Monday, October 29, 2012

HATIA 9


MTUNZI: George Iron Mosenya
CONT: 0655 727325

SEHEMU YA SABA

“Shiit!!! Nimeacha mguu wangu ndani ya gari!!!” John alijisonya baada ya kugundua amesahau bunduki yake garini, haukuwa utaratibu wake kutembea bila silaha. Lakini hakujisumbua kusimama na kuifuata. Kauli hiyo ilizidi kumtetemesha Michael.
Ina maana ndio amekuja kunifichulia maovu yangu na kuniua hapahapa!!!! Mungu wangu, lakini nilimwambia Matha kila siku kuwa ananitia matatani ona sasa!!! Aah!! Ona sasa Matha!! Aliwaza Michael kwa uchungu na kuzitupa lawama kwa Matha kabla John hajaendelea kuzungumza
“Eeeh!! Umeuliza kuwa nina maana gani, ujue Michael kuna wakati unafika lazima kila ukweli uwe wazi na uamuzi ufanyike mara moja, na uamuzi mgumu ni ule unaomuumiza aliyeuamua!!!” John aliendelea Michael akawa kimya, alikuwa amekodoa macho funda la mate alilotaka kumeza ni kama lilikuwa linataka kumshinda, koromeo lilionekana kuwa dogo lakini akajilazimisha likapita.
“Michael nakupenda sana lakini………” hakuweza kuendelea John muhudumu akawa amefika na vinywaji, akawafungulia , Michael akapiga mafunda mawili kulainisha koo lake, John hakupiga funda lolote bali alitia kiasi fulani kwenye glasi yake, wakati muhudumu huyu anaondoka kupisha faragha ya Michael na John, muhudumu wa kiume kutoka jikoni naye akafika kuwasikiliza.
Paja la mbuzi, weka pilipili, tenganisha sahani, ndizi nne zikaushe vizuri, mwambie huyu aongeze bia. Ni baadhi ya maneno mengi waliyozungumza na hatimaye mada ikawa imesahaulika!!! John hakuendelea na maelezo. Simu aliyopigiwa na Bruno ikawa imeingilia kati.
Michael akapata ahueni!!

*******

Joyce Keto alionekana kuwa kikwazo pekee kwa John Mapulu katika mipango yake ya kujipanga upya katika shughuli zake. Alitambua ni kiasi gani wasichana ni dhaifu. Hivyo kuwa mikononi mwake lilikuwa jambo salama sana.
Iwapo Joyce angetiwa mikononi mwa polisi, lazima angesema lolote analojua kuhusu Michael hali ambayo ingemuweka matatani Michael, kijana ambaye ametokea kushibana naye.
Sasa Joyce alikuwa mikononi mwake katika nyumba ya mafichoni nje kidogo ya mji wa Mwanza. Kama ilivyokuwa kwa Michael. Joyce naye alijazwa chuki na kujihisi yupo hatiani. Hasahasa baada ya kuelezwa kuwa Michael anakabiliwa na kesi ya mauaji.
“Kuonekana kwako tu pale kituoni..unatafutwa sasa ukasaidie upelelezi. Maana Michael alitoroka.” John alimwogopesha Joyce. Kisha akamalizia kwa kumueleza juu ya Michael kumkimbia.
“Kwa hiyo mlivyotoroka, amekutoroka na wewe.”
John akakubali kwa kutikisa kichwa juu na chini.
Sumu pandikizi ikapenya katika akili ya Joyce. Akawa mtumwa wa kifikra.,
Uhusiano wa kimapenzi ambao Joyce alimueleza John kati yake na Michael haswa ndio ulimfanya John asipendezwe na kitendo cha wawili hao kukutana mapema. Alihofia kusalitiwa. Hivyo alijionya kuwa muangalifu sana.
Akaamua kumuweka Joyce mbali na Michael hadi wakati stahili utakapowadia.



