MTUNZI: Emmy JohP.
CONT: 0654 960040
SEHEMU YA TATU
3
Mchomo wa wivu ukanishambulia na kunijeruhi moyoni, nikaanza kuhisi zile ndoto zangu zimeanza kufifishwa. Happy alinisalimia akiwa na tabasamu mwanana. Dokta akiungana naye kutabasamu. Nami nikajilazimisha nikatabasamu!!!
“Kesho nitarejea nyumbani mara moja….kuna dharula imejitokeza. Lakini kitu kimoja nahitaji mfanikiwe kupitia mimi.” Alianza kutueleza dokta, tukiwa ndani ya gari la kukodi. Kisha akaendelea, “Nitarejea hivi punde tu!! Na nikiwa huko nitakuwa nawasaidia, msisite kunieleza lolote nami nitawasaidia, hata mimi kufika hapa nilikuwa nasaidiwa kwa hiyo ni zamu yangu kusaidia.” Aliongea kwa ukarimu mkubwa.
Kwa mahesabu ya harakaharaka zile dola thamani yake ilikuwa milioni sita za kitanzania. Hizo ndizo Dokta alituachia tugawane.
Kwangu mimi ilikuwa kama ndoto ya mchana!!!
Siku iliyofuata dokta huyu wa ajabu akarejea huko anapojua yeye!! Hakutaka kusindikizwa uwanja wa ndege.
****
Ile hali ya kumshuhudia Happy akiwa na Dokta Davis ilinitia mashaka sana na kuhisi kwamba muda wowote ule nitanyang’anywa tonge mdomoni. Hivyo nikalazimika kuchukua tahadhari na kuanza kumpeleleza Happy kujua iwapo ana mawasiliano ya ukaribu na Davis ama ni wasiwasi wangu tu.
Niliamini kabisa Davis alikuwa ni mali yangu na si ya mtu mwingine hivyo, Happy kama alitaka kunizunguka basi alikuwa hanitendei haki hata kidogo.
Ilikuwa siku tulivu ya jumamosi nikiwa chumbani kwangu. Chumba ambacho kwa sasa kilikuwa na mabadiliko kidogo tofauti na awali. Simu yangu iliita alikuwa ni dokta Davis. Nikapokea.
Dokta alizungumza mengi huku kubwa zaidi akinigusia kuhusu biashara tuliyozungumza. Ni hapo ndipo nikaikumbuka biashara ya mtandao. Siku tulivyochat naye katika mtandao wa facebook huenda sikumuelewa vyema. Sasa alikuwa ananielewesha vyema ni jinsi gani mimi nitahusika katika biashara hiyo inayolipa mamilioni mengi kwa muda mfupi.
“Sasa hapo biashara hiyo inafanyikaje? Huo mtandao uko vipi?.” Nilimuuliza kwa utafiti. Kwani hakuwahi kunielekeza moja kwa moja juu ya biashara hiyo ya mtandao.
“Umeuliza swali hili wakati muafaka sana. Nilitaka kukueleza kuwa umependekezwa kuwa mwakilishi wetu katika nchi yako. Hongera sana.” Aliniambia na kabla sijauliza chochote aliendelea, “Ni lini utapata walau siku nne za kuwa free uweze kunitembelea huku niweze kukupa maelekezo zaidi?”
“Wewe upo wapi??” Nilimuuliza.
“Lusaka Zambia, lakini tutakutana Ndola.”
“Ndola ndio wapi?.” Nilijawa na maswali mfululizo.
“Mkoa mmoja hapahapa Zambia.”
“Kwa sasa nipo free sana. Hatujaanza kuwa bize.” Nilimjibu huku nikiwa nafurahia mazungumzo hayo.
“Waweza kukimbia mara moja kuja huku ofisini kwetu kwa ajili ya kusaini mikataba?.” Aliniambia, nikacheka kimya kimya yaani yeye Zambia alipaona karibu sana eti ananiambia nikimbie mara moja.
“Naweza ila…”
“Usijali mambo ya nauli na kila kitu kampuni itakulipia. Kesho zitaingizwa kwenye akaunti yako.”
Ni hilo haswaa nilitaka kumuulizia na sasa alikuwa amenipa jibu tayari.
