Tuesday, October 6, 2015

THE PAINFUL TRUTH 6

 



RIWAYA: PAINFUL TRUTH (UKWELI WENYE KUUMA)
MTUNZI: Nyemo Chilongani
MAWASILIANO: 0718 06 92 69

SEHEMU YA SITA

Bwana Brown alionekana kuchanganyikiwa mara baada ya kuyasikia maneno yale ambayo alikuwa ameambiwa na kijana wake, Wayne. Kitu cha kwanza akazirudisha kumbukumbu nyuma na kuanza kukumbuka kama kuna siku yoyote Wayne alikuwa ametembea na msichana na kumpa mimba lakini hakupata jibu.
Hakuelewa ni mtoto gani ambaye Wayne alikuwa amemzungumzia mahali hapo. Akakiinua kichwa chake kutoka karibu na Wayne na kisha kuyapeleka macho yake usoni kwa mke wake, Bi Lydia. Uso wa Bwana Brown ulionyesha waziwazi kwamba ulikuwa umetawaliwa na maswali mengi, akaanza kupiga hatua na kumfuata mke wake.
“Vipi?” Bi Lydia aliuliza huku akionekana kuwa na hamu ya kutaka kufahamu kitu.
“Anamtaka mtoto wake” Bwana Brown alimjibu.
“Mtoto gani?”
“Sijui”
“Kwani katika kipindi ambacho alipata ajali, Kristen alikuwa mjauzito?” Bi Lydia aliuliza.
“Hapana”
“Sasa mtoto gani anayemtaka?”
“Hata mimi mwenyewe nashangaa. Ila nafikiri atakuwa hajakaa sawa, si unajua mishipa yake ya fahamu ndio inaanza kurudi katika hali yake”
“Inawezekana”
Hakukuwa na mtu ambaye alijisumbua kufuatilia maneno ambayo alikuwa ameyaongea Wayne kwani walijua kwamba akili yake wala haikuwa imekaa sawa. Daktari mmoja na manesi wawili wakaingia ndani ya chumba kile na kisha kuwataka Bwana Brown na Bi Lydia kutoka ndani ya chumba kile kwa ajili ya kuanza kazi yao.
Kila siku Wayne alikuwa akiwaambia maneno yale yale kwamba alikuwa akitaka kumuona mtoto wake. Maneno yale yakaendelea kuwashtua kupita kawaida kitu kilichowapelekea kuanza kufuatilia. Walifuatilia kwa muda wa mwezi mmoja lakini hawakufanikiwa kujua mtoto ambaye Wayne alikuwa akimzungumzia.
Hali ya Wayne ilikuwa ikizidi kutengemaa kadri siku zilivyokuwa zikizidi kwenda mbele. Kutokana na fedha nyingi ambazo alikuwa nazo Bwana Brown, madaktari kutoka katika hospitali kubwa wakaanza kuingia ndani ya hospitali ile kwa ajili ya kumtibia Wayne.
Miezi tisa ikakatika na ndipo hali ya Wayne ikarudi kabisa ila mwili wake ulikuwa na tofauti kubwa sana. Alichokifanya daktari ni kuwaita wazazi wake ndani ya ofisi yake na kisha kuanza kuongea nao huku kila mmoja akionekana kuyafurahia maendeleo ya Wayne.
“Tunamshukuru Mungu kwa kuwa Wayne anaendelea vizuri” Dokta aliwaambia huku akiyaweka vizuri miwani yake pamoja na kulichukua faili kubwa ambalo lilikuwa juu ya meza yake.
“Hata sisi tunashukuru” Bwana Brown alimwambia daktari huku akiwa amemshika mkono mkewe pale vitini walipokuwa wamekaa.
“Kuna mambo mawili ambayo yametokea katika mwili wake. Kwanza ninasikitika kuwaambia kwamba mtoto wenu Wayne hatoweza kutembea tena. Miguu yake pale ilipo ilikuwa imesagika kidogo. Katika kipindi chote tulikuwa tukiangaika nayo. Namshukuru Mungu kwamba tulifanikiwa kwa asilimia themanini kwani kama tungeshindwa kabisa, haina budi tungeikata miguu yake” Daktari aliwaambia.
