HATIA --- 02
Na GEORGE IRON
Hospitali ya mkoa wa Shinyanga kwa ujumla haikuwa mbali sana kutoka
mahali basi hilo la Najimunisa lilipopatia hiyo tafrani, kwa maamuzi
yaliyoafikiwa na kila abiria yule binti walimzoazoa kutoka pale chini na
kumweka katika siti ya mbele ambayo ilikuwa na uwezo wa kupokea watu
watatu, hakuwa akitokwa na damu lakini alikuwa akigumia kwa sauti ya
chini sana, mwanamke mmoja alikaa pamoja naye kwa ajili ya kumsaidia
huku Michael naye akiwa karibu yake.
******
Hospitali ya mkoa wa Shinyanga ndio kwanza ilikuwa katika mgomo wa
madaktari wakitaka mwenzao aliyewekewa zengwe na kufukuzwa kazi baada
ya kushindwa kuokoa maisha ya mtoto wa Kigogo arejeshwe kazini hivyo
hakuna huduma zilizokuwa zikitolewa pale licha ya madaktari kuwepo eneo
hilo la Hospitali mjini Shinyanga. Kundi la wanaume wanne wakiwa
wamembeba mgonjwa wao liliingia kwa uharaka wa kuhitaji huduma pale
ndani, hakuna yeyote aliyewakaribisha zaidi ya ukarimu walioupata kwa
mlinzi pale mlangoni huku akiwaonea huruma, kila mtu alikuwa bize sana
na mambo yake binafsi yasiyoendana na mandhari ya hospitali.
“Nesi
nesi…” mwanamme moja aliita lakini alijibiwa kwa jicho kali kisha
mwanamama huyo akatoweka. Kwa ujasiri waliamua kujitafutia wodi mojawapo
na kumlaza yule binti kitandani kisha wakaanza kuhaha kuwatafuta
madaktari ambao hata hawakuonyesha kujali. Mwanzoni walikuwa wanaume
wanne pamoja na mwanadada asiyejitambua hata kidogo akiwa katika maumivu
makali sana ambayo hakuhitaji kujieleza mwenyewe bali jinsi alivyokuwa
ameuma meno na kuikunja sura yake lilikuwa jibu tosha, baada ya muda
wakabaki watatu, wawili na hatimaye mmoja Michael!! Ndio alikuwa Michael
peke yake pamoja na binti.
Nafsi ya Michael ikaingia katika
mgogoro mkali, mgogoro binafsi, maamuzi yalikuwa mengi lakini hakujua
lipi ni sahihi. Akiwa katika wimbi la mawazo alisikia anaguswa begani.
“Aah!! Kijana nimekutafuta kweli, ni zaidi ya saa zima sasa nilikuwa
napita hapa lakini sijui kwa nini hii wodi nilikuwa naivuka.” sauti
nzito kutokana na umri kwenda ilimweleza Michael ambaye alibaki kuduwaa
ilikuwa mara yake ya kwanza kufika katika mkoa huu uliotawaliwa na jamii
ya wasukuma halafu anatokea mtu anamfahamu.
“Mimi?.”
“Ndio wewe!!!.”
“Aaah!!! Eheee.” aliuliza Michael ili apate kujua shida ya yule mtu.
“Unawahi kusahau wewe, mimi ni yule mlinzi wa pale getini mwanangu
poleni sana baba!!!! Pole sana” alijieleza yule mlinzi. Michael hakuwa
na kumbukumbu kabisa kwamba pale kwenye basi walipofikia muafaka wa
kumwahisha binti hospitali watu walichangachanga walichonacho na
kufikisha shilingi laki mbili na nusu ambayo walimkabidhi, alipozipokea
mkononi ndivyo hivyo hivyo alizishika hadi waliposhuka na kumfikia
mlinzi wa geti, wakati anaandika jina lake katika kitabu cha orodha ya
wageni ndio wakati huo huo aliziachia zile pesa na kuzisahau, jambo jema
mlinzi huyu aliyejitambulisha kama mzee Matata aliona tukio hilo na
kuokoa pesa za Michael na sasa alikuwa amempata kwa ajili ya kumpatia.
Michael alishangazwa na uaminifu aliokuwa nao babu huyu wa makamo
mrefu, mwenye mwili uliojengeka na ndevu zake zilizokuwa na mvi kiasi,
“Kwa nini amenirejeshea hizi pesa??.” Alijiuliza Michael
“Asante sana mzee wangu asante sana.” Michael alijaribu kumpatia kiasi
fulani cha pesa lakini mzee Matata alikataa kabisa huku akimwonea huruma
Michael kwa hali aliyokuwa nayo.
