Monday, September 17, 2012

HATIA---03


Na George Iron


“Binti!!!...binti!!!! we dada….” Aliita huku akijaribu kumtikisa kidogokidogo, hakupata jawabu lolote lile. Funda la hasira likitiwa hamasa na uoga aliokuwa nao lilimkaba na kujikuta akijuta kumsaidia yule binti kulipa nauli na kujitambulisha mbele za watu kwamba anafahamiana naye. Uvumilivu ukamshinda mtoto wa kiume akajikuta anamwaga chozi, ilianzia hasira kumkaba kooni, mara macho yakawa mekundu, kisha machozi yakatoka halafu kikafuatia kilio cha kwikwi. Michael alilia sana kwa mtihani mkubwa uliokuwa mbele yake hakuelewa ni vipi anapata suluhu kwa sasa.
“Kaka…..kaka…..” sauti ya kike ilimshtua Michael kutoka katika kilio kikuu
“Mh!!! Aah!! Binti…..umekuwaje…”
“Nikuulize wewe….aaaaah!!! nimeteleza kutoka bafuni…kichwa kinaniuma jamani ah!” alilalamika kwa uchungu, Michael hakuamini macho yake kwamba binti alikuwa anazungumza huku akiwa amekaa kitako.
“Pole sana pole…..unaweza kusimama????” aliuliza
“Hapana kiuno kinauma sana sidhani kama naweza kusimama” jibu hilo lilirudisha mawazo upya kwa Michael lakini wakati huu hakuumia kama alivyoumia awali. Binti alijivutavuta kwa msaada wa Michael hadi akakaa kitandani kwa kujilaza maana hakuweza kukaa imara.
Baada ya muda binti alipitiwa na usingizi na kumpa fursa Michael kuwaza ni nini atafanya kuepuka hilo janga alilolivaa mwenyewe.
“Kesho sisafiri na huyu binti..wema wangu umetosha sasa, sibadili mawazo tena kama nilisema kuwa NIPO NAYE hilo neno nalifuta rasmi, mimi simjui bana!!!” alijichukulia maamuzi hayo kijana Michael.
Majira ya saa tatu usiku binti alikuwa ameamka tayari kutoka usingizini, kwa upande wa Michael bado alikuwa hajalala kwa sababu ya kuumiza kichwa juu ya uamuzi anaotaka kuuchukua.
“Umeamka??” Aliuliza swali ambalo alilitambua jibu lake
“Eeh!!!”
“Nikuletee chakula gani???”
“Maji kwanza halafu chakula nichagulie”
“Mh!! Wewe chagua bibie wala usiogope sawa eeh!!!” alijibu Michael
“Haya chipsi na mishkaki, tia pilipili, tomato, ukwaju, saladi, chumvi, na nini vile ndimu eeh!!” aliongea haraka haraka kwa utani Michael akajikuta anatoa tabasamu huku akisugua viganja vyake katika mkono wa yule binti. Bila kuaga alitoka nje na kurejea baada ya nusu saa akiwa na chakula na maji, akamsaidia binti aweze kukaa kisha akafungua chakula, kwa akili ya kujiongeza akaanza kumlisha yule binti, kila macho yao yalivyogongana Michael alikuwa wa kwanza kukwepesha, alikuwa ni mwanaume mwenye aibu sana mbele ya wanawake huo ni udhaifu uliokuwa wazi kwake. Walitumia saa moja zima kula chakula hadi kukimaliza, Michael licha ya kumwonea huruma binti lakini azma yake ya kumwacha pale gesti ilikuwa palepale.
“Michael wewe ni mwema sana asante sana kwa wema uliouonyesha kwangu…” sauti nyororo ya binti ilipenyeza katika masikio ya Michael..
“Sijui nikulipe nini lakini ubarikiwe sana, naomba kitu kimoja nikuombe na ninaamini utanielewa.”
“Kitu gani tena.”
“Waonaje kama ukiniacha hapa uendelee na shughuli zako mimi nimekuwa mzigo mkubwa sana kwako angali u kijana mdogo tu, naomba kesho unitoe nje na uniache barabarani hapo heri niwe ombaomba maana ndio maisha niliyoyachagua tofauti na kule nilipokuwa, nia yangu ya kuondoka kule imefanikiwa huo kwangu ni ushindi mkubwa sana…” aliendelea kuzungumza huku akijilazimisha kutabasamu.
Maneno ya yule binti yalimshtua sana Michael kwani alikuwa amepanga kumuacha kinyemela lakini anashangaa binti kwa hiari yake mwenyewe anaomba aachwe.
“Kwa nini unaongea maneno hayo dada yangu, mimi bado sijakuchoka.” alidanganya Michael
“Sijasema umenichoka wewe unadhani utaendelea kuwa namimi hadi lini na wapi???.” Swali hilo lilikuwa gumu sana kwa Michael kwani hakika jibu lake lilikuwa ni muda muafaka wa kumwacha yule binti.
“Usiumie sana kaka Michael….wewe ni mwanaume wa kipekee, Mungu atakulipa katika njia zako utakazoenda nitakukumbuka sana na siku moja utakutana tena na mimi nikiwa salama mimi sitakusahau na hata wewe ukiniona usisite kuniita kwa nguvu zote JOYCEEEEEEEEE!!!!!! Mimi nitageuka”
“Hah!! Kwani unaitwa nani wewe na huyo Joyce ni nani??.” Aliuliza Michael huku akiweka kiuno chake vizuri pale kitandani.
“Ooh!! Ulizoea kuniita binti mwone!! Naitwa Joyce mie” Alizungumza yule binti
“Unaitwa Joyce….we acha utani”
“Utani gani mie Joyce jina langu la kuzaliwa kwani vipi??”
“Kuna msichana mmoja anaitwa Joyce…”
“Vipi wifi yangu nini??.” alidakia Joyce
“Hapana alikuwa rafiki tu ndio maana nilishtuka kumbe na wewe ni Joyce…” alizungumza kwa uchangamfu mkubwa Michael.