Kila mmoja akaonekana kushtuka, maneno ambayo alikuwa ameyaongea daktari yalionekana kuwagusa kupita kawaida, walimwangalia daktari mara mbili mbili kana kwamba yeye ndeye ambaye alikuwa amesababisha yale yote.
“Ila tunashuru kwamba ni mzima” Bi Lydia alimwambia daktari.
“Jambo la pili ni kwamba tuligundua kwamba mtoto wenu amekatika mshipa mkubwa ambao unawezesha uume wake kusimama. Mshipa ule haufanyi kazi tena, kwa maana hiyo mtoto wenu hatoweza kusimamisha uume wake tena jambo ambalo halitoweza kumpa mtoto katika maisha yake yaliyobakia” Daktari aliwaambia.
Taarifa hiyo ndio ambayo ilionekana kumshtua zaidi kila mmoja. Wakamwangalia daktari kwa macho yaliyojawa na mshtuko, hawakuonekana kukiamini kile ambacho daktari alikuwa amekiongea mbele yao. Kwa mtoto wao Wayne kukosa uwezo wa kuwa na mtoto kulionekana kuwakosesha raha, waliyaona maisha yake kujaa giza huko mbeleni.
Hawakujua Wayne angeishi katika maisha gani, kutokutembea na kutokuwa na uwezo wa kusimamisha uume wake yalionekana kuwa matatizo makubwa ambayo yalikuwa yameupata mwili wake. Bi Lydia akashindwa kujizuia, akainamisha kichwa chake chini, alipokiinua, machozi yalikuwa yakimtoka.
Ni kweli kwamba walikuwa na mtoto mwingine, huyu alikuwa akiitwa Esther, lakini kwa upande wao walikuwa na mapenzi ya kweli kwa Wayne. Hata kama Esther angepata watoto kumi lakini furaha yao isingekamilika bila Wayne kutokuwa na mtoto.
Hawakujua ni kitu gani ambacho walitakiwa kukifanya, kukubaliana na matokeo yale ikaonekana kuwa kazi kubwa sana mioyoni mwao. Walichokifanya mara baada ya kutoka ndani ya hospitali ile ni kuanza kuwasiliana na madaktari waliokuwa wakubwa zaidi kutoka katika nchi mbalimbali.
Wayne akaanza kusafirishwa na kupelekwa katika nchi mbalimbali duniani kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa kulitatua tatizo lile ambalo alikuwa nalo mwilini. Walitembea zaidi ya nchi kumi duniani tena kwa madktari mabingwa ambao walikuwa na uwezo mkubwa lakini kote huko hawakufanikiwa kabisa jambo lililowafanya kurudi nchini Marekani.
Wote wakakubaliana na matokeo. Wayne akaanza maisha mapya ya kuwa mlemavu wa miguu yake. Kila siku waandishi wa habari walikuwa wakielekea ndani ya nyumba hiyo na kuanza kuongea na Wayne ambaye siku zote hakuonekana kuwa na furaha.
Kitu ambacho alikuwa akitaka kuwaambia wazazi wake ni kuhusu Happy, msichana wa Kitanzania ambaye alimuacha akiwa mjauzito. Hakutaka kufanya haraka katika kuwaaambia hilo kwani aliamini kwamba ni lazima apate muda wa kutulia kabla ya kuongea kitu chochote kile.
Siku ziliendelea kukatika lakini Wayne hakuongea kitu chochote kile kwa wazazi wake. Kila siku alikuwa akijitahidi kutafuta njia mbalimbali za kumuwezesha kuwasiliana na Happy lakini ilishindikana kabisa. Miezi miwili ikakatika na ndipo hapo Wayne alipoamua kuwaita wazazi wake na kuanza kuongea nao.
“Nahitaji kwenda Tanzania” Wayne aliwaambia.
“Kuna nini?”
“Hapana. Ninahitaji tu kwenda Tanzania” Wayne aliwaambia.
“Hali yako si nzuri kusafiri masafa marefu. Tuambie kitu chochote kijana wetu tutakufanyia ila si kukuruhusu kuelekea nchini Tanzania” Bwana Brown alimwambia Wayne.
