MTUNZI: Emmy John P
MAWASILIANO: 0654 960040
SEHEMU YA KUMI
ILIPOISHIA
Nilitaka kumuita jina lake kwa sababu nilihisi ninalijua jina hilo. Hata sura mbona nilikuwa nimewahi kuiona hapo kabla? Lakini kabla sijajua anaitwa nani. Teksi ilipigiwa honi ikapisha njia ikaondoka zake.
“Ah!! Huenda aliwahi kunibeba hapo kabla.” Nilijipa moyo.
Nikafungua pochi yangu na kuhifadhi hicho nilichookota.
“Mungu wangu!!!!” nilipiga kelele kwa nguvu sana. Nilikuwa nimesimama wima.
Kwa kuwa halikuwa eneo la watu wengi nilipata sekunde kumi za kuhakikisha nilichokiona.
Hakika kilikuwa chenyewe.
Kilikuwa kitambulisho cha chuo ni heri kingekuwa changu.
Kitambulisho cha John mikononi mwangu. Kitambulisho kinachoaminika kupotea ,msibani huko Iringa , kitambulisho nilichokiona ndotoni.
Kitambulisho cha muuaji!!!
Ewe dunia funguka unimeze!!! Ni sala niliyoiomba kimyakimya.
Nilikuwa nimezizima siwezi kwenda mbele wala kurudi nyuma.
Harufu ya kifo!!!!
***NI jambo juu ya jambo…….ISABELA ISABELA ISABELA.
Lakini je ungekuwa wewe ungefanya nini sasa….John unampenda, John umeota akiwa anaua, kweli mtu kafa. Huyu mtu ni binamu wa John. John anapoteza kitambulisho. Na ndotoni muuaji anadondosha kitambulisho.
John na muuaji wa ndotoni wanafanana….Kabla ya kujua Isabela mimi nilifanya nini…je WEWE UNGEFANYA NINI HAPO.
Pagumu!!!!!
ENDELEA
ITAENDELEA.
Nilisahau ni jambo gani lilikuwa limenipeleka huko mjini. Yale mawazo niliyoamini nimeyapunguza kwa kunywa pombe sasa yalikuwa yamerudi kikamilifu. Tena mara mia zaidi.
Hofu ikatanda. Nikachukua teksi nyingine nikarejea nyumbani kwangu.
Nilikuwa natetemeka, na kila nilipoguswa na kitu nilishtuka. Hata nywele zangu za bandia kichwani ziliponigusa shingoni nilitetereka.
Nilipohakikisha kuwa nimeifunga milango vyema kabisa na ndani nilikuwa peke yangu. Nilifungua mkoba wangu nikakitoa kitambulisho.
Hapakuwa na mabadiliko. Kilikuwa kitambulisho rasmi cha chuo kikuu matakatifu Augustino. Mmiliki akiwa John Joseph.
Mpenzi wangu.
Nililazimisha akili yangu kutafuta kumbukumbu huenda siku moja aliwahi kunipatia kile kitambulisho. Hapana kitu kama hicho.
Au aliweka mwenyewe bahati mbaya akakisahau? Hilo swali walau kidogo liliamsha uhai na kunipunguzia hofu.
Akija nitamuuliza!!! Nilimaliza hivyo. Nikautua mzigo wa mawazo.
Nikaingia maliwatoni nikasafisha mwili wangu kijuu juu. Nikajitupa katika sofa iliyokuwa sebuleni. Ule uchovu wa ulevi jana usiku ukawa unanishawishi kusinzia.
Nikajifikiria kwenda kulala chumbani. Mara mlango ukagongwa.
Nikajikausha!! Ukagongwa tena.
Nikaenda kufungua. Alikuwa ni John.
Alilazimisha tabasamu!! Nami nikatabasamu. Hatukusalimiana.
Tayari kakereka jana sikulala nyumbani!!! Niliwaza, huku nikijiandaa kukabiliana na maswali atakayoniuliza kwa fujo.
Wanaume wana mikwara jamani!!!!
Akafika hadi katika lile sofa nililokuwa nimejilaza awali. Akajitupa hapo. Akazishusha pumzi kwa nguvu sana. Kisha akajishika kichwa. Mimi yangu macho nikawa nasubiri lawama.
“I hate this…..” Alisema huku akiwa kama anajisea mwenyewe.
Yaleyale!!! Nikajisemea.