Kwa maongezi yao ya usiku uliopita Michael alijikuta akivunja kwa mara nyingine tena makubaliano yake na moyo wake, kwa kuwa Joyce alikuwa na uwezo wa kutembea japo kwa shida sana Michael aliongozana naye kuelekea kituo cha mabasi wakiwa katika teksi iliyowafikisha haraka, Michael akamsaidia Joyce wakapanda ndani ya basi la Mombasa Raha katika siti za mbelembele na safari ya kuelekea Mwanza ikafuata. Ubora wa barabara hiyo ya kuelekea Mwanza ulimpa ahueni Joyce kwani hakutoneshwa kiuno chake.
“Nitakuacha Mwanza sawa.” ndilo neno la muafaka kati ya Joy na Michael waliloamua usiku uliopita. Safari ilionekana fupi sana kwa Michael kwani nafsi ilikuwa haijaridhika kumuacha njia panda Joyce ambaye kwa majina amefanana na binti aliyempenda wakati akiwa jijini Dar es salaam.
Saa tano asubuhi safari ya masaa mawili ilikuwa imefikia kikomo katika stendi ya Nyegezi jijini Mwanza. Si Michael wala Joyce aliyekuwa anaufahamu fika mji huu uliotawaliwa na milima ya hapa na pale hivyo kila mmoja alimtazama mwenzake.
“Tupeleke lodge yoyote iliyopo karibu na iwe nafuu kiasi.” alijieleza Michael kwa sauti ya chini mbele ya dereva.
“Poa..” alijibu dereva kisha Michael na Joyce wakapanda safari ya dakika kumi ikawafikisha mbele ya lodge iliyojulikana kwa jina la DOUBLE G, baada ya kupewa pesa yake akatokomea yule dereva.
“Chumba bei gani???...aah!! kwanza vyumba vipo??” Aliuliza Michael
“Vipo lakini subiri kidogo hebu…we nanii Dory, hivi chumba namba 18 kipo wazi au alilipia kulala yule bwana.” waliulizana wahudumu katika hali ya kunong’ona kisha likapatikana jibu kwamba kilikuwa wazi
“Chumba kipo elfu kumi si mnalala au ni show time kama ni show basi elfu tano!!”
“Hapana tunalala” Alisema Michael huku akitoa pesa mfukoni na kulipia chumba.
Hakuna aliyekuwa amechoshwa na safari lakini kutokana na kila mtu kuwaza la kwake walijikuta wakipitiwa na usingizi kila mmoja kwa wakati wake. Hadi saa moja usiku ndipo mkojo ulimwamsha Joy na yeye akamwamsha Michael.
“He!! Tumelala hivyo…..” Alijiuliza Michael wakati huo tayari Joy alikuwa ameingia msalani.
Aliporejea Michael yeye alikuwa amevaa viatu vyake na alikuwa na kila dalili ya kutaka kutoka.
“Wapi tena ndugu yangu jiji lenyewe hulijui tuachie sisi.” Alitania Joy
“Naenda kucheki benki kama mkopo umeingia si unajua tena…vipi twende wote”
“Mimi sitoki humu ndani usije ukanipoteza bure” alijibu Joy, Michael akajiondokea.
Dakika thelathini baadaye mlango uligongwa.
“Hebu ingia au unadhani umepotea” alijibu Joy na kweli kitasa kikashushwa wakaingia watu watatu waliojazia miili yao. Bunduki ndogo iliyowatangulia mkononi ilitosha kumnyamazisha Joy.