KILICHOJIRI BAADA YA WATUHUMIWA KUTOROKA

Askari wa zamu usiku wa tukio la mauaji na kutoroka mahabusu wa kituo kikuu cha polisi wapatao kumi kwa kulinda maisha yao waliificha siri ya kutoroka kwa mahabusu wanne katika mazingira tatanishi. Pia mauaji ya askari usiku huo huo. Kwa uzembe huo kama wangethubutu kubaki, kifungo cha maisha ilikuwa halali yao kwani watuhumiwa wote wanne waliofanikiwa kutoroka walikuwa wanahusika na mauaji, John akiwa mkongwe anayefahamika kwa kesi hizo, Michael akiwa amesingiziwa lakini ushahidi ukimuhitaji sana kwa upelelezi na wengine wawili wakiwa na kesi ya kuiba na kuua kwa kutumia bunduki.
Kwa watuhumiwa wa kesi nzito kama hizo ni nani angepona kwa kusema kuwa hajui wanne wametoroka toroka vipi??? Bila kushirikishana lakini kila mmoja akijua lake moyoni, wanne kati yao wakaamua kutoroka wawili wakajiua na wanne waliojisalimisha wakaanza kusota rumande na baadaye gerezani Butimba kwa kesi ya kuwasaidia mahabusu kutoroka pia kuhusika katika kuua askari mmoja. Wema waliodhani ni silaha ukawa umewaponza, upelelezi unaendelea ndio kauli pekee iliyosalia wakati wanazidi kuteketea mahabusu. Mmoja baada ya mwingine wakaanza kupoteza maisha kutokana na mateso makali na msongo wa mawazo huku wengine wakigeuzwa wake za watu angali walikuwa mahabusu.
Akabakia askari mmoja huyo alikuja kutoka kwa msamaha wa raisi miezi miwili baadaye baada ya kesi yake kukosa ushahidi wa kutosha, huyu aliweza kuona na kutembea kama aliyekamilika lakini hakuwa na uwezo tena wa kuzaa, mateso aliyopitia tayari yalikuwa yamemvuruga uzazi lakini kubwa zaidi ni kuingiliwa kimwili mara kadhaa na wafungwa wazoefu wakati yupo gerezani akisubiri hukumu yake. Hakurudishwa kazini baada ya msamaha hakuwa na vigezo tena. Uaskari wake ukawa umeishia katika simulizi mbaya na ya kuumiza kama hiyo. Huyu aliyepona aliyebahatika kurejea uraiani alikuwa ni Sajenti Kindo Malugu, hakuwa sajenti tena alibakia kuwa mzee Malugu.
Siku chache kabla ya kukamatwa kwake alipokea taarifa ya mwanae mpendwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha, ni baada ya kukumbana na unyanyasaji wa kijinsia kutoka kwa baba yake mdogo aliyekuwa amechukua jukumu la kumlea baada ya mzee Kindo kuhamishwa kikazi kutoka Singida na kuhamishiwa Mwanza.
Baada ya mwanae huyo wa pekee wa kike aliyezungukwa na wenzake wawili wa kiume ambao walikuwa wameathirika na matumizi ya madawa ya kulevya ndio kwanza alikuwa amejitahidi na kumaliza kidato cha sita.
Hakuwa tayari kuolewa bali alitaka kundelea na masomo yake ya chuo kikuu. Mateso, kejeli na dharau kubwa kutoka kwa baba yake mdogo pamoja na mkewe zilikuwa zimemsukuma kutoroka katika mji huo na kwenda mahali alipopajua mwenyewe. Baada ya kupata taarifa hiyo mzee Kindo alinuia kuchukua ruhusa na kurejea nyumbani kushughulikia suala hilo, halikuwa suala dogo hata kidogo ile ilikuwa ni damu yake inatangatanga. Lakini akiwa katika kusubiri ruhusa yake ipitishwe ndipo linatokea tukio la mauaji katika nyumba ya kulala wageni jijini Mwanza.
Hakuwa mmoja kati ya askari walioenda kwenye tukio kwani alikuwa anahangaikia ruhusa lakini alikuwa ni yeye aliyeandika maelezo mafupi ya awali kuhusu mali alizonazo mtuhumiwa kwa wakati ule yaani PPR baada ya Michael kukamatwa. Ruhusa ilizidi kumchelewesha hadi linapotokea tatizo jingine kubwa la kuuwawa kwa askari aliyekuwa lindoni na kutoroka kwa watuhumiwa wanne wa kesi za mauaji, hata siku hii pia alichelewa sana kuingia kazini kwani suala la ruhusa yake lilikuwa bado gumu. Siku hiyo alikuwa zamu, hivyo alikuwa anahusika katika kujibu kitakachoulizwa.