“Ngoja niangalie kama utapata huduma walau ya kwanza maana huyu nani vile anaitwa??.”
“Aaah!!! Mhh!! Huyu?? Anaitwa nanii Mariam eeh!!! Mariam.” alijibu Michael kwa kujiumauma
Mzee Matata alipotoka Michael naye alifikiria kuondoka na kumwacha
binti peke yake, akili ilikuwa imemruhusu lakini wakati anapiga hatua
mlangoni aliisikia nafsi yake ikimtamkia neno ‘NIKO NAYE’ ambalo
alilitaja pale ndani ya basi, nafsi pia ilimsuta kwa pesa aliyorejeshewa
na mzee Matata, kwa kutoroka ilimaanisha kwamba amefanya dhulumati na
kuweka maisha ya binti katika hatihati. Michael alizishusha pumzi zake
kisha akarejea tena pale wodini kusubiria harakati za mzee Matata kama
zitazaa matunda.
******
Akiwa ni mtoto wa tatu wa mzee Akwino Msombe ni yeye pekee aliyejaaliwa
kielimu hadi hapo alipofikia, jina Michael Msombe lilikuwa maarufu sana
katika shule ya sekondari Musoma Technical alipomalizia kidato cha nne
kutokana na umahiri wake katika kucheza mpira wa miguu, jina hilo
likaendelea kupeta katika shule za Mara Secondary na baadaye Minaki
kutokana na ubora wa Michael katika suala zima la uhamasishaji wa
maendeleo na kuwa mshauri bora kwa wenzake hasahasa baada ya kufanya
jitihada kubwa na kuunda tawi la FEMA katika shule yake.
Katika
chuo kikuu cha Dar es salaam Michael hakuwa akicheza mpira tena lakini
aliendelea kuhamasisha hapa na pale lakini athari kubwa iliyopunguza
uwezo wake wa kutimiza wajibu ilikuwa ni jinsia ya kike ambayo kwa mara
ya kwanza alikuwa nayo karibu zaidi ya awali alipokuwa katika shule za
wanaume watupu. Wasichana hawakuchelewa kutambua kitu fulani katika
mwili wake, kijana aliyecheza mpira kwa kujituma miaka kadhaa iliyopita
mwili wake ukiwa umejengeka vyema, mrefu wa wastani na rangi yake maji
ya kunde ilimfanya aonekane mtanashati pindi anapochomekea shati lake la
mikono mirefu katika suruali yake iliyopigwa pasi vyema, anapovaa jeans
na fulana yake bado alionekana nadhifu, na hakuharibikia siku
aliyojisikia kuvaa pensi kwani mguu wake ulistahili kuonwa na watoto wa
kike.
Hayo yote yalisindikizwa na jicho hadimu sana ambalo
likimtazama mwanamke atajiuliza mara mbilimbili Michael anamaanisha
nini?? Maskini Michael wa watu hakuyajua hayo yeye alikuwa akihisi
huenda kizuri katika mwili wake ni kishimo kidogo (dimple) katika shavu
lake la kuume jambo alilojitambia tangu utotoni.
Akiwa na miaka 24
tu aliingia katika msukosuko wa kimapenzi wasichana wengi walimtamkia
kwa midomo yao kuwa anawatesa lakini alichukulia ni utani hadi siku moja
na yeye alipogundua kwamba anateswa. Ni siku ambayo alikutana na Joyce
msichana ambaye walicheza naye utotoni na kisha kusoma wote shule ya
msingi baada ya kumaliza shule ndipo rasmi wakapotezana baada ya Michael
kuchaguliwa kujiunga Musoma tech kwa ajili ya kuendelea na kidato cha
kwanza huku Joyce yeye akienda Nganza sekondari Mwanza.
Hapo chuoni
walikutana mgahawani wakati Michael ananawa na Joyce anatafuta meza ya
kukaa, ilikuwa ni furaha ya hali ya juu ambayo iliunda upya urafiki wao
wa utoto na kuufanya wa ukubwani, kwa Joyce ilionekana kama imetosha
lakini kwa Michael alitaka zaidi ya pale jambo lililomvuruga sana akili
yake. Siku ya kuzaliwa kwake alitamani ibadilike kwani bila hivyo
angeendelea kuumia miaka nenda miaka rudi.