****

Michael alikuwa na furaha ya ajabu sana na alijiona ni mtu mwenye bahati kila mara, ndio alikuwa na bahati! Maana pale benki hapakumkatisha tamaa ila kumwongezea furaha tele, pesa ilikuwa imeingia katika akaunti yake pesa ya mkopo!
“Huyu Joy huyu ana miujiza yake na nikifika lazima nimwambie baraka anazoniletea.” alisema Michael bila watu wengine kujua alikuwa anaongea nini, alipovuka barabara kuelekea upande mwingine akili ilimrudisha tena upande aliokuwa lengo ni kununua hiki na kile kwa sababu ya safari ya kesho yake safari ya kuelekea Mugumu Serengeti, alinunua vitu kadhaa wakati huo akiwa na jeuri ya pesa mfukoni mwake.
“Joy, Joy, Joy…mh!! Ni msichana wa aina yake” alikiri Michael baada ya kufanya tathmini ya Joy akiwa si mgonjwa kama alivyo wakati huo.

Ni mrefu kama mnyarwanda, si mweupe sana lakini weusi wake unatosha kumwona gizani na kwenye mwanga, midomo yake ina majeraha lakini kama ikipona ni mtego tosha kwa mwanaume yeyote asiye na subira, kifua chake ambacho Michael aliweza kukiona bahati mbaya alipokuwa ameanguka kutoka bafuni kilikuwa na mzigo mdogo wa embe dodo ambazo hazikuwa na mpango wa kuanguka katika siku za karibuni, tabasamu lake la nadra liliruhusu vishimo vilivyojificha kuchomoza na kuzidi kuing’arisha nuru ya uso wake. Hiyo ni picha ambayo aliijenga Michael akiwa katika manunuzi ya hapa na pale, mawazo hayo yalimpeleka katika ushawishi, ushawishi nao ukachipua upesi akajikuta anashawishika, kishawishi cha kuondoka na Joy kuelekea Mugumu Serengeti mahali ambapo hajawahi kufika kabla.
“Nitaondoka naye…atapona mbele kwa mbele naamini atafurahi sana” Alisemezana na moyo wake huku akirejea kule alipomwacha Joyce.

