Na GEORGE IRON
Dakika tano ziliwatosha kumpekua Michael na
kufanikiwa kukutana na pesa kidogo tu kama shilingi elfu ishirini, badala ya
kufurahia kidogo kilichopatikana bila jasho lao walipandwa na hasira.
“Pesa zipo wapi????.” lilikuwa swali moja
zito sana kwa Michael hakufahamu hawa watu wamejuaje kuwa ameingiziwa pesa za
mkopo katika akaunti yake ndani ya dakika chache zilizopita.
“Nakuuliza wewe pesa ziko wapi????” hakuwa
na cha kujibu Michael, pigo jingine la nguvu katika mgongo wake, akajikunja kwa
uchungu kisha akajikunjua baada ya kugundua ameegemea sana katika mdomo ambao
risasi hupitia kwenye bunduki iliyokuwa jirani na shingo yake.
“Sina pesa mimi jamani ni mwanafunzi…..mimi
mwanafunzi jamani…” alijitetea wakati huo Joy yeye yupo kimya. Jibu hilo
lilikuwa karaha kwa watu hawa wabaya, waliendelea kumpiga Michael kwa awamu
huku kwa maksudi wakiwa wameifungulia luninga iliyokuwa hapo ndani sauti ya juu
hivyo mtu wa nje hakuweza kusikia kinachoendelea. Kadri jinsi Michael
alivyojitetea ndivyo majambazi hawa walianza kupatwa na wasiwasi huenda wanamuhukumu
mtu ambaye si sahihi
“Kocha….una uhakika ni chumba namba
18……mbona humu tumekuta mwanafunzi!!!.....” Mawasiliano hayo kidogo yakafufua
ndoto za Michael na Joy kupona dhidi ya watu hawa.
****
Jitihada za Joyce Keto jijini Dar es salaam
kumpata Michael hazikuzaa matunda, pale nyumbani alipokuwa akiishi Michael
walidai kuwa aliondoka ghafla na hawafahamu alipo japo si mara ya kwanza
kufanya hivyo. Rafiki zake Michael walimuelezea kwamba alikuwa katika hali ya
unyonge sana kabla ya kutoweka bila kuaga. Majibu hayo yalimtia mashaka sana
Joyce, aliogopa sana kuwaambia watu ukweli juu ya nini kilichotokea walipoonana
na Michael kwa mara ya mwisho.
Michael alikuwa amemfumania akiwa na
mwanaume mwingine!! Hilo ndilo jambo aliloamini kuwa limesababisha kutoweka kwa
Michael katika mazingira ya kutatanisha.
“Lakini mimi sikuwahi kuwa na uhusiano na
Michael licha ya watu wengi sana kuhisi mimi na yeye ni wapenzi.” aliwaza na
kuwazua Joyce Keto. Ina maana alichukulia serious watu walipotuita wapendanao!!
Alijiuliza. Aliogopa sana kumshirikisha mtu yeyote juu ya uhusiano wa kutoweka
kwa Michael na tukio la kufumaniwa kwake. Kichwa kilimuuma sana kila
alipojaribu kumpigia simu Michael na kuendelea kupata jibu lile lile kwamba
namba anayopiga haipatikani.
“Kama amejiua je???.” ghafla wazo hilo
liliiteka akili ya Joyce. Mh!! Mtihani!! Alihitimisha mawazo yake kwa kupanda
gari na kuelekea chuoni, foleni kubwa barabarani ilimtia hasira. “ah!! Elfu
tatu kitu gani bwana.” alijisemea huku akiomba kushuka kisha akakwea bajaji, ghadhabu
yake ikapungua kidogo kutokana na kupata hewa ya kutosha. Dakika kadhaa
zilitoweka Bajaji ikawasili katika viunga vya chuo. Joyce akashuka na kulipa
pesa, kisha hatua kwa hatua akajikongoja taratibu hadi mbele ya ofisi alizokuwa
amepanga kwenda.
