Na George Iron
“Binti!!!...binti!!!! we dada….” Aliita
huku akijaribu kumtikisa kidogokidogo, hakupata jawabu lolote lile. Funda la
hasira likitiwa hamasa na uoga aliokuwa nao lilimkaba na kujikuta akijuta
kumsaidia yule binti kulipa nauli na kujitambulisha mbele za watu kwamba
anafahamiana naye. Uvumilivu ukamshinda mtoto wa kiume akajikuta anamwaga
chozi, ilianzia hasira kumkaba kooni, mara macho yakawa mekundu, kisha machozi
yakatoka halafu kikafuatia kilio cha kwikwi. Michael alilia sana kwa mtihani
mkubwa uliokuwa mbele yake hakuelewa ni vipi anapata suluhu kwa sasa.
“Kaka…..kaka…..” sauti ya kike ilimshtua
Michael kutoka katika kilio kikuu
“Mh!!! Aah!! Binti…..umekuwaje…”
“Nikuulize wewe….aaaaah!!! nimeteleza
kutoka bafuni…kichwa kinaniuma jamani ah!” alilalamika kwa uchungu, Michael
hakuamini macho yake kwamba binti alikuwa anazungumza huku akiwa amekaa kitako.
“Pole sana pole…..unaweza kusimama????”
aliuliza
“Hapana kiuno kinauma sana sidhani kama
naweza kusimama” jibu hilo lilirudisha mawazo upya kwa Michael lakini wakati
huu hakuumia kama alivyoumia awali. Binti alijivutavuta kwa msaada wa Michael
hadi akakaa kitandani kwa kujilaza maana hakuweza kukaa imara.
Baada ya muda binti alipitiwa na usingizi
na kumpa fursa Michael kuwaza ni nini atafanya kuepuka hilo janga alilolivaa
mwenyewe.
“Kesho sisafiri na huyu binti..wema wangu umetosha
sasa, sibadili mawazo tena kama nilisema kuwa NIPO NAYE hilo neno nalifuta
rasmi, mimi simjui bana!!!” alijichukulia maamuzi hayo kijana Michael.
Majira ya saa tatu usiku binti alikuwa
ameamka tayari kutoka usingizini, kwa upande wa Michael bado alikuwa hajalala
kwa sababu ya kuumiza kichwa juu ya uamuzi anaotaka kuuchukua.
“Umeamka??” Aliuliza swali ambalo
alilitambua jibu lake
“Eeh!!!”
“Nikuletee chakula gani???”
“Maji kwanza halafu chakula nichagulie”
“Mh!! Wewe chagua bibie wala usiogope sawa
eeh!!!” alijibu Michael
“Haya chipsi na mishkaki, tia pilipili,
tomato, ukwaju, saladi, chumvi, na nini vile ndimu eeh!!” aliongea haraka
haraka kwa utani Michael akajikuta anatoa tabasamu huku akisugua viganja vyake
katika mkono wa yule binti. Bila kuaga alitoka nje na kurejea baada ya nusu saa
akiwa na chakula na maji, akamsaidia binti aweze kukaa kisha akafungua chakula,
kwa akili ya kujiongeza akaanza kumlisha yule binti, kila macho yao
yalivyogongana Michael alikuwa wa kwanza kukwepesha, alikuwa ni mwanaume mwenye
aibu sana mbele ya wanawake huo ni udhaifu uliokuwa wazi kwake. Walitumia saa
moja zima kula chakula hadi kukimaliza, Michael licha ya kumwonea huruma binti
lakini azma yake ya kumwacha pale gesti ilikuwa palepale.
“Michael wewe ni mwema sana asante sana kwa
wema uliouonyesha kwangu…” sauti nyororo ya binti ilipenyeza katika masikio ya
Michael..
“Sijui nikulipe nini lakini ubarikiwe sana,
naomba kitu kimoja nikuombe na ninaamini utanielewa.”
“Kitu gani tena.”
“Waonaje kama ukiniacha hapa uendelee na
shughuli zako mimi nimekuwa mzigo mkubwa sana kwako angali u kijana mdogo tu,
naomba kesho unitoe nje na uniache barabarani hapo heri niwe ombaomba maana
ndio maisha niliyoyachagua tofauti na kule nilipokuwa, nia yangu ya kuondoka
kule imefanikiwa huo kwangu ni ushindi mkubwa sana…” aliendelea kuzungumza huku
akijilazimisha kutabasamu.