* * *

Kaubaridi ka asubuhi asubuhi katika jiji la Mwanza maeneo ya Nyegezi karibu na chuo kikuu cha mtakatifu Augustino kaliwachochea wavutaji wengi wa sigara kununua pakiti kwa pakiti kukabiliana nayo huku wasiokuwa wavutaji wakipekua huku na huku kujua ni wapi waliyaacha masweta yao hapo ni baada ya kuingia hasara ya kununua miamvuli mipya kutokana na mvua iliyonyesha kuanzia alfajiri.
Kijiwe cha Bob Soya cha hapo Nyegezi kona kilikuwa na wadau wengi sana, wachache walikuwa na uwezo wa kununua kete za bangi huku wengi wakisubiri za ‘kugongea’ kwa wenzao. Ushikaji uliwekwa pembeni kutokana na hali halisi ya hewa, kila mmoja alitamani moshi mkali wa madawa hayo uendelee kupenyeza ndani ya mapafu yake kisha kutoka nje kupitia pua na mdomo wake. Pusha aliifurahia sana hali hiyo ya hewa kwani aliuza kwa wingi sana bidhaa zake. Mteja mmoja peke yake ndio alikuwa hazungumzi sana, yeye na bangi, bangi na yeye huku muda ukisogea.
Matusi makali makali yalizunguka eneo hilo ambalo lilikuwa jirani na nyumba ya kuishi watu. Matusi hayo mwishowe yakavunja amani iliyotawala kwa muda mrefu na kuzaa vita ndogo iliyosababishwa na ukosefu wa ustaarabu wa bwana mmoja aliyelazimisha kupewa kipisi cha bangi kwa ulazima huku akiwa hana pesa ya kukidhi hiyo haja yake. Ubabe wake uliwatetemesha wengi lakini leo alikuwa amempata kiboko yake.
“Mkishagombana ndio mtapata zawadi ya ‘ndumu’ ama!!!” alizungumza yule mzee ambaye alikuwa kimya muda wote akivuta bangi kistaarabu. Wote waligeuka kumwangalia kwa sekunde kadhaa kisha wakataka kumpuuza na kuendelea kushabikia ugomvi.
“Kaka, hebu wapatie idadi wanayotaka nitalipia” aliongea kwa jeuri akimtazama yule muuzaji. Amri hiyo ilipunguza makali ya ugomvi na kuuvunja kabisa, maadui wakawa marafiki na hasira kuwa vicheko. Huyu alikuwa ni mzee Robert Chacha, mfanyabiashara maarufu wa samaki katika jiji la Mwanza ambaye kutokana na kabila lake la kikurya isitoshe alikuwa mwanajeshi mstaafu alitokea kuwa maarufu kwa jina la ‘poti’. Ilikuwa mara yake ya kwanza kukifikia kijiwe hichi cha Bob Soya na hakuna aliyemtambua zaidi ya kujua kuwa ni mvuta bangi wa kawaida aliyezidiwa na baridi.

Ndio Poti alikuwa amezidiwa na baridi hilo halikuwa na ubishi, lakini jeuri yake ya kukivutisha kijiwe kizima ndio ilimshtua kila mtu.
“Shilingi ngapi jumla??” aliuliza Poti baada ya kila mmoja kuwa ameridhika na pia mzigo kumwishia muuzaji. Muuzaji alimtajia bei kwa uoga akidhani huenda ni bangi zilikuwa zimemchanganya huyu mzee na kujikuta anazungumza vitu asivyovijua lakini haikuwa hivyo, Poti alizama katika kibegi kidogo alichokuwanacho akakipekua kwa kubahatisha akachomoka na noti kadhaa zilizotosha kutibu njaa ya muuza.
“Hiyo nyingine tunza…” alikataa kupokea chenchi aliyorudishiwa, akafunga kibegi chake na kutoweka.
Alipoondoka nyuma aliacha gumzo huku kijiwe kikiwa kimesahau kuhusu ugomvi uliotaka kuibuka. Safari ya Poti ilikuwa haina uelekeo maalum ndio maana alijikuta akiishia katika nyumba ya kulala wageni ambayo alienda kwa minajiri ya kubadili nguo zake zilizolowana lakini kama bahati mbaya na nzuri kwake akamkuta msichana asiyekuwa na uelekeo ni huyo aliyemsindikiza chumbani kwenda kuwa jalala kwa muda, yaani kuuchukua uchafu wa Poti na kuuhifadhi.

Poti alipofika ndani aligundua hiyo haikuwa tabia yake labda huenda ni bangi aliyovuta imemchanganya, badala ya kumtumia yule msichana aliyetegemea ujira baada ya kazi alimshangaza alipomlipa na kumruhusu kuondoka. Baada ya yule changudoa kuondoka Poti alibadili nguo zake na kupitia mlango wa nyuma akatokomea.