“Nimejaza namba ya simu ambayo si
sahihi!!.” alijieleza Joyce mbele ya mkuu wa kitengo hicho.
“Bwana eeh!! Mmezidi na nyie haya chukua
uangalie mwenyewe wino wa kufutia huo hapo utajirekebishia, yaani watu wazima
tunakuwa kama shule ya chekechea ah!!!” alizungumza kwa hasira mwanamke
aliyekuwa katika kitengo hicho. Kwa Joyce huo ulikuwa ushindi mkubwa sana, ni
jambo lililompeleka.
“Huku wasichana huko wavulana” maelezo
tosha kabisa kwa Joyce. Haraka haraka alianza kupekua katika majina ya wanaume
1…2….3….4….5…..alizihesabu namba hadi akafikia thelathini na tatu ‘Michael
Msombe’!! moyo ulimpasuka na kumuongezea hamu ya kujua kilichoandikwa mbele
yake, Mugumu Serengeti!! Ndio wapi sasa huku!!! Alijiuliza Joyce huku akirudia
mara mbilimbili kulisoma jina hilo bila dalili yoyote ya kuliweka akilini mwake
ipasavyo.
Mkoa wa Mara!! Msamiati mwingine tena. Ili
kuhifadhi kumbukumbu hiyo aliamua kuitumia simu yake kuandika kila alichoona ni
kigumu kumeza kwa haraka haraka.
“Michael ameenda wapi huku…hivi ni
Tanzania…” alijiuliza Joyce.
“Hivi wewe, mbona mzembe hivyo humalizi
tu!! Unaboa bwana.” alilaumu yule mama aliyempa Joyce faili kwa ajili ya
kufanya marekebisho.
“Ah!! Samahani na ikiwa unataka kuhamishwa
sehemu ya kufanya field unafuata process gani???” badala ya kujibu aliuliza
swali jingine Joyce na kumtia hasira yule mama.
“Hebu nipishe hapa ushanitia hasira….toka
toka toka…tafadhali!” Joyce hakutaka shari huyoo akajiondokea, aliona nyumbani
ni mbali sana akiwa ndani ya daladala alifungua simu yake katika sehemu ya
internet akaenda google kisha akatafuta google map na kuandika Mugumu
Serengeti, ilichukua sekunde kadhaa kutoa jawabu kwamba haikufanikiwa kupakua
(load).
Simu ya Joy haikuwa na salio la kutosha.
Kompyuta yake ndogo nyumbani ilitumia sekunde chache ikaleta majibu ya
kuridhisha.
“Michael ndo ameenda huku kweli ama
amelaghai pale ili nisifahamu alipoelekea??” kabla hajapata jawabu simu yake ya
mkononi iliita, ilikuwa namba mpya kwake.
“Haloo!!.” aliita
“Haujambo mwanangu!!!.”
“Sijambo, nani??” aliuliza Joyce
“Mama yake Michael….” Moyo ulimpasuka Joyce
kama vile amepigwa shoti ya umeme alitulia tuli
“Shikamoo mama….shikamoo.”
“Marahaba Joy, za siku nyingi mwanangu??”
“Ni nzuri mama, sijui nyie.”
“Sisi wazima kidogo, lakini huyo mwenzako
hata kwenye simu hatumpati kulikoni.” aliuliza mama yake na Michael kwa sauti
iliyosawazika.Kimya kilidumu kwa sekunde kisha Joyce naye akaelezea kutompata
kwake hewani.
“Nadhani yatakuwa matatizo ya simu yake,
nitaenda kwake kumuarifu kuwa unamtafuta” alisema tu kumridhisha mama huyo
lakini ukweli ni kwamba Michael hakuwepo. Kwa jinsi Michael alivyomueleza Joyce
juu ya uhusiano wake mzuri na mama yake tangu akiwa mtoto mdogo aliyetelekezwa
na baba yake mzazi, Joyce aligundua kuna tatizo linataka kuibuka tena tatizo
kubwa sana.