Maneno ya yule binti yalimshtua sana
Michael kwani alikuwa amepanga kumuacha kinyemela lakini anashangaa binti kwa
hiari yake mwenyewe anaomba aachwe.
“Kwa nini unaongea maneno hayo dada yangu,
mimi bado sijakuchoka.” alidanganya Michael
“Sijasema umenichoka wewe unadhani
utaendelea kuwa namimi hadi lini na wapi???.” Swali hilo lilikuwa gumu sana kwa
Michael kwani hakika jibu lake lilikuwa ni muda muafaka wa kumwacha yule binti.
“Usiumie sana kaka Michael….wewe ni
mwanaume wa kipekee, Mungu atakulipa katika njia zako utakazoenda nitakukumbuka
sana na siku moja utakutana tena na mimi nikiwa salama mimi sitakusahau na hata
wewe ukiniona usisite kuniita kwa nguvu zote JOYCEEEEEEEEE!!!!!! Mimi
nitageuka”
“Hah!! Kwani unaitwa nani wewe na huyo
Joyce ni nani??.” Aliuliza Michael huku akiweka kiuno chake vizuri pale
kitandani.
“Ooh!! Ulizoea kuniita binti mwone!! Naitwa
Joyce mie” Alizungumza yule binti
“Unaitwa Joyce….we acha utani”
“Utani gani mie Joyce jina langu la
kuzaliwa kwani vipi??”
“Kuna msichana mmoja anaitwa Joyce…”
“Vipi wifi yangu nini??.” alidakia Joyce
“Hapana alikuwa rafiki tu ndio maana
nilishtuka kumbe na wewe ni Joyce…” alizungumza kwa uchangamfu mkubwa Michael.
Kwa maongezi yao ya usiku uliopita Michael
alijikuta akivunja kwa mara nyingine tena makubaliano yake na moyo wake, kwa
kuwa Joyce alikuwa na uwezo wa kutembea japo kwa shida sana Michael aliongozana
naye kuelekea kituo cha mabasi wakiwa katika teksi iliyowafikisha haraka,
Michael akamsaidia Joyce wakapanda ndani ya basi la Mombasa Raha katika siti za
mbelembele na safari ya kuelekea Mwanza ikafuata. Ubora wa barabara hiyo ya
kuelekea Mwanza ulimpa ahueni Joyce kwani hakutoneshwa kiuno chake.
“Nitakuacha Mwanza sawa.” ndilo neno la
muafaka kati ya Joy na Michael waliloamua usiku uliopita. Safari ilionekana
fupi sana kwa Michael kwani nafsi ilikuwa haijaridhika kumuacha njia panda
Joyce ambaye kwa majina amefanana na binti aliyempenda wakati akiwa jijini Dar
es salaam.
Saa tano asubuhi safari ya masaa mawili
ilikuwa imefikia kikomo katika stendi ya Nyegezi jijini Mwanza. Si Michael wala
Joyce aliyekuwa anaufahamu fika mji huu uliotawaliwa na milima ya hapa na pale
hivyo kila mmoja alimtazama mwenzake.
“Tupeleke lodge yoyote iliyopo karibu na
iwe nafuu kiasi.” alijieleza Michael kwa sauti ya chini mbele ya dereva.
“Poa..” alijibu dereva kisha Michael na
Joyce wakapanda safari ya dakika kumi ikawafikisha mbele ya lodge iliyojulikana
kwa jina la DOUBLE G, baada ya kupewa pesa yake akatokomea yule dereva.
“Chumba bei gani???...aah!! kwanza vyumba
vipo??” Aliuliza Michael
“Vipo lakini subiri kidogo hebu…we nanii
Dory, hivi chumba namba 18 kipo wazi au alilipia kulala yule bwana.”
waliulizana wahudumu katika hali ya kunong’ona kisha likapatikana jibu kwamba
kilikuwa wazi
“Chumba kipo elfu kumi si mnalala au ni
show time kama ni show basi elfu tano!!”
“Hapana tunalala” Alisema Michael huku
akitoa pesa mfukoni na kulipia chumba.
