Na George Iron ( Ubunifu Wetu)
Safari nzima hakutaka kuzungumza na mtu yeyote hivyo alikuwa amepachika ‘earphone’ masikioni mwake ili hata asiweze kusikiliza watu walikuwa wanazungumza nini mara chache sana alipata nafasi ya kusikia mawili matatu hasahasa pale wimbo ulipokuwa unaisha na kuachia nafasi ya wimbo mwingine kuingia, katika kibegi chake kidogo alikuwa na takribani betri nne zilizokuwa zimechajiwa usiku uliopita ili asipatwe na usumbufu wa kuzimikiwa simu katika safari yake hiyo ndefu kiasi ya kuelekea wilayani Serengeti mkoa wa Mara. “Hivi wazazi wangu ni wendawazimu…sas a waliniita Michael ili iweje kwa nini hawakuniita hata Masumbuko???.” Alijiuliza kijana huyu mrefu wa wastani ambaye umbo lake kwa kumtazama ungemkadiria kuwa na miaka ipatayo thelathini lakini kiukweli ndio kwanza siku tatu zilizopita alikuwa ametoka kusheherekea kutimiza miaka ishirini na tano siku ambayo ilianza vizuri sana asubuhi kwa kupokea jumbe tofautitofauti kutoka kwa ndugu jamaa na marafiki waliokuwa wanaikumbuka tarehe hiyo.
Karibia kila mmoja alimtakia heri na fanaka katika maisha yake, huku wakikumbuka pia kumtakia aishi miaka mingi. “Joyce atakuwa ameisahau hii siku au kuna tatizo jingine??.” Michael alijiuliza baada ya kutouona ujumbe wake kati ya jumbe zote alizopokea. Kwa kuwa Joyce hakuwa akikaa mbali sana na mtaa anaoishi Michael jijini Dar es salaam, basi Michael alitumia fursa hii kwenda kumpa surprise rafiki yake huyo wa kike tangu utotoni japo hawakuwahi kuvuka urafiki na kuwa wapenzi lakini ndipo walikuwa wanaelekea. Michael alikuwa anatabasamu njia nzima, kwani aliamini kuwa ile hali tu ya kumkumbusha Joyce tukio hili ni lazima atamrukia na kumkumbatia, kitendo ambacho kwa Michael ni zaidi ya zawadi, lile joto la kipekee la binti huyo lingeweza kumchangamsha na kujisikia kweli amezaliwa siku hiyo.
Utajuaje, huenda pia atanibusu?? Alijisemea Michael kisha akafanya kicheko kidogo cha kujilazimisha. Kisha akatikisa kichwa kama vile kuna jambo alikuwa analikataa. Sasa alikuwa ameufikia mlango. Akalazimika kunyata ili amshtue Joyce, na hatimaye apokee lile kumbatizi maridhawa. Alichokikuta Michael nyumbani kwa akina Joyce ndicho kilibadili ghafla mipango yake ya kufanyia mazoezi ya vitendo (field) katika jiji la Dar es salaam na kuamua kuelekea mji mdogo wa Mugumu Serengeti mkoa wa Mara bila kutarajia. Hakujua kwa nini ameuchagua mji huo lakini alijikuta katika maamuzi hayo. “Lakini kwani nilikuwa nimemtamkia kuwa nampenda?...mim i ni mpuuzi huenda labda ndio maana hakushtuka nilipomkuta.” Alijiuliza Michael huku akijaribu kunywa maji ili kulegeza donge la hasira lililokuwa limemkaba kooni . “Hivi ninachokasirika ni nini hasa wakati hajui kama nilikuwa namtaka?...ah!! huu ni upuuzi hakika.” Alijiliwaza Michael huku akishindwa kuyanywa yale maji na kuyafunika kisha kuendelea kupata burudani ya muziki baada ya muda alipitiwa na usingizi alikuja kushtuka baada ya mwanamama aliyekuwa pembeni yake kumlaumu kuwa alikuwa anamlalia kila anaposinzia. “Unasema??.” Aliuliza kwa sauti ya juu Michael baada ya kuwa ameathiriwa na sauti kali ya muziki masikioni. “Unanilalia bwana!!!.” “Ah!! Samahani…” Wakati huu alikuwa ameondoa ‘earphone’ masikioni mwake.