“Uko ok!! John!!” Hatimaye nilimuuliza. Hakunijibu!!
“John jamani….” Nilibembeleza. Bado hakunijibu kitu. Nikaamini kuwa John amekerwa sana na kitendo changu cha kulala nje bila taarifa.
Wazo!!! Wazo likanijia. Nikasimama tena bila kumuaga nikatoweka pale hadi chumbani. Nikazama katika mkoba. Nikachomoa kile kitambulisho.
Nikakisokomeza katika sidiria niliyokuwa nimevaa. Kisha nikarejea sebuleni. Wanaume dawa yao ndogo tu!! Mfanyie kitu anachopenda kwa wakati!! Baaasi hakuna ujanja tena.
John akishaona kitambulisho chake ndo basi tena anasahau kuhusu suala langu la kulala nje. Najua mada itageuka na yatazaliana maswali.
Umekitoa wapi? Ilikuwaje? Dah!! Siamini.
Kwisha mchezo!! Nilijiaminisha.
Sasa nilikuwa mbele ya John. Bado alikuwa kama anayefikiria kitu kabla ya kuzungumza. Nikamsubiri labda atasema kitu hakusema. Nikamuita akaitika kwa kichwa chake kutingishika.
“I hate…my country (naichukia nchi yangu).” Alisema huku akitazama mbele. Nikaurudisha mkono uliokuwa umekamata kile kitambulisho tayari kwa kumshangaza. Nikakirudisha katika sidiria ili nipishe kwanza anachotaka kusema John.
“Nini tena mpenzi wangu jamani.” Tayari nilikuwa ubavuni mwake wakati anayasema haya. Hakujibu upesi bali alicheka kwanza. Kicheko cha kujilazimisha.
“Eti kile kitambulisho….kile kitambulisho kile.” Alianza kuzungumza, nikafarijika kusikia mada ni juu ya kitambulisho na sio wivu wowote wa kimapenzi. Kisha akamalizia, “kile kitambulisho eti kimeibiwa ama kupotea katika mazingira ya kutatanisha. Serikali yetu bwana..haya sasa kuna haja gani ya kuipenda?” Alimalizia, bado alikuwa ametazama mbele tu. Akiyang’ata meno yake kukabiliana na pepo la hasira.
Mshtuko!! Nikatoa kelele ya kuogopa, lilikuwa yowe ambalo hata John aliyekuwa anatazama mbele lilimshtua akapata nafasi ya kuniangalia.
Nilikuwa wima!!! Mikono kichwani mara kiunoni, wakati mwingine najiziba uso. Mithili ya mwendawazimu.
John alidhani nasikitika kwa jinsi alivyonitazama lakini sikuwa katika kusikitika, nilikuwa naogopa sana. Kitambulisho kilichoibiwa si ndio hichi katikati ya maziwa yangu ama!!! La haula!!
Ndio hiki kitambulisho cha muuaji. Muuaji mwenyewe si ndio huyu mbele yangu. John ndiye muuaji anayejitafuta mwenyewe.
Mbiombio nikakimbilia chumbani. Sikujiamini tena kuwa mbele ya John. Sikuwa na uwezo wa kumueleza chochote juu ya kitambulisho chake. Kitambulisho kile kilikuwa na utata mkubwa.
Nilipokuwa natimua mbio kwenda chumbani, John naye nyuma akanifuata. Muuaji nyuma yangu, lengo langu nifike chumbani niwahi kujifungia mlango. Maziwa yakaruka kwa fujo wakati nakimbia, kitambulisho kikazidiwa ujanja kikakosa pa kujificha. Upesi kikachoropoka.
Kitambulisho haramu kikadondoka katika marumaru.
Nikasita kuendelea mbele. Sikutaka John akione kile kitambulisho.
Niliweza kusimama nikageuka. John huyo anakuja mbiombio. Macho ya John kwangu. Macho yangu katika kitambulisho kilichokuwa katika marumaru. Kila mmoja na wazo lake.
Kitambulisho sasa kikawa katikati yetu. John na moka zake modeli ya ‘wanchoma kumoyo’ akakikanyaga bila kutambua kile kitambulisho wakati ananikimbilia. Kitambulisho ni manira laini sana, kikaisikia kero ya kukanyagwa na bwana John. Zilikuwa zimebaki hatua moja na nusu niweze kukichukua ndipo nikakumbana na wakati mwingine matata ambao nisipousimulia utanilaumu mwisho wa simulizi. Mi sitaki lawama!!!