Hakuna aliyekuwa amechoshwa na safari
lakini kutokana na kila mtu kuwaza la kwake walijikuta wakipitiwa na usingizi
kila mmoja kwa wakati wake. Hadi saa moja usiku ndipo mkojo ulimwamsha Joy na
yeye akamwamsha Michael.
“He!! Tumelala hivyo…..” Alijiuliza Michael
wakati huo tayari Joy alikuwa ameingia msalani.
Aliporejea Michael yeye alikuwa amevaa
viatu vyake na alikuwa na kila dalili ya kutaka kutoka.
“Wapi tena ndugu yangu jiji lenyewe hulijui
tuachie sisi.” Alitania Joy
“Naenda kucheki benki kama mkopo umeingia
si unajua tena…vipi twende wote”
“Mimi sitoki humu ndani usije ukanipoteza
bure” alijibu Joy, Michael akajiondokea.
Dakika thelathini baadaye mlango uligongwa.
“Hebu ingia au unadhani umepotea” alijibu
Joy na kweli kitasa kikashushwa wakaingia watu watatu waliojazia miili yao.
Bunduki ndogo iliyowatangulia mkononi ilitosha kumnyamazisha Joy.
****
Michael alikuwa na furaha ya ajabu sana na
alijiona ni mtu mwenye bahati kila mara, ndio alikuwa na bahati! Maana pale
benki hapakumkatisha tamaa ila kumwongezea furaha tele, pesa ilikuwa imeingia
katika akaunti yake pesa ya mkopo!
“Huyu Joy huyu ana miujiza yake na nikifika
lazima nimwambie baraka anazoniletea.” alisema Michael bila watu wengine kujua
alikuwa anaongea nini, alipovuka barabara kuelekea upande mwingine akili
ilimrudisha tena upande aliokuwa lengo ni kununua hiki na kile kwa sababu ya
safari ya kesho yake safari ya kuelekea Mugumu Serengeti, alinunua vitu kadhaa
wakati huo akiwa na jeuri ya pesa mfukoni mwake.
“Joy, Joy, Joy…mh!! Ni msichana wa aina
yake” alikiri Michael baada ya kufanya tathmini ya Joy akiwa si mgonjwa kama
alivyo wakati huo.
Ni mrefu kama mnyarwanda, si mweupe sana
lakini weusi wake unatosha kumwona gizani na kwenye mwanga, midomo yake ina
majeraha lakini kama ikipona ni mtego tosha kwa mwanaume yeyote asiye na
subira, kifua chake ambacho Michael aliweza kukiona bahati mbaya alipokuwa
ameanguka kutoka bafuni kilikuwa na mzigo mdogo wa embe dodo ambazo hazikuwa na
mpango wa kuanguka katika siku za karibuni, tabasamu lake la nadra liliruhusu
vishimo vilivyojificha kuchomoza na kuzidi kuing’arisha nuru ya uso wake. Hiyo
ni picha ambayo aliijenga Michael akiwa katika manunuzi ya hapa na pale, mawazo
hayo yalimpeleka katika ushawishi, ushawishi nao ukachipua upesi akajikuta
anashawishika, kishawishi cha kuondoka na Joy kuelekea Mugumu Serengeti mahali
ambapo hajawahi kufika kabla.
“Nitaondoka naye…atapona mbele kwa mbele
naamini atafurahi sana” Alisemezana na moyo wake huku akirejea kule alipomwacha
Joyce.
* * *
Kaubaridi ka asubuhi asubuhi katika jiji la
Mwanza maeneo ya Nyegezi karibu na chuo kikuu cha mtakatifu Augustino
kaliwachochea wavutaji wengi wa sigara kununua pakiti kwa pakiti kukabiliana
nayo huku wasiokuwa wavutaji wakipekua huku na huku kujua ni wapi waliyaacha
masweta yao hapo ni baada ya kuingia hasara ya kununua miamvuli mipya kutokana
na mvua iliyonyesha kuanzia alfajiri.