“Lazima nifanye kitu mimi ndiye chanzo cha
haya yote.” alijishauri.
“Hivi kwani alinitambulishaje kwa mama
yake!!!!.....nipo hatiani Joyce mimi”
BAADA YA SIKU TATU
Joyce Keto kwa ujasiri wa hali ya juu baada
ya kuwa amemaliza hatua zote za kuhama sehemu ya kufanyia field na kuwa
Serengeti Mugumu, alikuwa ndani ya gari akielekea katika mkoa asioufahamu hata
kidogo, lengo likiwa kujitoa katika kitanzi cha hatia inayomkabili. Mama yake
Michael ndiye alimuumiza sana kwani Michael alikuwa ndiye mtoto wake wa pekee
aliyezaa na mzee Msombe kabla ya kutelekezwa na kisha mzee Msombe naye kupotea
ghafla katika mazingira ya kutatanisha. Michael ndiye faraja pekee iliyokuwa
imebaki katika dunia ya mama yake.
Kama amekufa itakuwaje!! Eeh!! Mungu
muepushe!! Aliomba Joyce wakati safari inaendelea.
****
Matumaini waliyoyapata Joy na Michael kuwa
huenda wale watu watawaacha kwa kugundua si watu sahihi hayakuwa sawa hata
kidogo, kwani waliendelea kuulizwa maswali ambayo majibu yake yalikuwa magumu
mno. Baada ya Michael kubanwa maswali huku akipokea kipigo hatimaye
aliwakubalia kwamba ana pesa kiasi lakini katika akaunti yake.
“Tunaongozana hadi hapo ATM, ole wako upige
kelele aina yoyote ile mara moja nausambaza ubongo wako na wewe kuku hapo
kitandani tulia hivyo hivyo nadhani unajua madhara ya kupiga kelele.” alifoka
jambazi mmoja huku akimalizana na Michael na kumgeukia Joy.
“Weziiiiii……weziiiiiiiii..tusaidieniiiiii”
Joy alipiga kelele ghafla baada ya umeme kuwa umekatika na kusababisha ukimya
pale ndani, sauti yake ilimshtua kila mtu hata Michael alishindwa kuelewa ni
wapi Joy ameutoa ujasiri huu, baada ya hizo kelele kimya kikuu kilifuata baada
ya mshindo kusikika.
****
Kituo kikuu cha polisi Mwanza, chumba cha
mahabusu kilikuwa kimejaa sana lakini bado wengine waliendelea kuongezwa,
kelele za mahabusu hazikuwakera polisi waliozidi kutoa amri kwa watuhumiwa
waliokamatwa kuvua mkanda, saa, viatu na kuingia mahabusu. Majira ya saa mbili
usiku aliingizwa mtuhumiwa mwingine
“Mapulu!!! Mpeleke chooni huyo” sauti kali
ya afande iliamuru. Mapulu alikuwa ni mahabusu aliyekaa siku nyingi sana katika
kituo hicho, alikuwa na muda wa mwezi mzima hivyo alikuwa ni mzoefu sana na
alitokea kuitwa ‘faza hausi’, huyo ndiye aliyewapokea mahabusu wapya na
alizifahamu taratibu zote za hapo ndani. Alikuwa ni mjelajela kweli kwani
haikuwa mara yake kufungwa na kuhusu kutiwa mahabusu ilikuwa ni kama kamchezo
flani hivi hakuwa na hofu.
Mahabusu aliyeingia alikuwa akilia kama
mtoto mdogo licha ya umbo lake kuonyesha ujasiri wa hali ya juu.