Baada ya kukata simu ile nilitamani sasa kila mtu aitambue furaha yangu, nipo chuo mwaka wa pili napata kazi nje ya nchi, mshahara zaidi ya milioni mbili. Nani kama Isabella.mara nikamsahau Happy aliyekuwa anakisumbua kiichwa changu.
Nikafumba macho, nikatamani sana kumshrikisha mwalimu Nchimbi ambaye ni mama yangu mzazi lakini nikaona ni mapema sana, nikataka kumwambia Happy lakini nikahisi huyo alikuwea mpinzani wangu katika kumuwania Davis. Nikakaa kimya sikumwambia mtu yeyote.
Siku moja kabla ya kuondoka nilizungumza na kiongozi wa darasa letu Class Represenative ‘CR’ kuhusu kazi zitakazokuwa zinatolewa darasani awe ananiandika kuwa nipo japo sitakuwepo, mwanzoni alinikatalia lakini nilipotoa noti moja baada ya nyingine hadi zikafika noti kumi nyekundu alilainika na kugeuka kibaraka. Tena akawa mzungumzaji mkuu!! Pesa bwana!!
Kesho yake asubuhi nilikuwa katika basi la kampuni ya Abood kuelekea Mbeya kisha Tunduma halafu safari ya kwenda Ndola. Kusaini mkataba!! Mkataba nisioufahamu!!
Nilijihisi kama malikia na lilikuwa kosa kubwa sana kujaribu kunifananisha na mwanafunzi yeyote wa chuo kikuu cha mtakatifu Augustino ambacho nilikuwa nasoma. Hata wale wa huko Dar pia hawakutakiwa kufananishwa na mimi Hakuna ambaye angeweza kukaa ngazi moja na mimi kwa sababu wengi wao waliishi kwa kutegemea mkopo sasa mimi nilikuwa nina pesa yangu na kubwa zaidi nilikuwa naingia kazini. Hao watoa mikopo ningepata fursa ya kukutana nao nadhani ningekuwa na jeuri ya kuwashushia mvua ya matusi.
Nikiwa safarini kuelekea Mbeya nikitokea mjini Dodoma baada ya safari ndefu kutoka Mwanza siku iliyopita, tulipofika Makambako nilianza kuifikiria familia yangu niliwaza kumjengea mama yangu nyumba ya kifahari kisha nimtoe baba yangu katika ulevi sugu kwa kumuwekea pombe za kisasa ndani. Hizo niliamini zitamnenepesha badala ya kumkondesha. Wadogo zangu waliokuwa wakisoma shule za kata nao nadhani walitakiwa kusoma shule zenye hadhi ya mshahara nitakaokuwa napokea dada yao. Tena wote nawapeleka shule za bweni!!! Nilijiapiza huku pua zangu zikinusa kwa mbali harufu nzuri ya sabuni ambayo nilitumia asubuhi kuoga katika hoteli ya kifahari mjini Dodoma.
Nilitoa tabasamu hafifu kisha nikaendelea kuuchapa usingizi.
Nilifika Mbeya salama. Dereva teksi wa kwanza niliyekutana ndiye alipata bahati ya kuniendesha msichana ambaye nilikuwa na malengo makubwa kama mimi. Alitakiwa kujisifu kama angekuwa kichwani mwangu.
Alinifikisha hadi hoteli maridadi yenye hadhi ya kulaliwa na watoto wa vigogo na vigogo wenyewe. Nililipia na kulala hapo kesho yake mapema nikawa Tunduma halafu mwisho ikafuata safari ya Ndola. Hata ule uchovu haukusumbua mwili wangu.
Ndani ya basi tulilokuwa tumepanda walikuwepo watu mchanganyiko. Hakuna aliyekuwa na hadhi kama mimi. Yaani nilikuwa najisikia kuwa na uwezo hata wa kuamuru basi hilo lisimame na likasimama lakini sikufanya hivyo.
Majira ya saa kumi na moja jioni kwa mara ya kwanza katika maisha yangu nilikanyaga ardhi ya nchi tofauti na Tanzania. Isabella ndani ya Ndolla
Mwanzo wa safari ya kwenda Marekani!!! Nilijiwazia hivyo.