Mwanzoni alikubaliana na wenzake kuhusu kutoroka lakini alipompigia mkewe simu na kumuomba ushauri alipinga vikali na kumsihi asijaribu kutoroka kwani alikuwa na mtihani mwingine wa kumtafuta mwanae je angeuweza vipi huu mtihani wakati asingekuwa huru tena??? Maneno hayo makali yaliyosindikizwa na kilio kisha meseji kadhaa za kumsisitiza asifanye alichokusudia zilibadili mawazo ya Sajenti Kindo, yeye pamoja na askari wengine watatu wakajisalimisha, siku hiyo ndiyo ilikuwa ya mwisho kwake kuwa huru hadi alipotoka kwa msamaha wa raisi.
“Vua gwanda, vua mkanda, saa na hiyo kofia” haya yalikuwa maneno yaliyowaamrisha siku wanaingia mahabusu, ilikuwa kama utani lakini miaka miwili ikathibitisha si utani ule.
“Mwanangu Joyce, sijui alipatikana???” ni swali la kwanza alilojiuliza mzee huyu, punde tu baada ya kuambiwa yuko huru.
“Poti!! Poti!!....” Kindo alisikia sauti ikimuita wakati akiondoka katika mahakama hiyo ambapo alikuwa amemaliza hatua zote za kuachiwa huru kutokana na msamaha wa Raisi, hakugeuka mara moja kwani aliamini kuwa si yeye aliyekuwa anaitwa. Sauti ile ilipoendelea kusisitiza alisimama na kugeuka. Sura haikuwa ngeni sana machoni mwake lakini hakutaka kuonyesha dalili zozote za kuikumbuka sura hiyo.
“Poti!! Pole sana kaka….nafurahi kukuona mtaani tena dah!! Ya Mungu mengi” mtu huyo mfupi mnene aliyekuwa ananyemelewa na kitambi alizungumza kwa furaha.
“Sijakukumbuka ujue!!!” Kindo alinyanyua mdomo wake na kuzungumza. Bwana yule alifuta tabasamu lake usoni na kuvaa huzuni alimsikitikia Kindo kwani aliamini ni maisha ya kukosa uhuru yalikuwa yamemsababishia hali hiyo ya kukosa kumbukumbu.
“Kura tumekura pakurara je!!!!” badala ya kujibu alitoa kauli hiyo, Sajenti Kindo akashtuka sana kisha akamkumbatia kwa nguvu zake zote mzee huyo, machozi yakawa urembo katika nyuso za wawili hawa.
“Poti Magembe ni wewe kaka???” aliuliza Kindo pasipo kuamini macho yake.
“Ni mimi poti!!! Pole sana kaka, tuliumia sana kukupoteza uraiani” alizungumza kwa huzuni huku akimkagua Kindo kwa macho jinsi alivyozeeka ghafla ndani ya miezi ishirini na nne (24). Walizungumza mengi wakiwa wamesimama wima, Kindo bado alikuwa mkakamavu kiasi licha ya masumbufu ya maisha ya mahabusu bado alikuwa imara. Walikumbushana mengi sana yakiwemo maisha yao ya uaskari tangu wakutane Singida na baadaye Kindo akahamishwa kwenda Mwanza.
“Vipi na wewe ulihamishwa nini??” aliuliza Kindo.
“Ndio hivyo kaka, yaani baada ya wewe kutupwa huko ndani wiki mbili baadaye nikahamishiwa hapa, hivyo niliipata stori yako punde tu baada ya kuhamia hapa. Mazungumzo yalikuwa mengi sana lakini hasahasa kumbukumbu ndio zilitawala.
“Poti hapa nilipo ni kama nashuhudia muujiza nimeachiwa, sina kazi nimefukuzwa tayari, hapa nilikuwa natembea kwenda nisipopajua nashukuru nimekuona, huu mji ninauchukia sana nahitaji sana kurudi nyumbani kwangu huko Singida hapa Mwanza hapana, ngoja nirudi nyumbani…lakini poti!! Mi hapa sina hata nauli, tusizungumzie njaa ninayoisikia hapa hii nitaivumilia…suala ni nauli” alijieleza Kindo kwa sauti ya chini. Magembe akawa amemuelewa.
Kitu cha kwanza walipata chakula ambacho Kindo hakikukifurahia sana, baada ya hapo wakaelekea nyumbani kwa Magembe maeneo ya National housing. Alipumzika kwa siku mbili pale wakati Magembe akihangaika huku na huko hatimaye akapata kiasi cha pesa akampatia Surgent Kindo, akashukuru akaaga na kuondoka.
Siku iliyofuata akaiacha ardhi ya Mwanza.

