Na George Iron
MUGUMU SERENGETI
Usumbufu aliokuwa akiupata kutoka kwa mama
yake Michael kuhusu mwanaye ulimkosesha amani Joyce Keto sasa alikuwa ameeamua
kubadili laini ya simu yake ili aweze kuwa na amani walau kiduchu. Mara moja
moja alikuwa akiiweka ile laini na kusoma baadhi ya jumbe zilizokuwa zimeingia
kisha kuitoa katika simu.
“Mwenye namba 0657727324 amekupigia simu
saa……” ulisomeka ujumbe katika simu yake.
“Mh!! Atakuwa nani huyu jamani…” alijiuliza
Joyce akiwa katika kitanda chake katika nyumba aliyopanga kwa muda. Haraka
haraka alizinakiri zile tarakimu katika karatasi na kisha akatumia simu yake
nyingine kupiga.
“Hallow!!” upande wa pili ulipokea ilikuwa
sauti nzito ya kiume.
“Samahani kaka, nimekuta ujumbe wako kwamba
ulinipigia simu lakini sikuwa napatikana” alijieleza Joyce
“Hii simu wanatumia watu wengi, afande
Matiko Mwanza hapa je kuna uhusiano wowote” aliuliza
“Ahh!!! Sijaelewa.”
“Labda kuna ndugu yako ni mahabusu maana
hawa ndio wanapiga piga simu sana kwa ndugu zao, kwani hiyo namba yako ni ipi”
aliuliza na Joy akamtajia naye akawa anaiandika.
“Aaaah!! Kuna ndugu yako huku tena ana siku
nyingi sana anaitwa Michael Msombe” alijieleza yule afande.
“Nani Michael????......upo wapi afande
wewe, kwani amefanya nini tena…aah!!! Umesema Mwanza” alijikanyaga kanyaga
Joyce baada ya kupokea taarifa hiyo.
“Mwanza kituo kikuu cha polisi…usiku mwema”
aliaga na kukata simu.
Bila kuchukua ruhusa kazini, siku
iliyofuata Joyce alidamka mapema sana na kupanda mabasi yaendayo Mwanza, ni
mwendo wa masaa manne hadi matano kulifikia jiji la Mwanza. Siku hii aliiweka
hewani ile namba yake ya siku zote na tayari alikuwa amempigia mama yake
Michael na kumweleza kuwa Michael yupo Mwanza na anakwenda kuonana naye.
“Mwambie anipigie kuna tatizo huku sawa
mwanangu, asante eeh!!” alijibu mama yake Michael kwa furaha.
Safari ilikuwa ndefu sana lakini hatimaye
wakalifikia jiji la Mwanza hii ni baada ya kupanda mabasi mawili kwani basi la
moja kwa moja halikuwepo siku hiyo.
“Naitwa Joyce Keto….natokea….”
“Sema shida yako…” alikatishwa na polisi
aliyekuwa kaunta
“Kuna ndugu yangu hapa anaitwa Michael
Msombe nimekuja kumwona nasikia amekamatwa”
“Anaitwa nani na amekamatwa lini???”
aliuliza kwa hofu afande
“Sifahamu….”
“Haya subiri hapa dakika mbili…. Una
uhakika wewe ni ndugu yake” alihoji Joy akatikisa kichwa kuashiria kukubali
“Hakuna mtu kama huyo hapa” lilikuwa jibu
la afande.
“Hapa ndio central….” Aliuliza Joyce
“Ndio hapa kwani hujui kusoma” alijibiwa
kwa mkato na yule afande ambaye alionyesha kuwa hakupenda kuzungumza na Joyce.
****
Taratibu Michael na John Mapulu wakawa
marafiki ndani ya lock up, mara kwa mara walipiga stori za hapa na pale
kuhusiana na maisha halisi huku simulizi za John zikimsisimua sana Michael
ambaye hakuwa na jambo lolote lile la kutisha nje ya chuma hizo za mahabusu.
“Mimi ni mbaya naua dakika yoyote ile kisha
nasahau!!!!” alisisitiza John na kumwacha Michael mdomo wazi akiwa haamini kama
yupo karibu na mtu wa hatari kiasi kile, japokuwa John hakuwa na mwili uliojaa
sana lakini alikuwa na makovu mengi sana kuonyesha kwamba amebobea.
“John Mapulu!!!!!” iliita sauti ya afande
aliyekuwa ameikaza sura yake kana kwamba analinda mahabusu hata mmoja
asitoroke, huku John akiamini sauti hiyo ilikuwa ni ishara kwamba mahabusu mpya
ameingia hivyo aje kumpokea la! Haikuwa hivyo John baada ya siku nyingi
alihitajika nje ya selo hiyo, labda kwa ajili ya mahojiano!!!, labda kupelekwa
mahakamani, au kuachiwa huru kabisa!!! Hapana haiwezekani kwa muharifu kama
huyu.