“Kwanini Joy amenitenda hivi??.” alijiuliza kila siku.
*****
Baada ya kuamua kusubiri hadi kufikia kupitiwa na usingizi Michael
alikuja kushtuka binti hayupo kitandani, mbio mbio akatoka pale wodini
lakini hakujua hata ni wapi anaelekea. Madaktari wote walikuwa wamenuna
ni nani utamuuliza swali akupe jibu lililomaanisha ukweli, huku na huko
bila mafanikio hatimaye aliamua kumuuliza daktari mmoja nadhani jibu
alilopewa kama mtu akiwa katika hali ya kawaida anaweza kutenda dhambi.
“Samahani kaka si una namba yake huyo mgonjwa hebu mpigie umuulize yuko
wapi.” sauti ya kike ilimjibu Michael donge zito la hasira likambana,
ili kuliondoa akajisogeza ukutani akaruhusu machozi yamdondoke, alidhani
yatatoka kidogo lakini yalimwagika mengi huku kwikwi nayo ikichukua
nafasi yake.
“Nchi yangu Tanzania…yaani mimi nimpigie mgonjwa simu aaah!!!.” alilaumu huku akijigongagonga kifua chake.
*****
Kutoonekana kwa binti na majibu mabovu aliyopewa na yule nesi yalimtia
hasira sana Michael, ni mzee Msombe pekee aliyekuwa na uwezo wa
kumtambua Michael (mwanaye) wakati anakuwa na hasira na si mwingine,
Michael alitamani kumvaa yule nesi na kumchapa vibao lakini nafsi
ikamsihi awe mtulivu. Kama vile mwendawazimu ama mtu aliyepoteza kitu
cha thamani na sasa anakitafuta kwa udi na uvumba ndivyo ilivyokuwa kwa
Michael alizurura pande tofautitofauti hadi akakata tamaa na kukaa chini
bila kujua kama amekaa chini tena mbele ya mlango wa kuingilia chumba
cha upasuaji.
“Oya vipi wewe mbona umeziba njia??.” swali hilo ndilo
lilimshtua na kutoka pale mara moja, wakati anaondoka hakuacha kuangaza
huku na huko kama kuna uwezekano wa kumwona binti, pesa iliyokuwa
mfukoni mwake ndio iliyomnyima amani laiti kama asingekuwa na ile pesa
aliyochangiwa kwa ajili ya matibabu ya yule binti basi huenda angekuwa
ametokomea tayari, lakini hata kama asingekuwa na hiyo pesa kauli
iliyotoka katika kinywa chake bado ilimfunga ‘NIPO NAYE’…… “Hata!!!!
Huyu ni ndugu yangu siwezi kumuacha!!!!” alijikuta akisema kwa sauti ya
juu kijana huyu.
“Vipi tena mjukuu wangu mbona upo hapa??? Kwani
kuna mkeo hapa ndani amejifungua!!” alipokea swali hilo Michael huku
akijipatia jibu lake kwa kutazama maandishi yaliyoandikwa mlangoni ‘Wodi
ya wazazi’
“Aaaah!! Mzee ni wewe, simuoni mgonjwa wangu mzee wangu.” alikuwa ni yule mlinzi aliyeiokota pesa na kumpatia Michael
“Haaa!!!! Ina maana wakati tunamtoa pale wewe ulikuwa umelala, basi una usingizi mbaya.”
“Mlimtoa wapi?? Saa ngapi??...eeeh!! mzee wangu.” aliuliza kwa wasiwasi.
“Kumbe kweli ulikuwa unaota..yaani umetuambia kabisa tutangulie we tutakukuta mh!! Hebu tuachane na hayo…yule sijui mkeo ame…”
“Aaah!!! Babu si mke wangu yule bwana” alikanusha kwa aibu aibu Michael
“Yote sawa….kama nilivyokuhaidi nilimpata rafiki yangu mmoja hivi ni
Daktari alinisaidia tukambeba hadi katika chumba kimoja hapo juu
akampatia huduma ya kwanza kwa siri sana wenzake wasigundue……”
“Ana tatizo gani?? Amepona???” aliingilia kati Michael
“Tulia mjukuu wangu….yule binti ulisema sijui Maria eeh!!”
“Eeh!! Maria anaitwa Maria.”