Kijiwe cha Bob Soya cha hapo Nyegezi kona
kilikuwa na wadau wengi sana, wachache walikuwa na uwezo wa kununua kete za
bangi huku wengi wakisubiri za ‘kugongea’ kwa wenzao. Ushikaji uliwekwa pembeni
kutokana na hali halisi ya hewa, kila mmoja alitamani moshi mkali wa madawa
hayo uendelee kupenyeza ndani ya mapafu yake kisha kutoka nje kupitia pua na
mdomo wake. Pusha aliifurahia sana hali hiyo ya hewa kwani aliuza kwa wingi
sana bidhaa zake. Mteja mmoja peke yake ndio alikuwa hazungumzi sana, yeye na
bangi, bangi na yeye huku muda ukisogea.
Matusi makali makali yalizunguka eneo hilo
ambalo lilikuwa jirani na nyumba ya kuishi watu. Matusi hayo mwishowe yakavunja
amani iliyotawala kwa muda mrefu na kuzaa vita ndogo iliyosababishwa na ukosefu
wa ustaarabu wa bwana mmoja aliyelazimisha kupewa kipisi cha bangi kwa ulazima
huku akiwa hana pesa ya kukidhi hiyo haja yake. Ubabe wake uliwatetemesha wengi
lakini leo alikuwa amempata kiboko yake.
“Mkishagombana ndio mtapata zawadi ya
‘ndumu’ ama!!!” alizungumza yule mzee ambaye alikuwa kimya muda wote akivuta
bangi kistaarabu. Wote waligeuka kumwangalia kwa sekunde kadhaa kisha wakataka
kumpuuza na kuendelea kushabikia ugomvi.
“Kaka, hebu wapatie idadi wanayotaka
nitalipia” aliongea kwa jeuri akimtazama yule muuzaji. Amri hiyo ilipunguza
makali ya ugomvi na kuuvunja kabisa, maadui wakawa marafiki na hasira kuwa
vicheko. Huyu alikuwa ni mzee Robert Chacha, mfanyabiashara maarufu wa samaki
katika jiji la Mwanza ambaye kutokana na kabila lake la kikurya isitoshe
alikuwa mwanajeshi mstaafu alitokea kuwa maarufu kwa jina la ‘poti’. Ilikuwa
mara yake ya kwanza kukifikia kijiwe hichi cha Bob Soya na hakuna aliyemtambua
zaidi ya kujua kuwa ni mvuta bangi wa kawaida aliyezidiwa na baridi.
Ndio Poti alikuwa amezidiwa na baridi hilo
halikuwa na ubishi, lakini jeuri yake ya kukivutisha kijiwe kizima ndio
ilimshtua kila mtu.
“Shilingi ngapi jumla??” aliuliza Poti
baada ya kila mmoja kuwa ameridhika na pia mzigo kumwishia muuzaji. Muuzaji
alimtajia bei kwa uoga akidhani huenda ni bangi zilikuwa zimemchanganya huyu
mzee na kujikuta anazungumza vitu asivyovijua lakini haikuwa hivyo, Poti
alizama katika kibegi kidogo alichokuwanacho akakipekua kwa kubahatisha akachomoka
na noti kadhaa zilizotosha kutibu njaa ya muuza.
“Hiyo nyingine tunza…” alikataa kupokea
chenchi aliyorudishiwa, akafunga kibegi chake na kutoweka.
Alipoondoka nyuma aliacha gumzo huku kijiwe
kikiwa kimesahau kuhusu ugomvi uliotaka kuibuka. Safari ya Poti ilikuwa haina
uelekeo maalum ndio maana alijikuta akiishia katika nyumba ya kulala wageni
ambayo alienda kwa minajiri ya kubadili nguo zake zilizolowana lakini kama
bahati mbaya na nzuri kwake akamkuta msichana asiyekuwa na uelekeo ni huyo
aliyemsindikiza chumbani kwenda kuwa jalala kwa muda, yaani kuuchukua uchafu wa
Poti na kuuhifadhi.
Poti alipofika ndani aligundua hiyo haikuwa
tabia yake labda huenda ni bangi aliyovuta imemchanganya, badala ya kumtumia
yule msichana aliyetegemea ujira baada ya kazi alimshangaza alipomlipa na
kumruhusu kuondoka. Baada ya yule changudoa kuondoka Poti alibadili nguo zake
na kupitia mlango wa nyuma akatokomea.