Nilitegemea kuhangaika sana baada ya kuwa nimeshuka pale kituoni. Lakini la!! Haikuwa hivyo. Nilipotelemka tu. Nilitumia dakika moja tu kushangaa wanawake wawili waliokuwa wamependezea katika mavazi yao ya suti walinipokea begi langu dogo huku wakinisalimia kwa nidhamu kubwa sana.
Niliwajibu kwa tabasamu, sasa nilianza kuamini kuwa Dokta Davis atakuwa ni mtu mkubwa sana. tofauti na mwonekano wake
Niliongozwa hadi katika gari aina ya Noah, nilitaka kuingia humo lakini nikaambiwa hilo ni kwa ajili ya mizigo. Nikacheka moyoni huku nikiwaza kuwa laiti kama ningepewa hilo gari. Chuo wangekoma!!
Mh!! Mzigo gani sasa?? Nilijiuliza. Hakuwepo wa kunijibu.
Baada ya hapo nikapelekwa katika gari iliyokuwa na milango sita. Hapo nikafunguliwa milango nikaingia ndani. Niliokutana nao mle ndani wote walikuwa na nyuso zilizong’aa tofauti na ule wa dokta Davis. Japo walikuwa weusi na sura zao zikitangaza roho flani hivi isiyokuwa na ukarimu sana lakini walitabasamu.
Naishi kama mfalme nchi za watu?? Mwalimu Nchimbi natamani ungeyaona haya goodbye umasikini!!!! Nilijitamba kichwani mwangu huku nikikaa vyema na kuzijibu salamu za watu pale ndani.
Safari ikaanza. Sikuwa naujua mji hata mmoja lakini safari nayo haikuwa fupi.
Nilitamani sana niulize kuwa pale ni wapi lakini ningeanza kumuuliza nani?? Hilo likawa swali. Laiti kama dokta angekuwepo hapo sawa.
Nikiwa bado nashanga shangaa hapa na pale mara mwendo ulipungua kisha honi ikapigwa. Geti likafunguliwa na watu waliovaa nguo nyeupe sana. Gari zikaanza kuingia, yetu ikiwa ya pili kuingia.
Tulipotaka kushuka milango ilifunguliwa na akina kaka wenye kila sababu za kuitwa watanashati na wanamazoezi. Nikazidi kuvimba kichwa kwa mema haya niliyokuwa natendewa.
Nikiwa bado sijafungua kinywa kuzungumza tangu nijibu salamu garini, walinifuata akina dada watatu wakanielekeza kwa ishara za mikono niwafuate. Sikuwa na kipingamizi niliwafuata. tuliingia katika chumba kilichokuwa na mvuto hata kwa yule asiyejua ubora wa chumba. Lakini mimi nilikuwa naujua ubora niliambua.
“You have to re-dress madame” (Unatakiwa ubadili mavazi yako). Waliniambia kwa pamoja. Sauti zao tamu zilinikonga moyoni.
Wakanipa maelekezo na baada ya dakika kadhaa nilitoka mle ndani nami nikiwa nang’ara katika mavazi meupe sana.
Nilikuwa nimependeza sikuhitaji kumuuliza mtu.
Sasa tukarejea katika magari tena. Mi nilijua tumefika mwisho kumbe lile lilikuwa geti la kwanza tu.
Mwendo wa dakika tano tukashuka tena. Tukaingia geti jingine kubwa. Hapo tukatelemka na kuanza kutembea juu ya kapeti jekundu.
Red kapeti!!! Niliwaza. Nikafanya tabasamu.
Nikiwa juu ya lile kapeti nikajihisi kuwa na hadhi ya Rihanna, Beyonce ama Lady Gaga. Kisa tu nipo juu ya zulia jekundu.
Hapa kama ni kazi nimepata!! Nilijiaminisha.
**ISABELLA ndani ya nchi ya Zambia, mkoa wa Ndolla. Je hiyo kazi ni kazi gani???
***Je? Davis yuk wapi???
***KWA NINI ANASEMA ‘SITAISAHAU facebook!!!!”
ITAENDELEA KESHO!!!!!
No comments:
Post a Comment