“Tatizo alilonalo si kubwa sana lakini ni kubwa kwa upande mwingine…alishtuka kiuno”…(Michael akakunja uso kwa uchungu)
Mzee akaendelea.. “Ilibaki kidogo tu avunjike jumla lakini daktari
amejaribu na kukirudisha mahali pake..kinachotakiwa sasa ni mazoezi ili
azoee hiyo hali na kurejea kuwa mzima tena” alimaliza
“Sasa ina maana hayo mazoezi anafanya kwa siku ngapi…asante sana babu”
“Anafanya kwa siku kumi na nne kama asipokuwa mzembe anapona hata kwa siku kumi” alielekeza yule babu
“Yule sio mzembe mi namfahamu sana” alidanganya, kwani hata alikuwa
hajawahi kuzungumza naye huyo binti na kama hiyo haitoshi hata jina
alikuwa hamfahamu
“Haya sasa itambidi kesho afanye mazoezi
halafu…..mh!!! una sehemu ya kuishi hapa Shinyanga au upo gesti??” mzee
huyo mrefu mwenye lafudhi ya kisukuma alimuuliza Michael.
“Kwa kweli
mimi hapa ni mgeni sio siri nilikuwa naelekea naye Mwanza huko ndo nina
wenyeji babu” alijieleza kwa upole sana Michael.
“Hamna shaka
nitazungumza tena na daktari yule rafiki yangu aangalie uwezekano wa
kukupatia chumba mgonjwa awe anapumzika wewe utakuwa unalala gesti
nadhani itakusaidia”
“Yaani sana mzee wangu nashukuru kwa wema wako..”
“Usijali hata mimi nina wanangu wanasoma huko Arusha na Manyara,
nisipotenda wema kwa watoto kama nyie na wangu mimi nani atawatendea
wema???”
******
Joyce
alishikwa na butwaa kali sana, si kwa sababu alimwona Michael
alivyowafumania akiwa uchi wa mnyama na mwanaume mwingine ila ni kwa
jinsi Joyce alivyowahi kumueleza Michael wakati wapo chuoni kwamba
alikuwa akimchukia sana yule mwanaume ambaye leo hii amefumaniwa naye.
“Mama yangu!!! Nitauficha wapi uso wangu mimi na tunaenda kufanya kazi
sehemu moja dah!!!” alijiuliza bila kupata majibu. Hofu ilimtawala
akashindwa hata kupiga namba za simu za Michael kwa kuhofia kuzidi
kumkwaza.
Michael hakuwa na mahusiano ya kimapenzi na Joyce binti wa
miaka ishirini na nne mtoto wa mwisho wa mfanyabiashara ya mitumba
Stanley Keto, lakini ilikuwa kazi rahisi kuhisi watu hawa walikuwa na
mahusiano ni wao pekee walilijua jibu sahihi la fumbo hilo. Michael na
Joyce walikuwa wanatamaniana lakini hakuna aliyemuanza mwenzake, hali
hiyo ikamfanya Joyce aamini, kwa jinsi Michael alivyokuwa akiwavutia
wasichana basi lazima atakuwa na mahusiano na msichana flani hapo
chuoni.
Hisia zake hizo zikamsukumia na yeye kuamua kujivinjari na
mwanaume mwingine, kwa muda mrefu alikuwa hajamkubalia Victor Nicholaus
katika suala zima la tendo la ndoa lakini katika siku kuu ya kuzaliwa
Michael Msombe akajikuta amemruhusu kaka huyo kuutawala mwili wake na ni
katika siku hiyo Michael kwa macho yake anawafumania.
Joyce
alijua ni jinsi gani Michael aliumizwa na kitendo kile. Kosa kubwa
alilofanya ni kukaa kimya kwa siku mbili akiamini hasira za Michael
zitakuwa zimepoa, siku ya tatu Michael hakuwepo tena katika viunga vya
jiji la Dar es salaam na hakujua ni wapi alipoelekea nani
angemwelekeza!!!. Alivuta subira hadi muda wa kufanya field ulipofika
lakini hiyo haikuwa suluhisho Michael hakuonekana na simu yake haikuwa
ikipatikana.
“Atakuwa ameweka ile namba nyingine lakini nayo
sikuwahi kuichukua” hakuwa na ujanja mwingine Joyce kwani kwa marafiki
pote hapakuwa na jibu la kuridhisha
******
Siku tisa pekee zilitosha kwa binti kupona kabisa kiuno chake,
ilibaki michubuko kadhaa tu katika paji la uso na mikononi lakini
haikuwa na madhara makubwa sana.