“Maisha yangu yametawaliwa na majonzi, kila siku nilikuwa nikikaa nikimfikiria msichana mmoja ambaye nilikutana nae katika mazingira ya kutatanisha na kumfanyia kitu ambacho kimekaa na kuniumiza moyoni” Wayne alisema huku akianza kulengwa na machozi.
Kila mmoja alikuwa kimya akimwangalia Wayne, maneno ambayo aliyaongea yalikuwa yamewagusa mioyoni mwao lakini pia yalikuwa yamewachanganya kupita kiasi. Wayne akaonekana kuwa na kitu kizito ambacho alikuwa akitaka kuwaambia kwa wakati huo.
“Unatuchanganya” Bwana Brown alimwambia.
“Nafahamu kama mmechanganyikwa na maneno yangu ila ninahitaji kwenda nchini Tanzania kuonana na Happy” Wayne aliwaambia. Wote wakaonekana kushtuka zaidi.
“Happy! Ndiye nani huyo?” Bi Lydia aliuliza kwa mshtuko.
“Msichana niliyemuacha akiwa na ujauzito wangu” Wayne alijibu.
Kwa mshtuko ambao walikuwa wameupata mioyoni mwao, walijihisi kwamba muda wowote ule wangeweza kuzimia. Maneno yale yaliwachanganya zaidi kuliko hata maneno mengine ambayo walikuwa wameyasikia kutoka kwa Wayne.
Wakamwangalia Wayne na kuanza kumsoma saikolojia yake kuona kwamba alikuwa akitania au alikuwa akimaanisha kile ambacho alikuwa akikiongea. Wayne alionekana kumaanisha. Jina la Happy ndilo ambalo lilizua mjadala mkubwa vichwani mwao, wakatamani kumfahamu huyo Happy, mbali na huyo, pia walitaka kufahamu kuhusu huo ujauzito.
“Umesemaje?” Bwana Brown aliuliza huku akionekana kuwa na mshtuko uliojaa furaha.
Hapo ndipo Wayne akaanza kuwaadithia kila kitu ambacho kilikuwa kimetokea katika safari yake ya kwanza ya kitalii kuelekea nchini Tanzania miaka sita iliyopita. Hakuficha kitu chochote kile, alikuwa wazi kwa kila kitu ambacho alikuwa amekifanya kipindi kile.
Bwana Brown na mkewe, Bi Lydia wakaonekana kushtuka kwa furaha, hawakuamini kama kijana wao alikuwa na uwezekano wa kuwa na mtoto ambaye alikuwa nchini Tanzania. Wakajikuta wakisimama na kukumbatiana, machozi ya furaha yakaanza kuwatoka.
“Msifurahi kwa sasa mpaka pale ambapo mtakapomuona mtoto wangu mbele ya macho yenu. Hamuwezi kujua kwamba labda Happy alipata matatizo na mimba kutoka au hata mtoto kufariki” Wayne aliwaambia.
“Ni lazima nisafiri kuelekea huko Tanzania. Ni lazima nikamchukue mjukuu wangu” Bwana Brown alisema huku akionekana kuwa na furaha.
“Nami pia ninataka kwenda huko. Ninataka kumuona mjukuu wangu” Wayne aliwaambia.
“Wewe pumzika nyumbani. Tutakwambia kila kitu kitakachojili” Bwana Brown alimwambia Wayne.
Hakukuwa na cha kuchelewa, kwa haraka haraka viza zikaandaliwa na baada ya siku mbili safari ikaanza. Ndani ya ndege, Bwana Brown na mkewe, Bi Lydia walikuwa wakizungumzia kuhusu mtoto huyo ambaye walikuwa wakielekea kumuona nchini Tanzania.
Sala zao bado zilikuwa zikiendelea mioyo mwao kwa kumuomba Mungu awe Amemlinda mtoto yule mpaka katika kipindi ambacho watamchukua na kumpeleka kwa baba yake. Waliiona ndege ikienda kwa mwendo wa taratibu sana, walitamani wapotee kama wachawi na kujikuta ndani ya nyumba hiyo ambayo walikuwa wameelekezwa.