*****

Maongezi kati ya Michael na John yaliendelea baada ya John kumaliza mazungumzo yake kwenye simu na Bruno mazungumzo yaliyochukua takribani nusu saa huku John akizungumza kwa makini na utulivu asiweze kusikiwa na mtu yeyote. Hali hiyo ilizidi kumtia Michael katika jitimai la nafsi. John aliporejea mezani tayari huduma kutoka jikoni ilikuwa tayari, wakaanza kula na kunywa baada ya hamu kuanza kuwaisha ndipo maongezi yakaendelea.
“Michael naamini una ukaribu flani na Matha!!!” John alisema, lilikuwa shambulizi kubwa sana lililomzidi ujanja Michael akayumba kimawazo lakini hakuanguka, wasiwasi wake ulikuwa wazi sana lakini bahati ilikuwa kwake kwani John alikuwa ameinama akichezea vipande vya mifupa vilivyosalia katika sahani.
“Ndio kwa sasa nipo naye karibu tofauti na mwanzo wakati sijamzoea” alijaribu kujibu mashambulizi Michael.
“Unamchukuliaje kwa jinsi alivyo sasa na kipindi cha nyuma”
Mimba!! Mimba!! Mimba!! Kengere za hatari zililia kichwani mwake.
“Sijaona mabadiliko sana” alijibu huku akiwaza juu ya uwezekano wa swali hilo kuhusisha mimba.
“Michael natamani sana ungejua ni kiasi gani mimi nampenda Matha na nilivyohangaika naye hadi hapa tulipo, ungelijua hilo nadhani ungenionea huruma” aliongea kwa huzuni sana John. Michael akaanza kutetemeka miguu alitamani amtumie ujumbe Matha lakini alihofia huenda tayari simu yake ipo mikononi mwa John hivyo kwa kitendo cha kutuma ujumbe angeongeza maradufu hasira za John.
“Michael Msombe!!!! Nisaidie kitu kimoja tu!! Naamini unakiweza”
“Ni kipi hicho??”
“Unapafahamu kwa Matha??”
Mtego!!!! Alishtuka Michael
“Hapana sipafahamu, sijawahi kwenda” alidanganya Michael kwani aliwahi kukitumia kitanda cha Matha kwa masaa kadhaa kufanya mapenzi na binti huyu mpenzi wa John Mapulu. John alimtazama Michael usoni kwa muda huku akiwa kama anasoma kitu fulani.
“Ok!! Nitakuelekeza….au nitakupeleka…nahitaji msaada wako, wewe ni mwanaume kama mimi” alizungumza John, pombe ilikuwa kidogo imemchangamsha.
“Nimekuelewa kaka” alijibu huku akimeza funda la bia na kukunja sura yake ili kuupokea ukali wake tumboni.
Kimya kikuu kilitawala kwa muda kila mtu alikuwa anawaza na kutenda la kwake hadi walipomaliza na kulipia huduma walizofanyiwa kisha wakaondoka baada ya kuwa wamechukua makopo kadhaa yaliyojazwa bia.
“Endesha!!!!” John alimwomba Michael.
“Sina uzoefu na hizi left hand kaka” alijitetea Michael.
“Ah!! Madereva wa VETA na nyie mna matatizo kweli” alitania John huku akiingia katika kiti cha dereva, safari nyingine ikaanza. Muziki wa hip hop ndio ulitawala ndani ya gari, John aliweza kuimba mistari aliyoifahamu na Michael akijiumauma pale anapoweza hadi gari iliposimama maeneo ya Buzuruga jirani na stendi ya mabasi yaendayo mikoani, ni ya pili kwa ukubwa baada ya ile ya Nyegezi.
“Unaona lile ghorofa pale, acha hilo linalomeremeta hiyo ni bar, hili la pembeni yake, chumba cha tatu juu, hapo ndipo anakaa Matha, fanya kama surprise sawa” alielekeza John.
“Sasa naenda kufanya nini???” aliuliza Michael. John alijigongesha kichwa chake katika usukani na kusababisha gari ipige honi isiyo na maana, John alikuwa anajishangaa kwani alikuwa hajampa maelekezo yoyote yale Michael.
“Dah!! Mapenzi haya, ok!! Michael kwa maneno yako yote yaliyo kichwani naomba ukamweleze Matha kuwa ninammpenda sana” John alisema kisha akatulia kidogo.
“Najua hakuna rafiki yangu mwingine ambaye ataeleweka kwa Matha lakini wewe naamini atakuelewa, naamini hivyo Michael” John akatulia akamwangalia Michael, macho yake yalikuwa mekundu sana dalili zote za kutaka kulia.
“Ni kitu gani simpi mimi?? Najua amepata kimwanaume kinamzuzua lakini mwambie akumbuke tulipotoka!!!!” alishindwa kuendelea akaanza kulia, Michael akashuka garini akaupunga mkono ishara ya kuaga na kutokomea.