“Pumbavu!! Unamlilia nani hapa unadhani kwa
mamako hapa, kuja huku nikupe chumba!!!” John Mapulu alimkaripia huyo mgeni
huku akimzaba kibao katika mgongo wake, Mapulu alipokelewa na mahabusu wengine
waliogundua kwamba huyo mgeni alikuwa dhaifu sana na ilikuwa mara yake ya
kwanza kuingia mahabusu.
Moja kwa moja alipelekwa bila kupinga
katika mlango wa choo, harufu iliyompokea kuanzia mbali alitamani sana ardhi
ifunguke ajitie humo ndani milele lakini hiyo ilikuwa ndoto ya linacha.
“Umefanya nini mpaka umeletwa hapa ndani??”
aliulizwa
“Sijui hata!!!.” alijibu
“Hujui!!! Kwa hiyo wamekuchukua tu…au huna
sehemu ya kulala wamekupa hifadhi kwa leo???.” aliulizwa tena kwa kuzodolewa.
Hakujibu kitu!.
Hakika ilikuwa mara yake ya kwanza kuingia
katika sehemu hiyo lazima ajisikie mpweke. Usingizi hakujua ataupatia wapi
kutokana na ile harufu lakini alishangaa alipoamshwa asubuhi kwa kukanyagwa
kanyagwa na watu waliokuwa wakielekea chooni, usingizi ulimpitia bila kujua.
“Amka usafishe choo!!!!” aliamriwa na
kijana ambaye laiti kama wangekuwa nje ya selo hiyo angeweza kumuita ‘dogo’
lakini nyuma ya chuma hizo hakuwa na ujanja alisimama na kufanya kama
alivyoelekezwa mwili mzima ulikuwa unanuka!!
“Michael msombe!!!” sauti ya afande iliita,
lilikuwa jina geni pale ndani kila mtu akaanza kumuangalia mwenzake.
“Michael!!” ilirudia sauti ile kwa ukali
“Naam!!!!” ilisikika sauti kutokea chooni
“John!! We mtu mbaya sana kumbe umemlaza
chooni kweli” afande alisema kwa utani baada ya kumsikia aliyemuita akiita
kutokea chooni.
Suruali yake ya jinsi ilikuwa inamtelemka
kutokana na kukosa mkanda wa kuikamata, macho yake yalikuwa yamevimba kwa
kutokwa machozi sana huyu alikuwa ni Michael Msombe.
Si kweli kwamba hakujua kwanini yuko pale
ila ni uoga tu wa kuingia selo kwa mara ya kwanza ulimtetemesha. Michael
alikuwa anatuhumiwa kwa kesi ya mauaji ya mtoto wa kike katika guest ya Double
G jijini Mwanza. Kesi ambayo kwa asilimia kubwa haikuwa na ushahidi wa kumfunga
lakini alikuwa ndani kwa ajili ya upelelezi, hakuwepo mtu anayemshtaki Michael
tofauti na jamuhuri ya muungano ya Tanzania.
“Huna ndugu yako umpigie aje akuwekee
dhamana??” aliulizwa Michael baada ya kulifikia geti la chuma lililokuwa
limefungwa imara.
“Nilikuwa nasafiri!!!.”
“Pumbavu, sijakuuliza kama ulikuwa
unasafiri ama la..nimekuuliza una ndugu we fala nini??” alifoka askari, Michael
akakosa cha kusema.
“Mpuuzi wewe, nakuuliza unadengua unadhani
mi nakutongoza au??? Haya utaozea humu ndani” maneno hayo ya afande
yaliugalagaza vibaya moyo wa Michael, hakuwa na hatia lakini alinyanyasika.
Michael alikuwa ameikariri vizuri namba ya mama yake mzazi lakini aliamini kuwa
kwa kuruhusu mama yake apigiwe simu ilikuwa ni tiketi sahihi ya kumruhusu mama
huyo mjane aitenge roho yake na dunia hii, mara chache sana Michael aliacha
kujutia kitendo cha kumsaidia Joyce katika safari waliyokutana, Joy ameharibu
mipango yangu yote!! Aliwaza lakini akayapinga mawazo yake baada ya kukumbuka
huyo Joy anayemzungumzia yeye sasa ni marehemu si hai tena
“0717..7….3…76..12” aliitaja namba hiyo kwa
askari wa zamu ambaye kidogo alikuwa mstaarabu.