Mara baada ya ndege kutua katika uwanja wa Mwl Julius Nyerere, wakatoka nje ambako wakaomba kupelekwa katika ofisi za shirika la ndege la Precious Airlines na kukata tiketi ya ndege tayari kwa ajili ya kuelekea jijini Arusha.
Kutokana na kutokuwa na wasafiri wengi siku hiyo, wakapata ndege na saa tisa jioni safari ikaanza. Walichukua dakika arobaini na tano mpaka ndege kuanza kutua katika uwanja wa KIA ambapo wakaanza kuelekea katika moja ya hoteli ya nyota tano ya Jupiter iliyokuwa hapo Arusha.
Wakapata chumba na kutulia. Wakatoa ramani ambayo walikuwa wamechorewa na Wayne na kisha kuanza kuiangalia vizuri. Kila mmoja akaonekana kuridhika, ramani ya kuelekea nyumbani kwa Bi Selina ilionekana kueleweka vichwani mwao.
Siku iliyofuata asubuhi na mapema safari ya kuelekea nyumbani kwa shangazi yake Happy, Bi Selina ikaanza. Walikuwa wakiifuatilia ramani ile kama jinsi ilivyokuwa imeelekeza. Walipata tabu sana kutokana na nyumba nyingi kujengwa na hata mazingira kuwa tofauti sana, mwisho wa siku wakafanikiwa kuiona nyumba hiyo.
Wakaanza kuugonga mlango na baada ya muda fulani, mwanamke mmoja aliyekuwa na nywele zilizoanza kupatwa na mvi akafungua mlango, alikuwa Bi Selina. Wakajitambulisha kwake, wakaonekana kueleweka.
“Mmmhh!”
“Mbona umeguna?” Bwana Brown aliliza.
“Sidhani kama Happy atakubali kuonana nanyi” Bi Selina aliwaambia.
Hapo ndipo walipoanza safari ya kuelekea Machame. Njia nzima Bwana Brown na mkewe walikuwa wakijitahidi kuuliza maswali mengi kuhusu mjukuu wao lakini Bi Selina hakutaka kujibu chochote kile. Wakaingia ndani ya daladala, Bwana Brown hakujali kama alikuwa tajiri mkubwa, kitu ambacho alikuwa akikijali kwa wakati huo ni kumuona mjukuu wake tu.
Wakaanza kuingia katika eneo la nyumba ya mzee Lyimo. Bi Selina akaanza kuufuata mlango na kisha kuugonga, baada ya muda, Bi Vanessa akaufungua mlango ule. Wazungu ambao walikuwa wakionekana mbele yake hakuwa akiwafahamu lakini akaonekana kuhisi kitu fulani. Baada ya salamu, akawakaribisha ndani.
Maongezi yakaanzia hapo huku nae mzee Lyimo akiwa pembeni. Bwana Brown alijitahidi kujielezea kwamba alikuwa nani na alikuwa amefuata kitu gani mahali hapo. Hakukuwa na mtu ambaye alikuwa amemuelewa, walionekana kupinga kupita kawaida.
Kila walipokuwa wakikumbuka siku ambayo Wayne alikuwa amekuja hapo na kisha kuondoka kwa hasira mara baada ya kuambiwa kwamba Happy alikuwa mjauzito waliona hakukuwa na sababu za kuwakubalia ombi lao.
“Amechukua miaka sita na huu unakwenda kuwa mwaka wa saba, hajawahi kumjulia hali mtoto wake, mbaya zaidi alikataa mimba na kusema kwamba si ya kwake, iweje leo anakuja kudai mtoto? Hata kama ni mahakamani tutakwenda lakini Andy atabaki kuwa kwetu” Mzee Lyimo aliwaambia huku akionekana kukasirika.
Hapo ndipo Bwana Brown alipoanza kuelezea kila kitu ambacho kilikuwa kimtokea katika maisha ya Wayne toka katika kipindi kile alichokuwa amepata ajali na kulazwa kitandani kwa muda wa miaka sita. Wote wakaonekana kushtuka, hasira ambazo walikuwa nazo zikaonekana kupotea.
“Hapo alipo hawezi hata kutembea. Na kamwe hatoweza kutembea katika maisha yake” Bwana Brown aliwaambia.