Hicho kilikuwa chumba namba 18, chumba ambacho Michael na Joyce wake walikuwa wamekilipia kwa ajili ya hifadhi ya usiku mmoja bila kujua kama kilitumika siku hiyo hiyo.

TATIZO

Mdomo wa bunduki uliokuwa umemuelekea Joy pale kitandani haukuwa umekosea njia hata kidogo, walikuwa ni walewale wavuta bangi waliopewa ofa ya kuvuta bure, tayari walikuwa wameusahau wema wa Poti kuwatoa katika baridi bila gharama yoyote sasa wanataka kujua ana nini katika begi wakiamini ni halali yao, ama kweli kijiweni hakuna rafiki wa kweli!!. Poti hakuwa pale ndani tena, walikuwepo watu wasiokuwa na hatia yoyote.
“We Malaya yuko wapi bwana yako????” sauti nzito ilimuuliza Joy pale kitandani wakati huo alikuwa anatetemeka na kuyasahau maumivu yaliyokuwa yanamkabili.
“Sina….bwaaa..na!!!.” alijibu kwa kutetemeka sana Joyce. Kitako kimoja tu cha nguvu cha bunduki kiliiweka akili yake sawa
“Bwana yako yuko wapi malaya wewe!!!.” sauti hii ilikuwa kali kuliko ya kwanza Joy hakutaka kuleta ubishi.
“Ametoka kidogo….atarudi” alilazimika kujibu kwa hofu ya mtutu wa bunduki.
“Soya….tumsubirie…..atarudi huyo fala muda si mrefu..” walinong’onezana wao kwa wao, wakati huu walikuwa wameutoa ule mtutu wa bunduki jirani na Joyce lakini alikuwa anatetemeka sana. Baada ya dakika kumi zilisikika hatua zikijongea katika mlango wa chumba namba 18. Majambazi watatu walijibanza nyuma ya mlango huku mmoja akiingia uvunguni mwa kitanda. Mlango ukarudishiwa kidogo.
“Surpriiiiise!!!!!!!!” ukelele ulisikika kutokea nje ya mlango, ilikuwa sauti ya Michael ni Joy pekee aliyeitambua, moyo wake ukakata tamaa, alijua Michael alisubiri ajibu chochote. Laiti kama angejua kilichopo hapa ndani wallah!! Asingethubutu kuingia! Alijisemea Joyce huku Michael akiendelea kupiga kelele pale nje.
Joy hakujibu chochote kile kwani alikuwa na hofu juu ya wale watu wabaya waliokuwa chumbani hapo. Sura zao hazikuwa na mzaha hata kidogo walimaanisha walichokuwa wamekifuata hapo ndani. Taratiibu mlango ukaanza kufunguliwa kwa mguu kumaanisha kwamba kuna kitu mikono ilikuwa imebebwa hivyo kushindwa kutimiza wajibu huo.
Uso wa Michael ulikuwa umechanua kwa tabasamu murua, hakuwa amevaa zile nguo alizotokanazo nje. Wakati huu sasa aliweza kuyaonyesha maungo yake vyema, kifua kilichogawanyika katikati kutokana na mazoezi ya hapa na pale kilichomoza katika fulana iliyokuwa imembana hasa, suruali aina ya jinsi ilimchora miguu yake ilivyokuwa imara bila kuyumbishwa na matege ya aina yoyote kilikosekana kitu kimoja tu kukamilisha utanashati wa Michael, hakuwa akitabasamu! Ndio na hakupaswa kufanya hivyo maana Joy alikuwa ameyatumbua macho yake na kutokwa jasho kitu kibaya kilikuwa kimemtokea!! Taratibu bila kuzungumza chochote Michael ambaye alikuwa amesimama sasa mbele ya chumba hicho kimoja naye alimkazia macho Joy. Michael hakupaswa kusubiri kuambiwa akae chini, pigo moja tu katika mbavu zake lilimfanya ajikunje huku akitoa ukelele mdogo, akili ilikataa asikae chini lakini mwili bila ubishi ulilainika hatimaye akasalimu amri mbele ya Joy, mtutu wa bunduki ukafuata katika shingo yake, hofu ikaanza kutanda hofu ikamtawala na uoga.

ITAENDELEA















No comments:

Post a Comment

Recent Posts