kuilazimisha irejee ili aweze kumsalimia huyu kiumbe lakini iligoma kabisa.
“Mambo!!!!” alisalimiwa Michael kwa sauti laini sana iliyopenya katika
masikio yake kisha katika koo na kuilainisha sauti yake hatimaye akajibu
“Safiii….karibu!!!” yule binti akaanza kusogea mahali alipokuwa
ameketi Michael akimaanisha ameitikia wito, sehemu zake za nyuma
zilikuwa zinatikisika kila hatua aliyopiga. Bila kutambua Michael
akajikuta ameingia katika hisia nyingine na maungo yake kujikuta
yakiinyanyua suruali yake, kwa haraka sana alichukua kitambaa
kilichokuwa mezani na kujifunika lakini alikuwa amechelewa sana.
Tabasamu zito kutoka kwa yule binti lilimpumbaza akabaki kama zoba.
“Naitwa Matha….unanifahamu sijui???...lakini haunifahamu”
“Yeah!! Sikufahamu nadhani”
“Ni mchumba wa John..unamjua??”
“Ndio John namjua!!!”
“Wewe unaitwa Michael eeh!!!”
“Umenijuaje kwani???” badala ya kujibu Michael aliuliza huku macho yake yakiendelea kumchunguza kwa chati binti huyu.
Matha Mwakipesile alikuwa amepewa jukumu kubwa la kumfundisha Michael
jinsi ya kutumia silaha mbalimbali, John alikuwa ameamua kumchukua
rasmi Michael katika shughuli zake za ujambazi.
Matha alimueleza
Michael kwa utaratibu kabisa jukumu alilopewa, hali ya Michael iligeuka
kuwa ya uoga sana hakuamini kuwa binti mrembo kama Matha anaweza hata
kuwa na uwezo wa kushika bunduki sembuse kisu na kuua mtu. Mh!!! Usione
ukadhani. Alisema kimya kimya Michael. Somo alilopewa na Matha halikuwa
limemuingia hata kidogo, aliamini sasa alikuwa anapelekwa njia
asiyoitaka hata kidogo. Kutoroka!!! Ndio wazo kuu lililomjia lakini
atatoroka na kuelekea wapi. Akiwa bado katika mawazo hayo mara aliingia
Bruno alikuwa mwingi wa furaha iliyojionyesha waziwazi, alimsabahi
Michael kisha akaingia chumbani na kurejea tena baada ya muda mfupi
akiwa amebadilisha nguo zake.
“Bruno nahitaji sana kwenda nyumbani,
nimekaa hapa imetosha nadhani mama atakuwa akinitafuta sana.” Michael
alimwambia Bruno baada ya kuwa amekaa kitako.
“John anakuja muda si
mrefu utamweleza nadhani itakuwa vyema zaidi mi sijui lolote kuhusu wewe
na John” alijibu kwa sauti iliyokuwa na uulizi ndani yake, Michael
akatambua kuwa Bruno ameshtuka.
Baada ya masaa kadhaa John alifika na baada ya kuzungumza pembeni na Bruno alimfuata Michael.
“Nimeambiwa ombi lako si baya sana, lakini kabla sijakuruhusu naomba
nikukumbushe kitu, unakabiliwa na kesi ya kumuua askari pale kituoni,
una kesi kubwa ya kutoroka mahabusu hivyo umehalalisha kuwa ni wewe
uliyemuua binti uliyekuwa naye nyumba ya kulala wageni, hizo ni kesi
chache za halali zinazokukabili sijui kama zipo za ubakaji na wizi kwa
kutumia silaha…kwa ufupi unarudi mtaani kupambana na hukumu ya kunyongwa
baada ya fedheha ya kufanywa mke wa mtu gerezani….kama unaamini unaweza
kupambana na haya yote peke yako mimi nitakusaidia nauli kesho uende
mdogo wangu hata usijali.” alieleza John huku macho yake yakiwa
yameutazama uso wa Michael aliyekuwa anaukwepesha uso wake kila
anapogundua kuwa John anamwangalia.
Baada ya kumaliza kuzungumza
hayo John aliyanyuka na kuondoka zake akimwacha Michael akiwa ameduwaa.
Neno alilokuwa akilirudia mara kwa mara John kuhusu kuolewa na wanaume
wenzake ni hilo lilimsumbua akili Michael hakuwa tayari hata kidogo kwa
hiyo fedheha. Macho yalikuwa yamemtoka pima, aliingiwa na hofu ya
kutoroka kwa mara ya kwanza!!.
“John!!! Kaka John.” aliita Michael kwa nguvu wakati John akikaribia kutokomea.
“Sema dogo!!!”
“Naomba basi walau niwasiliane na mama najua ananitafuta sana mh!!.”
“Polisi sio wajinga kama unavyodhani…wewe unamuwazia mtu ambaye kwa
sasa anawasaidia upelelezi wa kujua wewe ulipo??? Wewe kumuona mama yako
haina tofauti na kuonana na polisi” alijibu John Mapulu kisha akacheka.
Neno hilo nalo likamshtua Michael na kuamini kuwa lilikuwa na ukweli
ndani yake na mama yake huenda anaweza kumsaliti.
“Kwa hiyo hata Joyce Keto anaweza kuwa anasaidiana na polisi?.” alijikuta akiuliza.
“Tena kwa ukaribu sana…nakutakia safari njema Michael” alifungua mlango na kuingia ndani.
Kesho yake hakuondoka!!!!!
Pabaya hapo!!
No comments:
Post a Comment