“Dogo kama nisiporudi mamlaka yote sasa juu
yako, naweza kuwa napelekwa sehemu inaitwa ‘Sitaki maelezo’ huko ni hatari sana
mdogo wangu hakuna mwanaume hata mmoja anayeweza kusita kutoa machozi, wanatesa
vibaya sana na bila kujali lolote unaweza ukafa na usishtue jamii, na ujasiri
wangu wote kule napaogopa sana, ukifanikiwa kutoka salama wewe si mwanaume
tena!! Kule wananyanyaswa wenye makosa na wasio na makosa, hakuna huruma kule”
kwa mara ya kwanza Michael akaisoma hofu aliyokuwa nayo John baada ya
kuhitajika nje ya selo hiyo.
Michael hakuwa na la kuongezea, moyo wake
ulidunda mara mbili ya mwendo wa kawaida huko Sitaki maelezo aliwahi kupasikia
tu kuwa ni kituo cha polisi cha Mkuyuni lakini maalumu kwa ajili ya mahojiano
na watuhumiwa wa makosa ya jinai. Mh!! Hivi na mimi nina kosa la jinai eeh!!!
Alijiuliza Michael na kuzidi kupatwa hofu.
“John!!! Nakusubiri wewe!!!” alizidi
kusisitiza afande, kwa unyonge John akaiangalia selo na kutoka nje, suruali
aliyoivaa haikuwa na uwezo wa kukaa kiunoni. Alikuwa amekonda sana!!
Michael alibaki mkiwa japo hakuna
aliyethubutu kumsumbua kwa lolote amani haikuwepo nafsini mwake, huku akiwa
anaamini fika kuwa John Mapulu hatarejea, muda wa saa tatu usiku akiwa amelaa
baada ya kuwa wamehesabiwa alimsikia John akirudishwa pale mahabusu.
“Kwa kesi niliyonayo sasa hivi
wataninyonga!!! Sipo tayari kufa kwa sasa” ni maneno ya kwanza kabisa John
kumnong’oneza Michael ambaye alikaa kitako kumsikiliza vyema.
“Kwanini kaka unasema hivyo na imekuwaje
umerudishwa hapa ndani??” alihoji Michael kwa mtindo uleule wa kunong’oneza.
“Nitakueleza lakini kwa sasa hebu
ngoja….watu wote wamelala hapa ndani??.”
“Nahisi watakuwa wamelala ni muda mrefu
sana tangu waache kuzungumza” alipojibiwa hivyo aliingiza mkono wake mmoja
sehemu zake za siri na kuibuka na kitu ambacho Michael hakukifahamu si tu
kutokana na giza hapana hakuwahi kukiona kabla.
“Dogo umewahi hata siku moja kufikiria kuwa
maisha yako yanaweza kuishia gerezani??.”
“Hapana kwani vipi??.”
“Vipi kuhusu kufanywa nyumba na mwanamme
mwenzako??.”
“Nyumba?? Ndio nini!!!” aliuliza kwa
mshangao lakini kwa sauti ile ile ya chini
“Kuolewa!!!”
“Hapana na haitatokea…”
“Ukienda jela utaolewa bila kupenda na
mwishowe utazoea.” alijibu John huku akijikuna mgongo wake, Michael alibaki
anashangaa kama aliyeambiwa mke wake ana mimba isiyokuwa yake.
“Una maana gani??.”
“Namaanisha utaolewa kama unapenda kwenda
jela.”
“Sipendi kwenda jela!!!.” bila kutarajia
alijikuta anamjibu
“Mimi pia sipendi kunyongwa hadi kufa ni
heri nife kwa risasi…..hivi unafahamu kesi yako hukumu yake ni ipi??.”
“Hapana sifahamu!!.”
“Unapenda kifo cha aina gani??.” John
alimuuliza
“Mhh!! Sipendi kufa.”
“Basi wao watakunyonga hadi ufe maana wewe
uliua!! Utajisikiaje siku unahukumiwa??” aliuliza kama swali la kawaida kabisa
“Lakini mimi sikunyonga!!!” alijitetea
Michael bila kujua kwamba pale hapakuwa mahakamani, John Mapulu akacheka kwa
sauti ya juu kidogo.
“Mimi leo hii usiku natoroka sijui wewe
mwenzangu” John aliyatamka hayo kama vile anayeaga kwenda msalani mara moja na
kurejea tena baada ya muda mfupi tu.