Hicho kilikuwa chumba namba 18, chumba
ambacho Michael na Joyce wake walikuwa wamekilipia kwa ajili ya hifadhi ya
usiku mmoja bila kujua kama kilitumika siku hiyo hiyo.
TATIZO
Mdomo wa bunduki uliokuwa umemuelekea Joy
pale kitandani haukuwa umekosea njia hata kidogo, walikuwa ni walewale wavuta
bangi waliopewa ofa ya kuvuta bure, tayari walikuwa wameusahau wema wa Poti
kuwatoa katika baridi bila gharama yoyote sasa wanataka kujua ana nini katika
begi wakiamini ni halali yao, ama kweli kijiweni hakuna rafiki wa kweli!!. Poti
hakuwa pale ndani tena, walikuwepo watu wasiokuwa na hatia yoyote.
“We Malaya yuko wapi bwana yako????” sauti
nzito ilimuuliza Joy pale kitandani wakati huo alikuwa anatetemeka na kuyasahau
maumivu yaliyokuwa yanamkabili.
“Sina….bwaaa..na!!!.” alijibu kwa
kutetemeka sana Joyce. Kitako kimoja tu cha nguvu cha bunduki kiliiweka akili
yake sawa
“Bwana yako yuko wapi malaya wewe!!!.”
sauti hii ilikuwa kali kuliko ya kwanza Joy hakutaka kuleta ubishi.
“Ametoka kidogo….atarudi” alilazimika
kujibu kwa hofu ya mtutu wa bunduki.
“Soya….tumsubirie…..atarudi huyo fala muda
si mrefu..” walinong’onezana wao kwa wao, wakati huu walikuwa wameutoa ule
mtutu wa bunduki jirani na Joyce lakini alikuwa anatetemeka sana. Baada ya
dakika kumi zilisikika hatua zikijongea katika mlango wa chumba namba 18.
Majambazi watatu walijibanza nyuma ya mlango huku mmoja akiingia uvunguni mwa
kitanda. Mlango ukarudishiwa kidogo.
“Surpriiiiise!!!!!!!!” ukelele ulisikika
kutokea nje ya mlango, ilikuwa sauti ya Michael ni Joy pekee aliyeitambua, moyo
wake ukakata tamaa, alijua Michael alisubiri ajibu chochote. Laiti kama angejua
kilichopo hapa ndani wallah!! Asingethubutu kuingia! Alijisemea Joyce huku
Michael akiendelea kupiga kelele pale nje.
Joy hakujibu chochote kile kwani alikuwa na
hofu juu ya wale watu wabaya waliokuwa chumbani hapo. Sura zao hazikuwa na
mzaha hata kidogo walimaanisha walichokuwa wamekifuata hapo ndani. Taratiibu
mlango ukaanza kufunguliwa kwa mguu kumaanisha kwamba kuna kitu mikono ilikuwa
imebebwa hivyo kushindwa kutimiza wajibu huo.
Uso wa Michael ulikuwa umechanua kwa
tabasamu murua, hakuwa amevaa zile nguo alizotokanazo nje. Wakati huu sasa
aliweza kuyaonyesha maungo yake vyema, kifua kilichogawanyika katikati kutokana
na mazoezi ya hapa na pale kilichomoza katika fulana iliyokuwa imembana hasa,
suruali aina ya jinsi ilimchora miguu yake ilivyokuwa imara bila kuyumbishwa na
matege ya aina yoyote kilikosekana kitu kimoja tu kukamilisha utanashati wa
Michael, hakuwa akitabasamu! Ndio na hakupaswa kufanya hivyo maana Joy alikuwa
ameyatumbua macho yake na kutokwa jasho kitu kibaya kilikuwa kimemtokea!!
Taratibu bila kuzungumza chochote Michael ambaye alikuwa amesimama sasa mbele
ya chumba hicho kimoja naye alimkazia macho Joy. Michael hakupaswa kusubiri
kuambiwa akae chini, pigo moja tu katika mbavu zake lilimfanya ajikunje huku
akitoa ukelele mdogo, akili ilikataa asikae chini lakini mwili bila ubishi
ulilainika hatimaye akasalimu amri mbele ya Joy, mtutu wa bunduki ukafuata
katika shingo yake, hofu ikaanza kutanda hofu ikamtawala na uoga.
ITAENDELEA