John akateleza, baada ya kukanyaga kile kitambulisho. Marumaru ikampokea kwa shangwe, kisogo kikatoa mlio kama chuma kilichogongana na chuma kingine. Kitambulisho kikaachana na kile kiatu kikawa mbele yangu.
Shida yangu ilikuwa kukiwahi kitambulisho. Sasa kitambulisho kimetulia na John ametulia tuli sakafuni.
Mamaaaa!!! Niliita tena, mama mwingine nani sasa zaidi ya mwalimu Nchimbi huko Makambako? Atanisikiaje sasa wakati nipo Mwanza. Ujinga!!
Nikimbie!!! Nilijiuliza huku nikitetemeka.
Kwenda wapi sasa?? Ujinga mwingine.
Mara damu nzito nyuma ya kisogo cha John. Macho yamefumbwa kistaarabu. Mdomo wazi.
Nikahisi kuchanganyikiwa sasa. Damu ikazidi kusambaa katika marumaru ile nyeupe.
“Atakufia huyu Isabella shtuka fanya kitu.” Sauti ikaniambia. Sasa hapo nikashtuka, nikainama nikakwapua kitambulisho chenye utata. Nikakimbia nje.
Taksiii!! Nikapiga kelele. Ikasimama, ikaanza kurudi nyuma. Macho ya dereva taksi badala ya kunitazama usoni na kunisikiliza shida yangu, yakawa yananitazama huku mapajani. Nilipojitazama, mbio nyingine mpya kurudi ndani. Nilikuwa nimevaa kinguo kifupi sana. Hakina tofauti na chupi. Kanga iliyokuwa inanisitiri ilikuwa imedondoka huko ndani.
Dereva teksi alinisubiri. Nikarejea nikiwa nimeegesha kanga kiunoni.
Nina mgonjwa!! Ni mume wangu. Ameanguka!!! Nilimsihi huku nikimvuta. Akanifuata. Tulipofika ndani bado John alikuwa ametulia tuli vilevile.
“Ameanguka!!.” Nilijibu bila kuulizwa. Dereva akafanya jitihada za kumnyanyua John. Wapi haikuwezekana. Kila aliposhikwa ili anyanyuliwe alilegea na kuangukia upande mwingine.
Mimi nilikuwa mtazamaji na nilikuwa namuogopa sana John.
“Hebu ngoja nakuja!!!.” Aliniaga dereva. Nikaamini anaenda kuleta msaada zaidi. Nikangoja kwa muda fulani dereva hakurudi!! Nilipotoka nje hapakuwa na dereva wala teksi.
Nilitamani kupiga kelele. Nikahaha huku na huko. Baada ya robo saa nikaona teksi. Ilikuwa inakuja pale kwangu. Iliposimama alikuwa ni yule dereva. Nyuma yake ikafuatia Ambulance.
Wakashuka wataalamu. Wakamtwaa John asiyejitambua.
Bahati nzuri walikuwa wananitambua. Ukarimu ukaongezeka maradufu.
John akafikishwa hospitali. Agha Khan.
Hakuwa amepasuka sana. Ulikuwa ni mpasuko wa kawaida. Akashonwa. Lakini akatakiwa kupumzika. Fahamu zilimrejea baadaye. Hakuwa msumbufu, alielewa upesi nini kinachoendelea.
Siku iliyofuata ndio siku ambayo John alitakiwa kutoka.
Nililazimika kurejea nyumbani kuchukua pesa kwa ajili ya malipo.
Nikiwa katika teksi, niliwaza juu ya kile kitambulisho. Nikahisi kitaniletea matatizo iwapo nitaendelea kukishikilia, tayari kilitaka kuutwaa uhai wa John. Sasa kitazua mengine.
Sasa nimpatie ama vipi? Nilijiuliza. Sikupata majibu.
Ile ndoto ya muuaji anadondosha kitambulisho ilikuwa inanikera maana haikutaka kufutika kabisa. Haikuwa ndoto kama ndoto nyingine maana sasa niliiona sura ya muuaji. Muuaji alikuwa John.
Nguvu ya penzi lake ikanikwamisha kumwambia mtu yeyote ukweli huu. Hata yeye pia sikumwambia.
“Hichi kitambulisho simpatii.” Niliamua kusimamia upande huo.