“Unatoroka!!! Kiaje mimi a a siwezi.”
aligutuka Michael
“Haya mimi nilikuwa nakuaga tu!! Kama vipi
utamsalimia bwana mmoja anaitwa Dunga Dunga kama ukipelekwa gereza la Butimba
na yeye anasubiri kunyongwa kwa hiyo utakuwa naye, yeye ni bingwa wa kuoa
wenzake halafu yeye kuolewa hataki lazima atakuchangamkia, lakini kama akiwa
amenyongwa tayari sina budi kusema alale pema peponi.” alimaliza kwa kucheka
hasahasa baada ya kukumbuka kuwa amesema alazwe pema peponi. Muharifu kama
huyu!!!
“…….halafu kama wasipokunyongea hapa Mwanza
basi wanaweza kukurudisha kwenu……huko Dar gereza moja hivi linaitwa Keko. ni
heri ufanye sala kwa Mungu wako unayemwamini wakunyongee hapahapa Mwanza….”
Aliongezea John.
Mh!! Nifanye sala kwa ajili ya kuchagua mahali
pa kunyongewa??!!! Alishangaa Michael.
Michael alishikwa na hofu kuu ni kama John
alikuwa ameshika kitanzi kwa ajili ya kumnyonga baada ya hukumu kupitishwa.
Fundo la hasira lilimkaba kooni, alitamani sana kila mtu afahamu kuwa yeye hana
makosa lakini hilo halikutokea.
“Mapulu nimesema sipo tayari kufa….”
“Umewahi kusikia mtu ananyongwa halafu
anapona??.”
“Hapana!!!”
“Sasa wewe unasemaje hutaki kufa wakati upo
tayari kunyongwa???” aliuliza kwa sauti iliyodhihirisha kukerwa na msimamo wa
Michael.
“Tuondoke wote John.”
“Sio tuondoke sema tutoroke!!!.” John
alimrekebisha Michael usemi wake. Michael akalazimisha kutabasamu. Wakalala!!
Ni kama vile John alikuwa na saa
ameitegesha, usiku wa manane kila mahali pakiwa kimya alisimama wima kwa
tahadhari kubwa akawaruka wenzake kwa kunyata hadi akaufikia mlango wa stoo
iliyokuwa inatumika zamani sana, kufuli lake lilikuwa kubwa lakini lenye muundo
wa kizamani. Akachomeka kifaa alichomuonesha Michael baada ya kuingia, kwa muda
wa sekunde kama tatu kufuli likasalimu amri.
Mlango ulikuwa mgumu sana kufungua na
ulielekea kumshinda John.nimuamshe Michael!!! Hapana. Alijiuliza kwa sekunde
kadhaa kisha akaingia chumba kimoja akawaamsha watu wawili hawa walikuwa na
kesi ya kukutwa na bunduki. Hakika John alikuwa hajakosea baada ya sekunde
kadhaa mlango ulikuwa wazi.
“John Mapulu!!!!!” ilisikika sauti kali
ikitokea mlango mkuu wa kuingizia mahabusu, John na wenzake wawili walibaki
wakishangaana kwani tayari walikuwa wamefungua mlango. Jonh aliwaonyesha ishara
ya kukaa kimya nao wakatii.
“John!!! mteja wako mpya huyu hapa….ingia
huko nenda moja kwa moja huko mwisho” ilisikika sauti ya afande akitoa maelezo
kwa mahabusu. Haraka haraka John alivyosikia mlango umefungwa aliwaacha wenzake
wawili waliokuwa katika azma moja na kumuwahi huyo mahabusu mgeni asijue nini
kinaendelea.
“Lala hapo hapo wasikuzingue hao!!!” John
alimkaribisha yule mahabusu mahali pazuri kabisa naye akashukuru na kujilaza.
“Michael…..Mi…. amka wewe” John alimtikisa
Michael na yeye akiwa na kumbukumbu sahihi kabisa alisimama wima na kumfuata
John Mapulu.kuolewa!!kuteswa ….kunyongwa…hapana bora kutoroka!! Ni uamuzi
alioufikia Michael akauvaa ujasiri.
“Nikikamatwa nimekwisha!!!!” alijisemea
Michael bila kumpa nafasi John kugundua kwamba alikuwa na wasiwasi mkubwa.
Mlango ulikuwa wazi Michael akatangulizwa kisha wale wengine wawili ambao John
alitokea kuwakubali ghafla kisha akajitosa ndani mwenyewe ukawa umebaki mlango
mmoja pekee waweze kufika nje na kuwa huru.
Kiongozi wa msafara akiwa ni John hivyo
alisikilizwa kwa kila kitu. Wakati huu aliwasihi wenzake watulie tuli tena
wakatii. Alifanya kitendo cha dakika chache kuvua suruali yake, kuchuchumaa
chini kisha akapeleka mkono wake katika sehemu ya haja kubwa akaibuka na simu
ndogo nokia 1100 ile ya tochi.