“Furaha pekee ambayo imebaki kwake ni kumuona mtoto wake tu. Nafikiri ataweza kufanya jambo lolote baya kama tu hatutarudi na kile ambacho amekitarajia” Bi Lydia aliwaambia.
Habari za kupata ajali kwa Wayne zikaonekana kuwa mpya kwao, ni kweli kwamba Wayne alikuwa ameikataa mimba ile lakini katika upande wao mwingine wa moyo walijua kwamba kama asingepata ajali basi angekuwa amekwishafika nyumbani hapo siku nyingi.
Alichokifanya Bi Vanessa ni kuinuka na kuelekea chumbani kwa Happy ambaye alikuwa amelala. Ile kuufungua mlango, Andy akatoka huku akikimbilia pale sebuleni na kumfuata mzee Lyimo na kuishika miguu yake.
“Babu atata mma” Andy alisema katika lafudhi ya kitoto.
Bwana Brown na mkewe hawakuamini mara macho yao yalipotua kwa Andy. Andy alikuwa amefanana kwa kila kitu na mtoto wao, Wayne. Wote wakaonekana kufarijika, wakajikuta wakitokwa na machozi ya furaha.
“Ndiye yeye. Mwangalie alivyofanana na baba yake” Bi Lydia alisema huku akitamani kumfuata Andy na kumkumbatia.
Wala hazikupita dakika nyingi, Happy akatokea sebuleni hapo akiongozana na mama yake. Macho yake yakatua kwa Bwana Brown na Bi Lydia ambao macho yao bado yalikuwa yakimwangalia Andy. Alichokifanya Happy ni kumfuata mtoto wake, Andy kumchukua na kumpakata.
Mazungumzo yakaanza upya, walielezea kila kitu ambacho kilikuwa kimetokea katika maisha ya Andy mara baada ya kuondoka nchini Tanzania na kuelekea nchini Marekani. Tofauti na matarajio yao, Happy alikuwa akitabasamu muda wote ambao alikuwa akielezewa kuhusu Wayne.
“Hayo ndio malipo. Hivyo ndivyo Mungu alivyotaka iwe. Andy ni mtoto asiyekuwa na baba. Nafikiri huyo Wayne ambaye amewatuma mje kumchukua si yule Wayne ambaye nini baba yake. Kama mlivyokuja na ndivyo ninavyotaka muondoke. Mtakapomuona, naomba mmwambie kwamba baba yake Andy alikwishafariki hata kabla Andy hajazaliwa. Mtakapoona haelewi naomba mmwambie kwamba Andy alifariki kwa ugonjwa wa Tete kuwanga ambao ulikuwa umemsumbua sana utotoni” Happy alisema.
Bila kutarajia, Happy akajikuta akianza kutokwa na machozi, uwepo wa Bwana Brown na mkewe ulionekana kumkumbusha mbali sana tangu kipindi cha kwanza ambacho alikutana na Andy. Kamwe hakutaka kumuona mwanaume huyo, alikuwa akimchukia kupita kiasi. Ilikuwa ni afadhali kukutana na shetani angempenda kuliko kukutana na mwanaume ambaye alikuwa ameikimbia mimba yake.
“SITAKI KUONANA NAE WALA MTOTO WANGU KWENDA POPOTE” Happy alisema na kisha kuingia chumbani kwake pamoja na mtoto wake, Andy.
Walijaribu kuugonga mlango lakini wala mlango haukufunguliwa. Bwana Brown na mkewe wakakaa mahali hapo huku wakimtaka mzee Lyimo na Bi Vanessa waongee na Happy lakini hilo nalo halikuwezekana kwani Happy alikuwa amejifungia mlango na wala hakukuwa na dalili za kuufungua.
“NIMESEMA SITAKI....SITAKI....SITAKI......SITAKI...”Sauti ya Happy ilisikika kwa nguvu masikioni mwao.

Je nini kitaendelea?
Je Happy ataendelea na msimamo wake huo?
Je uamuzi gani atauchukua Wayne baada ya kusikika kwamba Happy amekataa kumtoa mtoto?
Itaendelea.


No comments:

Post a Comment

Recent Posts