Safari ilikuwa inaendelea, safari ya kutoka jijini Dar es salaam kuelekea Mwanza kisha mkoa wa Mara. Hii ndio ilikuwa mipango yake. Mipango ya kukimbia maumivu. Baada ya kuomba radhi alitaka kurejesha tena earphone masikioni lakini alisita kidogo baada ya kuvutiwa na vurumai iliyokuwa inaendelea kati ya makondakta wa hilo basi na mwanadada, kisa kilikuwa ni kukosa nauli kwa huyo dada huku akidai kuna mtu anamlipia yuko nyuma. “We mbona unasema kuwa kuna mtu analipa na sisi hatumuoni… nenda ukamguse basi mwambie alipe, yaani wewe umepandia njiani halafu unasema kuna mtu anakulipia, acha kutuzingua basi na ujanja wa kizamani.” Kondakta mmoja alibwatuka kwa ghadhabu akionyesha dhahiri kukerwa na maneno ya yule dada aliyekuwa hajakaa kisafari ndefu kabisa. “Ebwana anayemlipia huyu dada yuko wapi?? Sisi tunamshusha hivyo.” alitangaza kondakta lakini hakuna aliyejitokeza kubeba mzigo huo. “Mi sishukiiiii…sis huki, niacheni, niache hukooo, sitaki kushukaa.” Alilia yule dada kwa sauti ya juu huku akiwa ameng’ang’ania mkono wa yule kondakta hapo ni baada ya gari kuwa limesimama ili ashushwe. Kila mtu alikuwa na shughuli zake hakuna aliyejishughuli sha na sakata hili kwa asilimia kubwa. Waliojaribu kujishughulisha walikuwa wakitabasamu ama kucheka huku wengine wakiongea sauti za chinichini. Haikujulikana wapo upande upi.
Michael alikuwa bado anaangalia hilo vurumai linavyoendelea, kitendo cha huyo dada kilimkumbusha adha ya usafiri katika jiji alilokuwa ametoka la Dar es salaam lakini kikubwa zaidi ni umasikini unaotawala sehemu kubwa ya Tanzania, lakini kilichomuumiza ni unyanyasaji wa wanawake katika jamii jambo ambalo alikuwa analipinga na hadi kufikia kusomea masuala ya sheria na haki za binadamu akiwa mwaka wa pili katika chuo kikuu cha Dar es salaam na sasa alikuwa anaelekea katika field. Alikumbuka jinsi alivyokuwa anajisikia vibaya iwapo mzee wake anatokea kumnyanyasa mama yake. Ile hali ikajirudia tena baada ya sakata hili. Moyo ukamuuma!!! “Nipo naye huyo!!!.” Alitamka kwa sauti kuu Michael. Hakujua maneno haya aliyatoa wapi lakini aliyatamka kiufasaha na kusikiwa na kila abiria ndani ya basi hilo la Najimunisa wakati huo tayari tairi sita za basi hilo zilikuwa katika ardhi ya Dodoma. Watu wote waligeuka kumtazama kwa mshangao huku kondakta akitaharuki na uso wake haukutabasamu bali ulipambwa na ndita zilizomaanisha hasira. “Sasa muda wote huo ulikuwa wapi kujibu mbona mnaleta ujanja wa kishamba hapa..sasa ulitegemea nitamuacha huyu malaya wako asafiri bure au, acha hizo jombaaa!! Mbona tunatafutiana sababu za kutukana halafu mwishowe mnasema makonda wana matusi.” Kondakta ambaye kimabavu alimzidi Michael alitoa karipio. “Nauli ni shilingi ngapi??.” Badala ya kujibu lawama za yule Kondakta Michael kwa kujiamini kabisa aliuliza swali bila wasiwasi. Ilikuwa ni kama hakumsikia kipindi anabwatuka. “Sio ishu hizo kaka…nigei elfu ishirini na tisa hiyo.” Alijibiwa kwa jazba. Taratibu alijipekua na kutoa noti tatu za elfu kumi kumi akampatia akarudishiwa elfu moja. “Kakae kule nyuma na jamaa yako nafasi inatosha ile pale.” Alielekezwa yule binti ambaye bado machozi yalikuwa yanamtiririka mashavuni na kudondoka chini.
Kwa kusuasua alienda na kujibanabana pembeni ya Michael wakati huo gari zima lilikuwa linaitazama filamu hii tamu ya kusisimua. Binti alipofika pale tayari Michael alikuwa amerejesha ‘earphone’ masikioni mwake na wala hakumjibu alipotoa shukrani ya msaada huo. “Mh!! Wanaume wanajua kutesa wanawake da!! Sasa hapo wamegombana nyumbani anauleta ugomvi wao kwenye usafiri ah!!! Ujinga kweli huu.” Alisikika abiria mmoja mwanamke wa makamo akilalamika lawama ambazo hazikupenya katika masikio ya Michael. “Pole dadangu!!!.” mwanaume mwingine upande wa kulia alimwambia yule binti naye akamjibu kwa kichwa. Michael hakuwa na habari kabisa, japo aliamini kuwa mengi tu yalikuwa yanazungumzwa juu yake.