Michael akakodoa macho lakini wale wengine
hawakushangaa kwani huo mtindo walikuwa wanaufahamu mtindo huo unaitwa
kupandisha na kushusha. John akamsoma Michael usoni alivyoshtuka akajenga
tabasamu bandia bila kusema neno lolote. Simu iliwashwa, ujumbe ukatumwa kisha
ikazimwa baada ya kujibiwa ujumbe.
“Dakika tatu zinazokuja tutakuwa nje, msiwe
na papara zozote zile ili tufike salama!!!” alizungumza kwa kumaanisha John
Mapulu, Michael alikuwa anatetemeka, alitambua kuwa hakuwa na hatia lakini sasa
alikuwa anajiingiza katika hatia ya ukweli. Lakini kipi bora kunyongwa bila
hatia au ukiwa na hatia!!! Alijiuliza lakini alikuwa amechelewa sana kupata
jibu litakalompa maamuzi sahihi mlango wa pili ukawa wazi.
“JOHN Mapulu….kuja hapa…kuja hapa haraka”
ilisikika sauti ya amri ni sauti John aliyoifahamu ilikuwa sauti ya mpelelezi
wa kesi yake Sajenti Romagi, mpelelezi aliyesifika kwa ukatiri wake
Mkojo wa moto kabisa ulikuwa umeshapenya
katika suruali ya Michael, alikuwa muoga kuliko wenzake hii ni kwa kuwa
hakuwahi kuzoea hizo pilika pilika. John alisimama thabiti akakuna kichwa chake
kutafuta maamuzi sahihi ama kurejea na kuitikia wito ama kuendelea na safari
yao ya hatari kabisa.
“Twendeni!!!” aliamuru John, akafuatiwa
nyuma na kundi la watu watatu wote wanaume lakini mmoja akiwa anatetemeka sana
kama mwanamke huyo alikuwa ni Michael. mlango wa kutokea nje ulikuwa
umefunguliwa na vijana ambao walikuwa wameziba nyuso zao kwa kutumia vitu kama
soksi kubwa hivyo sura zao hazikuonekana. Hawakuzungumza kitu lakini John
alielewa kipi kinachoendelea, upepo wa nje majira ya usiku ulipokelewa vilivyo
na mapafu ya Michael na kumsahaulisha kosa kubwa alilokuwa amelitenda kosa la
kutoroka!!!! Akiwa hajui la kufanya na wapi pa kwenda John Mapulu alimshika
mkono wakaanza kutokomea taratibu kuelekea walipojua wao lakini Michael alikuwa
kama kipofu anayefuata mkondo.
Hatua kadhaa mbele Michael akiwa ameamini
tayari wapo huru bila kupata usumbufu wowote katika giza walimkuta askari
aliyekuwa lindoni akiwa amejiegemeza ukutani, John akamshtukia kuwa tayari
alikuwa ameuchapa usingizi maeneo yale ilisikika harufu kali ya bangi bila
shaka kabla ya kusinzia askari yule alivuta misokoto kadhaa ya mmea huu halali
katika nchi ya Jamaika.
Michael ambaye muda wote alikuwa
anatetemeka alimshuhudia John akinyata kwa tahadhari kubwa na kumrukia yule
askari kilichofuata ni kitendo cha John Mapulu kuwa juu ya askari huku mikono
yake ikiwa imelikamata koromeo la huyu kiumbe barabara, baada ya dakika kadhaa
akamwacha huru, licha ya kuachiwa huru hakuweza hata kusema neno. Alikuwa
maiti!!!
“Washenzi sana hawa!!!” alisema John kisha
akampa ishara Michael amfuate, wale waliofungua mlango na akina John wakatoka
walikuwa wamepita njia nyingine pamoja na wale wawili wenye kesi ya bunduki
waliopata upenyo wa kutoroka pamoja na John baada ya kuamshwa wasaidie kufungua
mlango. John tayari alikuwa na bunduki mkononi nani wa kumtisha kiumbe huyu
hatari linapokuja suala la kutumia bunduki!!!! Michael alijiona muuaji na
anayezidi kupotea njia pumzi za uhuru alizozikurupukia sasa zilikuwa
zinamuwasha zaidi ya kawaida. Hatua kwa hatua, mtaa kwa mtaa, hatimaye walikuwa
katikati ya kundi la raia wema ndani ya daladala zinazoelekea Nyakato Mecco nje
kidogo ya jiji la Mwanza.
Michael bado alikuwa kipofu!!!
No comments:
Post a Comment