Michael aliamini yupo katika mtego mkubwa kuliko yote maishani mwake, suala la kuagizwa usiku wa saa tano kwenda nyumbani kwa Matha aliamini kuwa ni mpango wa kumtia katika hatia yenye ushahidi wa kutosha ili kuhalalisha hukumu yake. Alitamani sana kumpigia simu Matha lakini bado nafsi yake ilikuwa na mashaka.
“Hapana sipigi simu yoyote ile…nitawapa uhakika mapema sana” alizungumza peke yake. Akiwa na simu yake mkononi badala ya kumpigia Matha alimpigia John, simu yake ikawa inatumika. Akakata baada ya dakika tano John akapiga.
“Vipi mdogo wangu umepotea nini??”
“Umejuaje?? Umesema chumba namba??” alizuga Michael
“Namba tatu upande wa kulia, pembeni yake kuna jiko” alielekeza John baada ya kujilazimisha kucheka kidogo.
“Poa kaka nimeuona mlango, haya baadae” aliaga.
Kwa tahadhari kubwa sana aliufikia mlango, palikuwa kimya sana lakini hilo halikumtisha haikuwa mara ya kwanza kwenda mahali usiku, mara nyingi akiwasindikiza akina John huwa ni usiku. Mlango ulikuwa umerudishiwa kidogo bila shaka muhusika alikuwa hajalala bado. Michael aligonga mlango kwa utaratibu sana. Sauti kutoka usingizini ilimuuliza yeye ni nani hakujibu akausukuma mlango na kuingia ndani.
“Matha!!! U hali gani??”
“Michael!!!!” aliita kwa mshangao mkubwa Matha huku miguu yake tayari ikiwa sakafuni, mikono ikiyapikicha macho yake yaweze kupambana na giza lililokuwa limetanda.
“Upo na nani??”
“Peke yangu kwani vipi???” alihoji Matha kwa sauti ya chini sana huku akiuendea mshumaa na kuuwasha, chumba kikapata mwanga.
“Matha umemfanya nini John”
“Hamna kitu kwani vipi??”
“Una uhakika upo peke yako??”
“Nipo peke yangu jamani sasa haka kachumba na wewe huoni au??” alisema kwa ghadhabu kidogo.
“John ameanza kutushtukia” Michael alisema kisha akaelezea stori yote ya siku hiyo wakiwa na John, Matha alionekana msikivu sana na ambaye huenda angeuliza maswali mengi sana baada ya hiyo simulizi lakini haikuwa hivyo.
“Ujue Michael, huyu John huyu anataka kuchanganyikiwa yule John yule niachie mimi, wewe haumuwezi hata kidogo, yaani yule John….” Matha akiwa anayazungumza hayo alikuwa mbele ya Michael, akiyabinyabinya mabega yake, punde akawa amemkumbatia kabisa, joto kali kutoka kwa Matha, pombe alizokunywa Michael zikaungana kwa pamoja kumshabikia shetani, mapepo yakaruhusiwa kuamka Michael akawa ameagizwa na John kwenda kuzini na Matha, Michael akakisahau kilio cha mwanaume jasiri kama John. Michael akatumia masaa manne kumbembeleza Matha, wakaoga pamoja kwa mara ya kwanza. Walisahau hata mimba iliyokuwa inakua taratibu katika nyumba ya uzazi ya Matha.