“Haya nitampigia….”
“Tafadhali mwambie asimwambie mama” afande
hakujibu akajiondokea. Zilikuwa ni siku tatu tangu atiwe selo, hata siku moja
hakuwahi kupelekwa mahakamani kisa ushahidi haujakamilika.
Mazingira ya selo yalikuwa magumu sana
kuzoeleka kwa upande wake, japo alikuwa ameanza kupata marafiki ambao walikuwa
wakimkaribisha chakula aliamini hapo si mahali sahihi kwake yeye, bado elimu
yake ilimtia ushawishi kwamba watu wenye elimu hawatakiwi mahali pale.
“Mbona sasa hawa wasio na elimu
wameninyanyasa, lakini hata sikuulizwa nina elimu gani wakati naingizwa hapa
ndani, kweli wanajali elimu hapa!!!! Hapana sidhani” alipata jawabu na kuanzia
siku hiyo akaifuta dhana hiyo. Siku ikapita bila kumwona tena yule afande, wakati
huu alikuwa halali tena kule chooni bali walilala wale wageni.
Zilikuwa zimepita siku sita tangu Michael
aingizwe pale ndani, walikuwa wanaingia wengine na kutoka lakini yeye hakuwahi
kuja kutembelewa na ndugu yeyote yule. Ilifikia wakati baada ya John Mapulu ni
yeye aliyekuwa anafuata kwa uzoefu pale ndani.
“Hivi wewe huna ndugu!!!” John alimuuliza
Michael siku hiyo wakiwa wanakula ugali na maharage ulioletwa kwa ajili ya
mahabusu.
“Ninao ila wako mbali.”
“Huwa namsikia afande anasema uliua, je ni
kweli??.”
“Hapana kaka sikuua ila, kuna binti
nilikuwa naye……” Michael alisimulia kila kitu jinsi alivyokutana na Joyce
katika basi, maswahibu waliyoyapata Shinyanga na makubwa zaidi yaliyochukua
uhai wa Joy hapo Mwanza. Michael alielezea kitendo cha Joy kupiga kelele
kilivyowatia hasira majambazi na kufikia hatua ya kumpiga hadi kumuua.
“Wewe sasa umekamatwaje??.”
“Baada ya Joy kuwa ameuwawa niliwataarifu
mapokezi, wao wakapiga simu polisi. Polisi walichelewa kuja lakini baadaye
walikuja, walimchunguza Joy kwa macho kisha wakamwacha kama alivyo, kesho yake
walikuja na daktari akamfanyia uchunguzi sijui alitoa majibu gani, baada ya
siku mbili nikiwa mtaani nilipigiwa simu na watu nisiowafahamu….”
“Ukawaeleza ulipo wakaja kukukamata…”
alimalizia John kuonyesha kwamba anayajua sana mambo hayo.
“Ni kweli na walinikamata kwa shari sana,
walinipiga na kunitia pingu.” alimalizia Michael.
“Ulifanya kosa kubwa sana kuwasubiri, baada
ya tukio usingebaki…hawana dogo hawa wanapenda sana………mh!!! Umeandikisha
shilingi ngapi katika PPR yako??”
“PPR?? Ndo nini.” aliuliza Michael
“Kikaratasi kilichoandikwa vitu ulivyoacha
hapo kaunta”
“Aah!! Elfu tatu”
“Elfu tatu?? Hawakuachii hawa” alihamaki
Mapulu. Michael akasononeka waziwazi na kukata tamaa. John akainuka na kuelekea
katika chumba kingine.
*****
ITAENDELEA
No comments:
Post a Comment