“Mkeo ni jasiri sana!!!!” daktari
alimsifia Michael wakati anamuelezea jinsi yule binti waliyemtambua kwa
jina la Maria alivyopona upesi. Michael alicheka kwa kujilazimisha,
moyoni alikuwa anahofia kuhusu suala la pesa maana katika akaunti yake
pesa ya field ilikuwa haijaingia bado, na mfukoni alikuwa na shilingi
elfu hamsini pekee na alijua ni lazima amlipe yule daktari, kwa kuwa
alikuwa amezoeana na yule babu alimvuta pembeni kwa ishara kisha
akamueleza kuhusu hilo tatizo lakini hata kabla hajamaliza mzee
akaingilia kati
“Michael mjukuu wangu mimi nimekusaidia kwa vyote hivyo ile ishirini uliyotoa kwa ajili ya dawa imetosha sana….”
“Aah!! Babu kweli!!!”
“Ndio wewe usijali…vipi safari lini sasa au tuko pamoja bado…umeionaje Shinyanga kwanza”
“Shinyanga ni nzuri na mnaipendezesha wema kama nyie..kesho asubuhi nitadamka mapema na kuwahi gari za awali sana”
“Ukipita Shinyanga usikose kuja kunisalimia” baada ya maongezi ikiwa
saa sita mchana aliwaaga na kuwashukuru daktari na mzee Matata kisha
akamchukua yule binti na kuondoka naye kwa mwendo wa taratibu.
“Unajisikiaje??”
“Nafuu sana asante Michael”
“Nani amekwambia naitwa Michael”
“Mzee Matata na daktari..”
“Wamekudanganya!!”alijibu kwa ufupi Michael.
Saa moja usiku Michael na binti walikuwa chumbani Michael hakuwa
muongeaji sana licha ya binti kujisemesha kila mara, hata jina pekee
bado Michael alikuwa hajamuuliza. Tayari Michael alikuwa ameoga wakati
huo binti akiwa nje hadi alipomaliza kuvaa ndo akamruhusu na yeye aingie
kuoga wakati yeye (Michael) akatoka nje. Michael alitembea huku na huko
bila sababu ilimradi binti amalize kuoga na kuvaa wapate kulala.
“Nikirejea nampiga maswali kisha nampa nauli aende anapojua yeye.” Alijisemea wakati huo dakika ishirini zilikuwa zimepita.
“Mh!! Hamalizi tu kuoga wanawake nao.” akiwa ametoka dukani kumnunulia
binti mswaki alijisemea hivyo baada ya kuona kimya kikali kikiendelea.
Simu ya mkononi ya Michael iliita, kumbe alikuwa ameisahau ndani ya
chumba, hiyo ndiyo ilimlazimu kushusha kitasa chini na kuuruhusu mlango
ufunguke haraka haraka akaingia ndani. Almanusura apoteze fahamu
aliyatumbua macho yake, mdomo ukabaki wazi lakini sauti haikutoka,
baridi kali ikaukumba mwili wake, miguu ikaanza kuishiwa nguvu hakuamini
kilichokuwa kinatokea.
Alisahau kwamba ni mlio wa simu yake
uliomlazimu kurejea ndani bila kuruhusiwa na yule binti. Marumaru nyeupe
iliyokuwa chumbani hapo ilikuwa imechanganyikana na wekundu, mwili wa
binti ulikuwa uchi juu hadi maeneo ya mapajani, hakufanya maksudi kuwa
katika hali ile lakini alikuwa hajitambui tena.
Binti alikuwa
amezirai, Michael alibaki amezubaa asijue wapi pa kuanzia, hakuchelewa
sana kugundua chanzo baada ya akili yake kukaa sawa, binti alikuwa
ameteleza wakati anatoka bafuni na kuanguka chini vibaya, Michael
hakuweza kukisikia kishindo hicho kwani alikuwa ametoka mbali kidogo na
eneo la mlango wa kuingilia chumbani hapo.
“Binti!!!...binti!!!! we dada….” Aliita huku akijaribu kumtikisa kidogokidogo, hakupata jawabu lolote lile.
NINI KIMEMSIBU…..
Endelea nayo jumatatu ijayo
HII KILI
ReplyDelete