“Mwambie John asante sana kwa zawadi eeh!!..mwambie awe anakuagiza kila siku tena usiku ndo inapendeza” Matha alimtania Michael wakati anaondoka. Michael akatikisa kichwa akatabasamu akaondoka. Tayari ilikuwa saa kumi adhuhuri. Kutoka Buzuruga kwenda Mecco ni mbali kiasi lakini Michael aliamua kutembea kwa miguu. Wakati akiwa kwa Matha hofu haikuwepo lakini alipokaribia Mecco, hofu ikamtwaa upya akaanza kumuogopa John, kitendo alichotoka kufanya na Matha kikamtia hatiani tena, hatia ikainyanyasa nafsi yake akaukosa uhuru wa nafsi.
“Hujalala mpaka sasa hivi kaka??” aliuliza Michael baada ya kumkuta John sebuleni akiwa macho anaangalia luninga.
“aaah!! Nilale wakati askari wangu hujarejea bwana!!!” alijibu kwa furaha John .
“Dah!! Nimekuja kwa miguu, si unajua tena daladala hazijaamka bado” alisema kwa utulivu huku naye akichukua nafasi.
“Mh!! Una mambo kaka, nadhani shughuli ilikuwa nzito sana”
“Aah!! Kiasi chake lakini kawaida”
“Si kawaida yaani hadi kufikia suala la kuoga si mchezo ati!!!” alisema John, kauli iliyovunjavunja ujasiri wa Michael, almanusura apige goti kuomba msamaha kwa aliyoyafanya muda mfupi uliopita lakini alisita akabaaki kushangaa.
“Mh!! Aaah!!! Umejuaje kaka” alijipa ujasiri wa bandia na kuuliza.
“Marashi gani ya Matha nisiyoyajua mimi???? Sabuni uliyotumia ni Candy na marashi ni Halloween uongo uongo!!!” alisema kwa utani John ili kumdhihirishia Michael kuwa anamfahamu Matha nje ndani.
“Dah!! Na Matha kanambia hivyo hivyo nikakataa kumuamini mh!! Mnajuana nyie watu si kitoto” alipata uongo wa kujibu Michael.
“Hah!! Matha kakwambia ehee ilikuwaje??” John alikaa vizuri aweze kumsikia Michael vyema.
“Siwawezi nyie…hamuwezi kuibiana kama mnajuana hivyo” alijibu pasipo imani hata kidogo kwani alijua kila kitu tayari John anajua. Michael hakuelewa kuwa kuendelea kusema uwongo ndio yupo sahihi ama auseme ukweli aujue mwisho wa mchezo.
“Nimezungumza na Matha, kwanza amestushwa na imani yako ndogo na amesema kesho niende anipe kitu nikuletee na amesema asante sana kwa Surprise!!!!!” alijilazimisha kufurahi Michael lakini hatia yake iliimeza furaha yote.
“Hata mimi kanitumia meseji!!! Kashtuka sana najua kukuona usiku huu??” aliongezea John. Michael bado hakuelewa kama John alikuwa hajashtukia kinachoendelea ama la!!!
“Vipi kesho muibukie basi au vipi, mi ntakutoa za viroba na nyama choma” kwa sauti iliyojaa ubembelezi John alimsihi Michael.
“Ngoja nikalale maana nimechoka mie, shem kanidekeza hadi nimeoga dah!! Sijui alijuaje kuwa sikuoga wakati natoka” Michael alisema, John akamuunga mkono kwa kicheko kikali cha furaha. Siku ikaisha hivyo tena walakini ukiwa bado umetawala.