Safari iliendelea kama kawaida hadi liliposimama kwa dakika kumi katika hoteli moja kubwa ya kisasa kwa ajili ya abiria kujipatia chochote kitu katika matumbo tayari kwa kuendelea na safari iliyobakia. “Twende.” Michael alimwambia yule binti naye akafuata kwa nyuma hadi walipofika mgahawa mmoja ambapo binti alichukua chipsi kavu na juisi. “Muwekee na kuku robo.” Aliamuru Michael bila kumuuliza kama huwa anatumia kuku ama la, muhudumu alifanya kama alivyoagizwa. “Mimi naomba maji hayo ya Kilimanjaro makubwa.” Aliongezea Michael kisha baada ya kupewa huduma wakatoweka na kurejea ndani ya gari ambalo tayari lilikuwa limeanza kupiga honi ya kuwaita abiria. Michael na huyo binti walikuwa wa mwisho kuingia kila mtu aliwatazama, Michael alijua hilo na wala hakujali. Safari ilianza tena huku binti pamoja na abiria wengine wakipata haki za matumbo yao kwa chati tofautitofauti. Michael alikuwa anatafuna big G huku akinywa na yale maji taratibu. Ilionekana dhahiri kwamba yule binti alikuwa na njaa kali kutokana na mwendo wake katika kula ambao ulimpelekea kukwamwa na chakula. Michael aliliona hilo na bila kusita akampatia maji huku akimgonga gonga mgongoni. “He he heeeeee!!!! Wagombanaooooo. ” Wanawake waliokuwa wakifatilia tukio hili walijikuta wanacheka kwa pamoja Michael aliwaangalia mara moja na kuendelea na zoezi la kumpa huduma ya kwanza yule binti. Ni kama walikuwa wapenzi!!
******
Basi lilikuwa katika mwendo mkali lakini salama hapo likikaribia ardhi ya Shinyanga majira ya saa mbili kasorobo jioni, dereva ambaye tangu safari ianze alikuwa anazungumza mara kwa mara na abiria aliyekuwa pembeni yake alijikuta akifumba macho na kuyafumbua ghafla huku masikio yake yakijibiwa kwa kilio kikali kutoka upande fulani wa gari, ni uzoefu aliokuwa nao ndio sababu pekee iliyozuia gari lile lisipinduke baada ya kulivaa shimo ambalo hakuliona kwa kukosa umakini wakati wa kuendesha. Gari liliposimama, Michael alikuwa wima, macho yamemtoka pima huku chini akiwepo yule binti ametulia tuli huku akitoa kilio kwa sauti ya chini mno.
Abiria kadhaa walisogea kule alipokuwa Michael na kumsaidia kushangaa huku hata mmoja hakuthubutu kumgusa yule binti kwa jinsi alivyokuwa amejikunjakunja katika hali isiyokuwa ya kawaida kabisa. “Gari ilipopiga lile bonde tulirushwa juu niliweza kumshuhudia akitua kwenye siti yake kwa kishindo halafu…sijui ni nini kimetokea baada ya hapo.” Alizungumza Michael baada ya maswali kumwangukia yeye juu ya kilichomsibu yule binti ambaye watu walimtambua kama mpenzi ama ndugu yake. “Mambo mengine kujitakia tu tazama sasa huyu wamegombana nyumbani amemnyanyasa kwenye gari hadi ameaibika ona sasa mwisho wake.” Alilalamika mwanamke mmoja aliyeonekana kuguswa sana na hilo jambo. Michael alitamani sana kujieleza kwamba hafahamiani na yule binti lakini aliamini kwamba hakuna hata mtu mmoja ambaye angeamini hivyo aliendelea kubaki kimya asijue la kufanya. Ile kauli aliyoitoa kuwa yeye yupo na yule binti tayari ikaanza kumuingiza matatani. Na hakuwa na ujanja wa kujinasua. Kauli ile ilisikiwa na wengi!!! *** Huyu binti kimemsibu nini??
***
Michael amejiingiza katika utata wa mtu asiyemfahamu, je atajinasua vipi? ITAENDELEA
No comments:
Post a Comment