Michael aliingia chumbani kwake, hakuamini kama siku hiyo inakatika bila John Mapulu kuusema ukweli wote juu ya uovu aliougundua dhidi yake. Usingizi ulimchukua mapema sana kutokana na uchovu na ulevi wa siku hiyo. Alijilazimisha kuwa na amani ilhali moyoni haikuwepo hata chembe. Michael aliamini kuwa alikuwa mtegoni.
“Mh!! Sijui kama patakucha salama!!” ni wazo la mwisho kichwani mwa Michael kabla hajapitiwa na usingizi mzito.
Majira ya saa nne asubuhi ndipo alishtuka kutoka usingizini lakini alitumia nusu saa nyingine kuuruhusu mwili wake ubanduke kitandani. Njaa ilikuwa inamuuma lakini hakuwa na hamu na kitu kingine zaidi ya supu. Hang over zilikuwa zimemtawala!!
“Oyo!! Huoni au mbwembwe tu!!!” sauti ya John ilimsimamisha Michael aliyekuwa anataka kutoka nje huku akipiga mluzi bila hata kutoa salamu. Michael alisimama na kumwangalia John kwa hofu.
“Ah! Sijakuona wala nini, nawaza tumbo tu hapa nataka nikarekebishe kiaina si unajua tena!!!” alijibu Michael huku akijiegemeza kwenye mlango ambao ulikuwa nusu wazi nusu umefungwa.
“Nilikuchukulia supu na chapati nenda ukacheki jikoni!!” John alimwambia Michael kwa sauti ya upole sana. Kengele za hatari zikalia kichwani mwa Michael. Sumu!!! Aliwaza mara moja kabla ya kushukuru na kujongea jikoni kwa ajili ya hicho alichohifadhiwa.
“Ukimaliza kula uniambie kuna jambo nahitaji tuzungumze!!” John alimwambia Michael ambaye aliupokea ujumbe huu akiwa anakaribia kulifikia jiko. Uoga ulikuwa umeitwaa nafsi yake, kila jambo alilofanyiwa na John alitia walakini ndani yake Hatia iliyokuwa inamkabili ndiyo ilimhangaisha. Kwa mwendo wa kunyata kama mwizi wa njiwa Michael alichukua kipande kidogo cha nyama iliyokuwa katika supu na kurushia paka aliyekuwa akifugwa hapo kwao. Paka alikitafuna kipande kile kwa shangwe zote hata kabla hakijatua chini vizuri kisha akajilambalamba ulimi na kutoa mlio wa nyauuu!!! Huku jicho lake likimtazama Michael kwa matamanio ya kupewa tena kipande cha nyama. Michael alisubiri kwa dakika kadhaa na yule paka naye akisubiri kuongezwa kipande kingine. Paka hakukumbwa na mushkeli yoyote ile. Chakula kilikuwa salama!! Michael alikuwa katika maisha ya mashaka sana!!
“Ah!! Kama ameniwekea sumu juu kwa juu bwana maisha gani haya ya wasiwasi? Bora nife!” alijisemea kwa sauti ya chini Michael huku akiivamia supu ile ambayo ilikuwa ya moto bado, hakujiandalia chakula mezani alimaliza kila kitu pale pale jikoni.
“Asante sana braza maana mh!!!” Michael akiwa na glasi ya maji ya kunywa baridi kabisa alimshukuru John.
“Hapo sasa safiiiiiii!!!!” alizungumza John kwa furaha.
“Ah!! Hapa hata nisipouona mchana poa tu” Michael alijibu huku akichukua nafasi yake katika sofa iliyokuwa ikiangaliana na sofa aliyokalia John.
“Michael nina zawadi yako nahitaji nikupe leo nadhani utafurahia”
“Zawadi kwa lipi kaka nililofanya”
“Jana umetumia muda wako mwingi sana kuzungumza na Matha nimeyaona mabadiliko leo mabadiliko makubwa nilikuwa na Matha asubuhi ya leo hapa!!” John alizungumza huku tabasamu likichanua katika mdomo wake.
“Aaah!! Amakweli leo nimelala sana”
“Kwa suala hilo nahitaji kukupongeza!!!”
“Usijali wewe ni kaka yangu” Michael alisema huku hasira zikiwa zimemtawala ndani ya nafsi yake pepo wa wivu akaanza kumtafuna taratibu, akaanza kuhisi Matha ni mali yake peke yake.
“Hata kama lakini unastahili zawadi” alisisitiza John. Michael hakupinga zaidi ya kukubali kwa shingo upande hiyo zawadi.
“Matha amekuja??? Muda gani na saa ngapi ameondoka?? Au mtego huu?? Eeh!! Mungu nisaidie” baada ya muda mrefu sana kupita Michael alikumbuka kupiga dua.
Au wananichora hawa kasha wanitoe kafara! Alijiuliza.
****

***MICHAEL anazidi kujikita katika penzi la MATHA.
***JOHN hajaushtukia mchezo...anamuamini sana Michael.....
***NINI KITATOKEA SIKU AMBAYO JOHN ATAGUNDUA KUWA MICHAEL ANAMZUNGUKA.
KUMBUKA JOHN NI MTU KATILI NA ANAUA ANAVYOTAKA.

ITAENDELEA

No comments:

Post a Comment

Recent Posts